Monday, March 30, 2015

UJUMBE WA BABA MTAKATIFU SIKU YA VIJANA (JUMAPILI YA MATAWI 29/03/2015)

Heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo inayoadhimishwa na Mama Kanisa, Jumapili ya Matawi tarehe 29 Machi 2015 kama sehemu ya maandalizi ya Siku ya 30 ya Vijana Kimataifa itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Cracovia, Poland, mwezi Julai 2016.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa maadhimisho ya Siku ya vijana kijimbo anagusia hamu ya vijana kuwa na furaha na anaendelea kuchambua kwa kina na mapana kauli mbiu ya ujumbe huu kwa kuwakumbusha vijana kwamba, Kristo ni utimilifu wa furaha ya mwanadamu, changamoto kwa vijana kuhakikisha kwamba, wanatunza ndani mwao moyo safi na kamwe wasibeze upendo wa dhati.

Baba Mtakatifu anawataka vijana wakati mwingine kwenda kinyume cha mawimbi ya maisha ya ujana, kwa kutambua kwamba, fainali iko uzeeni. Wawe ni watu makini katika maisha na maamuzi yao na kamwe wasikubali na kumezwa na malimwengu kwani watajikuta wapweke na hawana matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Vijana katika maisha waoneshe ari na moyo wa kupenda kwa dhati.

Hija ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa huko Cracovia, Poland inaongozwa na Hotuba ya Heri za Mlimani, ambayo kimsingi ni muhtsari wa mafundisho makuu ya Yesu, chemchemi ya furaha ya kweli na amani ya ndani. Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, kila mtu duniani yuko kwenye mchakato wa kutafuta furaha ambayo inapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayeijaza mioyo ya waja wake, kama yanayobainisha Maandiko Matakatifu, kielelezo cha umoja na mshikamano kati ya mwamini na nafsi yake; mwamini na Mungu pamoja na jirani zake.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, dhambi ilipoingia ulimwenguni, ilichafua usafi wa mioyo ya binadamu, kiasi kwamba, dhambi ikawa ni kizingiti cha mwanadamu kuweza kukutana moja kwa moja na Muumba wake; furaha ya kweli ikakosa dira na mwelekeo sahihi; mwanadamu akatumbukia katika huzuni na mahangaiko ya ndani. Mwanadamu akamlilia Mwenyezi Mungu, naye akakisikia kilio chake na kumtuma Mwanaye mpendwa, Yesu Kristo ili aweze kumfungulia mwanadamu malango mapya ya kukutana na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaambia vijana kwamba, ni kwa njia ya Yesu Kristo wanaweza kupata utimilifu wa wema na furaha ya kweli. Yesu Kristo ndiye mwenye uwezo wa kuzima kiu ya matarajio ya vijana katika maisha, ambao wakati mwingine wanadanganywa na malimwengu kwa kuwapatia njia za mkato.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa anawaalika vijana kuhakikisha kwamba, wanatunza usafi wa moyo kwa kujenga na kudumisha mahusiano mema na matakatifu kati yao na jirani zao. Moyo wa mtu n ikisima cha mawazo na vionjo, changamoto kwa vijana kuhakikisha kwamba, mawazo yao yanakuwa safi pasi na mawaa mbele ya Mungu na binadamu. Moyo safi wenye uwezo wa kujenga mahusiano bora.

Baba Mtakatifu anawaalika pia vijana kujenga utamaduni wa kutunza mazingira kwani hii ni sehemu ya ekolojia ya binadamu, ambayo inapaswa kuwa kweli ni safi, kama kielelezo makini cha mahusiano bora  kati ya mwamini na Muumba wake pamoja na kazi ya uumbaji ambayo Mungu amemkabidhi mwanadamu kuitunza na kuiendeleza. Vijana waonje upendo wa Mungu anayewaangalia kama mboni ya jicho lake!

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, ujana ni moto wa kuotea mbali; ni wakati ambapo mbegu ya upendo ambao unajikita katika ukweli, wema na ukuu unaanza kuchanua pole pole katika maisha ya vijana. Baba Mtakatifu anawaangalisha vijana kuwa makini ili mbegu hii ya upendo isije ikachafuliwa na hatimaye kuharibiwa. Hapa vijana wanatakiwa kuwa makini na kamwe wasikubali kuyumbishwa na mawimbi ya maisha ya ujana kwa kubeza upendo, kiasi cha kuugeuza kuwa ni mahali pa kukidhi tamaa za mwili. Lakini ikumbukwe kwamba, upendo wa kweli unajikita katika wema, umoja, uaminifu na uwajibikaji. Vijana wanapaswa kuwa ni wana mapinduzi kwa kwenda kinyume na mawimbi haya potofu na dhidi ya utamaduni wa raha za mpito ambazo mara nyingi zimewaachia vijana machungu katika maisha.

Vijana wawe waaminifu na kuwajibika barabara kwa kuonesha jeuri kwamba, wanafahamu kupenda kwa dhati. Baba Mtakatifu anasema, ana imani kubwa na vijana na kwamba, anawaombea, ili kamwe wasitindikiwe na ujasiri huu. Vijana wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa na Baba Mtakatifu kuhakikisha kwamba, wanamtafuta Mwenyezi Mungu kwa njia ya: sala, tafakari ya Neno la Mungu na upendo kwa jirani. Kusali ni kuongea na kujadiliana na Fumbo la Utatu Mtakatifu yaani: Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Vijana wajenge utamaduni na mazoea ya kusali vyema na daima.

Tafakari ya Neno la Mungu imwilishwe kwa njia ya upendo na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa njia hii, vijana wataonja na kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao; Mungu ambaye anaendelea kutekeleza mpango wake kwa maisha ya kila kijana. Vijana wamkimbilie Mwenyezi Mungu wakiwa na mioyo safi pasi na woga wala makunyanzi mioyoni mwao. Vijana wanaposikia kwamba, wanaitwa na Mwenyezi Mungu katika miito mitakatifu, wasisite kusema, Ndiyo na kwa njia hii wataweza kuwa kweli ni mbegu ya matumaini kwa Kanisa na jamii inayowazunguka. Vijana watambue kwamba, mapenzi ya Mungu katika maisha yao ndicho kiini cha furaha yao ya kweli.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya Vijana Kimataifa katika ngazi ya kijimbo inayoadhimishwa Jumapili ya Matawi kwa kumshukuru Mtakatifu Yohane Paulo II ambaye miaka thelathini iliyopita alithubutu kuanzisha ndani ya Kanisa Siku ya Vijana Kimataifa. Hii ni hekima ya Kimungu na sauti ya kinabii ambayo imeliwezesha Kanisa kuwashirikisha vijana wengi matunda ya maisha ya kiroho. Mtakatifu Yohane Paulo II msimamizi wa Siku za Vijana Kimataifa, awaombee vijana wakati huu wa maandalizi kuelekea katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa itakayofanyika Jimbo kuu la Cracovia, nchini Poland. Bikira Maria aliyejaa neema, uzuri na usafi wote, awasindikize vijana katika hija hii.

Tazama aleleya kuu hapa

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR