Thursday, November 7, 2013

Masomo ya Dominika 32 jumapili ya tarehe 10/11/2013


click hapa kusikiliza tafakari ya masomo ya kesho. RealAudioMP3

  

10
   NOVEMBER
JUMAPILI DOMINIKA YA 32 MWAKA C



RATIBA ZA IBADA
KIGANGO CHA BOKO.
IBADA YA MISA YA KWANZA 12:15 – 1:45 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 2:00 – 3:50 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA TATU SAA 4:00-5:20 ASUBUHI
KIGANGO CHA MBWENI.
IBADA YA MISA YA KWANZA 1:15 – 2:55 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 3:00 – 4:50 ASUBUHI
KIGANGO CHA MT. RAFAEL.
IBADA YA MISA YA KWANZA 1:00 – 2:50 ASUBUHI
IBADA YA MISA YA PILI 3:00 – 4:50 ASUBUHI
KIGANGO CHA ANTHONY WA PADUA – MBWENI TETA.
IBADA YA MISA NI 3:00 – 5:00ASUBUHI



MASOMO YA DOMINIKA 32
SOMO LA 1: 2Mak. 7:1-2, 9-14

Ilitokea ya kuwa ndugu saba, pamoja na mama yao, walikamatwa kwa amri ya mfalme na kuteswa sana kwa mijeledi na mapigo ili kuwashurutisha kuonja nyama marufuku ya nguruwe. Mmoja akajifanya mnenaji wao, akasema, wataka kuniuliza nini juu yetu? Sisi tu tayari kufa kuliko kuzivunja amri za wazee wetu. Wa pili alipokuwa kufani alisema,wewe, mdhalimu, unatufarikisha na maisha ya sasa, lakini Mungu wa ulimwengu atatufufua sisi tuliokufa kwa ajili ya amri zake, hata tupate uzima wa milele. Na baada yake alidhihakiwa Yule wa tatu, naye mara alipoagizwa, alitoa ulimi wake, akanyosha mikono yake bila hofu akasema kwa ushujaa, kutoka mbinguni nalipewa hivi, na kwa ajili ya amri za Mungu navihesabu kuwa si kitu, na kwake natumaini kuvipokea tena. Hata mfalme na watu wake walishangazwa kwa roho ya kijana huyu, kwa jinsi alivyoyadharau  maumivu yake. Akiisha kufa huyu, walimtesa wa nne na kumtenda mabaya yale yale. Naye alipokaribia kufa alisema hivi; ni vema kufa kwa kwa mikono ya mwanadamu na kuzitazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa tutafufuliwa naye. Lakini kwako wewe hakuna ufufuo.


Somo 2: 2The.2:16 – 3:1-5

Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupatia faraja ya milelena tumaini jema, katika neema, awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neon na tendo jema. Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neon la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu; tukaokolewena watu wasio haki; wabaya; maana si wote walio na imani. Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na Yule mwovu. Nasi tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba unayafanya tuliyowaagiza, tena kwamba mtayafanya. Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na saburi ya Kristo.


INJILI:Lk. 20:27-38

Baadhi ya wasadukayo, wale wasemayo ya kwamba hakuna ufufuo, walimwendea Yesu, wakamwuliza, wakisema Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto, na amtwae huyo mke,  ampatie ndugu yake mzao. Basi,kulikuwa na ndugu saba . na wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; wa pili akamtwaa Yule mke, akafa hana mtoto; hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. Mwisho akafa Yule mke naye. Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. Yesu akawaambia, wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kafufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionyesha katika sura ya kijiti, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake.


Matangazo mbali mbali
Jumapili hii tarehe 10/11/13 kutakuwa na kikao cha Halmashauri ya Viwawa Parokia ya Boko, kikao kitafanyikia parokiani Saa 4:00 asubuhi mara baada ya ibada ya pili. Wajumbe ni viongozi wote wa Viwawa ngazi ya Vigango.
Agenda za kikao.
ü Maandalizi ya semina ya Tarehe 23/11/13 – Mbweni
ü Mapendekezo ya mipango ya mwaka 2014 – 2015
ü mengineyoendelea zaidi......

jdhibitisha ushiriki wako kwenye semina ya tarehe 23/11/13 kwa kulipa ada sasa ni tshng 5000 lipa kwa mhazini wako jumuiya, kigango au parokia.....tunawatakia maandalizi mema.

Wednesday, November 6, 2013

Mnaalikwa kwenye Karamu ya Bwana! Wakristo msiridhike kuwa katika orodha ya wageni waalikwa! Mnatakiwa kufanya makubwa zaidi!




Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, Jumanne, tarehe 5 Novemba 2013 anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanasherehekea kikamilifu Karamu ya Bwana. Wakristo watambue kwamba, wanaalikwa na Mwenyezi Mungu kushiriki karamu hii wakiwa na dhamiri safi na nyofu.

Karamu ya Bwana ni sherehe inayobubujika furaha, matumaini na mapendo kutoka kwa Kristo; sherehe ambayo inawakumbatia wote pasi na ubaguzi kwani wao ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kila mtu ana wajibu na dhamana ya kutekeleza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Wakristo wajitambue kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya Kanisa la Kristo! Karamu hii ni mwaliko wa kujenga na kudumisha umoja miongoni mwa Wakristo, kila mwamini akijitahidi kujitakatifuza kwa nyenzo mbali mbali zinazotolewa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Kanisa linawakumbatia watakatifu na wadhambi; na kwamba, kila mmoja wao ana karama na zawadi ambayo amekirimiwa na Roho Mtakatifu; zawadi ambayo anapaswa kuifanyia kazi barabara kwa ajili ya mafao ya Kanisa. Kanisa linapaswa kuwakumbatia wote kwa kuanzia na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya Wakristo wamepewa mwaliko na wako kwenye orodha ya waalikwa, lakini bado wanagoma kuhudhuria Sherehe ya Mwanakondoo wa Mungu kwa visingizio kibao! Wanashindwa kutambua kwamba, kuingia ndani ya Kanisa ni mwaliko na neema inayowataka waamini kujenga na kuimarisha Jumuiya ya Kikristo, kila mtu akitumia kikamilifu karama na vipaji vyake kwa ajili ya Kanisa na Jirani zake. Kristo anaendelea kuwaalika waamini kufanya hija inayowapeleka kwenye maisha ya uzima wa milele na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye kiongozi mkuu wa safari hii ya maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu ni mwingi wa huruma na mapendo, hata kwa wale wanaoonesha shingo ngumu kwa mwaliko wake. Anaendelea kuwasubiri kwa saburi na mapendo makuu. Yesu anawapenda watu ambao ni wanyofu na wa kweli katika maisha yao: kwa maneno na matendo.

Inapendeza ikiwa kama Wakristo wote wataweza kushiriki katika Karamu ya Bwana, ili kuonja furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na wala wakristo wasiridhike kwamba, majina yao yameandikwa kwenye orodha ya waalikwa kwenye Karamu ya Bwana, bali wanatakiwa kushiriki bila kutoa visingizio!

Monday, November 4, 2013

Kilele cha Mwaka wa Imani Kitaifa, Bagamoyo kufunika!



Maadhimisho ya Mwaka wa Imani  limekuwa ni tukio ambalo limeasidia kukuza na kuimarisha imani ya waamini kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini katika ngazi mbali mbali wamefanya tafakari ya kina kuhusu: Fumbo la Msalaba, Sakramenti za Kanisa na umuhimu wake, Maisha ya Sala na Ushuhuda wa maisha ya Kikristo kama kielelezo makini cha imani tendaji.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani nchini Tanzania yanakwenda sanjari na Jubilee ya Miaka 150 ya Ukristo nchini Tanzania. Katika kipindi chote hiki Kanisa Katoliki limejikita katika Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mheshimiwa Padre Patern Patrick Mangi, Katibu mtendaji Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania  anafafanua kuhusu mikakati ya Maaskofu Katoliki Tanzania katika kufunga Mwaka wa Imani huko Bagamoyo.

Maadhimisho haya yataanza hapo tarehe 8 Novemba 2013 na kilele cha Maadhimisho ya Kufunga Mwaka wa Imani Kitaifa ni hapo tarehe 10 Novemba 2013, ili kutoa nafasi kwa Familia ya Mungu Majimboni, kushiriki na Baba Mtakatifu Francisko katika kuufunga rasmi Mwaka wa Imani wakati wa Sherehe za Kristo Mfame wa dunia. Familia ya Mungu itapata nafasi ya kutafakari mada mbali mbali zilizoandaliwa na Maaskofu Katoliki Tanzania.

Sunday, November 3, 2013

Tafakari ya masomo ya leo dominika ya 31 mwaka C 03/11/13

Somo La Kwanza: Hek. 11:22-12:2
Wimbo Wa Katikati: Zab. 145: 1-2, 16-18, 123-14 (K)
Somo La Pili: 2 Thes.1: 11-2:2
Injili: Lk. 19: 1-10
Tafakari y ya masomo:
Injili ya leo, inatuadithia juu ya mtosa ushuru Zakayo. Zakayo alikuwa na mapungufu makuu mawili. Moja, alikuwa na upungufu wa asili, alikuwa mfupi wa kimo. Katika msongamano mkubwa uliokuwa unamfuata Yesu, alikuwa hana nafasi ya kumwona kwani watu warefu wangemzuia. Pili, alikuwa na upungufu wa kijamii. Kazi yake ya kutosa ushuru ilimfanya achukiwe na Wayahudi wenzake. Kwani, watosa ushuru walikuwa wadanganyifu kwa waliwatosa watu ushuru mkubwa zaidi, huku wakijitajirisha na pesa za ziada walizotosa watu. Hivyo basi, hawakupendwa na jamii ya  Wayahudi.

Pamoja na mapungufu haya ya kiasili na hata ya kijamii, ambayo yangekuwa sababu ya kutosha kabisa ya kumzuia Zakayo asimuone Yesu. Zakayo hakukubali, nafasi hii ya kumuona Yesu, impite. Alitoka mbio, akapanda juu ya mkuyu ili amuone Yesu. Yesu alizizawadia juhudi za Zakayo kwa kumuita, “Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa  kushinda nyumbani mwako.”

Yesu anamtumia Zakayo kutuonesha jinsi Mungu anavyozijali juhudi za wale wajitahidio bila kukata tamaa kutokana na mapungufu waliyonayo. Kama Zakayo asingejitahidi kutafuta mbinu za kumuona Yesu, hata kwa kupanda mkuyuni, angekufa bila kutimiza ndoto yake ya kutaka kumuona Yesu. Mara nyingi tumejiona kuwa kutokana na mapungufu yetu hatuwezi kutimiza ndoto zetu maishani. Tunapoteza muda tukisema kama ningekuwa na hili ama lile ningefanya hivi ama vile. Kama ningezaliwa mwanamke ama mwanaume ningefanya hili wala lile. Kama ningezaliwa katika familia iko hivi ningefanya hili ama lile; Kama ningekuwa na uwezo huu ama ule basi mambo yangu yangeenda vizuri; Kama muda huu, ndio ningekuwa mwanafunzi, ningesoma sana ili niwe na maisha mazuri zaidi. Mwanafunzi naye anasema, ningekuwa na akili kama fulani, ningefanya vizuri; ama ningekuwa shule bora zaidi ningesoma kwa bidii sana. Hizi ndoto za mchana hazitatusaidia. Kitakachotusaidia ni kukubali mapungufu yetu na hapo kuangalia ni kitu gani Mungu ametuwekea karibu kitakachotuwezesha kutimiza ndoto zetu. Kama Zakayo asingekuwa mtu wa jitihada, asingeona kuwa angeweza kupanda mtini na hivyo kuyashinda mapungufu yake. Kama Zakayo asingekuwa ni mtu wa maono, mkuyu ungeendelea kubakia mkuyu tu huenda ungekuwa mojawapo ya vikwazo vya kumzuia asimuone Yesu. Angeendelea kulalamika na hata kuulalamikia mkuyu. Zakayo alipoutazama mkuyu aliona jinsi unavyoweza kutumika kuwa kifaa cha kumwezesha kumuona Yesu na siyo kikwazo cha kumuona Yesu. Ufupi wake, japo ulikuwa ni upungufu wa asili ulikuwa sababu yake ya kuzitumia jitihada zake. Zakayo alikuwa na mtazamo chanya katika maisha. Mtazamo huu ulimfanya kuweza kuvibadilisha vizingiti katika njia yake ya maisha na kuvifanya ngazi ya kumwezesha kutimiza ndoto yake katika maisha. 

Sisi pia, inatubidi, kuangalia kwa makini kabisa ni mapugufu gani yanayotufanya tushindwe kutimiza ndoto zetu maishani.(ulevi? Wivu? Tamaa? Hasira? Uwongo? Uadui? Chuki? Uvivu? Nk.) Baada ya kuyaona mapungufu hayo, tuangalie kwa makini, tena sana, ni kitu gani Mungu ametuwekea karibu nasi ambacho kitatufanya tuweze kuyashinda mapungufu haya. Hakuna na tatizo lisilo na suluhu kwa wale wanaoamini. Ila tu ni lazima tukazie macho mapungufu yetu, tuangalie pia na zile nyenzo Mungu alizoweka karibu nasi ambazo zitatuwezesha kukwea na kuvishinda vikwazo hivvyo na baada ya kuviona tumuombe Mungu kwa bidii zote, kwani  yeye alikuja ili tuwe na uzima kamili (Jn 10:10) na siyo mapungufu. Zakayo aliona mti wa mkuyu, wewe pia inakubidi utafute mkuyu wako utakao panda, na hapo utamsikia Bwana akikuambia, “Leo, imenipasa niwe nyumbani mwako.” AMINA

Friday, November 1, 2013

Maadhimisho ya Siku ya Watakatifu wote na siku ya Marehemu wote

Papa afafanua kiini cha Maadhimisho ya Siku ya Watakatifu wote na siku ya Marehemu wote.



BabaMatakatifu Francisko akiendelea kutoa tafakari juu ya sala ya Nasadiki, kwa Jumatano hii, alilenga zaidi katika usharika na Watakatifu, kama Kateksimu ya Kanisa Katoliki inavyotukumbusha sisi kwamba, usharika huu ni kwa Mambo Matakatifu na kati ya watu Watakatifu (No. 948 ).

Papa alizama zaidi katika sehemu ya Pili ya kuw ana usharika na Marehemu Watakatifu , ukweli unaohitaji ufafanuzi zaidi katika imani yetu, akieleza pia kwamba, hutukumbusha pia kwamba, hatuko pweke, lakini kuna uwepo wa usharika wa maisha kwa wale wanaokuwa wa Kristu. Usharika mmoja unaoundwa na imani , katika ukweli wake, neno hili Watakatifu hurejea wale wanao mwamini Yesu Kristu kuwa ndiye Bwana wa Maisha na hivyo humwilishwa kwake Yeye ndani ya kanisa kupitia ubatizo. Na kwa namna hiyo , Wakristu wa kwanza waliitwa pia Watakatifu.

Papa aliendelea kufundisha , Usharika wa Watakatifu ni kina halisi cha maana ya Kanisa kwa sababu kama wakristu kupitia Ubatizo , tunafanywa kuwa washiriki wa maisha ya usharika mmoja na upendo wa Utatu Mtakatifu. Na hivyo sote tunaunganishwa mmoja kwa mwingine na kiungo cha ubatizo katika Mwili wa Kanisa. Na kupitia usharika huu wa kidugu, tunawekwa karibu zaidi na Mungu, na tukitakiwa kusaiidiana mmoja kwa mwingine kiroho.

Papa alieleza na kuirejea Injili Yohana ambayo inasema kwamba , kabla ya mateso yake, Yesu aliomba kwa Baba kwa ajili ya umoja kwa wanafunzi wake kwa maneno haya : “Naomba ili wote wawe kitu kimoja kama wewe, Baba , ulivyo ndani yangu , nami ndani yako. Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ndiye uliyenituma "( 17:21). Kanisa , katika kweli yake kamili , ni usharika na Mungu , usharika wa upendo na Kristo na Baba katika Roho Mtakatifu shina la usharika huo. . Uhusiano huu baina ya Yesu na Baba ni dhamana kati ya Wakristo, iwapo pia sisi tumo ndani yake katika umoja huu, na tanuru la moto huu wa upendo katika Utatu Mtakatifu, basi tunaweza kweli kuwa na moyo na roho moja kati yetu kwa sababu upendo wa Mungu unauguza ubinafsi wetu , chuki zetu, utengano na miganyiko yetu ya ndani na nje.

Papa Francisko amesema, iwapo ushariki huu chanzo chake ni mzizi wa upendo ambao ni Mungu, basi pia kuna sababu za kufanya hima kutoa jibu landiyo katika muungano huu na Mungu, maisha ya ushirika wa udugu unaoongoza katika kuwa msharika na Mungu.

Hii ni sehemu ya pili ya usharika, ambayo Papa alitoa msisitizo zaidi, kuwataka watu wa Mungu,kupta uelewa mpana kwamba, imani yetu inahitaji msaada wa wengine , hasa katika nyakati ngumu. Alisema, tazama pia jinsi ilinavyokuwa vizuri kutoa msaada kwa mwingine katika maajabu haya ya imani! Papa alieleza kukemea mwelekea kukubatia tabia ya kutaka kujifungia binafsi, hata katika mazingira ya kidini, kiasi kwamba, inakuwa hata vigumu kwa wengine, hata kuomba msaada wa kiroho, kwa wale wenye uzoefu katika maisha haya ya Kikristu.

Papa alihimiza katika nyakati hizi ngumu ni muhimu kuwa imani kwa Mungu kupitia sala, na wakati huo huo, ni muhimu kupata ujasiri na unyenyekevu kuwa wazi kwa wengine. Papa amekumbusha ushirika wa watakatifu ni familia kubwa, ambapo vipengele vyote ni kusaidia na kusaidiwa yaani kusaidiana mmoja kwa mwingine. Kushirkiana na wengine katika parokia zetu, katika vyama , jumuiya, harakati na vikundi, kama sehemu ya maisha katika safari yetu ya imani, ni kutochoka kuomba msaada wa maombezi na faraja ya kiroho. Ni wakati wetu wa kusikiliza na kuwasaidia wale ambao hawaja jiunga nasi katika safari hii.

Papa alikamilisha Katekesi yake kwa kuchambua kipengele kingine cha usharika wa watakatifu, akisema kwamba, ushariki wa wakatifu huenda zaidi ya maisha ya dunia, inakwenda zaidi ya kifo kwa kuwa huduma milele. Usharika wa kiroho tunaopokea wakati wa Ubatizo hauvunjwi na kifo , lakini umeinuliwa na ufufuko wake Kristu, unao ipeleka roho katika mapito ya utimilifu wa maisha ya milele.

Papa aliendelea kubaini kwmba, kuna dhamana ya kina na isiyokuwa na mwisho kati ya wale ambao bado mahujaji katika dunia hii na wale ambao wamevuka kizingiti cha kifo na kuingia katika umilele. Wote hao huuundwa wakati wa ubatizo hapa duniani,na nafsi hutakatifushwa toharani na kufanywa wenye heri, kuingia katika makazi ya mbinguni ambako ni makazi ya familia moja kubwa. Ushirika huu kati ya nchi na mbinguni ni barabara ya maombezi , ambayo ni aina ya juu ya mshikamano, na pia ni msingi wa maadhimisho ya kiliturujia ya Watakatifu wote na Maadhimisho ya Marehemu wote kama itakavyokuwa siku chache zijazo.

Papa alimalizia kwa kumtaka kila mmoja alifurahie fumbo hili , na kumwomba Bwana neema zake , ili tuweze kuwa karibu zaidi naye na katika usharika na waamini wote, wake kwa waume ndani ya kanisa.
Wito wa Kuombea Iraki
Baada ya Katekesi, Papa akisalimia makundi mbalimbali, pia alilitaja kundi la mahujaji kutoa Iraki ambao walikuwa wakiwakilisha makundi mbalimbali ya kidini, toka yanayojionyesha kama ni utajiri wa Ukristu katika taifa la Iraki . Kundi hili liliongozwa na Kardinali Tauran Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya majadiliano na dini zingine. Papa alitoa wito kwa watu wote kukumbuka kuliombea taifa la Iraki ambalo kila kukicha hukumbana na majanga ya fujo na ghasi za kusitisha zinazofaywa na makundi mabalimbali. Tusali ili Iraki ipate kurejea katika njia ya majadiliano, maridhianao , amani, umoja na utulivu wa kudumu kitaifa.

Sikuku ya Watakatifu woteleo tarehe 01/11/2013

Somo La Kwanza: Ufunuo.7:2-4, 9-14
Wimbo Wa Katikati: Zaburi: 24:1-6 (K) 6
Somo La Pili: 1 Yoh. 3:1-3
Injili: Mathayo 5:1-12
Sikukuu ya Watakatifu wote
Kalenda ya Kanisa Katoliki inajumuisha sikukuu za watakatifu wengi na hata wafia dini. Lakini Novemba mosi, ni sikukuu ya watakatifu wote. Kweli tunasherehekea sikukuu za watakatifu fulani fulani katika siku tofauti lakini Novemba Mosi, tunasherehekea sikukuu ya watakatifu wote, wale tunaowajua na wale tusiowajua. Watakatifu ni wengi na wamefanya kazi nyingi tofauti tofauti lakini zote zikiwa na umuhimu wake katika kuiendeleza na kuikuza imani yetu. Watakatifu ni wengi na hatuwezi kuwajua wote. Hivyo sikukuu hii inawajumuisha pamoja kama kundi moja la watu walioyaishi maisha yao vyema hapa duniani. Sikukuu hii ni kichocheo katika maisha yetu ya imani kwani inatubidi tufuate nyayo zao, tuishe tukimtegemea Mungu zaidi ya chochote. Watakatifu walio pamoja na Mungu mbinguni wanatuombea na kutupa moyo sisi watakatifu tulio safarini kwenda mbinguni. Watakatifu tunao sherekea siku yao leo ni  mashujaa wa imani na kielelezo kwetu, wanatupa moyo kuwa, “Ndiyo kumfuata Kristo kunawezekana.” Kesho Novemba mbili tutawakumbuka marehemu wote. Hawa ni ndugu zetu, wasafiri wenzetu ambao tayari wameiacha dunia hii lakini bado hawajafika mbinguni, wanavikwa mavazi meupe (Ufu.7:9) wanatakaswa kabla ya kuingia mbinguni
Sherehe ya watakatifu wote inatukumbusha kuufuata wito wetu wa kuwa wana wa Mungu. Baada ya mwanadamu kuupoteza utu wake kwa kutenda dhambi, Mungu alimtuma mwanae ulimwenguni ili wale wote wamuaminio wapate ufalme wa milele (Yn. 3:16). Watakatifu wameshaupata ufalme huu wa milele ni wajibu wetu sisi wakristo kufuata mfano wao. Wao walishinda adui wa roho kwa kutumaini neema za Mungu.
Injili ya leo inatuonesha furaha ya watakatifu ilivyo, na njia inayotuwezesha kufika kufika mbinguni. Tunasikia kwamba, “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Kumbe basi, tukitaka vita vya miaka michache hapa duniani vitatuletea furaha na heri ya milele. Inatubidi basi tuvumilie kabisa katika imani yetu, tujaribu kila tuwezavyo tuvishinda vishawishi kwani Mungu hatajaribu zaidi ya neema aliyotupa kuvishinda vishawishi hivyo.  Watakatifu tunaowakumbuka leo, wanatupenda wanatuombea kwa Mungu  ili tuwe pale walipo, karibu na Mungu na kwenye heri ya milele.  Sikukuu hii haina budi kuamsha matumaini makubwa mioyoni mwetu.
Sala:
Ee Mungu niongezee kiu na njaa ya kuyafanya mapenzi yako na siku moja niwe pamoja na watakatifu mbinguni tukikusifu na kuiombea dunia.
Amin

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR