Yesu Kristo (kutoka Kigiriki Ιησους Χριστός (Iesus Christos) ni jina la kawaida kati ya Wakristo kumuitia Yesu wa Nazareti (Yesu Mnazareti).
Kwa asili ni tamko la imani lenye sehemu mbili: jina "Yesu" na cheo "Kristo".
Kristo ni tafsiri ya Kigiriki ya neno la Kiebrania- "mashiah" (Masiya).
Katika lugha ya Kigiriki "Yesu Kristo" mara nying`i ni sentensi kamili, maana yake "Yesu ndiye Masiya wa Mungu", yaani Yesu ndiye Masiya aliyetangazwa na manabii wa Agano la Kale na kutazamiwa na Israeli.
Katika aya nyingine za Agano Jipya "Yesu Kristo" tayari imetumika kama jina. (linganisha: rais Mkapa, au: Mkapa rais - si yule Mkapa mwingine...)
Yesu alikuwa Myahudi mwanamume aliyeishi miaka 2000 hivi iliyopita (labda 6 KK - 30 B.K.). Kutokana na umuhimu wake katika historia ya binadamu, kwa kawaida miaka yote inahesabiwa kwanzia ujio wake (ulivyokadiriwa kimakosa katika karne ya 6).
Mazingira yake
Nchi ambayo Yesu alizaliwa akafundisha ni nchi ileile ambayo Mungu aliwaahidia Waisraeli tangu zamani za Abrahamu, ni nchi ileile waliyoiteka chini ya Yoshua, ni nchi ileile waliyoirudia kutoka utumwani Babeli.
Lakini wakati wote wa Agano Jipya, yaani tangu Yesu alipozaliwa hadi mwisho wa maisha ya mitume wake, nchi hiyo haikuwa huru, bali chini ya himaya ya Warumi, ingawa pengine hao waliwakabidhi vibaraka, yaani watawala wenyeji waliowekwa na wakoloni.
Vibaraka hao ni Herode Mkuu (37 KK-4 KK) na wazawa wake, ambao tena hawakuwa Waisraeli halisi bali Waedomu ingawa kabila lao lililazimishwa kuingia dini ya Kiyahudi karne iliyotangulia. Ukoo huo unajulikana kwa ukatili, uchu wa madaraka na uzinifu wake.
Vilevile maliwali wa Kirumi waliowekwa pengine kutawala nchi au
sehemu fulani walionyesha mara nyingi ukatili na dharau kwa Waisraeli na
dini yao, hata kusababisha chuki na mapigano kati ya jeshi na wananchi.
Mfano mmojawapo ni Ponsyo Pilato aliyesimamia Uyahudi kuanzia mwaka 26 hadi 36 B.K.
Mbali na hayo, utawala wa Roma, ulioenea Ulaya Magharibi na Kusini, Afrika Kaskazini na nchi za Mashariki ya Kati kupakana na Iraq ya leo, kwa jumla ulihakikisha hali ya amani kwa muda wote wa Agano Jipya na karne za kwanza za Kanisa.
Hali hiyo, pamoja na umoja wa dola hilo lote, na urahisi wa mawasiliano
kwa njia ya barabara zilizotengenezwa na Warumi, na uenezi wa lugha ya
kimataifa (Kiyunani yaani Kigiriki cha zamani), ilichangia kasi ya uenezaji wa habari njema (Injili).
Lugha hiyo ndiyo iliyotumiwa na waandishi wote wa Agano Jipya ili
vitabu vyao viwafaidishe watu wengi zaidi, ingawa baadhi yao hawakuijua
vizuri.
Lugha asili ya Yesu na ya Mitume ilikuwa Kiaramu
ambacho ni jamii ya Kiyahudi na ambacho polepole kilishika nafasi yake
kati ya Wayahudi kuanzia karne ya sita K.K. Hao wote walitokea mkoa wa Galilaya,
uliokuwa na mchanganyiko wa watu (Waisraeli na mataifa), kiasi kwamba
huko Wayahudi wenyewe walifuata kwa urahisi desturi za Kiyunani hata
wakadharauliwa na wenzao wa Kusini (Yerusalemu na mkoa wa Yudea).
Kati ya mikoa hiyo miwili ulienea mkoa wa Samaria ambao wakazi wake walijenga uadui mkubwa na Wayahudi baada ya uhamisho wa Babeli, walipokataliwa kuchangia ujenzi wa hekalu la pili la Yerusalemu.
Maisha yake
Dionisi Mdogo, mmonaki aliyeanzisha (mwaka 533 hivi) mtindo wa kuhesabu miaka kuanzia kuzaliwa Yesu kurudi nyuma (K.K.) au kwenda mbele (B.K.), alikosea hesabu zake. Leo tunakisia Yesu alizaliwa mwaka 6 hivi K.K. kwa sababu alizaliwa Bethlehemu chini ya Herode Mkuu aliyefariki mwaka 4 K.K.
Huyo alipojaribu kumuua mtoto Yesu, familia takatifu ilikimbilia Misri mpaka baada ya kufa kwake. Hapo ikarudi Galilaya hata Yesu akajulikana kwa jina la kijiji cha Nazareti kilichodharauliwa na Wagalilaya pia. Ndipo alipokulia na kuishi akifanya kazi ya ufundi.
Mwaka 26 hivi B.K. ndugu yake Yohane Mbatizaji aliacha maisha ya jangwani na kuanza kuhubiri toba kandokando ya mto Yordani. Kwa kuwa Waisraeli walikosa manabii kwa muda mrefu, na walitamani sana ukombozi, walimuendea kwa wingi hata wakamtia hofu Herode Antipa.
Ingawa huyo akamfunga mapema akamuua, kazi ya Yohane ilikuwa imetimia
kwa sababu aliweza kuwaandaa Waisraeli wengi (hasa watu wadogo na
wakosefu) wampokee Yesu aliyebatizwa naye. Katika nafasi hiyo Yohane
alimtambulisha kama Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu.
Ndipo Yesu naye alipoanza kuhubiri, lakini pia kutenda miujiza ya kila aina, akapata haraka wafuasi wengi. Kati yao akachagua Mitume wake 12 kama msingi mpya wa taifa la Mungu. Alifanya kazi hizo kuanzia Galilaya, akitangaza ujio wa ufalme wa Mungu, kwa maana ya kwamba ufalme uliotazamiwa na Wayahudi umewajia kwa njia yake.
Ingawa hakupitia shule yoyote ya Biblia, Yesu alionekana anafundisha vizuri kuliko walimu wa sheria wa kawaida, kama mtu mwenye mamlaka juu ya Torati. Mafundisho yake yalilingana na yale ya Mafarisayo kuliko na yale ya Masadukayo, lakini alishindana pia na hao wa kwanza.
Kijicho na upinzani vikazidi hasa Yerusalemu, walipoanza kufanya
njama za kumuua. Ingawa Yesu alijua hayo, alijikaza kwenda katika mji
mtakatifu autangazie habari njema na kufia huko. Baada ya kupokewa kwa
shangwe kabla ya sherehe ya Pasaka ya mwaka 30 (au 33) akakamatwa na baraza la Israeli
kwa tuhuma ya kufuru ya kujilinganisha na Mungu, halafu akakabidhiwa
kwa liwali wa Kirumi aliyekuwa na mamlaka ya kutoa adhabu ya kifo. Baada
ya kikao ambapo Wayahudi walitafuta kisingizio cha kisiasa, Ponsyo
Pilato akalazimika kuagiza Yesu asulubiwe, na kisha kufa kwake kaburi
lilindwe na askari.
Hata hivyo siku ya tatu kaburi likaonekana tupu, na Yesu akaanza
kuwatokea wanafunzi wake wa kike na wa kiume kwa muda wa siku arubaini,
halafu akapaa mbinguni mbele ya macho yao.
Habari hizo zikatangazwa kwa sauti tu kwa miaka kadhaa, halafu
zikaanza kuandikwa. Kanisa linaheshimu kwa namna ya pekee, kama ushuhuda
mkuu juu ya maisha na mafundisho ya Yesu na kama moyo wa Maandiko
matakatifu yote, Injili nne zilizoandikwa na Marko, Mathayo, Mwinjili Luka na Yohane kati ya mwaka 65 na 100 hivi.
>>>>>>>>>>>>>>>>>>inaendelea>>>>>>>>>>>>>>>>>>