Tunakuletea
habari njema ya furaha tunapotafakari pamoja Neno la Mungu katika
sherehe ya Watakatifu wote. Mama Kanisa akitaka kuhitimisha mwaka wa
Kanisa kwa furaha anaona ni vema awaoneshe watoto wake lengo la maisha
ya kikristu yaani ni kuelekea maisha ya utakatifu, maisha ya ya milele
mbinguni.
Kumbe,
Mama Kanisa amependa kila tarehe 1Novemba ya kila mwaka, sherehe hii
iadhimishwe katika Kanisa zima la ulimwengu. Adhimisho hili ni mwaliko
kwetu kuchuchumalia maisha yanayotimiza mapenzi ya Mungu, maisha ya
ufufuko ambayo Mtume Paulo anatuambia daima akisema basi mkishafufuliwa
mkayatazame yaliyo ya juu!
Mpendwa, yafaa kutambua watakatifu ni
akina nani? Watakatifu ni wale wanaokaa na Mungu katika kiti chake cha
enzi kadiri tusomavyo katika kitabu cha Ufunuo. Ni marafiki wa kweli au
tunaweza kusema ni marafiki wa dhati au wa kina. Katika lugha yangu ya
kihaya Watakatifu tunaweza kuwalinganisha na “Abatahanju” yaani wale
ambao huingia ndani ya nyumba mpaka sebule ya nyuma na hata jikoni.
Ni
wale ambao hula chakula pamoja na mkuu wa familia, na hivi wanafurahi
pamoja na Mungu Baba huko mbinguni. Ni wale ambao Injili ilikuwa chakula
chao cha kila siku walipokuwa duniani na walijikabidhi katika mikono ya
Mungu na kuwa mali yake. Ni wale walioishi heri nane mafundisho ya
Kristu aliyoyatoa pale mlimani. Ni wale ambao walitunza neema ya UTAKASO
waliyoipokea wakati wa Ubatizo.
Ni wale ambao walimpenda Mungu
kwa moyo wao wote, kwa akili yao yote na kwa nguvu zao zote na kisha
wakampenda jirani aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni wale ambao
katika ubinadamu wao walikubali mateso wakitambua na kujua siri ya
furaha watakayoipata milele. Sasa wanafurahia matunda ya msalaba wa
Kristu. Kwa kifupi ni wale walioshika vema amri kuu ya mapendo.
Ili
basi nasi tuweze kufikia hali hiyo iliyo heri na furaha upeo, somo la
kwanza linaweka mwaliko kwa watu wote kuwa, ili mmoja aweze kupokea heri
za milele yaani utakatifu, ni lazima kufua mavazi katika Damu ya
Mwanakondoo. Ni lazima kukinywea kikombe kimoja cha Damu Takatifu iliyo
thamani ya wokovu kwa wote. Ndiyo kusema ni kuishi kwa kutimiza mapenzi
ya Mungu.
Kwa kufua mavazi katika Damu ya Mwanakondoo
kunamwondoa mtu katika dhiki ya dhambi na dhiki ya upungufu wa upendo
mkamilifu. Mmoja ananyakuliwa toka taabu ya ulimwengu geugeu na kuvikwa
mavazi meupe ndiyo utakaso mkamilifu unaowezesha kuimba baraka na
utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu
wetu hata milele na milele. Amina. Huu ni wimbo wa sifa kwa Mungu ambao
unaweza kuimbwa na walio wake, ndiyo watakatifu.
Katika Injili ya
Mathayo tunapata mafundisho ya Yesu mlimani yaani Heri Nane. Bwana
anaonesha njia ya kufikia utakatifu, njia ya kuishi mapenzi ya Mungu.
Anaainisha namna ya kufika mbinguni, akisema, wanaheri wale walio
maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao. Wanaheri wenye upole
maana watairithi nchi. Anazidi kukazia utakaso wa roho akisema heri
wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu. Hizi ni baadhi ya heri nane
za mlimani njia kamilifu ya kufikia utakatifu.
Kwa kuzitafakari
heri nane tunaweza kusema mambo makuu mawili ni lazima katika kufikia
utakatifu. Jambo la kwanza ni kujitenga na chachu ya ulimwengu. Kumbuka
Bwana anasali na kusema tuko ulimwenguni lakini sisi si wa ulimwengu.
Hii yamaanisha kujitenga na kile kinachopingana na injili ya Bwana, na
hivi kuwa maskini wa roho. Kumbe mkristu anapaswa ajisikie daima kinyume
na mawimbi ya ulimwengu yanayopingana na Injili. Jambo la pili ni lile
la kupokea kikombe cha mateso daima na kulitangaza jina la Bwana.
Mateso
haya hugeuka na kuwa furaha katika maisha ya mkristu sasa anapoishi na
baadaye. Mtakatifu lazima aoneshe sura ya Kristu mteswa na mwenye furaha
kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Mtakatifu ni lazima amwilishe Heri
Nane katika maisha yake na hivi zingae daima na kuwa kielelezo cha
maisha ya upendo. >>>>Endelea hapa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
-
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya...
-
Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza anatualika kutambua kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya ...
-
Isidore Bakanja, ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya imani ya Kikristo, Akiongozwa na maisha rahisi kama layman Katoliki wakati wa mauaj...
No comments:
Post a Comment