Thursday, March 21, 2013

KIPINDI CHA KWARESIMA

Bibilia na Kipindi cha Kwaresima

Katika Agano la Kale Musa ndiye aliyeongoza Waisraeli. Sisi tunakumbuka na kufuata safari yao ya ukombozi, walipokaa jangwani miaka 40 ili kuelimishwa kinaganaga juu ya yale yatokanayo na maneno 10 ambayo Musa alipewa na Mungu alipofunga siku 40 juu ya mlima Sinai.
Hayo yalikamilishwa na Yesu katika Agano Jipya kama kiongozi na mkombozi wa wote. Kabla hajaanza utume wake, yeye pia alifunga siku 40 jangwani akijilisha matakwa ya Baba ili ayatekeleze na kuwatangazia watu wote.

Juhudi za Kwaresima

Kufuatana na hayo yote Kanisa linafunga siku 40 katika jangwa la kiroho. Wakati wa Kwaresima linawaongoza waamini katika safari ya kujirekebisha kulingana na Neno la Mungu la Agano la Kale na la Agano Jipya. Wote wanahimizwa kufunga safari hiyo kadiri ya hali yao: kwanza wale wanaojiandaa kubatizwa usiku wa Pasaka (hasa kwa kufanyiwa mazinguo matatu yanayofuatana katika Dominika III, IV na V), lakini pia waliokwishabatizwa, ambao kabla ya hapo wanatakiwa kutubu na kuungama dhambi ili warudie kwa unyofu ahadi za ubatizo.
Makundi yote mawili watakula pamoja Mwanakondoo ili kuishi upya kwa upendo, jambo litakalofanya hata wasio Wakristo wafurahie Pasaka.
Kazi za urekebisho zinahitaji juhudi za pekee. Vivyo hivyo kwa ukombozi wa kiroho Kwaresima inadai bidii nyingi pande mbalimbali: katika kufunga, kutoa sadaka, kusali na kusikiliza Neno la Mungu hasa wakati wa ibada. Hayo yote yanahusiana na kusaidiana.
Mkristo akijinyima chakula cha mwili anajifunza kufurahia zaidi mkate wa Neno la Mungu na wa ekaristi, tena anatambua zaidi anavyopaswa kuwahurumia wenye njaa na shida mbalimbali. Toba inahimizwa isiwe ya ndani na ya binafsi tu, bali pia ya nje na ya kijamii: itokane na upendo na kulenga upendo kwa kurekebisha kasoro upande wa Mungu (sala), wa jirani (sadaka) na wa nafsi yetu (mfungo).
Mfungo, yaani kujinyima tunavyovipenda na hata tunavyovihitaji, uwe ishara ya njaa yetu ya Neno la Mungu, ya nia yetu ya kushiriki mateso ya Yesu yanayoendelea katika maskini, ya kulipa kwa dhambi zetu na kuachana nazo. Sadaka inayotokana na sisi kujinyima inampendeza Mungu kuliko ile isiyotuumiza; msaada unaweza kutolewa pia kwa kutetea haki za binadamu dhidi ya wanyanyasaji. Sala inastawi kwa kusikiliza sana Neno la Mungu hasa kwa pamoja (katika familia, jumuia, liturujia n.k.). Ndiyo maana wakati wa Kwaresima Kanisa linazidisha nafasi za kulitangaza na hivyo kuelimisha wote kuhusu mambo makuu ya imani na maadili yetu.

Kwaresima katika liturujia.

Kuna mpangilio kabambe wa masomo ya Misa, hasa ya Dominika, ili wote wafuate hatua kuu za historia ya wokovu (somo la kwanza) na kuchimba ukweli wa ubatizo (mwaka A), agano na fumbo la Kristo (mwaka B) na upatanisho (mwaka C). Kwa njia hiyo tunatangaziwa jinsi Mungu anavyotuokoa; pia upande wetu kuanzia Dominika ya kwanza tunajielewa kuwa watu vishawishini ambao tunapaswa kushinda kwa kumfuata Yesu, si Adamu: kwenda jangwani ili kumtafuta Bwana na matakwa yake.
Kilele cha safari ya Kwaresima ni Dominika ya Matawi, tunapoingia Yerusalemu pamoja na Yesu anayekwenda kufa na kufufuka kwa ajili yetu. Liturujia ya siku hiyo ina mambo mawili: kwanza shangwe (katika maandamano), halafu huzuni (kuanzia masomo, ambayo kilele chake ni Injili ya Mateso).
Baada ya Kwaresima kwisha, tutapitia tena historia ya wokovu katika kesha la Pasaka ambapo hatua zote zinaangazwa na ushindi wa Kristo mfufuka.

JUMA KUU LA PASAKA

Juma kuu


Juma kuu ni juma la mwaka ambalo Ukristo unaadhimisha kwa namna ya pekee matukio makuu ya historia ya wokovu, kuhusiana na mwisho wa maisha ya Yesu huko Yerusalemu, uliofuatwa na ufufuko wake.
Katika madhehebu mengi, juma hilo linaanza na Jumapili ya matawi ambapo linaadhimishwa kwa shangwe tukio la Yesu Kristo kuingia huo mji mtakatifu kama mfalme wa Wayahudi huku akipanda punda na kushangiliwa na umati wa wafuasi wake, waliofurahia hasa alivyomfufua Lazaro wa Betania.
Lakini Yesu alieleza kuwa ufalme wake si wa dunia hii, na kuwa yeye hakuja kutumikiwa bali kutumikia na kutoa uhai wake uwe fidia ya umati.
Hivyo siku zilizofuata alikabili kwa hiari mateso na kifo kutoka kwa wapinzani wake na kwa mamlaka ya Ponsio Pilato, na hatimaye akafufuka mtukufu usiku wa kuamkia Jumapili.
Kabla ya hapo Yesu alijumlisha hayo matukio yajayo katika karamu ya mwisho aliyokula pamoja na mitume wake 12, akiwaachia agizo la kufanya daima karamu ya namna hiyo kama ukumbusho wake.
Basi, kuanzia Alhamisi kuu jioni hadi Jumapili ya Pasaka jioni Wakristo wanaadhimisha siku tatu kuu za Pasaka, zinazofanya ukumbusho wa Yesu mteswa, mzikwa na mfufuka.

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR