18
Januari
SOMO 1. 1 Sam. 3:3b-10, 19
Samueli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu; basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, mimi hapa. Akamwendea Eli kwa haraka, akasema mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena. Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, sikukuita, mwanangu; kalale tena. Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akamtambua ya kuwa Bwana ndiye alimwita yule mtoto. Kwa hiyo Eli akamwambia Samweli, enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena Bwana; Samweli akaenda akalala mahali pake. Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Samweli akakua, naye Bwana alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lo lote lianguke chini.