Mpendwa somo la kwanza linatoka katika kitabu cha kutoka likiweka mbele yetu amri za Mungu na linatupa mwaliko wa kushika amri hizo. Mungu anaweka amri ili ziwe ni dira ya kuongoza maisha ya watu. Mpendwa kabla ya kuwekwa amri hizi Waisraeli kwa sababu ya kutotii mapenzi ya Mungu walienda utumwani na hivi anapowatoa katika utumwa huo hapendi tena shida hii itokee na hivi anaweka dira na mwongozo wa mapendo yake.
Mpendwa, amri za Mungu hazikuwekwa tu kwa ajili ya kuzishika au kuzikariri bali ni namna ya kujibu mapendo kwa Mungu, ni njia ya kuelekea furaha ya kimungu, ni njia ya kukutana na Mungu atupendaye daima. Amri za Mungu ni namna ya kuongoza maisha ya watu yakae katika msimamo thabiti wa kimaadili ambao huruhusu amani na uelewano kati ya watu. Basi mpendwa unayenisikiliza shikeni amri za Mungu si tu kwa woga bali kama nyenzo, taa, na dira ya maisha yako.
Katika somo la pili, Mtume Paulo anawaandikia Wakorinto akiwataka watambue kuwa wale wote walioitwa na Kristu na watakaoitwa naye baadaye, kwao Kristu ni nguvu na hekima ya Mungu. Fundisho hili linalenga kuvunjilia mbali fikira potofu za Kiyahudi na Kiyunani. Fikira ambazo zilmweka Kristu katika nafasi ya waliolaaniwa na kwamba Mungu ni jambo la kutafuta kwa akili, ni jambo la kifalsafa tu na hivi hakuna haja ya imani.
Basi anakukumbusha wewe pia, kuwa uwe macho na wale wote ambao wanafikiria dini au imani ni jambo la miujiza na maajabu. Anakutahadharisha usije ukaanguka katika falsafa ya ujanjaujanja ambao huiweka imani katika kipimo lelemama yaani kutowajibika kwa sababu hakuna mahakama. Imani yetu, Neno la Mungu ni maisha na hivi yatupasa kuweka chachu ya Injili katika maisha ya kijamii. Dini si njia ya kujipatia kazi bali njia ya kwenda mbinguni.
Katika somo la Injili, Bwana yuko Yerusalemu, na ni muda mfupi umebaki ili pasaka ya Wayahudi iwadie. Anaona jinsi wafanya biashara ambavyo wanahangaikia mambo ya nje yaani biashara na wanasahau hekalu la Baba yake. Wanalifanya hekalu sehemu ya kawaida ambapo mambo ya kidunia yanaweza kusonga mbele! Anawakemea na anasafisha hekalu la Baba yake akisema: “msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara” Bwana anatimiza lile andiko lililonenwa na Nabii Zakaria yakuwa Masiha ajapo hakutakuwa na biashara katika nyumba ya Mungu, Zk 14:21.
Tunafundisha kuondoa ubaya wote moyoni ili Bwana aiingie na kupata kukaa nasi. Atufundisha kuwa mioyo yetu kwa njia ya ubatizo ni hekalu la Mungu, ni kikao cha hekima ya Mungu yaani Roho Mtakatifu. Bwana anatangaza ufalme wa kimasiha na hivi mchanganyo wa uchumi na dini anautupilia mbali.
Sehemu ya pili ya Injili yatufundisha juu ya NGUVU ya BWANA kujenga hekalu kwa siku tatu!, Umungu wake na Habari ya Ufufuko upeo wa wokovu wetu. Anatangaza mwanzo mpya wa ufalme wa Mungu, na anataka wale wote watakaomfuata watambue kuwa hekalu si jengo bali ni ufufuko wa Mwana wa Mungu. Hekalu ni jumuiya ya watu walio na imani ya kweli na wako chini ya Kristu mwenyewe aliye Masiha.
Kumbe mpendwa, ninakusindikizeni daima katika kukua na kutambua wajibu wako wa kusafisha hekalu kwa njia ya kitubio na Ekaristi na kwa namna hiyo Mwana wa Mungu ataweza kuja kwako nawe utazidi kusonga mbele katika safari ya wokovu ukiwa jiwe hai na hekalu safi lisilo na doa.
Nakutakieni heri na baraka za Mungu katika Dominika hii, tukutane tena siku kama ya leo kwa chakula zaidi cha roho zetu. Tumsifu Yesu Kristo.
Ni Padre Richard Tiganya, C.PP.S.