Saturday, November 1, 2014

Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo Katoliki Mahenge.

Jimbo Katoliki la Mahenge, Tanzania, linaadhimisha kilele cha Jubilee ya miaka 50 tangu lilipoanzishwa kunako mwaka 1964 na Marehemu Askofu Elias Mchonde aliyekuwa Askofu msaidizi wa Jimbo la Dar es Salaam akateuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Mahenge na kuliongoza Jimbo hili kuanzia wakati huo hadi mwaka 1969 alipofariki dunia. Baadaye Jimbo limeongozwa na Askofu Nikas Kipengele tangu mwaka 1970 hadi mwaka 1971; Askofu Patrick Iteka kuanzia mwaka 1973 hadi mwaka 1993.
Askofu Agapiti Ndorobo akapewa dhamana ya kuwaongoza waamini wa Jimbo Katoliki la Mahenge tangu mwaka 1995 hadi wakati huu, Jimbo linapomwimbie Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani na sifa kwa kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya uwepo wake. Askofu Ndorobo ameliongoza Jimbo kwa miaka 19 sasa. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha: mafanikio na changamoto anazokabiliana nazo katika kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu Jimboni Mahenge.Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la Ifakara lililoanzishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2012 na Askofu Salutaris Melchior Libena kuteuliwa akuwa Askofu wake wa kwanza ni matunda ya Jimbo Katoliki la Mahenge ambalo hapo awali lilikuwa na Parokia 38 lakini baada ya kuligawa ili kurahisisha shughuli za kichungaji kwa Watu wa Mungu, sasa Jimbo Katoliki la Mahenge lina Parokia 22, likiwa na waamini zaidi ya 215, 000 lakini hapo awali lilikuwa na waamini 487, 000.

Askofu Ndorobo anasema kwamba, katika kipindi cha miaka 50 ya uwepo wa Jimbo Katoliki la Mahenge kumekuwepo na maendeleo makubwa katika medani mbali mbali za maisha, lakini zaidi ni upendeleo kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kuna vituo vya kutunzia wagonjwa wa kifafa, kituo cha wagonjwa wa Ukoma pamoja na kituo cha Watoto Yatima.

Jimbo Katoliki la Mahenge linamiliki na kuendesha Sekondari 5; Vituo vya Afya na Zahanati 9 na kwamba kuna mpango mkakati wa kuanzisha Hospitali ili kujibu kilio cha watu wenye shida na mahangaiko wanaolazimika kutembea umbali mrefu ili kutafuta tiba kwa magonjwa yanayowasumbua, lengo ni kuendelea kutangaza Injili ya Uhai, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Askofu Ndorobo anakiri kwamba, Jimbo la Mahenge limeendelea kuwa na miito mbali mbali ya maisha ya: Kipadre, Kitawa na Ndoa. Kuna vyama vya miito vinavyosaidia mchakato wa malezi ya miito ndani ya Kanisa, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, unaowachangamotisha vijana kupenda kushiriki katika maisha ya Kipadre, Kitawa na Ndoa takatifu.

Askofu Ndorobo anasema miaka 19 ya utume wake kama Askofu wa Jimbo Katoliki Mahenge amekumbana na changamoto nyingi, lakini katika mahojiano na Radio Vatican anagusia changamoto kuu mbili, yaani umuhimu wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo na Maisha ya Sala na Kisakramenti. Anasema, kwa miaka hii yote amependa kukazia umuhimu wa waamini kushiriki katika maisha ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo kwani hizi ni shule ya Sala, Neno la Mungu na kielelezo cha imani tendaji.

Huu ndio mwelekeo ambao anapenda kuuendeleza hata baada ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo Katoliki Mahenge. Anasema, amependa kukazia umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika maisha ya Sala na Sakramenti za Kanisa ili waweze kujichotea neema na baraka; waweze kuonja huruma na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kufanya mabadiliko ya kina katika maisha yao, kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Viongozi wawe ni mfano bora wa maisha ya sala na Sakramenti za Kanisa, ili wao wakiishaimarika, waweze pia kuwaimarisha ndugu zao katika imani, matumaini na mapendo.

No comments:

Post a Comment

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR