Imani
, Imani, |
---|
|
Katika dini msingi wake ni mamlaka ya Mungu aliyeshirikishwa ukweli huo kwa njia ya ufunuo maalumu ili kumsaidia binadamu amjue yeye, ajifahamu pamoja na maisha yake duniani na ahera.
Kwa msingi huo, au wa namna hiyo, mtu anaweza kushikilia jambo bila ya uthibitisho mwingine, ingawa pengine Ukristo unatia maanani pia akili katika ujuzi wa ukweli.
Kadiri ya Mtume Paulo imani ikifuatana na tumaini na upendo ni adili kuu mojawapo, msingi, mzizi na chanzo cha wokovu.
Roho ya imani katika maisha ya kiroho
Kila mara mtu anafuata ama umbile, asipopita fikra za kibinadamu tu, ama imani, anapolenga mbinguni kwa njia ya utakatifu. Roho hizo zinazotuongoza maishani ni namna maalumu za kupima, kuona, kuhisi, kupenda, kushabikia, kutaka na kutenda. Basi, roho ya imani ni kupima yote kwa mtazamo wa juu ambao unapita maumbile na kutegemea mamlaka ya Mungu katika kujifunua, na ukweli wake katika kutushirikisha utukufu. Tunaelewa zaidi roho ya imani tukiangalia iliyo kinyume chake, yaani upofu wa roho unaozuia mtu asione mambo ya Mungu isipokuwa kidunia na kutoka nje. Hivyo Israeli haikuelewa uteuzi wake kadiri ya ukweli wa Mungu ulio wa juu kuliko ukabila au ubaguzi wowote.Imani ina mitazamo mipana kuliko huo kutokana na usahili wake unaoshiriki hekima ya Mungu. Juu sana kuliko mifuatano ya mawazo, ni tendo sahili ambalo tunamsadiki Mungu anayefunua na papo hapo anajifunua. Kwa tendo hilo lipitalo maumbile tunaambatana naye pasipo udanganyifu na hivyo katika giza tunalenga kutazama mambo ya Mungu, juu kuliko hakika zote za kibinadamu. Hakika inayotokana na imani tuliyomiminiwa na Mungu, inapita hata hakika ya akili tunayoweza kujipatia kwa kuzingatia miujiza inayothibitisha ufunuo wake.
Imani ni zawadi ya Mungu: “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu” (Ef 2:8). Ni kama hisi ya Kiroho inayotuwezesha kusikia ulinganifu wa mafumbo aliyotufumbulia, yaani kusikia sauti yake kabla hatujakaribishwa kumuona uso kwa uso.
“Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kujua tuliyokirimiwa na Mungu, nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi, mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu. Maana, ni nani aliyefahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo” (1Kor 2:12-16). Ili ifanye hivyo imani inasaidiwa na vipaji vya akili na hekima, lakini yenyewe ndiyo inayotufanya tushike Neno la Mungu pasipo udanganyifu.
Ingawa mafumbo yake ni ya giza kwetu, adili la imani ni bora kuliko ujuzi mwangavu walionao malaika kwa umbile lao, kwa sababu imani tunayomiminiwa inalingana na uzima wa milele, kwa kuwa ndiyo mbegu yake. Malaika wenyewe walihitaji zawadi hiyo waweze kulenga hali ipitayo maumbile waliyoitiwa.
Mungu anapotujalia imani, anapenya roho yetu na kusema nayo si kwa mifuatano ya maneno, bali kwa wazo la ghafla. Imani ikifika, tunaachana na mfuatano wowote wa mawazo tuliokuwanao pamoja na sababu zake: tunaviweka chini ili imani ivikalie kama mtawala. Imani ikiangaza akili kwa mng’ao wa kweli zake, mara utashi unahisi joto la upendo wa Mungu.
Imani tuliyomiminiwa inatakiwa kustawi hadi kifo
Imani inatakiwa kukua kila siku. “Imani inaweza ikawa kubwa ndani ya Mkristo mmoja kuliko ndani ya mwingine, upande wa akili kutokana na hakika na imara kubwa zaidi katika kushika ufunuo, na upande wa utashi kutokana na utayari na utiifu au tumaini kubwa zaidi” kwa kuwa “imani tunayomiminiwa inalingana na zawadi ya neema, ambayo si sawa kwa wote” (Thoma wa Akwino). Yesu Kristo aliwasema wanafunzi wake kuwa “wa imani haba” (Math 6:30); kumbe alimuambia mwanamke Mkananayo, “Mama, imani yako ni kubwa!” (Math 15:28).Imani inaweza kukua kwa upana na kwa dhati au nguvu. Inapanuka tunapozidi kujifunza yale yote Kanisa linayoyafundisha: wanateolojia wanayajua wazi, lakini si kwamba imani yao ni ya dhati na ya nguvu kadiri ilivyoenea. Kumbe tunakuta watakatifu wasiojua mengi katika hayo, lakini wanapenya mafumbo yalivyofumbuliwa na Injili kwa usahili. Mitume wa Yesu walimuomba imani hiyo waliposema, “Tuongezee imani” (Lk 17:5). Yesu akawaambia, “Yoyote mtakayoomba katika sala mkiamini, mtapokea” (Math 21:22). Tutayapokea hasa tukijiombea kwa udumifu yaliyo ya lazima au ya kufaa sana kwa wokovuwetu, kama vile ustawi wa maadili.
Ubora na uwezo wa imani
Thamani ya imani inapimwa na matatizo inayoyashinda katika majaribu: “Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu… yeye aliyeambiwa: Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu… Kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahad, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto… Wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizungukazunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za [mbuzi]], walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya – watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao” (Eb 11:17-19, 33-34, 36-38). Mambo kama hayo yanatokea hata siku hizi. “Basi na sisi pia, tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu” (Eb 12:1-2).“Mzingatieni Kristo aliyevumilia upinzani wa namna hiyo kutoka kwa wakosefu… Hapo katika tabu yoyote mtaona dawa katika msalaba wa Yesu. Humo mtakuta vielelezo vya maadili yote. Gregori Mkuu alisema tukiyakumbuka mateso ya Yesu hatutaona chochote kuwa kigumu au cha tabu tusiweze kukivumilia kwa subira na upendo” (Thoma wa Akwino). Imani ikistawi inatufanya kwa kawaida tuzidi kuhisi fumbo la Kristo; polepole hisi hiyo ipitayo maumbile inakuwa sala ya kumiminiwa yenye kupenya na kuonja, asili ya furaha na amani: “Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini… Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu” (Fil 4:4,7).
Tuishije kwa roho ya imani?
Tunapaswa kuishi hivyo kwa kupima yote kwa mwanga huo wa juu: kwanza Mungu, halafu nafsi yetu, jirani na matukio yote.Je, kuna haja ya kusema tumzingatie Mungu kwa imani? Bila ya shaka! Kwa kuwa mara nyingi tunamzingatia kwa dhana zisizo na msingi, kwa miguso ya kibinadamu mno na kwa maono yetu, badala ya kupitia ushuhuda alioutoa juu yake mwenyewe. Pengine hata tunaposali tunajisikiliza tu kwa kumkopesha Mungu mawazo yetu yanayotokana na umimi. Tunapojiamini kipumbavu tunaelekea kudhani huruma ya Mungu ni kwa ajili yetu, na haki yake kwa watu tusioelewana nao. Kumbe tukikata tamaa tunatilia shaka kimatendo upendo wa Mungu kwetu na huruma yake kuu. Kwa imani tunamuona Mungu kupitia mafumbo ya maisha na mateso ya Mwokozi na kupitia uhai wa Kanisa linalofanywa upya na ekaristi kila siku. Jicho la imani linasafika zaidi na zaidi kwa ufishaji wa hisi na maono, maoni na matakwa yetu: hapo tu unakuja kuanguka polepole ule utaj wa kiburi unaotuzuia tusione mambo ya Mungu au tuone tu vivuli vyake na tata zake.
Tunapaswa vilevile kujitazama kwa imani. Tukijitazama kibinadamu tu, tunaona ndani mwetu sifa za umbile ambazo mara nyingi tunazizidisha. Baadaye, majaribu yakituonyesha tulivyojidanganya tunavunjika moyo kwa urahisi. Kumbe kwa imani tunakuja kujua utajiri upitao maumbile ambao Bwana ametutia katika ubatizo na kutuongezea kwa ekaristi, yaani thamani ya neema inayotia utakatifu, ya uwemo wa Utatu mtakatifu pamoja na ukuu wa wito wa Kikristo. Tunakuja kujua pia vizuio vya ustawi wa uzima huo, k.mf. usahalifu wa mbegu ya uzima wa milele iliyopandwa ndani mwetu, na kiburi cha kipumbavu. Kwa mtazamo huo wa juu tunakuja kujua mapema kilema kinachotutawala na kivutio maalumu cha neema tulicho nacho, ambavyo cha kwanza kikomeshwe na cha pili kistawishwe.
Lakini tunayesahau zaidi kumtazama kwa imani ndiye jirani. Tunamtazama kibinadamu tu, tukiathiriwa na dhana zisizo na msingi, kiburi, wivu na vilema vingine. Kwa hiyo ndani yake tunakubali yale ambayo yanatupendeza kibinadamu, yanatufaidisha au kutukuza; kumbe tunahukumu yale ambayo yanatukinaisha, yanamfanya bora kuliko sisi na kutushusha. Dhambi ngapi za kuhukumu na kusingizia zinatokana na mtazamo huo uliofunikwa na utaji wa umimi! Tukijifunza kumtazama jirani kwa imani ni faida kubwa pande zote. Hapo tunakuja kuwaona wakubwa wetu kama wawakilishi wa Mungu, na kuwatii kwa moyo pasipo kuwasema. Tunaona kuwa wasiotupendeza wamekombolewa kwa damu ya Kristo, pengine ni viungo vya mwili wake vinavyokaribia moyo wake kuliko sisi: mara nyingi tunaishi miaka pamoja na watu safi tusitambue uzuri wa roho zao. Vilevile, tukija kuwatazama kwa imani wanaotupendeza, pengine tunavumbua wana maadili ya Kimungu kiasi cha kuzidisha na kutakasa mapendo tunayowaonea; pia kwa wema tunaona vizuio walivyonavyo kwa utawala wa Mungu na tunaweza kushauriana nao tusonge mbele katika njia yake.
Hatimaye tunapaswa kutazama kwa imani matukio yote ya maisha yetu, ya furaha na ya uchungu vilevile. Mara nyingi tunaridhika kuyaona upande wa hisi tu, au kwa akili iliyoathiriwa na dhambi. Mara chache tunayazingatia Kimungu, kwa kuona kwamba “katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema” (Rom 8:28): hata katika upinzani, matatizo makubwa yasiyotarajika na dhambi (tukiweza kujinyenyekesha kutokana nazo). Katika kukosewa haki na watu tunaweza kutambua haki ya Mungu ikiadhibu makosa ya siri ambayo hatulaumiwi na mtu; au tunahisi majaribu ya Kimungu, na utakaso unaokusudiwa kupatikana kwa njia ya hayo.
Kabla ya imani yetu kutakaswa kwa majaribu kadhaa ya aina hiyo, tujitahidi kukua katika imani, badala ya kupima yote kibinadamu tu. Ni lazima tujinyime mianga midogo na ya bandia ili tujaliwe ile ya juu; tuache kufuata mno akili yetu ili tuone uangavu mkuu wa mafumbo ya imani na kuishi kulingana nayo. Hivyo tunaelewa kwa nini hatutakiwi kuitikia vishawishi dhidi ya imani, bali kuvikataa au kuviruka kwa kukiri imani kwa dhati zaidi; Bwana anaviruhusu kwa maendeleo yetu tu.
Itaendeleaa ...........................