Kanisa litakianza kipindi cha Kwaresima hapo tarehe 18 Februari 2015 kwa kupakwa majivu, mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2015 unaongozwa na kauli mbiu "Imarisheni mioyo yenu" kwa kutambua kwamba, kila mtu anapendwa na Mwenyezi Mungu na anamfahamu kila mtu kwa jina na hata pale mwanadamu anapokengeuka, Mungu bado anamtafuta.
Read More
Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotisha waamini kuupokea na kuukumbatia upendo wa Mungu unaowatangulia daima kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye aliyeanza kwanza kumpenda binadamu na anaendelea kuliimarisha pendo lake na kwamba, ni wajibu wa waamini kuhakikisha kwamba, wanawasaidia jirani zao, kwa kuwashirikisha upendo ambao wamejichotea kutoka kwa Mungu na kuwawekea mbele yao, ili kuwahudumia hasa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Baba Mtakatifu anasema katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka huu kwamba, pale ambapo mwanadamu anaishi kwa raha mustarehe, anakuwa na kishawishi cha kuwasahau jirani zake wanaoteseka; katika shida na mahangaiko yao na kwa kutotendewa haki. Katika mazingira kama haya, moyo wa mwanadamu unatumbukia katika hali ya kutoguswa na mahangaiko yao, kishawishi kikuu kinachotoka kwa Shetani ambaye anaendelea kujiinua hadi amepata utambulisho wa kimataifa.
Hapa Baba Mtakatifu anazungumzia tabia ya ubinafsi kama utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Ni mtu yule tu ambaye aliwezeshwa kusafishwa miguu na Yesu anaweza kuwa ni sehemu yake kwa kushiriki kikamilifu katika kuwahudumia jirani zake. Lakini kwa wale wanaoelemewa na ubinafsi wao, wanajifungia ndani mwao, kiasi cha kushindwa kuwahudumia jirani zao.
Wakristo wanapaswa kutambua na kuonja upendo mkamilifu ulioneshwa na Yesu mwenyewe aliyejitaabisha kuinama na kuwaosha mitume wake miguu; ni kielelezo cha pendo kuu ambalo Yesu analionesha kwa umaskini wa binadamu. Kuna haja kwa waamini kujiachilia mikononi mwa Yesu, ili aweze kuwaosha miguu, yaani kuonja upendo wake unaoponya licha ya mapungufu yanayoweza kujitokeza katika kumpenda Kristo. Watu wanaweza kuonja upendo huu, kwa njia ya Kanisa na ndani ya Kanisa Mkristo anaweza kumwachia Mwenyezi Mungu kumvika wema na huruma yake na hivyo kumwezesha kuwa na uwezo wa kuwaosha wengine miguu yao; kwa kujisadaka kwa ajili ya Mungu na binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Wakristo kujenga na kudumisha moyo wa upendo na mshikamano wa dhati, ili kuachana na utamaduni usioguswa na shida pamoja na mahangaiko ya watu, kwa kutambua kwamba, wote ni viungo vya Fumbo la mwili huo mmoja, yaani Kanisa. Kila aliye wa Kristo ni sehemu ya Fumbo la Mwili wake, kumbe hapaswi kuwageuzia jirani zake kisogo. Baba Mtakatifu anasema... "na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho."
Hii ndiyo dira ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuionesha katika maisha ya Jumuiya na Parokia mbali mbali. Anauliza maswali ya msingi, ikiwa kama wanajumuiya wanajisikia kuwa ni sehemu ya mwili huo mmoja? Mwili ambao kwa pamoja unapokea na kushirikishana kile ambacho Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha. Mwili unaotambua na kuwawajibikia, maskini, wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Au wote wanajifunika katika "blanketi" la upendo wa juma kwa kujishughulisha na malimwengu kwa kumsahau Lazaro ambaye ameketi pembeni mwa mlango wao uliofungwa?
Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo kumwilisha upendo katika uhalisia wa maisha yao, kwa kushikamana na Kanisa la mbinguni kwa njia ya sala, ili kujenga na kuimarisha mahusiano kati ya Kanisa linalosafiri hapa duniani na Kanisa la mbinguni; umoja unaojikita katika huduma na mafao ya wengi na kuhitimishwa kwa kumfahamu Mwenyezi Mungu. Kanisa linalosafiri na Kanisa la mbinguni yanashirikiana ili kuhakikisha kwamba, hakuna mtu duniani ambaye anateseka au kuomboleza, ili furaha ya ushindi wa Kristo Mfufuka iweze kufika hata mbinguni kama anavyosema Mtakatifu Theresa wa Lisieux.
Kwa upande mwingine anasema Baba Mtakatifu Francisko, Kanisa kwa asili ni la Kimissionari na kwamba, linatumwa kwa watu wote na kamwe lisijitafute lenyewe na kwamba, Jumuiya ya Kikristo inachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inavuka mahusiano yanayojikita katika jamii inayowazunguka, kwa kuwaangalia maskini na wale walioko mbali zaidi.
Jitihada hizi zinapaswa kutekelezwa na kila mwamini mmoja mmoja, kwa kushinda kishawishi cha kuwageuzia wengine kisogo kwa njia ya sala, matendo ya huruma, ili daima mioyo ya waamini iendelee kumwongokea Mwenyezi Mungu ambaye ni mwenye nguvu, mwingi wa huruma, makini na mkarimu, ambaye hawezi kujifungia ndani mwake!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
-
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya...
-
Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza anatualika kutambua kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya ...
-
Isidore Bakanja, ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya imani ya Kikristo, Akiongozwa na maisha rahisi kama layman Katoliki wakati wa mauaj...
No comments:
Post a Comment