Katika
maadhimisho ya kumbu kumbu ya mwezi mmoja tangu Baba Mtakatifu
Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa, Jumamosi, tarehe 13 Aprili
2013 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na Wanajeshi wa
Kikosi cha Zimamoto cha Vatican na Watawa wa Upendo kwenye Kikanisa cha
Domus Sanctae martha, kilichoko mjini Vatican.
Papa
amewakumbusha kwamba, hata katika mahangaiko, mateso na shida mbali
mbali anazoweza kukabiliana nazo mwamini, kamwe asithubutu kutafuta njia
ya mkato bali wajiaminishe kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wa Kanisa la
Mwanzo, kadiri ya Matendo ya Mitume, walijikuta wanaanza kulalamikiana
na kubaguana katika huduma mambo ambayo yalikuwa yanadhohofisha umoja na
mshikamano wa upendo miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Mitume wakachukua
uamuzi wa kuwakutanisha na kujadiliana kwa pamoja na hatimaye, wakapata
suluhisho la matatizo yao.
Mitume walibainisha kwamba, dhamana
yao ya kwanza ni kusali na kutangaza Habari Njema ya Wokovu; kumbe
Mashemasi saba walioteuliwa walipewa dhamana ya kutoa huduma ya upendo
ambayo ni mwendelezo wa huduma na mshikamano wa upendo unaofanywa na
Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Kristo yuko daima pamoja na
wafuasi wake na kamwe hawezi kuwaacha wakaangamia.
Baba Mtakatifu
anasema, hivi ndivyo ilivyotokea pale mitume wake walipokuwa
wameelemewa na hofu pamoja na woga, akawatokea na kuwaambia wasiogope.
Hata kama waamini wanakosea, wasikate tamaa, bali watambue kwamba, Yesu
yuko pamoja nao. Wachunguze pale walipokosea, wajiwekee mikakati ya
kusahihisha na kurekebisha pamoja na kujipa moyo wa kusonga mbele kwa
imani na matumaini zaidi. Waamini kamwe wasitafute njia ya mkato katika
maisha!