Thamani ya Shilingi ya Tanzania imekuwa ikiporomoka kwa kasi sana ndani ya miezi mitano iliyopita
Itakumbukwa kwamba mpaka kufikia Januari mwaka jana Dola ilikuwa ikibadilishwa kwa Sh1,630 na ilikuwa ikiporomoka taratibu mpaka kufika Sh1,850 na Sh1,900 ilipofika Februari mwaka huu. Kwa sasa ni zaidi ya Sh2,000.
Kuna sababu mbalimbali zinasababisha kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
Zipo sababu za kiuchumi ambazo pia zimegawanyika kwa kigezo cha ndani na za nje. Vilevile zipo sababu za sera na usimamizi wa sheria za nchi kuhusu masuala ya kifedha.
Sababu ya kwanza ambayo husababisha kushuka kwa thamani ya fedha ya nchini yoyote ni urari wa kibiashara (balance of trade).
Katika urari wa biashara, kinachoangaliwa ni namna nchi inavyoweza kuuza vitu nje pia inavyoagiza vitu kutoka nchi za nje. Kama nchi inatumia bidhaa nyingi za nje kuliko zile za ndani na inauza vitu nje kwa kiasi kidogo kuliko inavyoviagiza basi thamani ya fedha ya nchi hiyo lazima ishuke kwa kasi.
Kwa Tanzania bidhaa nyingi tunazozitumia ni za nje hivyo tunahitaji zaidi Dola ili tuweze kununua bidhaa hizo katika soko la dunia. Hii inapekea hitaji la shilingi liwe dogo ikilinganishwa na hitaji la Dola hivyo thamani ya Dola inakuwa juu kuliko ya Shilingi ya Tanzania.
Suala jingine linaloweza kuathiri thamani ya fedha ya nchi yoyote ni masuala ya uwekezaji kutoka nje yaani Foreign Direct Investment (FDI).
Uwekezaji wa nje ukiongezeka kwa kiasi kubwa husababisha thamani ya fedha ya nchi husika kupanda kwa sababu hitaji lake linakuwa kubwa kwa wawekezaji ambao wanaendesha miradi yao kwa gharama kubwa kwa fedha ya nchi husika.
Hatujapata bado tamko la serikali ama takwimu zozote zinazoonyesha kama uwekezaji kutoka nje umepungua ama wawekezaji wamepunguza mitaji lakini ni moja kati ya sababu ambazo za kushuka ama kupanda kwa thamani ya fedha katika nchi husika.
Thamani ya fedha inaweza pia kuathiriwa na uwekezaji ambao unavuka mipaka ya nchi na sekta mbalimbali kwa lugha ya kimombo; portfolio Investment.
Hii ni aina ya uwekezaji ambao huendeshwa kwa mitaji ya hisa kwa watu kutoka katika mataifa mbalimbali kwa mfano mtu anaweza kuwa ni Mtanzania lakini akawa anahisa katika kampuni ya Uingereza.
Kukiwapo na portifolio investment nyingi hapa kwetu hisa zake zitakuwa zinauzwa kwa shilingi hivyo watu wa mataifa mbalimbali watahitaji kuinunua ili waweze kuwekeza.
Uwekezaji wa namna hii hapa kwetu upo kwa kiasi kidogo sana hivyo inasababisha hitaji la shilingi kwa watu wa mataifa mengine lisiwe kubwa kitu ambacho kinashusha thamani ya fedha yetu.
Nchi ambazo taasisi zake za kifedha zinatoa riba kubwa kwenye mitaji ya fedha ya wateja wake huvutia watu wengi kununua fedha ya nchi hiyo kwa ajili ya kunufaika.
Kwa bahati mbaya hapa nchini suala la riba limekuwa linanufaisha upande mmoja yaani taasisi za kifedha. Taasisi za fedha zinatoza wateja wake riba kubwa wakati mwingine zaidi ya asilimia 13 kwenye mikopo ambayo wateja wanakopa kutoka katika taasisi hizo.
Wakati huohuo, watu ambao wanawekeza fedha zao kwenye taasisi hizo kupitia mfumo wa akaunti ya muda maalumu ama fixed deposits, hupewa ongezeko la riba kwa kiasi kidogo, mara nyingi ikiwa ni chini ya asilimia sita.
Suala hili linaathiri thamani ya fedha ya Tanzania kwa sababu watu ambao wanawekeza katika mitaji ya fedha wanapata ongezeko dogo la riba.
Sababu ya nje ni kuimarika kwa Dola ya Marekani. Taarifa ya mwenendo wa Dola ya Marekani ya Oktoba 2014, inaonyesha kuwa imekuwa ikiimarika na inaweza ikaendelea kufanya hivyo mpaka mwishoni mwa mwaka 2015.
Wachambuzi wa uchumi wa kimataifa wanahusisha kuimarika kwa Dola ya Marekani na mambo ambayo tayari nimeyaainisha.
Moja ni kwamba baada ya mtikisiko wa kiuchumi (2008 – 2009) uwekezaji katika mitaji ya hisa kwa watu wa mataifa mbalimbali umerejea katika hali yake.
Benki Kuu ya Marekani imerejesha ongezeko la riba katika mitaji ya fedha hivyo watu wananua dola zaidi ili waweze kunufaika kwa kuziwekeza kupitia benki.
Marekani kwa sasa ni nchi ya kwanza duniani kwakuwa na uwekezaji kutoka nje ya nchi. Pia, ongezeko la uzalishaji wa mafuta katika nchi hiyo ambao umepunguza uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje umesababisha pia ongezeko la thamani ya dola kwani watu wa nchi hiyo wanahitaji fedha za nchi nyingine kama ilivyokuwa awali.
Sababu ya mwisho na muhimu ni suala la uwezo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuweza kusimamia kikamilifu sera, sheria na kanuni za fedha.
BOT inapaswa kusimamia matumizi ya fedha za Tanzania kwani kwa mujibu wa sheria ya fedha ya mwaka 2006, shilingi ya Tanzania ndio fedha halili kwa malipo ya bidhaa na huduma hapa nchini.