Mungu amepanga kwamba familia
ya
Kikristo iwe katika mfumo fulani. Kwa sababu mfumo huo unaleta uthabiti
katika maisha ya familia, Shetani hufanya kazi sana kupotosha mpango
aliokusudia Mungu.
Kwanza kabisa ni kwamba, Mungu amepanga mume awe kichwa
cha familia. Hii haimpi mume ruhusa ya kutawala mke wake na watoto
katika ubinafsi. Mungu amewaita waume kupenda, kulinda, kutimiza
mahitaji na kuongoza familia zao kama kichwa. Pia, Mungu alikusudia wake
wawe watiifu kwa uongozi wa waume zao. Hili ni wazi, kama Maandiko
yanavyosema.
Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu.
Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha
Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo
Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo (Waefeso 5:22-24).
Mume si kichwa wa mkewe
kiroho – Yesu ndiye
mwenye nafasi hiyo. Yesu ni kichwa wa kanisa kiroho, na mke wa Kikristo
ni mshirika wa kanisa sawa na mume wake ambaye ni Mkristo pia. Ila,
katika familia, mume Mkristo ndiye kichwa wa mke wake na watoto, nao
wanapaswa kutii na kunyenyekea mamlaka yake hayo aliyopewa na Mungu.
Je, mke anapaswa kumtii mumewe kwa kiwango gani? Kama
Paulo anavyosema, ni katika
kila jambo.
Wakati pekee anaporuhusiwa kuvunja sheria hiyo ni kama mume wake
anamtaka kuvunja Neno la Mungu au kufanya kitu ambacho kinapinganana
dhamiri yake. Ni wazi kwamba hakuna mume Mkristo atakayemtaka mke wake
kufanya chochote kinachovunja Neno la Mungu au kwenda kinyume na dhamiri
yake. Mume si Bwana kwa mkewe – Yesu tu ndiye mwenye nafasi hiyo
maishani mwake. Kama itafikia uchaguzi kuhusu nani wa kumtii, anapaswa
kuchagua kumtii Yesu.
Waume wanapaswa kukumbuka kwamba Mungu hayuko upande wao
mara
zote. Kuna wakati ambapo Mungu alimwambia Ibrahimu afanye kama
alivyoambiwa na Sara mkewe (ona Mwanzo 21:10-12). Maandiko pia yanataja
jinsi Abigaili alivyoacha kumtii Nabali mumewe, aliyekuwa mpumbavu, na
kwa kufanya hivyo aliepusha tatizo (ona 1Samweli 25:2 – 38).
Mungu anawaambia hivi waume:
Enyi waume, wapendeni wake zetu kama Kristo naye
alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake… Vivyo hivyo imewapasa
waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe
hujipenda mwenyewe, maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali
huulisha na kuutunza kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa
tu viungo vya mwili wake. … Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi
yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe (Waefeso 5:25, 28-30,
33).
Waume wanaagizwa kuwapenda wake zao kama Kristo
anavyolipenda Kanisa. Si wajibu mdogo huo! Mke yeyote atajinyenyekeza
kwa furaha kabisa kwa mtu anayempenda kama Yesu – aliyetoa uhai Wake kwa
sababu ya upendo wa kujitoa. Sawa na jinsi Kristo anavyoupenda mwili
Wake – yaani Kanisa – ndivyo na waume wanavyotakiwa kumpenda mwanamke
ambaye ni “mwili mmoja” nao (Waefeso 5:31). Kama mume Mkristo anampenda
mkewe kama anavyopaswa, atamtimizia mahitaji yake, atamtunza,
atamheshimu, atamsaidia, atamtia moyo, na atatumia muda kuwa naye.
Akishindwa katika wajibu wake kumpenda mkewe, mume huyo yuko hatarini
kuzuia majibu ya maombi yake mwenyewe.
Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima kama chombo kisicho na nguvu na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe (1Petro 3:7. Maneno mepesi kukazia).
Kihalisi ni kwamba hapajawahi kuwepo na ndoa isiyokuwa
na kutokuelewana na shida mbalimbali. Ila, kwa kujitoa na kukuza tunda
la Roho katika maisha yetu, waume na wake wanaweza kujifunza kuishi kwa
maelewano na amani, na kufikia mahali pa kutambua baraka zinazozidi
kuongezeka za ndoa ya Kikristo. Kila mwenzi anaweza kukua na kufikia
ukomavu mkubwa katika kufanana na Kristo kutokana na matatizo
yasiyoepukika yanayotokea katika ndoa zote.
Kwa maelezo zaidi juu ya wajibu na majukumu ya waume na
wake, tazama Mwanzo 2:15-25; Mithali 19:13; 21:9, 19; 27:15, 16;
31:10-31; 1Wakor. 11:3; 13:1-8; Wakolosai 3:18, 19; 1Timo. 3:4, 5; Tito
2:3-5; 1Petro 3:1-7.
Mungu ndiye mwanzilishi wa tendo la ndoa, na ni
dhahiri kwamba aliliumba ili kustarehesha na kusaidia katika uumbaji.
Pamoja na hayo,
Biblia inatamka wazi kwamba tendo la ndoa ni la kufurahiwa na wale walioungana pamoja katika agano la ndoa, la kudumu.
Kukutana kimwili nje ya mipaka ya ndoa huitwa zinaa au
uasherati. Mtume Paulo alisema kwamba wale watendao mambo kama hayo
hawataurithi ufalme wa Mungu (ona 1Wakor. 6:9-11). Ingawa Mkristo
anaweza kujaribiwa na pengine kufikia kuanguka katika tendo la uzinzi au
uasherati, atajisikia hatia kubwa sana rohoni mwake, itakayompelekea
kutubu.
Paulo pia alitoa mafundisho wazi kabisa kuhusu majukumu ya mume na mke kwa mwenzake, kuhusu tendo la ndoa.
Lakini kwa sababu ya zinaa, kila mwanamume na awe na
mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume
na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.
Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe. Vivyo hivyo, mume hana
amari juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa
muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije
akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu (1Wakor. 7:2-5).
Mistari hii inaweka wazi kabisa kwamba tendo la ndoa
lisitumiwe kama “zawadi” na mume au mke, maana hakuna mwenye mamlaka
juuya mwili wake mwenyewe.
Tena, tendo la ndoa ni zawadi kutoka kwa Mungu. Si dhambi
wala najisi inapokuwa katika ndoa. Paulo aliwatia moyo Wakristo wenye
ndoa kushirikiana kimwili. Tena, tunapata ushauri huu kwa waume Wakristo
katika kitabu cha Mithali:
Chemchemi yako ibarikiwe; nawe umfurahie mke wa ujana
wako. Ni ayala apendaye na paa apendezaye; maziwa yake ytakutoshe siku
zote; na kwa upendo wake ushangilie daima (Mithali 5:18, 19).[1]
Kama wanandoa Wakristo wanataka kufurahia mahusiano
kimwili yenye kutosheleza, waume na wake wanahitaji kuelewa kwamba kuna
tofauti kubwa sana kati ya wanaume na wanawake kwa habari ya
kushirikiana kimwili. Kiasili, mwanamume ni mtu wa kimwili sana kwa
habari ya kukutana kimwili. Asili ya mwanamke kwa habari ya kukutana
kimwili ni kitu cha hisia. Wanaume husisimka na kuwa tayari kukutana
kimwili na mwanamke kwa kuona tu (ona Mathayo 5:28). Wanawake wao
husisimka na kuwa tayari kukutana kimwili kwa mahusiano ya karibu sana,
na kwa kuguswa na kushikwa-shikwa (ona 1Wakor. 7:1). Wanaume huvutiwa na
wanawake wanaowapendeza macho; ila wanawake huvutiwa na wanaume
wanaowapendeza kwa sababu zaidi ya kuvutia kimwili. Hivyo, wanawake
wenye busara hupendeza ili kuwavutia waume zao wakati wote. Na waume
wenye hekima huonyesha upendo wao kwa wake zao kutwa nzima kwa
kuwakumbatia na kuwatendea mambo ya ukarimu, badala ya kuwatazamia wake
zao “kuwa tayari” kwa ghafula wakati wa usiku.
Kiwango cha ashiki ya mwanamume kukutana kimwili na
mwenzake huongezeka kulingana na kuongezeka kwa mbegu za uzazi katika
mwili wake. Kiwango cha ashiki ya mwanamke huongezeka au kupungua
kutegemeana na siku zake za mwezi. Wanaume wana uwezo wa kusisimka na
kuwa tayari kukutana kimwili na mwanamke, na kufikia kilele cha tendo la
ndoa baada ya muda mfupi sana – nukta chache tu au dakika, ila wanawake
huchukua muda mrefu. Ingawa mwanamume yuko tayari kimwili kukutana na
mwanamke upesi sana, mwili wa mwanamke unaweza usiwe tayari, mpaka baada
ya nusu saa au zaidi. Basi, waume wenye hekima huchukua muda katika
kuanza kuwasisimua wenzao kwa kuwapapasa, kuwabusu na kuwashika-shika
sehemu za mwili ambazo zinasisimua, ili kumsababisha mwanamke kuwa
tayari kukutana kimwili. Ikiwa hajui sehemu zinazohusika, amwulize.
Tena, anapaswa kujua kwamba, japo yeye anaweza kufikia kilele cha tendo
la ndoa mara moja tu, mwenzake anaweza kufikia kilele cha tendo la ndoa
mara nyingi. Mume anapaswa kuhakikisha kwamba mwenzake anapokea
anachotaka.
Ni muhimu sana kwa waume Wakristo na wake zao kuzungumza
kuhusu mahitaji yao kwa uwazi, na kujifunza juu ya tofauti zao kiasi
wanachoweza. Mahusiano kimwili kati ya waume na wake yanaweza kuwa
baraka inayozidi kuongezeka kutokana na mawasiliano ya miezi mingi na
miaka, na kugunduana na kuzoeana.
Watoto wanapaswa kufundishwa jinsi ya kunyenyekea
na kutii kabisa wazazi wao Wakristo. Wakifanya hivyo, wameahidiwa
maisha marefu na baraka zao.
Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana
hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya
kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia (Waefeso
6:1-3).
Akina baba Wakristo kama vichwa wa familia zao, wanapewa wajibu wa msingi kabisa kwa ajili ya kuwafundisha watoto wao, hivi:
Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana (Waefeso 6:4).
Ona kwamba wajibu wa baba ni wa namna mbili: kuwalea watoto wake
katika adabu na maonyo ya Bwana. Hebu tuanze kwa kutazama haja ya kuwafundisha watoto adabu.
Mtoto asiyetiwa nidhamu atakapokuwa mtu mzima
atakuwa mbinafsi na muasi kwa mamlaka. Watoto wanapaswa kutiwa nidhamu
wakati wowote wanapoacha
kwa makusudi kutii sheria halali
zilizowekwa na wazazi wao. Watoto wasiadhibiwe kwa makosa au
kutowajibika kwa sababu ya utoto. Lakini, watakiwe kukabiliana na
matokeo ya makosa yao na kutowajibika kwao, na kwa njia hiyo kuwasaidia
kujiandaa kwa ajili ya uhalisi wa maisha ya utu uzima.
Watoto wadogo wanapaswa kuadhibiwa kwa kiboko, kama Neno
la Mungu linavyofundisha. Lakini watoto wachanga wasipigwe viboko. Hii
haina maana kwamba watoto wachanga waruhusiwe kufanya wanachotaka.
Inatakiwa tangu wanapozaliwa wajue kwamba mama na baba ndiyo wenye
mamlaka. Wanaweza kufundishwa wakiwa wadogo sana maana ya neno “hapana”
kuwakuwakataza tu kufanya kitu wanachofanya, au wanachotaka kufanya.
Wakianza kuelewa maana ya neno “hapana”, wanaweza kuchapwa kofi dogo tu
matakoni ili kuwasaidia kuelewa vizuri zaidi wanapoendelea kufanya kile
ambacho wazazi wanasema kisifanywe. Kama hayo yatafanyika kwa utaratibu
na mara kwa mara, watoto watajifunza kuwa watiifu tangu umri mdogo sana.
Pia, wazazi wanaweza kuonyesha mamlaka yao kwa kutounga
mkono tabia zisizotakiwa za watoto wao. Mfano ni kuwapa mara moja kitu
wanachotaka, wakilia. Kufanya hivyo ni kuwafundisha watoto walie ili
wapate matakwa yao. Au, kama wazazi watakubaliana na madai ya watoto wao
kila mara wanaponuna au kukasirika ni kwamba wanawatia moyo kuendelea
na tabia hiyo isiyotakiwa. Wazazi wenye hekima huunga mkono tabia nzuri
tu katika watoto wao.
Kuchapa kiboko kusilete madhara kimwili, ila kusababishe
maumivu ya kutosha kumfanya mtoto yule asiyetii kulia kwa muda kidogo.
Kwa njia hiyo, mtoto atajifunza kuunganisha uchungu na kutokutii. Hata
Biblia inaunga mkono hilo.
Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; bali yeye
ampendaye humrudi mapema. … Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto;
lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali. … Usimnyime mtoto wako mapigo;
maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. Utampiga kwa fimbo, na kumwokoa
nafasi yake na Kuzimu. … Fimbo na maonyo hutia hekima; bali mwana
aliyeachiliwa humwaibisha mamaye (Mithali 13:24; 22:15; 23:13-14;
29:15).
Wazazi wanaposimamia sheria zao, hawana haja ya
kuwatisha watoto ili kuwafanya watii Mtoto anapoacha kutii kwa makusudi,
achapwe fimbo. Ikiwa mzazi
atatishia tu kumchapa mtoto wake
ambaye si mtii, anachofanya ni kuunga mkono uasi wa mtoto wake. Matokeo
ni kwamba mtoto anajifunza kutokujali utii mpaka vitisho vya wazazi wake
vya maneno vinapofikia kiwango fulani cha sauti.
Baada ya kiboko, mtoto anapaswa kukumbatiwa na kuhakikishiwa upendo wa mzazi aliyemchapa.
Wazazi Wakristo wanapaswa kutambua kwamba wana wajibu wa
kuwafundisha na kuwalea watoto wao, kama tunavyosoma katika Mithali
22:6, kwamba: “
Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee” (maneno
mepesi kukazia).
Kulea (au kufundisha) si kuadhibu tu mtoto anapoacha
kutii, bali ni kumpongeza pia wakati anapofanya vizuri. Watoto kila
wakati wanahitaji kusifiwa na wazazi wao ili kuunga mkono tabia zao
njema, na mambo mazuri wanayofanya. Watoto wanahitaji kuhakikishiwa mara
kwa mara kwamba wanapenda, wanakubalika na kufurahiwa na wazazi wao.
Wazazi wanaweza kuonyesha upendo wao kwa kusifu, kuwakumbatia na
kuwabusu watoto, na kwa kutumia muda mwingi nao.
“Kulea” maana yake “kufanya atii.” Basi, wazazi Wakristo
wasiwape watoto wao uchaguzi kama watakwenda kanisani au kuomba kila
siku au hapana. Watoto hawana ufahamu wa kutosha kujua kinachowafaa, au
kilicho bora. Ndiyo sababu Mungu aliwapa wazazi. Wazazi watakaofanya
bidii na kuweka juhudi na nguvu zao kuhakikisha kwamba watoto wao
wanalelewa vizuri, wana ahadi kutoka kwa Mungu kwamba watoto wao
hawataacha njia iliyo sawa hata wakiwa wakubwa, kama tulivyosoma katika
Mithali 22:6.
Pia, watoto wanapaswa kuongezewa majukumu wanavyozidi
kukua. Lengo la mzazi mwenye kufanikiwa ni kumwandaa mtoto hatua kwa
hatua ili kuwajibika kabisa akiwa mtu mzima. Mtoto anapozidi kukua,
apewe uhuru zaidi wa kujiamulia mambo yake mwenyewe. Tena, yule kijana
mkubwa anapaswa kuelewa kwamba daima akubali wajibu utokanao na maamuzi
yake, na kwamba wazazi wake hawatakuwepo siku zote “kumwokoa” katika
matatizo.
Kama tusomavyo katika Waefeso 6:4, akina baba si tu kwamba wanawajibika kuwafundisha adabu watoto wao, bali pia wanatazamiwa
kuwafundisha katika
Bwana. Si wajibu wa kanisa kumpa mtoto mafundisho kuhusu maadili ya
KiBiblia, tabia za Kikristo au theolojia – ni kazi ya baba. Wazazi
wanaoachia wajibu wote kwa mwalimu wa Shule ya Jumapili awafundishe
watoto wao kuhusu Mungu wanakosea sana. Mungu aliwaamuru Waisraeli hivi,
kwa njia ya Musa:
Na maneno haya ninayokuamuru leo yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo (Kumbu. 6:6, 7. Maneno mepesi kukazia).
Wazazi Wakristo wawafundishe watoto wao kuhusu Mungu
tangu wakiwa wadogo, wakiwaambia Yeye ni nani na anawapenda kiasi gani.
Watoto wadogo wafundishe habari za kuzaliwa kwa Yesu, maisha Yake, kifo
na kufufuka Kwake. Watoto wengi wanaweza kuelewa ujumbe wa Injili
wanapokuwa na umri wa miaka mitano au sita, na wanaweza kufanya uamuzi
wa kumfuata Kristo. Baada ya hivyo (wakiwa na miaka sita au saba, na
wakati mwingine hata wakiwa wadogo zaidi), wanaweza kupokea ubatizo wa
Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha kama ishara kwamba wamejazwa. Pamoja
na hayo, hatuwezi kuweka sheria kuhusu jambo hili kwa sababu kila mtoto
yuko tofauti. Ila hoja ni kwamba, wazazi Wakristo wanapaswa kutoa nafasi
ya kwanza kwenye kuwafundisha watoto wao mambo ya kiroho.
1). Usiwatie watoto wako mahali pagumu (ona Waefeso 6:4). Watoto
wasitazamiwe kutenda kama watu wazima. Ukitazamia mengi kupita kiasi
kutoka kwa watoto wako, wataacha kujitahidi kukupendeza maana wanajua
haiwezekani.
2). Usilinganishe watoto wako na watoto wengine. Wajulishe jinsi unavyofurahia sifa zao za kipekee na karama au vipaji vyao kutoka kwa Mungu. Wakubali wao kama wao.
3). Wape majukumu nyumbani, ili wajue kwamba wao
ni sehemu muhimu sana ya familia hiyo. Kufanikiwa ni matofali
yanayojenga kujiamini katika maisha ya mtu.
4). Tumia muda kuwa na watoto wako. Hiyo
inawajulisha kwamba wao ni wa maana kwako. Kuwapa vitu haichukui nafasi
ya wewe kujitoa kwao. Tena, watoto hushawishiwa zaidi na wale wanaokaa
nao muda mwingi.
5). Ikibidi useme kitu kibaya, jaribu kukisema kwa uzuri. Mimi
sikuwahi kuwaambia watoto wangu kwamba ni “wabaya” walipoacha kunitii.
Badala yake, nilikuwa namwambia hivi kijana wangu, “Wewe ni mtoto mzuri,
na watoto wazuri hawafanyi ulichofanya!” (Kisha nilikuwa namchapa
kiboko.)
6). Tambua kwamba, neno “hapana” linamaanisha “ninakujali”. Watoto wanaporuhusiwa mambo yao kila wakati wanatambua kwama hujali kiasi cha kutosha kuwakataza chochote wakati wowote.
7). Tazamia watoto wako kukuiga wewe. Watoto
hujifunza kwa mifano ya wazazi wao. Mzazi mwenye busara hawezi kumwambia
mtoto wake, “Fanya ninavyokwambia. Usifanye kama ninavyofanya mimi.”
8). Usiwaokoe watoto wako na matatizo yao yote. Ondoa mawe yanayoweza kuwakwaza tu; acha mawe ya kukanyagia yabakie mbele yao.
9). Mtumikie (na kumfuata) Mungu kwa moyo wako wote. Nimeona
kwamba watoto wa wazazi waliopoa kiroho huwa hawamfuati Mungu wakiwa
watu wazima. Watoto Wakristo wa wazazi ambao hawajaokoka, na watoto wa
wazazi Wakristo waliojitoa kabisa kwa Mungu huendelea na wokovu hata
“wakiondoka kwenye kiota” – nyumbani.
10). Wafundishe watoto wako Neno la Mungu. Mara
nyingi wazazi hutoa nafasi ya kwanza kwa elimu ya watoto wao, na
kushindwa kuwapa elimu ya muhimu zaidi wanayoweza kupata – elimu ya
Biblia.
Pengine kosa kubwa la kawaida kabisa lifanywalo na
viongozi wa Kikristo ni kutokujali ndoa zao na familia zao kwa sababu ya
kujitoa kwenye huduma. Wanajihesabia haki kwa kusema kwamba kujitoa
kwao “ni kwa ajili ya kazi ya Bwana.”
Kosa hili hurekebika wakati mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anapotambua kwamba
utii
wake halisi na kujitoa kwake kwa Mungu huonekana kwa mahusiano yake na
mke wake na watoto. Mtumishi hawezi kudai kwamba amejitoa kwa Mungu
ikiwa hampendi mke wake kama Kristo anavyolipenda kanisa, au kama
atapuuzia kutumia muda unaotakiwa na watoto wake, ili kuwalea na
kuwakuza katika kicho na kumcha Bwana.
Tena, kumpuuza mwenzi na watoto kwa sababu ya “huduma” ni
ishara ya huduma ya kimwili kabisa, inayofanywa kwa nguvu za mtu
binafsi. Wachungaji wengi wenye makanisa wanaobeba mizigo mizito ni
mfano wa hili, maana wanajichosha ili kuhakikisha kwamba kila utaratibu
wa kanisa unakwenda vizuri.
Yesu aliahidi kwamba mzigo Wake ni mwepesi na nira Yake
ni laini (ona Mathayo 11:30). Hamwiti mtumishi yeyote kuonyesha
anavyopenda dunia au anavyolipenda kanisa kwa kutowapenda watu wa
familia yake. Sifa mojawapo ya mzee ni kwamba, “awe mwenye kuisimamia
nyumba yake vema” (1Timo. 3:4). Mahusiano yake na familia yake ni kipimo
cha uwezo wake kufanya huduma.
Wale walioitwa kufanya huduma za kusafiri na ambao
inawabidi kuwa nje ya nyumbani mara kwa mara lazima watumie muda wa
ziada kufikiri kuhusu familia zao wanapokuwa nyumbani. Washirika wengine
katika mwili wa Kristo wafanye kinachowezekana ili kufanikisha hilo.
Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anatambua kwamba watoto wake
mwenyewe ndiyo wanafunzi wake wa kwanza. Akishindwa hapo, hana haki ya
kujaribu kuwafundisha wengine walio nje ya nyumbani mwake kuwa
wanafunzi.