Monday, October 6, 2014

Maporomoko ya Rusumo - Ngara

haya maporomoko ni ya maji Rusumo Falls
Mto huu unatokea upande wa Tanzania kuingia kwenye haya maporomoko
Maporomoko ya Rusumo-Ngara
Mungu azidi kushukuriwa na kutukuzwa kwa uumbaji




Kipa wa JKT Ruvu, Jackson Chove akiruka juu kuokoa hatari langoni mwake. Ambapo Hii Leo October 05,2014, huko Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, Yanga SC wameichapa JKT Ruvu Bao 2-1 na kukwea hadi Nafasi ya 3 ya Ligi Kuu Vodacom
Yanga walifunga Bao lao la kwanza Dakika ya 32 kupitia Kelvin Yondani na Bao hilo kudumu hadi Haftaimu.

 Dakika ya 73, Haruna Niyonzima aliipatia Yanga SC Bao la Pili lakini JKT Ruvu walipata Bao lao moja katika Dakika za mwishoni Mfungaji akiwa Jabir Aziz.


KONGAMANO NA UJIRANI MWEMA

Kongamano hili litakuwa la Mkesha washiriki watatakiwa kuwasili Parokiani Boko siku ya Ijumaa tarehe 28/11/2014 saa tisa alasiri,na tunatarajia kuwa na semina na midahalo kwa usiku mzima, jumamosi ya tarehe 29/11/2014, saa kumi alasiri washiriki wote watarejea majumbani kwao baada ya kushibishwa kwa semina, midaho na michezo.

Washiriki kwenye Kongamano hili ni Vijana wote wenye Umri kuanzia miaka kumi na nane(18) wa Parokia ya Boko, Bunju na  Vijana wengine kutoka kwenye Parokia Mbali mbali za Jimbo kuu la Dar es  .
MWAKA WA FAMILIA.
Inafurahisha kuona kwamba, wazee wawili na vijana wawili wanakutanishwa na Yesu. Hii
inaonesha kwamba, Yesu ana uwezo wa kukutanisha na kuunganisha vizazi, kwani Yeye ni
chemchemi ya upendo inayovuka ubinafsi, upweke na masikitiko. Baba Mtakatifu anasema,
familia katika hija ya maisha yao wanashirikishana na kumegeana mambo mengi mema:
chakula na mapumziko; kazi za nyumbani, starehe, sala, safari na hija ya maisha ya kiroho
pamoja na matendo ya huruma.
Pale panapokosekana upendo, hapo hukosekana furaha , Upendo wa kweli
unabubujika kutoka kwa Kristo kwa njia ya Neno lake ambalo ni mwanga katika mapito ya
waamini; anawapatia Mkate wa maisha ya uzima wa milele, unaowasaidia waamini kupambana
na changamoto za maisha ya kila siku.
Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya
Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2014 mjini Vatican, kwa
kuongozwa na kauli mbiu "Changamoto za kichungaji kuhusu familia mintarafu Uinjilishaji"
ameandika barua kwa familia zote duniani ili kukazia dhamana ya Kanisa kuendelea kutangaza
Injili kwa kukabiliana kinaga ubaga na changamoto mpya zinazohusu familia.
Baba Mtakatifu anasema, maandalizi haya yanawahusu Watu wote wa Mungu kwa kuhakikisha
kwamba, wanashiriki kikamilifu kwa kutoa mawazo pamoja na kusindikiza mchakato mzima kwa
njia ya sala, jambo muhimu sana kutoka kwa familia zote. Sinodi hii ni maalum kwa ajili ya: wito
na utume wa Kanisa na Jamii; matatizo yanayowakabili wanandoa; maisha ya kifamilia, elimu
na malezi kwa watoto; dhamana na utume wa familia katika maisha ya Kanisa.
Hivyo nakualika kijana mwenzangu uungane nasi hiyo siku katika kuyachambua haya kwa kina anza sasa kufanya maandalizi

ELIMU YA UJASIRIAMALI.
Elimu ya ujasiriamali katika nchi yetu haina ‘umri’ mkubwa kama zilivyo taaluma nyingine zikiwamo lugha, historia, siasa na sayansi. Hii ni kutokana na historia ya nchi yetu hasa baada ya kupata uhuru, kwamba tuliamua kufuata siasa ya ujamaa na kujitegemea kupitia Azimio la Arusha.
Siasa ya ujamaa na kujitegemea haikushadidia ujasiriamali kwa vile ulifananishwa na ubepari ambao ulichukuliwa kama unyama. Wale wote waliokuwa wanajihusisha na shughuli za kijasiriamali hasa biashara katika kipindi hicho walionekana kama ‘wanyama’ au watu ambao walikuwa wamechepuka kutoka katika njia kuu ambayo ilikuwa inaaminiwa na jamii kubwa wakati huo.
Wafanyakazi serikalini walikuwa hawaruhusiwi kujihusisha na biashara na kwamba shughuli za ujasiriamali zilionekana kufanywa na watu ambao hawakuwa na elimu ya kutosha kupata ajira, na wageni hasa kutoka Bara la Asia kama vile Wahindi.
Hata hivyo, kutokana na hali halisi ya maisha katika nchi yetu na duniani kwa jumla, kwenye miaka ya katikati ya 2000, taifa lilianza utaratibu wa kuingiza elimu ya ujasiriamali katika elimu ingawa haikuwekewa kipaumbele sana. Kwa sasa elimu ya ujasiriamali imekuwa kama wimbo wa taifa, siyo shuleni na vyuoni bali hata katika sekta ambazo si rasmi kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia matangazo mbalimbali juu ya kuendesha elimu ya ujasirimali katika makundi mbalimbali ya jamii yetu.
Kutokana na wanajamii na taifa kwa jumla kuanza kuona elimu ya ujasiriamali kama mwarobaini wa matatizo yanayowakabili kama vile ajira na umaskini, lengo la la Kongamano letu  ni kuelezea umuhimu wa elimu ya ujasiriamali katika Chama chetu cha VIWAWA  kama njia mojawapo yenye kuonyesha jinsi elimu ya ujasiriamali inavyoweza kuisaidia jamii na taifa katika kuleta maendeleo.
Ujasiriamali ni mchakato au hali waliyonayo baadhi ya watu ya kutaka mafanikio yanayoshadadiwa na moyo wa ushindani, kujiamini, uwezo binafsi wa kukabiliana na kutatua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na uthubutu wa kukabiliana na changamoto ambazo wakati mwingine huweza kuathiri maisha yao katika kipindi cha mpito.
Kumekuwa na mjadala wa muda mrefu kama ujasiriamali hufundishwa au mtu huzaliwa nao ingawa si lengo la kongamano letu si kujikita katika mjadala huo, kwa kuwa tunaelewa nguvu iliyonayo elimu katika kuyatengeneza maisha ya mwanadamu.
Tunaamini kuwa vijana wana maono na matamanio yao katika maisha kama walivyo watu wazima ingawa watu hawa wawili wanaweza kutofautiana hapa na pale kutokana na sababu za umri, mazingira, wakati na uzoefu katika maisha.
Elimu ya ujasiriamali katika Vyama au kikundi  hujenga msingi mzuri wa kujiamini miongoni mwa vijana na hivyo kuwafanya wayakabili maisha bila woga, jambo ambalo litawafanya kufanya kazi zao wanazozipenda kwa umahiri, weledi na kujiamini zaidi.
hivyo basi nakusi sana kuungana nasi katika kupata elimu hiyo, tunatarajia pia kuunda vikundi vya ujasiriamali kwa vijana watano watano na kuwapatia wataalamu watakao wasimamia.
kwa maelezo zaidi tuandikie kupitia viwawaboko@yahoo.com au piga 0713 900 905


Sunday, October 5, 2014

Maomo ya tarehe 05 October 2014 dominika ya 27 Mwaka "A" wa kanisa

05
 October
 JUMAPILI YA 27 YA MWAKA "A" 2014.


RATIBA ZA IBADA

KIGANGO CHA BOKO.
Kutakuwa na ibada ya Kipaimara itakuwa saa 5:00 asubuhi na itaongozwa na Askofu Mdoe.

IBADA YA MISA YA KWANZA 12:15 – 1:45 ASUBUHI.

IBADA YA MISA YA PILI 2:00 – 3:50 ASUBUHI.

KIGANGO CHA MBWENI.
Kutakuwa na Ibada moja saa: 1:15 – 2:55 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. RAFAEL.
Ibada itakuwa Moja tu: 1:00 – 2:55 ASUBUHI

KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA – MBWENI MPIJI.
IBADA itakuwa asubuhi;

SOMO  1. Isa. 5:1-7

Somo katika  kitabu cha Nabii Isaya.
Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi 

wangu katika habari za shamba lake la mizabibu.
Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, 
Kilimani penye kuzaa sana; 
Akafanya handaki kulizunguka pande zote, 
Akatoa mawe yake, 
Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri,
Akajenga mnara katikati yake, 
Akachimba shinikizo ndani yake;
Akatumaini ya kuwa utazaa mzabibu, 
Nao ukaza zabibu-mwitu. 
Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu. Je! ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu? Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa kitalu chake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa; nami nitaliharibu, wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake. kwa maana shamba la mizabibu la Bwana wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! alisikia kilio.


SOMO  2. Flp. 4:6-9
Somo katika waraka wa mtume Paulo kwa Wafilipi.
Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zujulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu,  mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote. yatafakarini hayo. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.



  INJILI.Mt. 21:33-43

Somo katika Injili ilivyoandikwa na Mathayo.


Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu, Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe, Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza, wakawatenda vile vile. Mwishowe akamtuma mwanae kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. wakamkamata wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule Bwana wa shamba la mizabibu. atawatendaje wale wakulima? wakamwambia, Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake. Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko,
Jiwe walilolikataa waashi,
Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni;
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu?
kwa sababu hiyo nawaambia, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake.

Matangazo


 
 

 


Thursday, October 2, 2014

FAMILIA YA KIKRISTO

Nafasi Ya Mume Na Mke

Mungu amepanga kwamba familia ya Kikristo iwe katika mfumo fulani. Kwa sababu mfumo huo unaleta uthabiti katika maisha ya familia, Shetani hufanya kazi sana kupotosha mpango aliokusudia Mungu.
Kwanza kabisa ni kwamba, Mungu amepanga mume awe kichwa cha familia. Hii haimpi mume ruhusa ya kutawala mke wake na watoto katika ubinafsi. Mungu amewaita waume kupenda, kulinda, kutimiza mahitaji na kuongoza familia zao kama kichwa. Pia, Mungu alikusudia wake wawe watiifu kwa uongozi wa waume zao. Hili ni wazi, kama Maandiko yanavyosema.
Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo (Waefeso 5:22-24).
Mume si kichwa wa mkewe kiroho – Yesu ndiye mwenye nafasi hiyo. Yesu ni kichwa wa kanisa kiroho, na mke wa Kikristo ni mshirika wa kanisa sawa na mume wake ambaye ni Mkristo pia. Ila, katika familia, mume Mkristo ndiye kichwa wa mke wake na watoto, nao wanapaswa kutii na kunyenyekea mamlaka yake hayo aliyopewa na Mungu.
Je, mke anapaswa kumtii mumewe kwa kiwango gani? Kama Paulo anavyosema, ni katika kila jambo. Wakati pekee anaporuhusiwa kuvunja sheria hiyo ni kama mume wake anamtaka kuvunja Neno la Mungu au kufanya kitu ambacho kinapinganana dhamiri yake. Ni wazi kwamba hakuna mume Mkristo atakayemtaka mke wake kufanya chochote kinachovunja Neno la Mungu au kwenda kinyume na dhamiri yake. Mume si Bwana kwa mkewe – Yesu tu ndiye mwenye nafasi hiyo maishani mwake. Kama itafikia uchaguzi kuhusu nani wa kumtii, anapaswa kuchagua kumtii Yesu.
Waume wanapaswa kukumbuka kwamba Mungu hayuko upande wao mara zote. Kuna wakati ambapo Mungu alimwambia Ibrahimu afanye kama alivyoambiwa na Sara mkewe (ona Mwanzo 21:10-12). Maandiko pia yanataja jinsi Abigaili alivyoacha kumtii Nabali mumewe, aliyekuwa mpumbavu, na kwa kufanya hivyo aliepusha tatizo (ona 1Samweli 25:2 – 38).

Neno La Mungu Kwa Wanaume

Mungu anawaambia hivi waume:
Enyi waume, wapendeni wake zetu kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake… Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe, maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. … Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe (Waefeso 5:25, 28-30, 33).
Waume wanaagizwa kuwapenda wake zao kama Kristo anavyolipenda Kanisa. Si wajibu mdogo huo! Mke yeyote atajinyenyekeza kwa furaha kabisa kwa mtu anayempenda kama Yesu – aliyetoa uhai Wake kwa sababu ya upendo wa kujitoa. Sawa na jinsi Kristo anavyoupenda mwili Wake – yaani Kanisa – ndivyo na waume wanavyotakiwa kumpenda mwanamke ambaye ni “mwili mmoja” nao (Waefeso 5:31). Kama mume Mkristo anampenda mkewe kama anavyopaswa, atamtimizia mahitaji yake, atamtunza, atamheshimu, atamsaidia, atamtia moyo, na atatumia muda kuwa naye. Akishindwa katika wajibu wake kumpenda mkewe, mume huyo yuko hatarini kuzuia majibu ya maombi yake mwenyewe.
Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima kama chombo kisicho na nguvu na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe (1Petro 3:7. Maneno mepesi kukazia).
Kihalisi ni kwamba hapajawahi kuwepo na ndoa isiyokuwa na kutokuelewana na shida mbalimbali. Ila, kwa kujitoa na kukuza tunda la Roho katika maisha yetu, waume na wake wanaweza kujifunza kuishi kwa maelewano na amani, na kufikia mahali pa kutambua baraka zinazozidi kuongezeka za ndoa ya Kikristo. Kila mwenzi anaweza kukua na kufikia ukomavu mkubwa katika kufanana na Kristo kutokana na matatizo yasiyoepukika yanayotokea katika ndoa zote.
Kwa maelezo zaidi juu ya wajibu na majukumu ya waume na wake, tazama Mwanzo 2:15-25; Mithali 19:13; 21:9, 19; 27:15, 16; 31:10-31; 1Wakor. 11:3; 13:1-8; Wakolosai 3:18, 19; 1Timo. 3:4, 5; Tito 2:3-5; 1Petro 3:1-7.

Tendo La Ndoa

Mungu ndiye mwanzilishi wa tendo la ndoa, na ni dhahiri kwamba aliliumba ili kustarehesha na kusaidia katika uumbaji. Pamoja na hayo, Biblia inatamka wazi kwamba tendo la ndoa ni la kufurahiwa na wale walioungana pamoja katika agano la ndoa, la kudumu.
Kukutana kimwili nje ya mipaka ya ndoa huitwa zinaa au uasherati. Mtume Paulo alisema kwamba wale watendao mambo kama hayo hawataurithi ufalme wa Mungu (ona 1Wakor. 6:9-11). Ingawa Mkristo anaweza kujaribiwa na pengine kufikia kuanguka katika tendo la uzinzi au uasherati, atajisikia hatia kubwa sana rohoni mwake, itakayompelekea kutubu.
Paulo pia alitoa mafundisho wazi kabisa kuhusu majukumu ya mume na mke kwa mwenzake, kuhusu tendo la ndoa.
Lakini kwa sababu ya zinaa, kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe. Vivyo hivyo, mume hana amari juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu (1Wakor. 7:2-5).
Mistari hii inaweka wazi kabisa kwamba tendo la ndoa lisitumiwe kama “zawadi” na mume au mke, maana hakuna mwenye mamlaka juuya mwili wake mwenyewe.
Tena, tendo la ndoa ni zawadi kutoka kwa Mungu. Si dhambi wala najisi inapokuwa katika ndoa. Paulo aliwatia moyo Wakristo wenye ndoa kushirikiana kimwili. Tena, tunapata ushauri huu kwa waume Wakristo katika kitabu cha Mithali:
Chemchemi yako ibarikiwe; nawe umfurahie mke wa ujana wako. Ni ayala apendaye na paa apendezaye; maziwa yake ytakutoshe siku zote; na kwa upendo wake ushangilie daima (Mithali 5:18, 19).[1]
Kama wanandoa Wakristo wanataka kufurahia mahusiano kimwili yenye kutosheleza, waume na wake wanahitaji kuelewa kwamba kuna tofauti kubwa sana kati ya wanaume na wanawake kwa habari ya kushirikiana kimwili. Kiasili, mwanamume ni mtu wa kimwili sana kwa habari ya kukutana kimwili. Asili ya mwanamke kwa habari ya kukutana kimwili ni kitu cha hisia. Wanaume husisimka na kuwa tayari kukutana kimwili na mwanamke kwa kuona tu (ona Mathayo 5:28). Wanawake wao husisimka na kuwa tayari kukutana kimwili kwa mahusiano ya karibu sana, na kwa kuguswa na kushikwa-shikwa (ona 1Wakor. 7:1). Wanaume huvutiwa na wanawake wanaowapendeza macho; ila wanawake huvutiwa na wanaume wanaowapendeza kwa sababu zaidi ya kuvutia kimwili. Hivyo, wanawake wenye busara hupendeza ili kuwavutia waume zao wakati wote. Na waume wenye hekima huonyesha upendo wao kwa wake zao kutwa nzima kwa kuwakumbatia na kuwatendea mambo ya ukarimu, badala ya kuwatazamia wake zao “kuwa tayari” kwa ghafula wakati wa usiku.
Kiwango cha ashiki ya mwanamume kukutana kimwili na mwenzake huongezeka kulingana na kuongezeka kwa mbegu za uzazi katika mwili wake. Kiwango cha ashiki ya mwanamke huongezeka au kupungua kutegemeana na siku zake za mwezi. Wanaume wana uwezo wa kusisimka na kuwa tayari kukutana kimwili na mwanamke, na kufikia kilele cha tendo la ndoa baada ya muda mfupi sana – nukta chache tu au dakika, ila wanawake huchukua muda mrefu. Ingawa mwanamume yuko tayari kimwili kukutana na mwanamke upesi sana, mwili wa mwanamke unaweza usiwe tayari, mpaka baada ya nusu saa au zaidi. Basi, waume wenye hekima huchukua muda katika kuanza kuwasisimua wenzao kwa kuwapapasa, kuwabusu na kuwashika-shika sehemu za mwili ambazo zinasisimua, ili kumsababisha mwanamke kuwa tayari kukutana kimwili. Ikiwa hajui sehemu zinazohusika, amwulize. Tena, anapaswa kujua kwamba, japo yeye anaweza kufikia kilele cha tendo la ndoa mara moja tu, mwenzake anaweza kufikia kilele cha tendo la ndoa mara nyingi. Mume anapaswa kuhakikisha kwamba mwenzake anapokea anachotaka.
Ni muhimu sana kwa waume Wakristo na wake zao kuzungumza kuhusu mahitaji yao kwa uwazi, na kujifunza juu ya tofauti zao kiasi wanachoweza. Mahusiano kimwili kati ya waume na wake yanaweza kuwa baraka inayozidi kuongezeka kutokana na mawasiliano ya miezi mingi na miaka, na kugunduana na kuzoeana.

Watoto Wa Familia Ya Kikristo

Watoto wanapaswa kufundishwa jinsi ya kunyenyekea na kutii kabisa wazazi wao Wakristo. Wakifanya hivyo, wameahidiwa maisha marefu na baraka zao.
Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia (Waefeso 6:1-3).
Akina baba Wakristo kama vichwa wa familia zao, wanapewa wajibu wa msingi kabisa kwa ajili ya kuwafundisha watoto wao, hivi:
Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana (Waefeso 6:4).
Ona kwamba wajibu wa baba ni wa namna mbili: kuwalea watoto wake katika adabu na maonyo ya Bwana. Hebu tuanze kwa kutazama haja ya kuwafundisha watoto adabu.

Nidhamu Ya Watoto

Mtoto asiyetiwa nidhamu atakapokuwa mtu mzima atakuwa mbinafsi na muasi kwa mamlaka. Watoto wanapaswa kutiwa nidhamu wakati wowote wanapoacha kwa makusudi kutii sheria halali zilizowekwa na wazazi wao. Watoto wasiadhibiwe kwa makosa au kutowajibika kwa sababu ya utoto. Lakini, watakiwe kukabiliana na matokeo ya makosa yao na kutowajibika kwao, na kwa njia hiyo kuwasaidia kujiandaa kwa ajili ya uhalisi wa maisha ya utu uzima.
Watoto wadogo wanapaswa kuadhibiwa kwa kiboko, kama Neno la Mungu linavyofundisha. Lakini watoto wachanga wasipigwe viboko. Hii haina maana kwamba watoto wachanga waruhusiwe kufanya wanachotaka. Inatakiwa tangu wanapozaliwa wajue kwamba mama na baba ndiyo wenye mamlaka. Wanaweza kufundishwa wakiwa wadogo sana maana ya neno “hapana” kuwakuwakataza tu kufanya kitu wanachofanya, au wanachotaka kufanya. Wakianza kuelewa maana ya neno “hapana”, wanaweza kuchapwa kofi dogo tu matakoni ili kuwasaidia kuelewa vizuri zaidi wanapoendelea kufanya kile ambacho wazazi wanasema kisifanywe. Kama hayo yatafanyika kwa utaratibu na mara kwa mara, watoto watajifunza kuwa watiifu tangu umri mdogo sana.
Pia, wazazi wanaweza kuonyesha mamlaka yao kwa kutounga mkono tabia zisizotakiwa za watoto wao. Mfano ni kuwapa mara moja kitu wanachotaka, wakilia. Kufanya hivyo ni kuwafundisha watoto walie ili wapate matakwa yao. Au, kama wazazi watakubaliana na madai ya watoto wao kila mara wanaponuna au kukasirika ni kwamba wanawatia moyo kuendelea na tabia hiyo isiyotakiwa. Wazazi wenye hekima huunga mkono tabia nzuri tu katika watoto wao.
Kuchapa kiboko kusilete madhara kimwili, ila kusababishe maumivu ya kutosha kumfanya mtoto yule asiyetii kulia kwa muda kidogo. Kwa njia hiyo, mtoto atajifunza kuunganisha uchungu na kutokutii. Hata Biblia inaunga mkono hilo.
Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; bali yeye ampendaye humrudi mapema. … Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto; lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali. … Usimnyime mtoto wako mapigo; maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. Utampiga kwa fimbo, na kumwokoa nafasi yake na Kuzimu. … Fimbo na maonyo hutia hekima; bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye (Mithali 13:24; 22:15; 23:13-14; 29:15).
Wazazi wanaposimamia sheria zao, hawana haja ya kuwatisha watoto ili kuwafanya watii Mtoto anapoacha kutii kwa makusudi, achapwe fimbo. Ikiwa mzazi atatishia tu kumchapa mtoto wake ambaye si mtii, anachofanya ni kuunga mkono uasi wa mtoto wake. Matokeo ni kwamba mtoto anajifunza kutokujali utii mpaka vitisho vya wazazi wake vya maneno vinapofikia kiwango fulani cha sauti.
Baada ya kiboko, mtoto anapaswa kukumbatiwa na kuhakikishiwa upendo wa mzazi aliyemchapa.

Mlee Mtoto

Wazazi Wakristo wanapaswa kutambua kwamba wana wajibu wa kuwafundisha na kuwalea watoto wao, kama tunavyosoma katika Mithali 22:6, kwamba: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee” (maneno mepesi kukazia).
Kulea (au kufundisha) si kuadhibu tu mtoto anapoacha kutii, bali ni kumpongeza pia wakati anapofanya vizuri. Watoto kila wakati wanahitaji kusifiwa na wazazi wao ili kuunga mkono tabia zao njema, na mambo mazuri wanayofanya. Watoto wanahitaji kuhakikishiwa mara kwa mara kwamba wanapenda, wanakubalika na kufurahiwa na wazazi wao. Wazazi wanaweza kuonyesha upendo wao kwa kusifu, kuwakumbatia na kuwabusu watoto, na kwa kutumia muda mwingi nao.
“Kulea” maana yake “kufanya atii.” Basi, wazazi Wakristo wasiwape watoto wao uchaguzi kama watakwenda kanisani au kuomba kila siku au hapana. Watoto hawana ufahamu wa kutosha kujua kinachowafaa, au kilicho bora. Ndiyo sababu Mungu aliwapa wazazi. Wazazi watakaofanya bidii na kuweka juhudi na nguvu zao kuhakikisha kwamba watoto wao wanalelewa vizuri, wana ahadi kutoka kwa Mungu kwamba watoto wao hawataacha njia iliyo sawa hata wakiwa wakubwa, kama tulivyosoma katika Mithali 22:6.
Pia, watoto wanapaswa kuongezewa majukumu wanavyozidi kukua. Lengo la mzazi mwenye kufanikiwa ni kumwandaa mtoto hatua kwa hatua ili kuwajibika kabisa akiwa mtu mzima. Mtoto anapozidi kukua, apewe uhuru zaidi wa kujiamulia mambo yake mwenyewe. Tena, yule kijana mkubwa anapaswa kuelewa kwamba daima akubali wajibu utokanao na maamuzi yake, na kwamba wazazi wake hawatakuwepo siku zote “kumwokoa” katika matatizo.

Wajibu Wa Wazazi Kufundisha

Kama tusomavyo katika Waefeso 6:4, akina baba si tu kwamba wanawajibika kuwafundisha adabu watoto wao, bali pia wanatazamiwa kuwafundisha katika Bwana. Si wajibu wa kanisa kumpa mtoto mafundisho kuhusu maadili ya KiBiblia, tabia za Kikristo au theolojia – ni kazi ya baba. Wazazi wanaoachia wajibu wote kwa mwalimu wa Shule ya Jumapili awafundishe watoto wao kuhusu Mungu wanakosea sana. Mungu aliwaamuru Waisraeli hivi, kwa njia ya Musa:
Na maneno haya ninayokuamuru leo yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo (Kumbu. 6:6, 7. Maneno mepesi kukazia).
Wazazi Wakristo wawafundishe watoto wao kuhusu Mungu tangu wakiwa wadogo, wakiwaambia Yeye ni nani na anawapenda kiasi gani. Watoto wadogo wafundishe habari za kuzaliwa kwa Yesu, maisha Yake, kifo na kufufuka Kwake. Watoto wengi wanaweza kuelewa ujumbe wa Injili wanapokuwa na umri wa miaka mitano au sita, na wanaweza kufanya uamuzi wa kumfuata Kristo. Baada ya hivyo (wakiwa na miaka sita au saba, na wakati mwingine hata wakiwa wadogo zaidi), wanaweza kupokea ubatizo wa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha kama ishara kwamba wamejazwa. Pamoja na hayo, hatuwezi kuweka sheria kuhusu jambo hili kwa sababu kila mtoto yuko tofauti. Ila hoja ni kwamba, wazazi Wakristo wanapaswa kutoa nafasi ya kwanza kwenye kuwafundisha watoto wao mambo ya kiroho.

Amri Kumi Za Kuwapenda Watoto Wako

1). Usiwatie watoto wako mahali pagumu (ona Waefeso 6:4). Watoto wasitazamiwe kutenda kama watu wazima. Ukitazamia mengi kupita kiasi kutoka kwa watoto wako, wataacha kujitahidi kukupendeza maana wanajua haiwezekani.
2). Usilinganishe watoto wako na watoto wengine. Wajulishe jinsi unavyofurahia sifa zao za kipekee na karama au vipaji vyao kutoka kwa Mungu. Wakubali wao kama wao.
3). Wape majukumu nyumbani, ili wajue kwamba wao ni sehemu muhimu sana ya familia hiyo. Kufanikiwa ni matofali yanayojenga kujiamini katika maisha ya mtu.
4). Tumia muda kuwa na watoto wako. Hiyo inawajulisha kwamba wao ni wa maana kwako. Kuwapa vitu haichukui nafasi ya wewe kujitoa kwao. Tena, watoto hushawishiwa zaidi na wale wanaokaa nao muda mwingi.
5). Ikibidi useme kitu kibaya, jaribu kukisema kwa uzuri. Mimi sikuwahi kuwaambia watoto wangu kwamba ni “wabaya” walipoacha kunitii. Badala yake, nilikuwa namwambia hivi kijana wangu, “Wewe ni mtoto mzuri, na watoto wazuri hawafanyi ulichofanya!” (Kisha nilikuwa namchapa kiboko.)
6). Tambua kwamba, neno “hapana” linamaanisha “ninakujali”. Watoto wanaporuhusiwa mambo yao kila wakati wanatambua kwama hujali kiasi cha kutosha kuwakataza chochote wakati wowote.
7). Tazamia watoto wako kukuiga wewe. Watoto hujifunza kwa mifano ya wazazi wao. Mzazi mwenye busara hawezi kumwambia mtoto wake, “Fanya ninavyokwambia. Usifanye kama ninavyofanya mimi.”
8). Usiwaokoe watoto wako na matatizo yao yote. Ondoa mawe yanayoweza kuwakwaza tu; acha mawe ya kukanyagia yabakie mbele yao.
9). Mtumikie (na kumfuata) Mungu kwa moyo wako wote. Nimeona kwamba watoto wa wazazi waliopoa kiroho huwa hawamfuati Mungu wakiwa watu wazima. Watoto Wakristo wa wazazi ambao hawajaokoka, na watoto wa wazazi Wakristo waliojitoa kabisa kwa Mungu huendelea na wokovu hata “wakiondoka kwenye kiota” – nyumbani.
10). Wafundishe watoto wako Neno la Mungu. Mara nyingi wazazi hutoa nafasi ya kwanza kwa elimu ya watoto wao, na kushindwa kuwapa elimu ya muhimu zaidi wanayoweza kupata – elimu ya Biblia.

Nafasi Ya Huduma, Ndoa Na Familia

Pengine kosa kubwa la kawaida kabisa lifanywalo na viongozi wa Kikristo ni kutokujali ndoa zao na familia zao kwa sababu ya kujitoa kwenye huduma. Wanajihesabia haki kwa kusema kwamba kujitoa kwao “ni kwa ajili ya kazi ya Bwana.”
Kosa hili hurekebika wakati mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anapotambua kwamba utii wake halisi na kujitoa kwake kwa Mungu huonekana kwa mahusiano yake na mke wake na watoto. Mtumishi hawezi kudai kwamba amejitoa kwa Mungu ikiwa hampendi mke wake kama Kristo anavyolipenda kanisa, au kama atapuuzia kutumia muda unaotakiwa na watoto wake, ili kuwalea na kuwakuza katika kicho na kumcha Bwana.
Tena, kumpuuza mwenzi na watoto kwa sababu ya “huduma” ni ishara ya huduma ya kimwili kabisa, inayofanywa kwa nguvu za mtu binafsi. Wachungaji wengi wenye makanisa wanaobeba mizigo mizito ni mfano wa hili, maana wanajichosha ili kuhakikisha kwamba kila utaratibu wa kanisa unakwenda vizuri.
Yesu aliahidi kwamba mzigo Wake ni mwepesi na nira Yake ni laini (ona Mathayo 11:30). Hamwiti mtumishi yeyote kuonyesha anavyopenda dunia au anavyolipenda kanisa kwa kutowapenda watu wa familia yake. Sifa mojawapo ya mzee ni kwamba, “awe mwenye kuisimamia nyumba yake vema” (1Timo. 3:4). Mahusiano yake na familia yake ni kipimo cha uwezo wake kufanya huduma.
Wale walioitwa kufanya huduma za kusafiri na ambao inawabidi kuwa nje ya nyumbani mara kwa mara lazima watumie muda wa ziada kufikiri kuhusu familia zao wanapokuwa nyumbani. Washirika wengine katika mwili wa Kristo wafanye kinachowezekana ili kufanikisha hilo. Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anatambua kwamba watoto wake mwenyewe ndiyo wanafunzi wake wa kwanza. Akishindwa hapo, hana haki ya kujaribu kuwafundisha wengine walio nje ya nyumbani mwake kuwa wanafunzi.

Monday, September 29, 2014

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA 24 YA MWAKA A, 28SEPTEMBA

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA 24 YA MWAKA A, 28SEPTEMBA



Tunakualika katika tafakari yetu, Dominika ya 24 ya mwaka A wa Kanisa tukilenga kukua katika toba na msamaha wa Mungu ulio wa kudumu. Katika historia, kadiri ya mangamuzi ya watu njia rahisi ya kujibu dhuluma ilikuwa ni kwa njia ya hasira na zaidi jino kwa jino (Kut 21:24) wakijaribu kutafuta mlinganyo sahihi (proportionality to the offence) lakini leo hii kadiri ya somo la kwanza toka kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira tunaalikwa kutawala hasira zetu, kuacha chuki na kuacha kulipiza kisasi maana haya ni machukizo mbele ya Mungu. Ni hali ambayo huongeza taabu katika jumuiya badala ya kupunguza taabu. Basi kama mmoja wetu atashupaa katika haya, naye vivyohivyo atatendewa vivyohivyo yaani atajiondoa katika ufalme wa Mungu. Kumbe ndugu yangu mpendwa, leo tunaalikwa kupiga hatua katika safari ya kiroho tukiunganika na mausia ya Bwana kadiri ya Injili.

Mtume Paulo akiendeleza fundisho tunalolipata katika somo la kwanza anasema sisi hatuishi kwa ajili yetu wenyewe kama watu wenye chuki na visasi waishivyo bali twaishi kwa ajili ya Bwana. Anafundisha hili kwa sababu katika jumuiya ya kirumi mjini Roma kuna utengano kati ya wanaoshika sheria ya kufunga kadiri ya utamaduni wa mwanzo walipopokea imani na wale wanaojiona wa kisasa wanoshika sheria ya mapendo kwa ndugu. Kumbe ili kusahihisha dosari hii Mt. Paulo anasema sisi sote ni mali ya Bwana katika yote na hata tukifa tunakufa katika yeye. Ndiyo kusema matendo, maneno yetu, nyajibu zetu, sheria tunazoshika, familia zetu, parokia zetu, majimbo yetu tunayoyasimamia ni mali ya Kristu. Kwa hivi tuwajibike tukitambua hilo na mwishoni mapenzi ya Mungu yafanyike. Mafundisho ya Mt Paulo ni msaada kwa jumuiya zetu zinapojikuta ziko katika mgongano kwa sababu ya mwono tofauti. Zinaalikwa pande mbili pinzani kuketi na kutatua shida kwa pamoja kwa kuheshimiana.

Tunaendelea bado kutafakari Injili ya Mathayo, na leo Mwinjili atuambia kuwa msamaha ni wa kudumu. Msamaha hauna mipaka bali kama ulivyo upendo unaovumilia basi na msamaha wapaswa kuwa namna hii. Mt Petro akiwa bado katika mawazo ya kiyahudi ya kusamehe kimahesabu, yaani mara saba, anamwuliza Kristu nisamehe mara ngapi ndugu akinikosea? Kristu anakuja na fundisho jipya ya kwamba hakuna tena suala la mahesabu katika kusamehe bali mapenzi ya Mungu yatimizwe daima. Kristu anataka tuondoke katika mazoea ya kila siku na hivi tuingie katika mpango wa milele ambao ni msamaha wa kudumu. Mfano wa mtumwa katika Injili, mtumwa aliyesamehewa deni, deni ambalo asingeweza kulilipa mpaka anakufa kwa hakika ni kielelezo cha huruma ya Mungu iliyo milele!

Pamoja na huruma ya Mungu iliyo milele bado mwanadamu ni dhaifu, haoni vema. Huyu mtumwa aliyesamehewa deni lote yeye mwenyewe hakuweza kuwasamehe wajoli wake. Hiki ni kielelezo cha udhaifu wa mwanadamu ambaye daima hushindwa kusamehe na hasa kosa au dhambi inapojirudia. Ni picha ya kuwa tunahitaji daima huruma ya Mungu. Basi ndugu yangu mpendwa, tukumbuke kuwa kusamehe ni zawadi, ni fadhila tunayopaswa kuiomba daima ili tuweze kuunganika na Kristu mfufuka anayetutaka kusamehe daima na anayesamehe daima. Kinyume cha fadhila hii basi tutakuwa tumejiweka pembeni katika ufalme wa Mbinguni.

Tumalizie tukisema, Suala la kusamehe ni wajibu wa kila mtu awaye yote si wenye mamlaka ya juu tu katika jumuiya bali na wale wanaoongozwa na tukumbuke kuanguka katika dhambi ya kutosamehe na kukuza chuki zisizoisha ni hatari kubwa iliyo mbele yetu. Yaweza kuzuia na hivi tukakosa kuingia mbinguni. Fikiri kidogo mtu asemaye “Mimi nitakapokufa mtu fulani asikaribie na hata kuweka udongo kwenye kaburi langu!! Chuki ya ujazo huu haina maelezo lakini yatishishia usalama wa roho ya mtu huyo aliyefariki!! Tafakari kidogo!Tumwombe Mungu daima atutangulie na kutulinda katika kutekeleza wajibu wa kusamehe. Tumsifu Yesu Kristu.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya Cpps
TAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA 24 YA MWAKA A, 28SEPTEMBA

MASOMO YA JUMAPILI TAREHE 28/09/2014 MWAKA" A" WA KANISA

28
 SEPTEMBER
 JUMAPILI YA 26 YA MWAKA "A" 2014.


RATIBA ZA IBADA

KIGANGO CHA BOKO.
IBADA YA MISA YA KWANZA 12:15 – 1:45 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 2:00 – 3:50 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA TATU SAA 4:00-5:20 ASUBUHI
KIGANGO CHA MBWENI.
IBADA YA MISA YA KWANZA 1:15 – 2:55 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 3:00 – 4:50 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. RAFAEL.
IBADA YA MISA YA KWANZA 1:00 – 2:55 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 3:00 – 4:50 ASUBUHI
KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA – MBWENI MPIJI.
IBADA YA MISA NI 3:00 – 5:00ASUBUHI

SOMO  1. Eze. 18:25-28
Bwana ameniambia hivi: Ninyi mwasema; Njia ya Bwana ni sawa. Sikilizeni sasa, Enyi nyumba ya Israeli; je! njia yangu siyo iliyo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa? Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, atakufa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa. Tenamtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai. kwa sababu atafakari, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa. 

SOMO  2. Flp. 2:1-11


Ikiwako faraja yo yote katika Kristo, yakiwako matulizo yo yote ya mapenzi, ukiwako ushirika wo wote wa Roho, ikiwako huruma yo yote na rehema, ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja, mwenye mapenzi mamoja, mwenye Roho moja, mkinia mamoja. Usitende neon lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa na bora kuliko nafsi yake. kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo yake mwenyewe. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa binadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

  INJILI.Mt. 21:28-32


 Yesu aliwaambia wakuu wa makuhanina wazee, Mwaonaje? mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, mwanangu, leo nenda kafanya kazi katika shamba la mizabibu. Akajibu akasema, Naenda, Bwana;  asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akijibu akasema, sitaki; baadaye akatubu, akaenda. je! katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin, nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini.


Matangazo
jiandaye na Kongamano la ujirani kati ya Parokia ya Boko na bunju' mwema, nunue Ticketi yako sasa kwa Tshs 18,000. Kongamano litafanyika kuanzia tarehe 28-29/11/2014, Parokiani Boko w

 

 

 


NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR