Bibilia na Kipindi cha Kwaresima
Katika Agano la Kale Musa ndiye aliyeongoza Waisraeli.
Sisi tunakumbuka na kufuata safari yao ya ukombozi, walipokaa jangwani
miaka 40 ili kuelimishwa kinaganaga juu ya yale yatokanayo na maneno 10 ambayo Musa alipewa na Mungu alipofunga siku 40 juu ya mlima Sinai.
Hayo yalikamilishwa na Yesu katika Agano Jipya kama kiongozi na mkombozi wa wote. Kabla hajaanza utume wake, yeye pia alifunga siku 40 jangwani akijilisha matakwa ya Baba ili ayatekeleze na kuwatangazia watu wote.
Juhudi za Kwaresima
Kufuatana na hayo yote Kanisa linafunga siku 40 katika jangwa
la kiroho. Wakati wa Kwaresima linawaongoza waamini katika safari ya
kujirekebisha kulingana na Neno la Mungu la Agano la Kale na la Agano
Jipya. Wote wanahimizwa kufunga safari hiyo kadiri ya hali yao: kwanza
wale wanaojiandaa kubatizwa usiku wa Pasaka (hasa kwa kufanyiwa mazinguo
matatu yanayofuatana katika Dominika III, IV na V), lakini pia
waliokwishabatizwa, ambao kabla ya hapo wanatakiwa kutubu na kuungama
dhambi ili warudie kwa unyofu ahadi za ubatizo.
Makundi yote mawili watakula pamoja Mwanakondoo ili kuishi upya kwa
upendo, jambo litakalofanya hata wasio Wakristo wafurahie Pasaka.
Kazi za urekebisho zinahitaji juhudi za pekee. Vivyo hivyo kwa
ukombozi wa kiroho Kwaresima inadai bidii nyingi pande mbalimbali:
katika kufunga, kutoa sadaka, kusali na kusikiliza Neno la Mungu hasa wakati wa ibada. Hayo yote yanahusiana na kusaidiana.
Mkristo akijinyima chakula cha mwili anajifunza kufurahia zaidi mkate wa Neno la Mungu na wa ekaristi, tena anatambua zaidi anavyopaswa kuwahurumia wenye njaa na shida mbalimbali. Toba inahimizwa isiwe ya ndani na ya binafsi tu, bali pia ya nje na ya kijamii: itokane na upendo na kulenga upendo kwa kurekebisha kasoro upande wa Mungu (sala), wa jirani (sadaka) na wa nafsi yetu (mfungo).
Mfungo, yaani kujinyima tunavyovipenda na hata tunavyovihitaji, uwe
ishara ya njaa yetu ya Neno la Mungu, ya nia yetu ya kushiriki mateso ya Yesu yanayoendelea katika maskini,
ya kulipa kwa dhambi zetu na kuachana nazo. Sadaka inayotokana na sisi
kujinyima inampendeza Mungu kuliko ile isiyotuumiza; msaada unaweza
kutolewa pia kwa kutetea haki za binadamu dhidi ya wanyanyasaji. Sala inastawi kwa kusikiliza sana Neno la Mungu hasa kwa pamoja (katika familia, jumuia, liturujia
n.k.). Ndiyo maana wakati wa Kwaresima Kanisa linazidisha nafasi za
kulitangaza na hivyo kuelimisha wote kuhusu mambo makuu ya imani na maadili yetu.
Kwaresima katika liturujia.
Kuna mpangilio kabambe wa masomo ya Misa, hasa ya Dominika, ili wote wafuate hatua kuu za historia ya wokovu (somo la kwanza) na kuchimba ukweli wa ubatizo (mwaka A), agano na fumbo la Kristo (mwaka B) na upatanisho
(mwaka C). Kwa njia hiyo tunatangaziwa jinsi Mungu anavyotuokoa; pia
upande wetu kuanzia Dominika ya kwanza tunajielewa kuwa watu
vishawishini ambao tunapaswa kushinda kwa kumfuata Yesu, si Adamu: kwenda jangwani ili kumtafuta Bwana na matakwa yake.
Kilele cha safari ya Kwaresima ni Dominika ya Matawi, tunapoingia Yerusalemu pamoja na Yesu anayekwenda kufa na kufufuka kwa ajili yetu. Liturujia ya
siku hiyo ina mambo mawili: kwanza shangwe (katika maandamano), halafu
huzuni (kuanzia masomo, ambayo kilele chake ni Injili ya Mateso).
Baada ya Kwaresima kwisha, tutapitia tena historia ya wokovu katika kesha la Pasaka ambapo hatua zote zinaangazwa na ushindi wa Kristo mfufuka.