Jimbo kuu la Dar es Salaam Alhamisi tarehe 26 Juni 2014, majira ya saa 5:00 asubuhi linatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Parokia ya Mtakatifu Gaudencia, Makoka kwa ajili ya kumwombea na hatimaye, kuanza safari kuelekea Jimboni Mbeya, atakapopumzishwa kwenye makao ya milele pamoja na watawa wenzake
Wasifu wa marehemu
Sr. Crescentia Kapuli wa Shirika la Watawa wa Bikira Maria Malkia wa Mitume Jimbo Katoliki Mbeya. Amezaliwa katika Kijiji cha Mkulwe, Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya, Agosti, 29, 1962 katika Kijiji cha mkulwe na kupata ubatizo Agosti, 31, 1962 huko Mkulwe na nambari ya cheti cha Ubatizo ni LB 19703, amepata Komunio ya kwanza Oktoba,11, 1972 na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara Oktoba, 12, 1972 huko huko Mkulwe.
Sr.Crescentia alikuwa ni mtoto wa mwisho kati ya watoto 12 wa Mzee Peter Kapuli na Mama Maria Nakana. Sr.Cresensia ameingia utawani kama mwomboaji kunako mwaka 1979. Upostulanti mwaka 1980. Unovisi mwaka 1981 hadi mwaka 1983. Akafunga nadhiri za kwanza tarehe 12 Desemba 1983 na baadaye kunako tarehe 12 Desemba 1991 akafunga nadhiri za daima. Tarehe 31 Mei 2009 akaadhimisha Jubilee ya miaka 25 ya maisha yakitawa.
ELIMU
Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Mkulwe mwaka 1972 hadi 1978, elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari ya Bigwa ( Bigwa SR’s Secondary School) Mwaka 1994 hadi Mwaka 1997, amesoma chuo cha maarifa ya nyumbani homecraft Mwanjelwa mwaka 1991 hadi mwaka 1992, amesoma Chuo cha Uhasibu Mbeya na Dare Es salaam Mwaka 2000 hadi Mwaka 2002.
UTUME
Sr. Crescentia amewahi kufanyakazi katika Convent ya Kyela akifanya Utume Parokiani mwaka 1984 na kusimamia mradi wa mashine ya kusaga katika nyumba ya watawa iliyoko Mlowo mwaka 1985. Msimamizi wa Jiko la Nyumba ya Utawala Jimbo Katoliki la Mbeya mwaka 1986 hadi mwaka 1989. Mlezi msadizi wa Wanafunzi wa Kitawa(Wanovisi) Mlowo mwaka 1993 hadi mwaka 1998. Mlezi Msaidizi wa Wanafunzi wa Kitawa - Kisa Aspiranti Mwaka 1999 hadi mwaka 2000.
Utume katika Convent Parokia ya Mwambani mwaka 2001. Utume Uaskofuni Convent akiwa Mama Mkubwa wa nyumba na Mhasibu Jimboni Mbeya mwaka 2002 hadi 2009. Utume Gua Convent akiwa Mama Mkubwa wa nyumba; Utume Parokiani na Mlezi wa Wawata 2009 – 2011.
Utume Jimbo kuu la Dar es Salaam akiwa Mama Mkubwa katika Convent ya Makoka, Mhasibu Sekondari ya Makoka na Chuo cha Ufundi cha Mwenyeheri Anwarite 2011 – 2014 hadi mauti yalipomfika.
Jimbo kuu la Dar es Salaam, Alhamisi asubuhi tarehe 26 Juni 2014 wanaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea na kumwaga Marehemu Sr. Crescentia Kaupili na baadaye msafara utaondoka kuelekea Jimboni Mbeya. Taarifa za awali zinasema mara baada ya kuwasili kwa mwili wa marehemu Sr.Cresensia utaingizwa katika makao makuu ya Shirika la Bikira Maria Malkia wa Mitume, Jimbo Katoliki la Mbeya.
Baada ya kutoka katika makao makuu ya Shirika safari itaanza kuelekea katika safari yake ya mwisho hapa duniani Sr.Cresensia katika shamba la Mungu la Masista maeneo ya Hasamba, wilayani Mbozi, mkoani Mbeya. Maziko yanatarajiwa kufanyika Jumamosi, tarehe 28 Juni 2014, Mama Kanisa atakapokuwa anaadhimisha Siku kuu ya Moyo Safi wa Bikira Maria.
Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umwangazie apumzike kwa amani, Amina.
No comments:
Post a Comment