Monday, November 10, 2014

semina ya awali ya kongamano la ujirani mwema yawa chachu ya maandalizi

Mkufunzi wa Semina ya Utawala Bora na Ujasiriamali, Ndugu Dniho alisema juzi kwenye ufunguzi wa semina kuwa; vijana ni tumaini la Kanisa na Jamii kwa ujumla.  
  
Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, kuna kundi kubwa la vijana wanaokimbilia mijini kutafuta riziki ya maisha, lakini mazingira wanamoishi ni hatari na ya kukatisha tamaa kiasi kwamba, vijana wanakosa dira na mwelekeo katika maisha.

Majiundo na malezi makini ni muhimu sana kwa vijana, ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya Jamii zao. Elimu ni ufunguo wa maendeleo na matumaini kwa vijana, lakini kuna haja ya kuwezeka na kuboresha zaidi mfumo wa elimu nchini Tanzania ili vijana waweze kuelimishwa barabara, kwani wao ni matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Shule za kata au sekondari zisiwe ni "mazizi" ya kuwakusanyia wanafunzi, bali mahali maalum pa vijana kuweza kupata: ujuzi, maarifa, maadili na utu wema. Hii ni changamoto kwa wadau mbali mbali wa elimu nchini Tanzania, kuhakikisha kwamba, wanafanya maboresho makubwa katika mfumo wa elimu, kwani matokeo ya mitihani ya hivi karibuni ni aibu kubwa kwa taifa linalotaka kuwekeza kwa vijana. 

Walimu wanapaswa kutambua dhamana na wajibu wao katika malezi na makuzi ya vijana wanapokuwa shuleni. Watambue kwamba, wana mchango mkubwa katika utoaji wa majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya. .
Ndugu Dniho, anasema kwamba, watanzania wengi ni watu wa kawaida kumbe, hawana uwezo wa kuwapeleka watoto wao katika shule za binafsi. Vijana popote pale walipo wahakikishiwe kwamba, wanapata elimu bora na wala si bora elimu ili kuweza kupambana na mazingira pamoja na changamoto za maisha kwa siku za usoni. Hii inatokana na ukweli kwamba, elimu ndiye mkombozi wa maskini!

Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Familia, Mama Kanisa anaendelea kukazia umuhimu wa malezi bora kwa vijana katika Familia , ili waweze kuja kuwa na Familia bora zenye misingi ya Imani ya  Kristo na Kanisa lake. Mikakati ya malezi ya vijana ipewe msukumo wa pekee katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.

Vijana wakifundwa barabara na kuwa ni Wakristo wema, hapana shaka kwamba, watakuwa pia ni raia wema watakaojenga na kuimarisha misingi bora ya kifamilia, hapa familia zitakuwa ni viota vya miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Malezi bora na makini ni ujenzi wa Jamii bora kwa sasa na kwa siku za usoni.

Ndugu Dniho, anasema, vijana wasaidiwe kuwa ni watu kadiri ya mpango wa Mungu. Jamii na Kanisa ni wadau wakubwa katika ujenzi wa vijana wa kizazi kipya katika medani mbali mbali za maisha. Elimu na malezi bora yapewe msukumo wa pekee katika maisha ya vijana.
Ndugu Kijana Nazidi kukualika uungane nasi Siku ya Ijumaa tarehe 28/11 mpaka Jumamosi tahere 29/11/2014 kwenye semina Muhimu sana ya Mwaka wa Familia na Elimu ya Ujasiriamali.

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR