Kabila la Wachaga linafahamika kwa wengi kuwa linapatikana mkoani Kilimanjaro. Kwa asili, Wachaga ni mchanganyiko wa Wamasai, Wasambaa, Wataita, W
Wachagga wana historia ndefu ya asili yao na ya maingiliano yao na  makabila mengine. Kabila la Kichagga ni mkusanyiko wa makabila  madogomadogo (ya Kichagga) yaliyosambaa kijiografia kuzunguka mlima  Kilimanjaro kuanzia mashariki (Tarakea, Rombo) hadi magharibi kwa  Kilimanjaro (Siha, Machame).
Makabila ya Kichagga ni Wa-Rombo,  Wa-Vunjo ambao wanajumuisha watu wa Mwika, Mamba, Marangu, Kilema na  Kirua ambayo ndio inajulikana na wengi kama Kirua Vunjo. Ukipenda  unaweza kuwagawa watu hawa wa Vunjo kama Wa-Mwika, Wa-Mamba  ,Wa-Marangu,Wa-Kilema,na Wakirua.Makabila mengine ni Wa-Old Moshi,  Wa-Kibosho, na Wa-Machame, Wa-Uru, na Wa-Siha.
Watu wengi wanafikiria kwamba Wachaga wanatokana na asili moja. Ukweli ni kwamba wamegawanyika katika himaya 15, wanatofautiana kwa lafudhi, lugha, rangi na mwonekano wa miili yao. Wachaga wapo katika makundi makuu matatu ya Hai, Vunjo na Rombo.
Wale wanaopatikana eneo la Hai ni Wasiha, Wamasama, Wamachame,Wangíuni, Wakibosho, Wauru na Wamoshi. Kwa wale wanaopatikana eneo la Vunjo ni Wakirua, Wakilema, Wamarangu, Wamamba na Wamwika. Kutoka eneo la Rombo ni Wamkuu, Wamashati na Wasseri.Hadi sasa haijulikani vizuri asili ya jina Wachaga, ila wanahistoria wanaeleza kwamba jina hilo linatokana na neno la Kiswahili
linaloitwa 'Kichaka'.Inaelezwa kwamba misafara ya wafanyabiashara iliyokuwa ikiongozwa na Waswahili pamoja na Waarabu, walipokuwa wakipita maeneo ya Vunjo waliwaona wenyeji wa huko wakiwa wamejenga vibanda vya kulinda mazao yao yasiliwe na wanyama waharibifu. Wakawaita wenyeji hawa kwamba wanaishi vichakani na kuanzia hapo wageni wafanyabiashara na Wamisionari walipokuwa wanakuja Kilimanjaro walielekezwa na waongozaji misafara yao kwamba wanakwenda
kwenye nchi ya “Uchakani”, wakimaanisha kwamba kwa watu wanaoishi vichakani. Hatimaye wageni wakashindwa kulitamka vizuri neno hili na kuliita ìUchagani, Jina hili likawekwa kwenye ramani na kuitwa nchi ya “Wachaga”. Hivyo ndivyo wenyeji waliokuwa wakiishi kwenye Miteremko ya Mlima Kilimanjaro walivyopewa jina lao. Wachaga.

Maendeleo ya Wachaga Maendeleo yao hapo awali yalitokana na zao la kahawa. Walifanikiwa kuanzisha vyama vya ushirika na hatimaye mwaka 1932 walianzisha Halmashauri ya Wachaga (Chaga Council) ambayo kwa sasa inatumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi. Halmashauri hii iliongozwa na Mangi Mkuu Mshumbue Thomas Marealle II. Mwaka 1946, utawala wa Waingereza
uliboresha Baraza la Halmashauri ya Wachaga. Himaya ndogo za Wachaga zipatazo 17 (himaya mbili za Wakahe na Waarusha chini zilijumuishwa kwenye Tarafa ya Vunjo) na kuundwa kwa Tarafa tatu za Hai, Vunjo na Rombo. Halmashauri ya Wachaga ilijenga miundombinu na huduma za jamii ikiwamo kuwasomesha watoto wao kwenye shule na vyuo mbalimbali kama Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda. Halmashauri ya Uchaga ilikuwa na bendera yake ambayo ipo hadi leo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, yenye nembo tano kuu:
1. Mlima Kilimanjaro uliochorwa katikati ya bendera ukionyesha mandhari nzuri ya kilele cha Kibo. Kilele cha Kibo kinatoa maji safi na ni kielelezo cha umoja wao.
2. Chini ya kilele cha Kibo, upande wa kushoto wa bendera kuna mgomba wenye ndizi. Hiki ni chakula kikuu cha Wachaga.
3. Upande wa kulia wa bendera ni tawi la mbuni ukiwa na matunda yake. Kahawa ni zao lililowaletea maendeleo.
4. Bendera imezungukwa na matawi ya 'sale' lenye matawi mawili (draceana plant). Matawi haya yamefanya mduara kuzunguka kilele cha Kibo, mgomba wa ndizi na tawi la zao la kahawa. Masale ni mmea unaoheshimiwa sana na Wachaga wote. Ni alama ya amani. Masale hutumika katika sherehe na shughuli zote za kimila zinazofanywa na Wachaga. Majani yake ni kijani kibichi yanayoonyesha jinsi Kilimanjaro ilivyo na rutuba nzuri inayostawisha mazao ya kila aina.
5. Juu kidogo ya kilele cha Kibo yupo chui ambaye amejipumzisha. Chui ni alama kuu ya mamlaka ya Wachaga. Hapo awali kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro walikuwepo chui wengi wa rangi
nyeusi lakini kutokana na ongezeko la watu pamoja na uharibifu wa mazingira chui hawa wametoweka. Sikukuu ya Wachaga Sikukuu ya Wachaga wote ilikuwa ikiadhimishwa Novemba 10 kila mwaka kama kumbukumbu ya siku ambayo Wachaga wote walipokusanyika na kumchagua Mangi Mkuu baada ya kuteuliwa na Halmashauri Kuu ya Uchaga. Maadhimisho ya kwanza ya mwaka 1952 yalitanguliwa na uchaguzi wa Halmashauri ya Wachaga wote kuanzia kwenye ngazi ya Uchili (kijiji), Umangi ( uchifu wa eneo) na mwisho ngazi ya baraza kuu.
WAJUE WACHAGGA
Lugha ya Kichagga
Lugha ya Kichagga inabadilika kuanzia unapotoka Tarakea mpaka unapofika Siha magharibi mwa Kilimanjaro.
Kutokana na tofauti hizo Kichagga kimegawanyika katika Kirombo, Kivunjo, Ki-Old Moshi, Kiuru,Kikibosho, Kimachame, na Kisiha.
Lugha hizo zinakaribia kufanana kadiri makabila hayo yalivyopakana. Kwa  mfano, Kivunjo kinafanana na Ki-Old Moshi. Vile vile Kisiha kinafanana  sana na Kimachame ambacho pia kinafanana kidogo na Kikibosho.
Baadhi  ya Wamachame walihamia sehemu za Meru, Arusha, na kuchanganyikana na  Waarusha, lugha yao ikabadilika kidogo na kuwa Kimeru. Kwa sababu hiyo  Wameru wanasikilizana sana na Wamachame ingawa lafudhi zao  zinatofautiana kidogo.
Historia ya elimu kati ya Wachagga
Wachagga wanajulikana kwa uwezo wao mkubwa wa kufanya biashara na pia  kilimo. Moshi ni maeneo ya mwanzo ambayo Wamisionari wa Ukristo  walijenga makanisa na shule.
Sababu hii imefanya Wachagga kuwa  kabila lenye watu wengi zaidi walio na elimu ya kisasa na mkoa wa  Kilimanjaro unaongoza kwa idadi ya shule za sekondari nchini Tanzania.  Kulingana na takwimu za elimu mkoa wa Kilimanjaro una shule za sekondari  zaidi ya 320. Pia mkoa una shule za msingi zipatazo 950. Idadi hii ya  shule ni kubwa zaidi ya idadi ya shule katika mikoa mingine Tanzania.
Shule nyingi za sekondari ziko katika mkoa huu kwa sababu zifuatazo: 1)  Hali ya hewa na vivutio vya kitalii katika mkoa huu viliwavutia zaidi  walowezi na wakoloni na kuweka makazi yao hapo. Hivyo wamisionari  walijenga shule za kwanza wakifuatiliwa na serikali za wakoloni 2)  Serikali ya Tanzania ilirithi shule zilizojengwa na wakoloni 3) Wachagga  waliobahatika kupata fedha binafsi baadaye waliwekeza kwenye ujenzi wa  shule binafsi kama kitega-uchumi, wakati wakazi wa mikoa mingine kadhaa  walisubiri serikali iwajengee shule. 4) Ukichanganya sababu 1, 2 & 3  utagundua shule katika mkoa Kilimanjaro zimezidi sana idadi ya shule  katika mikoa mingine yote.
Ni vema pia kusema kUwa shule hizo huvutia wanafunzi kutoka Tanzania nzima, haziwasomeshi Wachagga tu.
Kilimo na chakula
Wachagga hulima mazao ya chakula kama vile mahindi, maharagwe, viazi,  ndizi, ulezi na mboga mbalimbali. Pia mazao ya biashara kama vile  kahawa, nyanya na vitunguu.
Ndizi za Wachagga
Ingawa Wachagga wa leo wanakula vyakula mbalimbali kama vile ugali, wali na viazi, chakula kikuu cha Wachagga ni ndizi.
Kuna ndizi za aina mbalimbali na kwa matumizi tofauti. Mfano ndizi  sukari ni fupi na huachwa hadi ziive na huliwa mbivu kama tunda.
Ndizi mshale hukatwa zikiwa mbichi na kupikiwa vyakula mbalimbali pamoja  na nyama ya ng'ombe, kondoo au mbuzi. Mara nyingine hupikwa na  maharage, choroko, kunde au hata maziwa ya mtindi. Vyakula vya ndizi  huja kwa ladha tofauti kama vile ndizi nyama, mtori, machalari, kiburu  na kadhalika.
Aina nyingine ni ndizi ng'ombe ambazo huachwa ziive  halafu humenywa na kutumiwa kutengenezea pombe maarufu iitwayo mbege.  Mbege hutengenezwa kwa kutumia ndizi mbivu, maji, na ulezi.
Aina  nyingine ni ndizi mzuzu. Hizi zikikomaa huachwa zianze kuiva kidogo  halafu huchomwa na kuliwa kama kitafunwa pamoja na chai au pombe.  Ukipita mitaa ya Dar es Salaam utaona ndizi mzuzu zikichomwa sambamba na  muhogo au kuku vumbi au kiti moto.
Wachagga na muhogo
Inasemekana kuwa "Mchagga halisi hali muhogo - akila muhogo atakufa".  Usemi huu umetokana na historia ya mababu kuwa Wachagga waliopanda  mihogo Kilimanjaro enzi za kale walikufa baada ya kuila. Historia hiyo  yaweza kuwa ya ukweli kwa sababu aina nyingi za mihogo zinajenga sumu ya  sianidi ndani yake; watu waliozoea kutumia mihogo huwa na njia za  kuondoa sumu kwa kuiloweka mihogo katika maji kwa muda. Lakini kama  Wachagga wale wa zamani, hasa wa Machame, walifanya jaribio bila kujua  mbinu ya kuondoa sumu, ajali iliweza kutokea. Cha kushangaza ni kwamba  hukohuko Kilimanjaro, majirani na watani wa Wachagga, yaani Wapare,  walikuwa wameshazoea mihogo na ilikuja kuwa moja ya chakula chao kikuu.
Ulaji kiti-moto
Pamoja na kilimo cha mazao, Wachagga hupendelea sana kufuga nguruwe.  Tabia ya kula nyama ya nguruwe ijulikanayo leo kwa jina la "kiti moto"  ni moja ya mambo yaliyoenezwa na Wachagga. Ulaji wa "kiti moto" haukuwa  pendeza baadhi ya wenyeji wa Pwani kama Dar es Salaam ambapo Wachagga  walihamia, kwani wakaaji wengi wa Pwani ni Waislamu kwa hiyo nguruwe  kwao ni haramu. Wakazi wa Dar es Salaam watokao makabila mengine na  wasiyo Waislamu kwao kula nguruwe ilikuwa "ruksa".
Majina ya Kichagga
Majina ya kiukoo ya Kichagga pia huashiria wanatoka sehemu gani ya  Uchaga, japo si lazima kuwa hivyo: kwa mfano, familia maarufu za  Kichagga nchini Tanzania ni kama ukoo wa akina Mushi, Kimaro, Swai,  Massawe, Lema, Urassa, Nkya, Ndosi, Meena hutoka Machame.
Akina  Temu, Mlaki, Mlay, Lyimo, Moshiro, Mselle, Kamnde, Kileo, Kimambo,  Tesha, Msaki, Assey, Kyara, Kessy, Ndanu, Macha, Mbishi, Kombe, Njau  wanatoka Old Moshi na Vunjo.
Kavishe, Mariki, Tarimo, Laswai,  Mallya, Mrema, Mkenda, Massawe, Silayo, Lyaruu, Makyao, Mowo, Lamtey,  Tairo, Mramba, Kauki wanatoka Rombo.
Sawe, Usiri, Shayo, Kiwelu, Makundi, Urasa, Mtui, Moshi, Meela, Minja, Njau wanatoka Marangu na Kilema.
Rite, Makule, Minja, Mashayo, Chao, Shao, Makawia, Ndesano, Kimario,  Tilla, Mariale, Tarimo, Mafole, Kituo, Mrosso, Lyakundia, Kessy,  Mmbando, Matemba, Ndenshau, Morio, Akaro, Matowo, Towo, Mkony, Temba  Foya, Munishi, Kilawe na kadhalika hutoka Kibosho.
Ukoo wa akina  Teri wako Mamba, Chami, Chuwa, Kiria na wachache Sango, Old Moshi na  wengine walihamia Maji ya Chai, Mkoa wa Arusha.
Wachagga wengi hupenda kurudi nyumbani kipindi cha Krismasi, ikiwa ni kuwatembelea wazazi wao, rafiki, au ndugu.
Ingawa wengi hudhani kwamba Wachagga wameathiriwa sana na dini ya  Ukristo kwa kuwa wengi wao ni Wakristo na hiki huwa ni kipindi cha  likizo kwao, inaaminika pia kuwa kurudi kwao Uchagani wakati wa Krismasi  ni pamoja na kutembelea ndugu zao na kujumuika pamoja katika kuumaliza  mwaka baada ya kazi nyingi za kutafuta pesa kwa mwaka mzima.
Utawala wa jadi ya Wachagga
Watawala wa Kichagga waliitwa "Mangi". Hawa walihodhi mashamba, ng'ombe  na waliheshimiwa kama viongozi wa kikabila. Walikuwa na nguvu za  kisiasa na utajiri. Baadhi ya Ma-mangi mashuhuri katika historia ni kama  Mangi Rindi aliyeingia mikataba na wakoloni (Wajerumani), Mangi Sina wa  Kibosho - anajulikana kwa uhodari wake wa vita katika kupigana na  Wamachame na kupora ng'ombe na mazao yao na Mangi Marealle wa Marangu na  Vunjo.
Wakoloni walipokuja Kilimanjaro waliingia mikataba na  viongozi hawa wa kikabila ili kuweza kuweka misingi yao ya kikoloni. Pia  ndugu na watoto wa Ma-mangi walikuwa wa kwanza kupata elimu ya  kikoloni, kwa hiyo waliweza kushirikishwa katika serikali za kwanza.  Hawa pia wanaaminika walikuwa kama mabepari wa kwanza wa kijadi, maana  walifanyiwa kazi na watu wengine wakati wao Ma-mangi wamekaa kuhesabu  mali zao.
Usemi maarufu wa "u-Mangi-meza" nadharia inawezekana kuwa umetokana na watawala hawa wa Kichagga.
Ardhi
Ingawa ardhi ni msingi wa maendeleo kwa watu wote, kwa Wachagga, ardhi  ni mali sana kwa sababu kilimo chao ni cha mazao ya kudumu kama kahawa  na ndizi hukaa shambani kwa muda wa miaka mingi.
Mojawapo ya urithi  wapewayo watoto ni "kihamba". Hii ni sehemu ya ardhi ambayo mtoto  anategemewa atajenga na kuanzisha familia yake. Bahati mbaya watoto wa  kike walikuwa hawapewi kipaumbele katika ugawanaji wa vihamba. Uhaba wa  ardhi huko Uchaga ulipelekea Wachagga wengi kuhamia mikoa mingine. Hivi  leo utakuta Wachagga wakiishi Dodoma, Morogoro, Iringa, Mbeya n.k.  wakiwa wamepanda migomba yao na kuendesha biashara za maduka ya vyakula.
Ukienda kwenye mikoa hiyo utakuta wamejenga jamii zao na vyama vyao vya  kusaidiana wakati wa sherehe au matatizo. Aidha hata pombe ya mbege  utaweza kuikuta kwenye makusanyiko ya Wachagga katika mikoa mbalimbali.
Maoni juu ya Wachagga
Ingawa wanaume wa Kichagga hupendelea kufanya kazi mbali na kwao, wake  zao hukaa nyumbani (Moshi) na hufuga ng'ombe na kazi za shambani. ila  kwa sasa kutokana na ugonjwa wa ukimwi tabia hii imepungua miongoni  mwao.
Wanawake wa Kichagga (hasa kutoka Rombo) hujulikana kama  wafanyakazi hodari. Huchangia sana katika mapato ya nyumbani na chakula.
Ingawa kipato cha Wachagga ni kikubwa kulingana na cha makabila  mengine, takwimu zinaonyesha watoto wa mkoa wa Kilimanjaro kuongoza kwa  utapiamlo. Sababu kubwa ya watoto kuwa na utapiamlo ni wazazi kujali  zaidi kazi kuliko muda wa kuwahudumia watoto.
Wengi wa watoto hao ni  wale ambao wazazi wao ni watu wa pombe na kipato chao kinaishia  kilabuni. Utaona kwamba Uchagga una vilabu vingi vya pombe na  vinaongezeka kwa sababu imekuwa biashara kubwa. Karibu kila kaya kumi na  tano kuna kilabu cha pombe na kiwango cha chini kabisa cha pombe  inayouzwa kwa siku katika vilabu hivyo si chini ya madebe sita au lita  mia moja. Pombe ni sababu moja ya watoto kuwa na utapiamlo.
Hii  inawezekana kuwa matunda ya wazazi kutowalisha watoto wao chakula cha  kutosha au chakula bora. Kuna sehemu nyingine za Uchagga kama Old Moshi  na Kibosho ambapo watoto wadogo hupewa pombe ya mbege asubuhi, mchana na  jioni.
Sababu nyingine ni kazi; mama wa Kichagga anaweza kushinda  shambani kutwa na hana desturi ya kubeba watoto mgongoni kwenda nao  shambani, hivyo wanakuwa nyumbani ama wenyewe au na mayaya. Mfano ulio  dhahiri ni nyakati za asubuhi na mapema kwenye vyombo vya usafiri karibu  robo tatu ya abiria ni wanawake wakienda katika shuguli za biashara na  kilimo na vivyo hivyo nyakati za jioni wakirudi majumbani. Hao ni nje ya  wale wanaotumia usafiri wa miguu ambao ni wengi zaidi.
Pia baadhi  ya kina mama wa Kichaga wanawajali waume zao zaidi kwani nyama nzuri ni  ya baba. Kuepuka gharama baba ataandaliwa chakula kizuri, tofauti na  chakula walichoandaliwa watoto, japo ni chakula kilekile.
Pia  Wachagga wamekua na desturi ya kuwaenzi wazee wao waliotangulia mbele za  haki kwa kuwatambikia kwa pombe na nyama za mbuzi pale tu wanaporudi  nyumbani ifikapo mwezi Desemba. Hili limekuwa suala la kawaida sana na  halipingiki. Wengi wao huwa wanarudi na magari, ndiyo sababu utaona ya  kwambwa kila ifikapo mwezi Desemba kila mwaka foleni za magari zimekuwa  zikiongezeka kutokana na Wachagga kurudi nyumbani msimu wa sikukuu.  Wengi wao wamekuwa wakitoka sehemu mbalimbali za nchi na hata nje ya  nchi.