Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuhitimisha Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye ufuko wa Copacabana, Rio de Janeiro, Brazil, tukio ambalo limehudhuriwa na watu millioni tatu, amewashukuru na kuwaaga wananchi wa Brazil na kwa namna ya pekee, Rais Dilma Vana Rousseff kwa niaba ya wananchi wa Brazil kwa matendo makubwa waliyomfanyia Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, anarejea mjini Vatican akiwa amesheheni matukio ya furaha ambayo kwa sasa yanageuka kuwa ni sala. Anasikia ile hamu ya kuendelea kukaa na wananchi wa Brazil, waliomwonesha moyo wa ukarimu na urafiki. Anawashukuru kwa tabasamu la nguvu na la kweli walilommegea wakati wote alipokuwa anakutana nao bila kusahau sadaka na majitoleo ya vijana wengi walioacha shughuli zao ili kuweza kuwakirimia upendo na huduma, ndugu zao katika Kristo.
Anawakumbuka vijana aliokutana nao kwenye Hospitali ya Mtakatifu Francisko inayowahudumia waathirika wa dawa za kulevya, bila kusahau upendo wa wananchi wa kitongoji cha Varginha. Baba Mtakatifu anasema, kwa hakika anaona mkono wa Yesu ukitenda kazi miongoni mwa vijana na kwa umati mkubwa wa watu aliokutana nao katika kipindi cha juma zima, muda ambao kamwe hataweza kusahau katika maisha na utume wake!
Baba Mtakatifu anaendelea kuwashukuru kwa namna ya pekee vijana waliokuwa ni kiini cha Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Wengi wao walikuja kama wafuasi wa Kristo, sasa wanarudi makwao wakiwa wamefundwa na kuiva kama Wamissionari. Ni vijana ambao wako tayari kutolea ushuhuda wa maisha yao kwa njia ya furaha, huduma, daima wakijitahidi kujenga utamaduni wa upendo. Ni vyema vijana wakasimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu sanjari na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Injili ya Kristo.
Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Yesu ndiye aliyekuwa wa kwanza kuanza mchakato wa kuwatafuta, anapenda kuwasha moto wa Injili ili waweze kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Baba Mtakatifu anasema, yeye binafasi amekwisha onja baadhi ya matunda ya kazi hii, wengine wataendelea kufurahia katika utimilifu wake.
Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru Bikira Maria wa Aparecida. Anasema, kwenye madhabahu ya Bikira Maria wa Aparecida, amepiga magoti kwa ibada kwa ajili ya kuombea dunia, lakini kwa namna ya pekee wananchi wa Brazil. Anasema, amemwomba Bikira Maria ili aweze kuimarisha imani ya Kikristo nchini Brazil kama ilivyo hata kwa nchi nyingine duniani; imani ambayo ni amana kubwa kwa utamaduni wa wananchi wa Brazil.
Ni mwaliko anasema Baba Mtakatifu wa kuendelea kujenga na kudumisha amani na mshikamano kati ya watu. Mwishoni kabisa, Baba Mtakatifu anaendelea kuwaomba wananchi wa Brazil na wote wenye mapenzi mema kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya Sala, kwani anauhitaji mkubwa wa sala!