Hii ni Kwaresima
Nini maana ya Kwaresima?Kwa
Kilatini na Kiitaliano neno Kwaresima lilimaanisha “40” yaani siku 40
za kufunga za wiki kati ya Jumatano ya Majivu hadi Jumamosi Kuu. Kwa
Kijerumani Kwaresima maana yake “Kipindi cha kufunga.”
Kwaresima ilianzaje?
Kabla
ya kuona Kwaresima jinsi ilivyoanza, ni vizuri kuongea kidogo kuhusu
Sikukuu ya Pasaka ili tuweze kupata mwanga wa kuelewa mwanzo wa kipindi
hiki muhimu cha Kwaresima.
Habari Njema yatuambia kwamba YESU
KRISTO alifufuka “Siku ya kwanza ya juma.” “Hata sabato ilipokwisha,
ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule
wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.” (Mt.28:1) Hii ni kwasababu
Wakristo walianza kukutana pamoja kwa sikukuu ya ufufuko wa BWANA kila
wiki sio Jumamosi kama Wayahudi, bali siku iliyo fuata. “Hata siku ya
kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo
akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza
-`maneno yake hata usiku wa manane.” (Mdo.20:7). “Siku ya Kwanza ya juma
kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake:
ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja.” (1Kor.16:2), siku
ambayo Warumi waliita “Siku ya Jua”. Mara moja jina hilo lilibadilika na
kuwa “Siku ya BWANA”
Kanisa la mwanzoni halikusherehekea sikukuu
kama vile Noel, Sikukuu kwa heshima ya Mama Bikira Maria au sikukuu
yeyote ile. Kulikuwepo na adhimisho la ufufuko wa BWANA kila wiki na
hakuna zaidi.
Miaka mingi ikapita kanisa likiwa katika hali hii.
Baadaye kulikuwepo na hitaji la kusherehekea tukio la kiini cha imani
yetu kwa namna ya pekee. Wakristo waliona umuhimu wa kuwa na muda kwa
sikukuu ya kwanza kati ya sikukuu zao yaani “Jumapili ya Pasaka”, ambayo
ilifikiriwa kama “Mama wa Jumapili zote”, “Mama wa skikukuu zote”.
Waliiona sikukuu hiyo kama “Malkia wa sikukuu zote, wa Jumapili zote, na
kiujumla kama Malkia wa siku zote za mwaka. Tangu mwanzoni mwa karne ya
pili, Jumuiya zote za Kikristo walikuwa wanasherehekea sikukuu hii ya
Pasaka. Sherehe zilikuwa zinahitimishwa na kusanyiko la sala
lililofanyika usiku na kumalizikia na Ekaristi. Ushiriki wa kwenye ibada
hiyo, ulichukuliwa kama ni kitu muhimu sana kwa mkristo.
Kuanza kwa Kwaresima
Wote
tunafahamu kwamba, ufanisi au mafanikio yoyote ya sikukuu au ya jambo
lolote yanategemea sana maandalizi yake. Miaka miambili hivi baada ya
KRISTO, Wakristo walitaka kuvuna matunda ya kiroho ya Paska kwa wingi.
Ili kufanikisha hili, walianzisha utamaduni wa kuwa na siku tatu kabla
ya Pasaka kwa sala, tafakari na kufunga kwa nia ya kuonyesha masikitiko
yao juu ya kifo cha YESU KRISTO. Kutokana na ukubwa na umuhimu wa
sikukuu hii, mbali ya kuona umuhimu wa maandalizi, walitafuta njia za
kuongeza muda wa furaha na utajiri wa kiroho utokanao na Pasaka. Hivyo
walianzisha “Wiki Saba,” yaani siku 50 za Pentekoste ambapo
walisherehekea na kuzipitisha siku hizo kwa hali ya furaha. Askofu Mt.
Ireneus alisema kuwa muda huo wa siku 50 ni kama Sikukuu ya Siku moja
yenye umuhimu sawa na Jumapili. Katika kipindi cha siku za Pentekoste,
sala zilikuwa zinasaliwa hali wamesimama, kufunga kulikatazwa na
sakramenti ya ubatizo ilikuwa ikiadhimishwa. Ni kama vile sikukuu ya
Pasaka ilidumu kwa kipindi chote cha siku 50. Miaka 150 ilipita na
mwishoni mwa mwaka 350 B.K., Wakristo waliona kama siku tatu hazikutosha
kwa maandalizi ya sikukuu kama hii. Hivyo waliongeza hadi kufikia siku
40. Hivi ndivyo Kwaresima ilivyoanza.
Kwa nini siku 40?
Tunaposema
kuku wanne au kilo saba za mchele tuna maana kama ilivyo yaani kuku
wanne na kilo saba za mchele. Si zaidi au pungufu.
Namba au
tarakimu mbalimbali tunazokutana nazo katika Biblia zinaashiria lugha za
picha na siyo kuchukulia katika thamani ya kuhesabu. Hivyio basi,
tunapokutana na namba kama 40 huenda isimaanishe 40 kama tunavyo hesabu
fedha. Kati ya maana nyingi zilizotolewa kwa namba 40, kuna moja yenye
maana ya pekee, inamaana ya kipindi cha maandalizi cha kutosha
kisichokuwa na muda maalum, kwa tukio kubwa. Kwa mfano , Gharika ilidumu
kwa siku 40 usiku na mchana…na ilikuwa ni maandalizi ya ubinadamu mpya;
Waisraeli walitumia muda wa miaka 40 jangwani…maandalizi ya kuingia
nchi ya ahadi; watu wa Ninawi walifunga na kufanya kitubio siku
40…maandalizi ya kupokea msamaha wa MUNGU; Elia alitembea kwa siku 40
mchana na usiku…kama maandalizi ya kufika mlima wa MUNGU; Musa na YESU
walifunga kwa siku 40 mchana na usiku… kama maandalizi kabla ya kuanza
utume wao. “Kisha ROHO alimwongoza YESU mpaka jangwani ili ajaribiwe na
ibilisi. Akafunga siku arobaini usiku na mchana, na mwishoe akaona njaa”
(Mt.4: 1-4)
Natumaini hadi hapo tumeelewa nini maana ya namba
40. Je, ni siku ngapi ambazo zinahitajika kwa ajili ya maandalizi ya
sikukuu kubwa kuliko zote za kikristo? Bila shaka ni 40. (Kuanzia
Jumatano ya majivu hadi Jumamosi Kuu ukiondoa Jumapili zote) Siku 40 ni
muda wa kutosha wa kufanikisha kitu fulani chema, kizuri na chenye
thamani.
Lengo la Kwaresima ni nini?
Lengo
kuu la Kwaresima ni kufanya upya maisha yetu ya kiroho na kutufanya
kuwa watu ambao MUNGU anataka tuwe yaani ni kipindi chenye kutupatia
utakatifu, tukikumbuka kuwa sote tumeitwa kuwa watakatifu kama BABA yetu
wa mbinguni alivyo mtakatifu (Mt. 5:48). Ni kipindi cha kuuvua utu wetu
wa kale na kuvaa utu mpya. Kwani tunasoma:- “Mvue kwa habari ya
mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unao haribika kwa kuzifuata tamaa
zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho na nia zenu; mkavae utu
mpya, ulioumbwa na MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli. Basi uvueni
uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake…Mwibaji asiibe tena…Neno
lolote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema na
kufaa…tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane
kama MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi.” (Efe.4:22-32.)
Kwaresima
kwa hakika ni kipindi pia cha kuachana na matendo ya mwili. “Basi
matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya: uasherati, uchafu, ufisadi,
ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka,
uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo;” (Gal.5:19 –
20)
Kwa ufupi Kwaresima ni kipindi cha kuachana na maisha ya
dhambi na kurudi kwa MUNGU kwa kuishi maisha yanayompendeza MUNGU kwa
njia ya kufanya toba ya kweli isiyo ya mazoea, na malipizi yasiyo ya nje
tu, bali hasa mapinduzi ya kiroho. Katika kipindi hiki tunalazima ya
kubadili hali yetu ya ndani. Badala ya kujitafuta wenyewe na kufuata
mapenzi yetu, inatupasa sisi kumwelekea MUNGU na kuyatimiza mapenzi yake
katika mawazo, maneno na matendo yetu.
Nguzo tatu kuu za Kwaresima ni:
i. Sala.
“Wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani. Usali mbele ya BABA
yako aliye sirini; na BABA yako aonaye sirini atakujazi.” (Mt. 6:6)
Kupata
muda wa sala pamoja na MUNGU. Sio tu kunena maneno ya sala fulani,
lakini pia kumsikiliza MUNGU akizungumza mioyoni mwetu. Kumuomba MUNGU
nguvu ya kubadilika, yaani uongofu wa kweli. Ndiyo maana tunaambiwa.
“Tubuni na kuiamini Injili”. Hayo ndiyo MUNGU aombayo kwetu wakati wa
Kwaresima. MUNGU anatuita kutoka kwa dhambi, na tuupokee ujumbe wake
kwetu – Injili, na kuwa waamninfu kuishi kadiri ya Injili. Ni wakati pia
wa kuhudhuria misa mara kwa mara kwa ibada na uchaji, kuhudhuria ibada
mbalimbali, kama vile Baraka ya Sakramenti Kuu, Kuabudu Ekaristi
Takatifu, kusoma Neno la MUNGU na kuliishi baada ya kuyatafakari maneno
hayo ya MUNGU ambayo ndiyo sauti yake MUNGU na kutumia muda wetu kwa
mambo ya ki-MUNGU yaliyo matakatifu.
ii. Kufunga.
“Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso wako ili
usionekane na watu ukifunga, ila na BABA yako aliye sirini; na BABA yako
aonaye sirini atakutuza.” (Mt. 6:17-18). Kufunga sio tu kujinyima
kutokunywa pombe, kutokula chakula, kutovuta sigara n.k. Kifupi ni
kwamba kufunga kuondokana na ubinafsi wetu na kuwafikiria na kuwasaidia
wenye shida. Uovu hauwezi kushindwa bila kujitoa nafsi na bila kutoa na
kuwapa wahitaji vile tuvipendavyo. MUNGU hapendezwi na kufunga tu, bali
upendo kwa wanaoteseka utusukume na kufunga tupendavyo kwa ajili ya
kuwasaidia wahitaji. Hivyo kuna mahusiano makubwa sana kati ya kufunga
na ukarimu. Kufunga lazima kuendane na ukarimu. Kufunga bila ukarimu huo
ni mfungo tasa.
iii. Kutoa Sadaka.
“Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu kusudi mtazamwe nao. Bali
wewe utoapo sadaka hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wa
kuume; na BABA yako aonaye kwa siri atakujazi.” (Mt. 6:1) Hayo
yanamaanisha kwamba usidai shukurani wala malipo kwa wema wowote
uwatendeao jirani zako kwa sadaka yako. Malipo utakayopata uyatazamie tu
kutoka kwa BABA yako wa mbinguni. Kutoa tunachojinyima kwa kumsaidia
KRISTO anayeteseka kwa wenzetu. Kushirikiana na wengine tulivyo navyo
kama vile fedha, nguo, chakula, ama kuwakaribisha wahitaji nyumbani.
Hivyo
basi, Mazoezi tunayofanya katika kipindi cha Kwaresima kama kusali
zaidi, kusikiliza au kusoma Neno la MUNGU, kutenda matendo ya huruma kwa
wahitaji, kufunga chakula na kujihinisha kinywaji pamoja na kuzuia
tamaa potovu za mwili wetu, yawe na kusudi la kuibadili hali yetu,
kutufanya kuwa na upendo zaidi na huruma kwa wenzetu na kutufanya tuweze
kuunganika zaidi na KRISTO MFUFUKA. Tumvue mtu wa zamani katika nafsi
zetu na tumvae mtu mpya, yaani KRISTO Mfufuka.
Nini makusudi ya kufunga?YESU
alifunga ili awape wanadamu mfano au kielelezo halisi na sahihi cha
kuiga, na apate kuokoa roho zetu. Watu wawe na namna bora ya kufanya
malipizi, kuuadibisha na kuutumikisha mwili na tamaa kwa kuwa anatenda
dhambi.
Nani anapaswa kufunga?Inatubidi
tujiangalie sana kwani miili yetu ni midhaifu na myepesi kwa kutenda
dhambi na kuipeleka roho motoni. Tusiiendekeze miili yetu, bali
tuitawale kwa kufuata maadili ya kimungu na kuinyima madai yake, ambayo
ni kishawishi kinachotupeleka upotevuni. Tunapoamua kufuata njia hii,
hakika, KRISTO atatuimarisha na kutuongoza kwenye uzima wa milele; na
kutupa neema ya kupambanua mema na dhambi, huku tukielekea uzimani.
Mdomo unao nena dhambi, na mwili unaotenda dhambi, sherti vyote vitende
pia mema, siyo dhambi.
Mtu asiyetenda dhambi hana haja ya
kufunga. Lakini hakuna mtu anyefikia utu uzima ambaye hatendi dhambi
machoni pa MUNGU hata Wacha MUNGU wana dosari. Kwa hiyo, kila mtu afunge
kufidia dhambi zake. Tusipofunga kuna hatari kubwa ya kuungua moto. Ni
vizuri waamini wote wafunge ili kulipia fidia ya dhambi zinazotendwa.
Tumwabudu KRISTO kwa unyofu na unyenyekevu, ili kwa huruma yake kuu
atusamehe dhambi zetu na adhabu tunazostahili.
Ngazi tatu za kufunga chakula:
(a)
Ngazi ya kwanza, ni kuacha chakula kimoja fulani, au kitu kingine
unachopendelea. Kufunga huku ni rahisi hata kwa watoto. Kwa mfano,
kuacha kula nyama au kunywa soda yoyote kwa kipindi kizima cha
Kwaresima; au kula chakula bila chumvi, au kunywa chai bila sukari kwa
kipindi kizima cha mfungo. Huu ni mfungo rahisi.
(b) Ngazi ya
pili, ni kuacha kabisa kula siku nzima. Hii ni ngazi ya kawaida, yaani
mfungo wa kawaida. Huku ni kula mlo mmoja tu kwa siku hadi utosheke.
Yawezekana ikawa ukala mlo wa mchana au wa jioni tu. Asubuhi au jioni
(au asubuhi na mchana) ule kidogo sana. Katikati ya hapo usile chochote
tena wala kunywa chochote.
(c) Ngazi hii ya tatu ni ya wale
wanaotaka kufanya malipizi makali zaidi. Huu ni Mfungo mkali. Katika
ngazi hii ya kufunga watu wengi huaacha kabisa kula na kunywa siku
nzima, wakawa na huo mlo mmoja tu. Wanaotaka malipizi makali zaidi siku
ya kufunga chakula, asubuhi pokea Ekaristi Takatifu, na wala usiguse
chakula au kinywaji chochote kingine. Mchana unaweza kula slesi moja
(kipande) tu ya mkate na unywe glasi moja tu ya maji ya kawaida. Jioni
pia ule slesi moja ya mkate na unywe glasi moja tu ya maji. Na endapo
utaamua kutokula kabisa na kutokunywa kabisa hadi asubuhi kesho yake,
itampendeza zaidi Mwenyezi MUNGU. Hii ndiyo toba ya kweli.
Tukumbuke
kwamba kile tunachofunga kiwasaidie wasiojiweza. Si kufunga kwa nia ya
kuweka akiba ili baada ya mfungo uweze kutumia wewe mwenyewe! La hasha.
Huo si mfungo wenye kuleta faida kiroho, bali ni mfungo tasa.
Kuacha kula nyama Ijumaa Kuu na Ijumaa nyingine za mwaka.
Ufungapo
au uachapo kula nyama, funga kweli na acha kweli kula nyama kwa dhati
kwa toba ya dhambi. Vinginevyo utakuwa unajidanganya mwenyewe. Papo
uutolee mfungo wako na kutokula nyama huku kwa Mwenyezi MUNGU, kwamba
unafanya hivyo kwa kudhamiria. La sivyo utadhania unafunga na unaacha
kula nyama kwa manufaa ya kiroho wakati unashinda tu na njaa ! Kuacha
kula nyama maana yake ni kula vyakula vitokanavyo na ardhi tu; ndivyo
vyakula vya mfungo. Acha kula kila aina ya nyama, na mafuta yanayotokana
na wanyama. Usile nyama, mayai, mafuta ya wanyama, siagi na jibini,
wala maziwa. Kula vitu vyovyote vitokanavyo na wanyama au ndege
hurahishisha mfungo wako. Kumbuka pia kwamba siku za kufunga na kuacha
kula nyama, uwe macho sana, maana shetani mshawishi atakuja kupima
utashi wako. Shinda mwili (njaa na kiu) wako, mshinde shetani
anyekuongoza dhambini. Jambo la muhimu hasa ni kwamba matendo hayo yote
yatendeke kwa ajili ya BWANA. Tuyafanye kama alama ya kwamba tunataka
kurudi kwake. Yawe ni matendo kati ya MUNGU na mimi. Kwa sababu hiyo
lazima kulinda siri ya jambo lolote tutakalo tenda. “BABA yako aonaye
sirini atakujazi.”
Nini thamani na maana ya kujinyima jambo fulani ambalo kimsingi ni zuri na inafaa kwa ajili ya afya ya mwili?
Thamani
na maana ya kufunga tunaiona na kupata mfano kwa YESU. Ni vema
tukumbuke kwamba Kwaresima inatukumbusha siku 40 za mfungo wa BWANA wetu
jangwani, alivyofanya kabla ya kuanza Utume wake hadharani, (Mt.
4:1-2). Pia, kama Musa alivyofunga kwa siku 40 usiku na mchana kabla ya
kupokea zile Mbao za Sheria (Kut. 34:28). Eliya naye alifunga kabla ya
kukutana na BWANA katika Mlima Horeb (1 Wafal. 19:8), YESU vile vile kwa
njia ya sala na kufunga, akijitayarisha kwa ajili ya majukumu
yaliyokuwa mbele yake, alituonesha tangu mwanzo mapambano makali dhidi
ya Shetani.
Hivyo basi, Maandiko Matakatifu na mafundisho yote ya
desturi za ukristo yanafundisha kuwa mfungo ni msaada mkubwa katika
kukwepa dhambi na vishawishi vinavyoweza kutupeleka katika dhambi
yenyewe. Kwa kuwa kila mmoja wetu anaelemewa na dhambi na mafuatano
yake, kufunga kumependekezwa kwetu kama njia ya kurudisha urafiki wetu
na MUNGU. Hivi ndivyo alivyofanya Ezra (8:21), walivyofanya watu wa
Ninawi (Yona 3:9).
Je, unajua mfungo wa kweli ni upi?
Mfungo
wa kweli kama YESU alivyorudia mahali pengi, ni kufanya mapenzi ya Baba
aliye Mbinguni, “na BABA yako aonaye sirini, na atakujazi” (Mt. 6:18).
Mfungo wa kweli unaelekezwa katika kula chakula cha kweli; yaani
“kufanya mapenzi ya MUNGU” (Yn. 4:34).
Hivyo basi, kama katika
Kwaresima hii UMEAMUA kweli kusali, basi funga; kama unafunga, onesha
huruma; kama unataka maombi yako yasikiwe, sikiliza maombi ya wengine.
Endapo hufungi masikio yako kwa wengine, unafungua masikio ya MUNGU kwa
ajili yako.
Kwa hakika mfungo unaleta faida za kimwili, lakini
kwa Mkristo mfungo upo kwa ajili ya “Tiba” ya kuponya yale yote
yanayouzuia mwili kutekeleza utashi wa MUNGU. Pia kufunga ni njia ya
kuonesha “huzuni” (1 Sam 31:13; 1 Fal 21:27; Neh1:4); toba (1 Sam 7:6;
Yoe 2:12; Dan 9:3-4) au hali ya “unyofu katika maombi” (2 Nya 20:3-4;
Ezra 8:23).
Mpenzi msomaji wa kijitabu hiki, nakutakia Kwaresima
njema na mfungo wenye heri na toba ya kweli mbele za MUNGU kwa kuleta
mabadiliko ya kweli katika maisha yetu ili kufungua mifereji ya neema na
baraka katika mtu binafsi, familia na Jumuiya. Tukumbuke kwamba dhambi
huzuia baraka na neema toka kwa MUNGU hata kurudisha nyuma maisha yetu
ya kiroho na maendeleo katika familia. Hivyo, katika kipindi hiki cha
Kwaresima tukitumie kwa kufanya toba ya kweli kimatendo ili kuondoa
vikwazo vyote vinavyo zuia maendeleo yetu kiroho na ya kifamilia kwa
kuwa tayari kumegwa kuwa chakula kwa wengine kwa njia ya ukarimu wetu.
Tujitahidi katika kushiriki Ibada ya Njia ya Msalaba ikichukuliwa katika
mtazamo wa kufanya toba na kuomba msamaha kwa MUNGU. Kushiriki
Sakramenti vema hasa Sakramenti ya upatanisho ili mfungo, na toba yetu
vipate kibali machoni pake MUNGU na kushiriki matakatifu.
MUNGU akubariki na kukulinda. Nakutakia kwaresima njema.
“Wakati umetimia na ufalme wa MUNGU umekaribia, Tubuni na kuiamini Injili.” (Mk 1:16).
NJIA YA MSALABANjia
ya Msalaba ni ibada ya Mateso na Kifo cha KRISTO. Tunasafiri naye
kiroho kutoka kwenye nyumba ya Pilato hadi Kalvari. Tunakumbuka yote
yaliyotukia tangu alipohukumiwa hadi alipozikwa karibuni. Tunafanya
ibada hii kwa kuwa karibu na YESU anayeteseka kwa ajili yetu na kuwa
karibu na Bikira MARIA Mama wa Mateso. Hivyo, tufikiri juu ya ubaya wa
dhambi zetu na kuzijuta na kudhamiria kuziacha kweli. Pili, tufikiri juu
ya Fumbo la Mapendo ya YESU kwa BABA yake na kwetu sisi wanadamu. Ibada
hii itusaidie kuonja wokovu uliotujia kwa Mateso, Kifo na Ufufuko wa
Mkombozi wetu, YESU KRISTO.
Sala mbele ya AltareEe,
Mkombozi wangu, ninakuja leo kufuata njia ile uliyoshika siku ya kufa
sadaka yetu. Nimetubu dhambi zangu zote; ninataka kugeuza mwendo wangu;
ninaomba kwako niwapatie roho za waamini marehemu waliomo toharani,
rehema zote zilizotolewa na Kanisa kwa Njia ya Msalaba. Nawe MARIA
Bikira Mtakatifu, uliyefuata njia ile nyuma ya mwanao YESU, uniangalie
kwa wema, unitie Moyo Mkuu, nisipende dhambi tena, nikivumilia kazi na
usumbufu na mateso na matukano yatakayonipata.
**************
Umekosa nini we YESU,/ Kushtakiwa bure kwa Pilato
Wenye kustahili hukumu, Si wewe, si wewe BWANA, ni sisi.
KITUO CHA KWANZA - YESU anahukumiwa afe
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Pilato
anamhukumu YESU ingawa haoni kosa lake, anawaogopa Wayahudi.
Anabembeleza urafiki wa Kaysari. Ee YESU usiye na kosa, hata mimi
ningeweza kutenda mema mengi, lakini naogopa macho ya wenzangu, na
maneno yao. Ee BWANA, uniima-rishie utashi wangu, nijitegemee katika
kushika madaraka yangu.
BABA yetu… – Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
**************
Ole Msalaba huo mzito, / Apagazwa mwana mpenzi wa MUNGU. / Mwili waenea mateso, / Alipa, alipa madhambi yetu
KITUO CHA PILI - YESU anapokea msalaba
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
YESU
anakubali kuelemewa na msalaba kwa ajili ya wokovu wa watu. Ndivyo
anavyonifundisha moyo wa sadaka, moyo wa kujitolea na kujisahau kwa
ajili ya wengine. Ee YESU wangu mkarimu, mimi pia ninao msalaba wangu:
jirani zangu, mwenzangu wa ndoa, watoto, wazazi wangu, kazi zangu, joto,
baridi, njaa, kiu, vishawishi, magonjwa na matatizo mengine ya maisha,
wajibu wangu kwa MUNGU, kwa umma na kwa Kanisa. Hayo yote ni msalaba.
Unipe ukarimu wako ee YESU, niyapokee bila kunung’unika, na kuyabeba
vema.
BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
**************
Ona Muumba mbingu na nchi, / Yupo chini mzigo wamwelemea, / Na mtu kiumbe chake kwa ukali, / Ampiga, ampiga bila huruma.
KITUO CHA TATU - YESU anaanguka mara ya kwanza
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
YESU
amedhoofika sana, anaanguka chini, kisha anasimama, anaendelea na
safari ya ukombozi. Ee YESU uliyeanguka chini ya msalaba kwa ajili ya
udhaifu, ukasimama tena; usiniache katika tamaa nikianguka dhambini,
bali nisimame mara moja, nikufuate.
BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
**************
Huko njiani we MARIA, / Waonaje hali ya mwanao, / Ni damu tupu na vidonda, / Machozi, machozi yamfumba macho.
KITUO CHA NNE - YESU anakutana na mama yake
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Wote
wawili mama na mwanawe wanaumia sana moyoni kwa ajili ya dhambi zangu.
Ee YESU, Mwana wa MARIA, unitilie moyoni mwangu upendo na ibada kwa
Bikira MARIA; unijalie na ulinzi wake, nisitende dhambi tena.
BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
**************
Kwa Simoni heri ya kweli, / Mimi pia YESU nisaidie, / Kuchukua mzigo wa ukombozi, / Kuteswa, kuteswa pamoja nawe.
KITUO CHA TANO - Simoni wa Kirene anamsaidia YESU
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Nausifu
ukarimu wa Simoni wa Kirene. Ee BWANA unijalie ukarimu kama huo,
niitikie nami wito wa kukusaidia kuchukua msalaba. Nitoe zaka na
michango yote ya uenezaji wa dini; nijitolee mimi mwenyewe katika kazi
ya maendeleo ya dini. Uwajalie vijana wengi wito wa Upadre, waweze
kuchukua msalaba pamoja nawe kwa ajili ya wokovu wa dunia. Uwaimarishe
viongozi wa dini. Ustawishe moyoni mwa waamini wote mwamko wa utume.
BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
**************
Uso wa YESU Malaika, / Betlehemu walikuabudu, / Bahati yake Veronika, / Kupangusa, kupangusa Mfalme wa Mbingu.
KITUO CHA SITA - Veronika anapangusa uso wa YESU
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Mama
huyu ni kinyume kabisa cha Pilato. Veronika anajua analopaswa kutenda,
na analitenda bila kujali macho na maneno ya makundi ya watu waovu. Ee
YESU, uliyemtuza Veronika zawadi ya picha ya uso wako juu ya kitambaa,
unijalie ushupavu na ujasiri wake wa kutenda mema, ili roho yangu
ipambwe kwa chapa ya uungwana na utakatifu wako.
BABA yetu… -Salamu MARIA… -Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie. W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
Wakimvuta huku na huku, / Wauaji wanamchokesha bure, / Chini wanamtupa bado kwa nguvu, / Aibu, aibu yao milele.
KITUO CHA VII - YESU ANAANGUKA MARA YA PILI
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Ee
YESU uliyelegea mno kwa mateso makali, unapoanguka mara ya pili kwa
ajili ya udhaifu wa mwili, wanionya kwamba hata mimi naweza kurudi
dhambini kwa udhaifu wa moyo. Nipe basi neema ya kuepuka nafasi za
dhambi na visa vyenye kunikwaza na kunirudisha dhambini.
BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amni. Amina.
Wanawake wa Israeli, / Msilie kwa sababu hiyo, / Muwalilie hao kwa dhambi, / Upanga, upanga ni juu yao.
KITUO CHA VIII - AKINA MAMA WANAMLILIA YESU
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Asanteni
sana akina mama kwa moyo wenu wa huruma. Ee YESU uliyetulizwa na
wanawake, unipe moyo wa kuwaheshimu akina mama wote. Uwaite na wasichana
wengi waingie utawa, ili watulize moyo wako Mtakatifu kwa sala na
sadaka zao.
BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
Mwokozi sasa ni ya tatu, / Waanguka chini ya msalaba, / Katika dhambi za uregevu, / Nijue, nijue kutubu hima.
KITUO CHA IX - YESU ANAANGUKA MARA YA TATU
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Ee
YESU unayezidi kudhoofika kwa mateso unaanguka mara ya tatu, upate
kunistahilia neema ya kuutiisha mwili wangu na kuusulibisha, licha ya
kuepuka nafasi za dhambi. Mara nyingi mno ninajibovusha kwa kupenda mno
starehe, anasa na tafrija. Ee YESU mwema, nisaidie kuufuata mfano wa
Mtakatifu Paulo, niutese mwili wangu na kuutumikisha, ili nipate siku
moja tuzo mbinguni.
BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
Muje Malaika wa Mbingu, / Funikeni mwiliwe kwa huruma, / Vidonda vyake na utupu, / Askari, askari wamemvua.
KITUO CHA X - YESU ANAVULIWA NGUO
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Askari
wanamvua kwa nguvu nguo yake, iliyogandamana na madonda yake;
wanayaamsha mara moja mateso yote aliyoteswa tangu mwanzo. Ee YESU,
unayavumilia mateso makali haya, upate kunifundisha kuuvua kwa nguvu
moyoni mwangu urafiki mbaya, au kitu kingine chochote kile kinachoharibu
urafiki wa MUNGU, hata ikipasa kutoa sadaka kubwa.
BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
Hapo MKRISTO ushike moyo, / BWANA wako alazwa msalabani, / Mara miguu na mikono, / Yafungwa, yafungwa kwa misumari
KITUO CHA XI - YESU ANASULIBIWA MSALABANI
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Ee
YESU uliyepigiliwa misumari msalabani, nakutolea akili na utashi wangu,
vifungwe pamoja na miguu yako, nipate kuwaza, kusema na kutenda siku
zote yale tu yanayolingana na utukufu wa msalaba wako Mtakatifu. Ee
YESU, mimi ni mfungwa wako. Nisaidie kuimarisha kifungo hicho kwa sala,
Sakramenti na fadhila za KiKRISTO.
BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
**********
YESU mpenzi nakuabudu, / Msalabani unapohangaika, / Nchi yatetemeka kwa hofu, / Na jua, na jua linafifia.
KITUO CHA XII - YESU ANAKUFA MSALABANI
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Ee
YESU uliyekufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu, unijalie niichukie
dhambi, nisiishi kamwe katika dhambi. Nifahamu kwamba nilipobatizwa kwa
jina lako, nilibatizwa katika mauti yako ili utu wangu wa kale
usulibishwe nawe, mwili wa dhambi uangamizwe nisitumikie tena dhambi.
BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
**********
Mama MARIA mtakatifu, / Upokee maiti ya Mwanao, / Tumemwua kwa dhambi zetu, / Twatubu kwake na kwako.
KITUO CHA XIII - YESU ANASHUSHWA MSALABANI
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Ee
YESU uliyeshushwa msalabani baada ya kufa, unijalie nidumu katika
maisha ya kujitoa sadaka mpaka siku ya kufa kwangu. Nielewe na kukubali
kwamba baada tu ya kufa ndio mwisho wa vita na mashindano ya KiKRISTO.
BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
Pamoja nawe kaburini, / Zika dhambi na ubaya wa moyo, / YESU tuwe Wakristo kweli, / Twakupa twakupa sasa mapendo.
KITUO CHA XIV - YESU ANAZIKWA KABURINI
- Ee YESU, tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Ee
YESU, ulizikwa kaburini, ukafufuka siku ya tatu. Mimi pia nilizikwa
pamoja nawe kwa njia ya ubatizo katika mauti yako. Kwa vile wewe
ulifufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa BABA, unijalie nami
nifufuke, yaani nishike mwenendo mpya, mwenendo wa uzima wa milele.
BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
**********
Katika roho yangu BWANA, / Chora mateso niliyokutesa, / Nisiyasahau madeni, / Na kazi, na kazi ya kuokoka.(Hiari yako - Mbele ya Altare)
KITUO CHA XV - YESU AMEFUFUKA
- Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
- Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu
Habari
njema aliyotuletea YESU ni kwamba baada ya kila Ijumaa Kuu huja sikukuu
ya Pasaka; kwamba punje ya ngano isipoanguka ikafa, hukaa hali hiyo
hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa maozo mengi. Twakushukuru, ee YESU,
kwa mateso yako, lakini twakushukuru hasa kwa ufufuko wako, kwa kuwa huo
ndio unaotupa hakika ya kuwa hatukuzaliwa kwa ajili ya mateso na
maumivu, bali kwa ajili ya heri ya milele.
BABA yetu -Salamu MARIA -Atukuzwe BABA.
K. Ee BWANA, Utuhurumie W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
*********
SALA YA MWISHO
Mbele
ya Altare: YESU wangu, kwa uchungu wote ulioona juu ya msalaba, na kwa
kuzimia kwako kwa ukali wa mateso, unijalie nguvu ya kuvumilia kwa moyo
taabu zote sasa na saa ya kuzimia kwangu. Nawe MARIA Mamangu, kwa
uchungu wote ambao moyo wako umejaa ulipomwona mwanao mpenzi kuinama
kichwa na kuzimia, unifadhili nife kifo chema.
SALA YA KUMWOMBA YESU ALIYETESWA
YESU
wangu,/ kwa masikitiko uliyoyaona hata ya kuzimia roho,/ na kwa jasho
la damu ulilotoka kwa sababu ya dhambi zangu,/ unitie uchungu wa kweli
juu ya makosa yangu! YESU wangu, / kwa msongo wa moyo uliouona kutolewa
na Yuda,/ unifanyizie nikae amini kwako,/ nisikutoe bado vile
nilivyofanya mpaka leo!/ YESU wangu, uliyefungwa kama mtu mwovu,/
niunganishe nawe kwa vifungo vya mapendo yako! YESU wangu,/ kwa madharau
uliyodharauliwa, / na machukizo uliyochukizwa mbele ya Ana,/ Kaifa na
Herodi,/ uniwezeshe kuvumilia kwa saburi matukano nitakayotukanwa na
watu! / YESU wangu, kwa maumivu uliyovumilia mwilini mwako ulipopigwa
fimbo nyingi mno,/ nijalie nguvu ya kustahimili maumivu ya ugonjwa, / na
kukataa furaha zote mbaya!/ YESU wangu, /kwa mateso uliyoona ulipotiwa
taji la miiba,/ unipe neema ya kutokubali tena mawazo yoyote ya majivuno
na ya uchafu!/ YESU wangu, /uliyechukua msalaba wako mzito kwa ajili ya
dhambi zangu, / unitie moyo mkuu, / nikubali kwa uvumilivu taabu na
sulubu zote za maisha yangu! / YESU wangu, uliyemwaga damu yako yote juu
ya msalaba kwa ajili yetu,/ nifanyizie niwe hai kwa ajili yako tu!/
YESU wangu, kwa kiu kikali ulichoona kwa ajili yangu,/ nifanyizie
nisikukasirishe tena kwa kupenda mno chakula au kileo!/ YESU wangu, kwa
uchungu wote uliouona juu ya msalaba,/ na kwa kuzimia kwako kwa ukali wa
mateso,/ nijalie nguvu za kuvumilia kwa moyo taabu zote saa ya kuzimia
kwangu!/ Nawe MARIA Mama yangu, kwa uchungu wote ambao moyo wako umejaa /
ulipomwona Mwanao mpenzi akiinama kichwa na kuzimia,/ unifadhili nife
kifo chema! Amina.
na Abel Reginald