Ni Dominika nyingine tena katika kumega mkate, Neno la Mungu
litupalo furaha na tumaini la kweli. Basi karibuni tuendelee na wajibu wetu wa
kutafakari Neno la Mungu ili kwa njia hii tuweze kuliweka Neno la Mungu katika
matendo na kisha lizae matunda. Ni Dominika ya tatu ya Kwaresima na Neno
linatualika kusafisha kwa ndani Hekalu la Mungu, ndiyo mioyo yetu.
Mpendwa somo la
kwanza linatoka katika kitabu cha kutoka likiweka mbele yetu amri za Mungu na
linatupa mwaliko wa kushika amri hizo. Mungu anaweka amri ili ziwe ni dira ya
kuongoza maisha ya watu. Mpendwa kabla ya kuwekwa amri hizi Waisraeli kwa
sababu ya kutotii mapenzi ya Mungu walienda utumwani na hivi anapowatoa katika
utumwa huo hapendi tena shida hii itokee na hivi anaweka dira na mwongozo wa
mapendo yake.
Mpendwa, amri za
Mungu hazikuwekwa tu kwa ajili ya kuzishika au kuzikariri bali ni namna ya kujibu
mapendo kwa Mungu, ni njia ya kuelekea furaha ya kimungu, ni njia ya kukutana
na Mungu atupendaye daima. Amri za Mungu ni namna ya kuongoza maisha ya watu
yakae katika msimamo thabiti wa kimaadili ambao huruhusu amani na uelewano kati
ya watu. Basi mpendwa unayenisikiliza shikeni amri za Mungu si tu kwa woga bali
kama nyenzo, taa, na dira ya maisha yako.
Katika somo la
pili, Mtume Paulo anawaandikia Wakorinto akiwataka watambue kuwa wale wote
walioitwa na Kristu na watakaoitwa naye baadaye, kwao Kristu ni nguvu na hekima
ya Mungu. Fundisho hili linalenga kuvunjilia mbali fikira potofu za Kiyahudi na
Kiyunani. Fikira ambazo zilmweka Kristu katika nafasi ya waliolaaniwa na kwamba
Mungu ni jambo la kutafuta kwa akili, ni jambo la kifalsafa tu na hivi hakuna
haja ya imani.
Basi anakukumbusha
wewe pia, kuwa uwe macho na wale wote ambao wanafikiria dini au imani ni jambo
la miujiza na maajabu. Anakutahadharisha usije ukaanguka katika falsafa ya
ujanjaujanja ambao huiweka imani katika kipimo lelemama yaani kutowajibika kwa
sababu hakuna mahakama. Imani yetu, Neno la Mungu ni maisha na hivi yatupasa
kuweka chachu ya Injili katika maisha ya kijamii. Dini si njia ya kujipatia
kazi bali njia ya kwenda mbinguni.
Katika somo la
Injili, Bwana yuko Yerusalemu, na ni muda mfupi umebaki ili pasaka ya Wayahudi
iwadie. Anaona jinsi wafanya biashara ambavyo wanahangaikia mambo ya nje yaani
biashara na wanasahau hekalu la Baba yake. Wanalifanya hekalu sehemu ya kawaida
ambapo mambo ya kidunia yanaweza kusonga mbele! Anawakemea na anasafisha hekalu
la Baba yake akisema: “msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara”
Bwana anatimiza lile andiko lililonenwa na Nabii Zakaria yakuwa Masiha ajapo
hakutakuwa na biashara katika nyumba ya Mungu, Zk 14:21.
Tunafundisha kuondoa
ubaya wote moyoni ili Bwana aiingie na kupata kukaa nasi. Atufundisha kuwa
mioyo yetu kwa njia ya ubatizo ni hekalu la Mungu, ni kikao cha hekima ya Mungu
yaani Roho Mtakatifu. Bwana anatangaza ufalme wa kimasiha na hivi mchanganyo wa
uchumi na dini anautupilia mbali.
Sehemu ya pili ya
Injili yatufundisha juu ya NGUVU ya BWANA kujenga hekalu kwa siku tatu!, Umungu
wake na Habari ya Ufufuko upeo wa wokovu wetu. Anatangaza mwanzo mpya wa ufalme
wa Mungu, na anataka wale wote watakaomfuata watambue kuwa hekalu si jengo bali
ni ufufuko wa Mwana wa Mungu. Hekalu ni jumuiya ya watu walio na imani ya kweli
na wako chini ya Kristu mwenyewe aliye Masiha.
Kumbe mpendwa,
ninakusindikizeni daima katika kukua na kutambua wajibu wako wa kusafisha
hekalu kwa njia ya kitubio na Ekaristi na kwa namna hiyo Mwana wa Mungu ataweza
kuja kwako nawe utazidi kusonga mbele katika safari ya wokovu ukiwa jiwe hai na
hekalu safi lisilo na doa.
Nakutakieni heri na
baraka za Mungu katika Dominika hii, tukutane tena siku kama ya leo kwa chakula
zaidi cha roho zetu. Tumsifu Yesu Kristo.
Ni Padre Richard
Tiganya, C.PP.S.