Monday, October 28, 2013

Sala ya Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Familia



Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa ajili ya Familia limekuwa ni tukio la imani kwani kabla ya Misa Takatifu, waamini wengi walipata nafasi ya kuungama ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa kutambua umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho.

Mara baada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 27 Oktoba, 2013, Baba Mtakatifu Francisko amesali mbele ye Sanamu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, akiiendea kwa imani thabiti ili kutafakari umoja na upendo wa dhati, ili hatimaye, aweze kuzikabidhi Familia zote za Kikrito ambazo zinapaswa kuonja neema.

Familia Takatifu ni shule makini ya Neno la Mungu, Fadhila, hekima na nidhamu ya maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anaomba ili waamini waweze kuwa na jicho la kuona kazi ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Familia Takatifu ni hifadhi aminifu ya Fumbo la Ukombozi.

Baba Mtakatifu anaomba fadhila ya ukimya, moyo wa sala katika familia ili ziweze kuwa kweli ni Kanisa dogo la nyumbani; daima wanafamilia watamani utakatifu pamoja na kuwasaidia kukabiliana na changamoto za maisha, kwa kusikilizana, kuelewana na kusameheana.

Familia Takatifu iwasaidie walimwengu kutambua na kuthamini utakatifu wa maisha na kwamba, Familia ni hazina ambayo haina mbadala. Kila familia ijitahidi kupokea na kuenzi amani kwa ajili ya watoto na wazee; wagonjwa na wapweke; maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii.

Wednesday, October 23, 2013

Washeni moto wa imani duniani!



Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 20 Oktoba 2013 amewataka waamini na watu wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa kusali bila kuchoka; kwa kupaaza sauti kwa Mwenyezi Mungu, usiku na mchana kwani hiki ni kielelezo cha imani makini kwa Mwenyezi Mungu ambaye daima anasikiliza kwa makini na upendo mkuu na anayafahamu mahitaji ya waja wake.

Baba Mtakatifu amewahakikishia waamini waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwamba, Yesu anaendelea kufanya hija na wafuasi wake na wala hayuko mbali nao katika mapambano dhidi ya dhambi na kwamba, sala ni silaha muhimu inayomfanya mwaminifu kutambua na kuonja uwepo endelevu wa Kristo katika hija ya maisha yake hapa duniani.

Yesu anawakirimia wafuasi wake huruma na msaada wanaohitaji, kwa kutambua kwamba, mapambano dhidi ya dhambi si jambo la lelemama, bali linahitaji uvumilivu na udumifu katika sala kama alivyofanya Musa katika somo la kwanza, Jumapili ya ishirini na tisa ya kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Mwenyezi Mungu ni mwenza na nguvu katika mapambano haya na kwamba, sala ni kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kama waamini watauzima moto wa imani, kwa hakika watatembea katika giza totoro, kiasi kwamba, watapoteza dira na mwelekeo wa maisha.

Baba Mtakatifu amewapongeza wanawake wanaosimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani kwa ajili ya familia zao bila kuchoka wala kukata tamaa. Hiki ni kielelezo cha imani thabiti, ujasiri na mfano wa kuigwa katika maisha ya sala, changamoto ya kuendelea kusali daima kama ushuhuda wa imani tendaji kwa Mwenyezi Mungu anayewapenda waja wake pamoja na kuwahamasisha kushikamana naye katika mapambano dhidi ya dhambi, ili kuweza kuyashinda malimwengu kwa njia ya wema.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa Jumapili iliyopita ameadhimisha Siku ya 87 ya Kimissionari Duniani. Utume wa Kanisa ni kuhakikisha kwamba, linawasha moto wa imani uliowashwa kwa mara ya kwanza na Yesu mwenyewe duniani. Ni moto wa imani kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo. Huu ni moto ambao waamini wanapaswa kuwagawia wengine ili mioyo iweze kupata joto la ujumbe wa Mungu.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wale wote wanaoshiriki kwa hali na mali katika kutegemeza shughuli za kimissionari sehemu mbali mbali duniani, lakini kwa namna ya pekee, wale wanaomsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kueneza Injili sehemu mbali mbali za dunia. Mama Kanisa yuko karibu na wamissionari walioenea sehemu mbali mbali za dunia, wanatekeleza dhamana na wajibu wao katika hali ya ukimya pasi na makeke! Ni watu wanaojitosa kimasomaso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amemkumbuka Afra Martineli, mmissionari aliyefanya kazi za kitume nchini Nigeria kwa miaka mingi, akapendwa na wengi; lakini hivi karibuni aliuwawa kikatili nchini Nigeria. Watu wengi wamelia na kuomboleza kifo cha Afra Martineli. Hii ni kwa sababu alitangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa matendo yake, kwa kuanzisha shule, mahali ambapo aliwasha moto wa imani na kwamba, amevipiga vita vilivyo vizuri na sasa mwendo ameumaliza.

Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Mwenyeheri Stefano Sàndor aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri jumamosi iliyopita, huko Budapest kutokana na mchango wake mkubwa kwa majiundo ya vijana kiroho na kimwili.Mwenyeheri Sàndor alikabiliana uso kwa uso na utawala wa Kinazi, wakati ulipoanza madhulumu dhidi ya Kanisa. Akauwawa kikatiliki akiwa na umri wa miaka 39. Mama Kanisa anaishukuru Familia ya Wasaelisiani na Kanisa Katoliki nchini Hungaria.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka na kuonesha uwepo wa karibu kwa wananchi wa Ufilippini waliokumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha maafa makubwa kwa maisha na mali ya watu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea wananchi hao wakati huu mgumu katika historia ya maisha yao.

Baba Mtakatifu, mwishoni amewashukuru wadau mbali mbali walioshiriki katika "Mbio za Imani" kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, jumapili iliyopita; mbio za Marathoni zilizoandaliwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni na wadau mbali mbali kutoka Italia. Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, mwamini ni mwanariadha wa maisha ya kiroho.

Tuesday, October 22, 2013

MASOMO YA DOMINIKA YA 30 YA MWAKA C TAREHE 27/10/2013

JUMAPILI DOMINIKA YA 30 ya Mwaka C.
      RATIBA ZA IBADA 
KIGANGO CHA MH. ISIDORI BAKANJA- BOKO.
MISA YA KWANZA 12:15-2:00 ASUBUHI
MISA YA PILI     SAA 2:00-4:00 ASUBUHI
MISA YA TATU SAA 4:00-5:30 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. FRANCIS WA ASIZ-MBWENI 
MISA YA KWANZA SAA 1:10-3:00 ASUBUHI
MISA YA PILI SAA 3:00-4:30 ASUBUHI

KIGANGO CHA MT. RAFAEL-MBWENI MALINDI
SAA 1:00-3:00 ASUBUHI.
MISA YA PILI SAA 3:00-5:00

KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA-MBWENI TETA
MISA NI SAA 3:00-5:00.


MASOMO 

 Somo 1:Ybs.35:12-14, 16- 17
Kwa kuwa Bwana ndiye mhukumu wala hakijali cheo cha mtu. Hatamkubali ye yote juu ya maskini, naye ataisikiliza sala yake aliyedhulumiwa. Hatayadharau kamwe malalamiko ya yatima, wala ya mjane amwelezapo habari zake. malalamiko yake aliyeonewa yatapata kukubaliwa, na dua yake itafika hima mbinguni. Sala yake mnyenyekevu hupenya mawingu; wala haitatulia hata itakapowasili; wala haitaondoka hata Aliye juu  itakapoiangalia, akaamua kwa adili, akatekeleza hukumu. Wala Bwana hatalegea, wala hatakuwa mvumilivu kwa mwanadamu.

SOMO 2: 2Tim.4:6- 8, 16- 18
Mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda: baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambalo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake. katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewe katika kinywa cha simba. Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye na milele. Amina.

INJILI. :Lk.18:9-14
Yesu aliwaambia mfano huu watu wanaojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake.; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyanganyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakudhubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifuani akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.
             
  1.  Jumapili ya tarehe 03/11/13 tutakuwa na kikao cha halmashauri ya VIWAWA Parokia, kikao kitaanza saa tatu asubuhi mahali tutapeana taarifa.


  1. tunawakumbusha vijana wote kuendelea kulipa ada kwa maendeleo ya chama chetu..... mapendo sana malipo kwa njia ya benk kwa jina na number hii :viwawa parokia ya boko account no 01524526820100 crdb bank tegeta branch
JIANDAE NA ZIARA YA UINJILISHAJI MWAKA 2014.....................

Monday, October 21, 2013

Mwaka Mmoja Baada ya kifo cha Padre Massawe: aliyependa Vijana na Mwanahabari



NILIPOKEA taarifa za masikitiko na zenye mshtuko mkubwa kwa njia ya simu  kupitia kwa Paroko wa wanga PD. Dismas Mfungomali wa simu ya mkononi usiku wa manane kuamkia Oktoba 26, 2012 kuwa  aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Kimisionari la Kanisa Katoliki  la Consolata, Padri Salutarius Lelo Massawe (50) amezama baharini wakati akiogelea Bagamoyo na mwili wake haujaonekana.
Ilikuwa kama ni  ndoto, wakati Jumapili iliyopita tulikuwa naye tukijiandaa na mkesha wa kimisionari kwa vijana wote wa jimbi la Dar es salaam,   ambapo nililazimika kumpigia Mwenyekiti wa Mabalozi wa Vijana wa Consolata (CMC) Ndugu Machota , na kumuuliza, na yeye amepata habari jana.
  Padri Massawe alifariki mjini Bagamoyo wakati akiogelea katika  Bahari ya Hindi na wakuu wenzake wa Shirika la Consolata kutoka nchi  mbalimbali waliokuwa na mkutano  katika Kituo cha Kiroho cha Consolata kilichoko Bunju jijini Dar es Salaam. Baada ya mkutano aliwaeleza wenzake kuwa angependa wakapumzike Bagamoyo kwa kutembelea maeneo ya kimisionari sehemu ambapo Injili iliingia miaka ya 1800.
Walipofika Bagamoyo, walimaliza kutembelea makaburi, kanisa, na sehemu nyingine muhimu za kihistoria na kuamua kuanza kuogelea. Kwa mujibu wa padri aliyekuwa naye ni kwamba majira ya saa 10 jioni,  waliamua kuondoka kwenye maji lakini Padri Massawe alitokomea kimya kimya ndani ya maji na hakuonekana hadi  kesho yake asubuhi alipokutwa pembezoni mwa  bahari kwenye mikoko.
Kutokana na kutokuwa mbinafsi,  alionesha dhahiri moyo wa uzalendo kwa taifa lake.  Kila mara alikuwa akiniambia ninatamani sana Watanzania wawe matajiri wote, nisione masikini wakitaabika hasa kulala njaa. Ni vigumu  kutamka au kuandika sifa  zake  zote, Padri Massawe licha  ya kuwa alikuwa Mkuu wa Shirika la Kimisionari la Consolata hapa Tanzania wadhifa aliokabidhiwa mwaka jana, pia alikuwa mwanahabari makini, aliyefanya kazi  kwa kuzingatia misingi na weledi, huku akiamini kuwa habari njema siku zote humjenga binadamu kiafya na kiroho.
Alijitahidi kutumia jarida la  kimisonari  Enendeni linalotolewa mara nne  kwa mwaka  na shirika lake, yeye kama mhariri mkuu kuinjilisha, alitumia vyombo vya habari vya Tumaini Media, radio, TV na gazeti la Tumaini Letu kufundisha na kuwatia Wakristo moyo.
Padri Salus Lelo (kama tulivyozoea kumwita) ameishi Iringa ambako ndiko yaliko Makao Makuu ya wamisionari wa Consolata kwa kipindi cha takriban mwaka mmoja, hadi anafariki dunia lakini wananchi wa Iringa walionekana wenye majonzi mazito kuliko ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa naye siku zote sehemu nyingine. Hii inaonesha upendo wa dhati ambao aliwaonesha kwa muda mfupi.
Tunajiuliza ni nani kati yetu anayeweza kurithi tunu na  vipaji alivyokuwa navyo Padri Salus Massawe? Je, mioyo yetu inatamani kupata neema kama ya kwake? Tulipofika Iringa eneo la Kanisa Kuu la Jimbo (cathedral)  parokia ya Bikira Maria Consolata alfajiri  31, Oktoba 2012,  ilikuwa ni simanzi, vilio vilivyorindima na kuwafanya umati wa ndugu tuliosindikiza msiba kutoka Dar es Salaam na Moshi kuanza kulia tena.
Waumini walikuwa wamekesha kanisani hapo kwa siku mbili, walipouona mwili wa kipenzi chao waliangua kilio kikubwa. Vilio hivi, vilifuatiwa na mazishi yaliyofanyika katika Parokia ya Tosamaganga,  umati mkubwa ulishiriki, wananchi wa Iringa walitamka wenyewe kuwa tumempoteza kiongozi wa kabila letu, ‘Mtwa’ kwa Kihehe wakimaanisha chifu.
waamini , waliamua kumuwekea historia ya pekee kwa kumzika  kwa heshima za kichifu wa kabila la Wahehe kwa kupigiwa  mizinga  20 angani. Tulijiuliza hivi na mapadri wanapigiwa mizinga kama wanajeshi? Lakini hayo hata yeye hakujua kama yatatokea akifariki. Kifo cha Padri Massawe  kinaweza kujengwa taswira nyingi miongoni mwa jamii.  Ni kwanini yeye? Na ni kwanini pale Bagamoyo? Lakini  yote tumuachie Mwenyezi Mungu.
Waliosoma naye SAUT  wanasikitika hasa wanapokumbuka, uhamasishaji usio na kikomo wa Padri Massawe kwenye michezo, shughuli za kijamii, burudani, vikao, kuanzishwa kwa asasi ya kutetea uhai wa binadamu (Pro-Life) ambayo alikuwa mwasisi na mwenyekiti wa kwanza. Mashindano ya mpira wa miguu maarufu SAUT kama FAWASCO, alihakikisha darasa lake la ‘Mass Comm (2005-08)’ linachukua kombe na likafanya hivyo.
Jumapili jioni alikutana na kikundi cha  wazaliwa wa Kibosho ‘Konkya’ waliokuwa wakiishi Mwanza na mikutano ilikuwa ikifanyika pale Kilimanjaro Hotel Mabatini, tukiwa naye. Wakati wa Misa Baba Askofu  wa Jimbo la Iringa, Taracius Ngalalekumtwa,  alieleza jinsi ambavyo Padri Massawe amefanikiwa kujenga mahusiano mazuri na jamii nje na ndani kila mara akionesha uso wa matumaini na mapendo.
Pamoja na upadri wake,  kupangiwa kazi za ofisini,  hata wakati wa masomo alikuwa padri anayejitahidi kukutana na makundi ya watu wote, wenye mali, wasio na mali, wenye elimu na wasio na elimu, alikuwa padri anayetambua utu wa kila mtu, kuhakikisha kila mwanadamu anayekutana naye anakuwa na amani na furaha moyoni.  Mara kadhaa nilimpelekea watu walio kata tamaa na  wenye changamoto mbalimbali za kimaisha, lakini walirudi na hali mpya, wamebadilika.
Huyo hakuwa padri anayegawa fedha, mali ila alikuwa akigawa upendo wa dhati, furaha, amani na matumaini. Ndiyo maana askofu anasema: ‘ Padri Massawe alikuwa zaidi ya padre kwani alitumikia nafasi yake kama mkuu wa shirika, mwalimu, padri, daktari na kiongozi wa kijamii  huku akijitahidi kujenga mahusiano na kila anayepishana naye.
‘Usihesabu umri wako kwa miaka uliyonayo, hesabu umri wako kwa kuangalia watu ambao umehusiana nao vizuri. Padri Massawe alijitahidi kuhusiana  vizuri na kila aliyepishana naye bila kujali dini, imani au kabila lake,’ anasema  Baba Askofu.
Katika mkutano uliofanyika Bunju, ambao marehemu alikuwa mwenyeji,  ulihudhuriwa pia na padri Mtanzania ambaye ni Makamu Mkuu wa Shirika la wamisionari Wakonsolata duniani,  kutoka Roma,  Padri Detrick Mpandawazima,  ambaye walikuwa wote baharini na alishuhudia akifariki, alimtaja marehemu Padri Massawe kama kiongozi mwenye kipaji kikubwa ambaye bado alihitajika kulitumikia shirika hilo na taifa la Tanzania.
Tutamkumbuka kwa kujitahidi kuomba neema ya Mungu ili tuishi maisha mazuri ya kumtumikia Mungu. Kuishi maisha ya kujitoa kwa ajili ya wengine na kusambaza upendo wa Mungu. 
sasa ni mwaka mmoja toka ututoke tunazidi kukumbuka kwa mengi ulifanya kwetu, Tunamuombea Mwenyezi Mungu aipokee Roho yake na ampumzishe kwa amani. Amina!

Thursday, October 17, 2013

Katekesi ya Papa- Tunasadiki katika Kanisa moja la Kitume kwa sababu.....



Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kwa mahujaji na wageni, inaendelea kuitafakari sala ya Kanisa, ya Nasadiki, Jumatano hii akitazama kifungu Nasadiki katika Kanisa moja Takatifu na la Kitume. Na alianza kwa kuwahoji mahuajii na wageni wanaofika Roma kwa ajili ya hija , iwapo wamewahi kujiuliza ina maana gani kusema , Kanisa la Mitume na umuhimu wa Mitume Petro an Paulo, ambao waliyatoa maisha yao hapa Roma , kwa ajili ya kuifikisha Injili na kuishuhudia Injili . Lakini pia akasema, kuna zaidi katika hilo....

Papa alieleza na kusisitiza kwamba Kanisa la kitume, kwa sababu, lina uhusiano kina, katika urithi wake na Mitume kwa kwanza, lile kundi dogo la wanaume kumi na wawili walioitwa na Yesu kwa majina na kuishi nae na hatimae kuwatuma nje kuhubiri mafundisho yake ( Mk 3:13-19 ).

Papa alieleza na kufafanua maana ya neno “Apostolo” Mtume , kwamba ni neno la Kigiriki lenye maana ya "aliyetumwa ", ni mtu anayepeleka ujumbe wa kufanya jambo fulani. Ni neno lenye nguvu , na Mitume waliitwa na kuchaguliwa na Yesu kuendeleza kazi yake , ya kusali na kupeleka habari njema ya upendo wa kuokoa kwa watu wote. Hivyo sala na kutangaza Injili , inakuwa ni kazi ya kwanza muhimu ya mtume.. Papa ametaja hili ni muhimu kwa sababu, mara nyingi , wengi tunafikiri, kuwa mtume ni kwenda kuihbiri injili peke yake. Sivyo, ni kufanya kazi nyingi ...
Papa alifafanua, na kurejea siku za mwanzo wa Kanisa, akisema, pia kulikuwa na matatizo na vikwazo kwa mitume kulingana na wakati wao. Na hivyo walitayarisha watu wengine kama mashemasi, katika kukabilaina na kupungukiwa na wakati wa kuomba na kutangaza Neno la Mungu. Na kama tunavyo fikiri juu waandamizi wa Mitume - Maaskofu, na pia Papa,ambao nao pia wana tatizohili la kupungukiwa na muda wa kusali na kuitangaza Injili kama warithi wa mitume. kwa muono huo, Papa Francisko amesisitiza, kila muumini wa kanisa ni mtume, kwa sababu yumo ndani ya Kanisa la kitume. Na hivyo waamini wote wanatakiwa kuwa mitume katika kazi yake ya kuihubiri Injili ya wokovu wa ulimwengu.
Papa alieleza na kutaja mambo matatu katiak mafundisho yake kwamba, Kanisa ni la kitume kwa sababu, limejengwa juu ya maombi na mahubiri ya Mitume, kwa mamlaka yalitolewa kwa mitume na Kristo mwenyewe,kama alivyoandika Mtakatifu Paulo kwa Wakristo wa Efeso (2, 19-20) .
Pili Kanisa ni la kitume kwa sababu hudumisha ukamilifu wa mafundisho ya Kristu na njia za wokovu, kwa msaada wa Roho Mtakatifu , kama inavyo eleza Kateksimu ya Kanisa. Kanisa karne hadi karne limetunza hazina hii ya thamani, ambayo ni maandiko matakatifu , mafundisho , sakramenti, huduma ya wachungaji, ili twaamini waweze kuwa waaminifu kwa Kristo na kuyashiriki maisha yake.
Na tatu Kanisa ni la kitume kwa sababu, ujumbe wake uliodmanishwa kwa mitume ni ujumbe wa injili kwa dunia nzima, unaoendelea katika njia ya historia ya ujumbe huo, ambao Yesu aliukabidhi Mitume. Yesu mwenyewe alisema, nendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi . Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote , mpaka mwisho wa ulimwengu "( Mt 28:19-20). Na hivyo Kanisa mizizi yake imo katika mafundisho ya Mitume, mashahidi wa kweli wa Kristo. Hivyo , leo tunapaswa kufurahia na kulipenda kanisa kama ni mahali pa kukutana na Bwana Mfufuka , aliyewatuma mitume wake , kuwaalika wote waliokutana nao kuufahamu ukweli wa Injili , furaha ya imani na ahadi ya maisha ya Milele, iliyotangazwa na Mitume. 

JUMAPILI DOMINIKA YA 29 ya Mwaka C. Tarehe 20/10/2013

JUMAPILI DOMINIKA YA 29 ya Mwaka C.
      RATIBA ZA IBADA 
KIGANGO CHA MH. ISIDORI BAKANJA- BOKO.
MISA YA KWANZA 12:15-2:00 ASUBUHI
MISA YA PILI     SAA 2:00-4:00 ASUBUHI
MISA YA TATU SAA 4:00-5:30 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. FRANCIS WA ASIZ-MBWENI 
MISA YA KWANZA SAA 1:10-3:00 ASUBUHI
MISA YA PILI SAA 3:00-4:30 ASUBUHI

KIGANGO CHA MT. RAFAEL-MBWENI MALINDI
SAA 1:00-3:00 ASUBUHI.
MISA YA PILI SAA 3:00-5:00

KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA-MBWENI TETA
MISA NI SAA 3:00-5:00.


MASOMO 

 Somo 1:Kut.17:8-13
Wakati huo Waameleki walitokea, wakapigana na Israel huko Refidimu. Musa akamwambia Yoshua, Tuchagulie watu, ukatoke upigane na waameleki; kesho nitasimama juu ya kilele kile, na ile fimbo ya Mungu nitakuwa nayo mkononi mwangu. Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima. Ikiwa Musa alipoinua mkono wake, Israel walishinda; na aliposhusha mkono wake, Amaleki walishinda. lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; bali wakatwa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa. Yoshua akamwaangamizaAmaleki na watu wake kwa ukali wa upanga.

SOMO 2: 2Tim.3:14 - 4:2
Wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa Imani iliyo katika Kristo Yesu. kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema. nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayehukumu waliohai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake; lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho.

INJILI. :Lk.18:1-8
Yesu aliwaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote, wala msikate tamaa. Akasema, palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea endea , akisema, nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikata tamaa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema, sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?
             
  1.  Maandalizi ya Dekania Cup yanaendelea kwa upande wa tImu ya Mpira wa  Pete jumamosi tarehe 19 wanacheza kutauta mshindi wa tatu dhidi ya bunju.


  1. tunawakumbusha vijana wote kuendelea kulipa ada kwa maendeleo ya chama chetu..... mapendo sana malipo kwa njia ya benk kwa jina na number hii :viwawa parokia ya boko account no 01524526820100 crdb bank tegeta branch
JIANDAE NA ZIARA YA UINJILISHAJI MWAKA 2014.....................

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR