Showing posts with label Kardinal Pengo. Show all posts
Showing posts with label Kardinal Pengo. Show all posts

Tuesday, June 24, 2014

Kardinali Pengo aweka jiwe la msingi la Chuo Kikuu MUCO Bagamoyo!

Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaendelea kuwekeza kikamilifu katika sekta ya elimu ili kuwasaidia watanzania kuwa na majiundo kamili ili kukabiliana barabara na changamoto za maisha, ili hatimaye, Tanzania iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Shirika la Roho Mtakatifu ambalo kwa miaka mingi limewekeza na kuona mafanikio makubwa katika sekta ya elimu nchini Tanzania, sasa limeanza kujielekeza katika kuanzisha Kitivo cha Sayansi kitakachokuwa chini ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino cha Tanzania, SAUT. Kitivo hiki kitajulikana kama “Marian University College”, kwa kifupi MUCO, ambacho kinajengwa kwenye mji mkongwe wa Bagamoyo, Mkoani Pwani, nchini Tanzania.

Hivi karibuni, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo kikuu cha MUCO na kwamba, mwezi Septemba, 2014 kitaanza kuandikisha wanafunzi, wakati huo huo ujenzi wa majengo mengine ukiendelea kukamilishwa hatua kwa hatua. Katika hafla ya kuweka jiwe la msingi, Kardinali Pengo amesema, nchi ambayo haina wataalam wa sayansi, kwa hakika itachechemea katika ushindani wa maendeleo na mataifa mengine. Umefika wakati kwa watanzania kujiekeza zaidi katika masuala ya kisayansi ili kupata maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili.

Akizungumza katika tukio hili Padre Florentin Mallya, Makamu mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu Afrika Mashariki amesema, MUCO itaendelea kushirikiana na SAUT, hadi pale mchakato wa kukiwezesha Chuo kikuu cha MUCO kujitegemea na kuwa Chuo kikuu kamili. Kuanzishwa kwa MUCO ni kujibu kwa dhati changamoto inayotolewa na Serikali ya Tanzania kwa sekta binafsi kusaidia mchakato wa kukuza na kuendeleza sekta ya elimu hususan katika mchepuo wa sayansi, ili kujibu mahitaji makubwa yanayoendelea kujitokeza ndani na nje ya Tanzania katika masuala ya elimu.

Huu ni mwendelezo wa huduma ya elimu inayotolewa na Shirika hili katika shule zake za awali na sekondari ambazo kwa miaka mingi zimeendelea kupeta nchini Tanzania kutokana na wanafunzi wanaohitimu katika shule hizi kuwa na kiwango kikubwa cha ufaulu kwenye mitihani. Wazazi waliokuwa wanahaha kuwatafutia watoto wao mahali pazuri zaidi pa kusoma, sasa MUCO itakuwa ni jibu lao makini.

Ni kutokana na changamoto zote hizi, Shirika la Roho Mtakatifu liliomba ushirikiano na Serikali ya Tanzania ili kutekeleza azma hii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania tangu shule za msingi hadi chuo kikuu. Shirika linapania kuendelea kutoa kiwango bora cha elimu kwa kutambua kwamba, hii ni sehemu ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Shirika linaiomba Serikali ya Tanzania pamoja na wazazi kuendelea kuonesha mshikamano katika kufanikisha malengo ya maboresho ya elimu nchini Tanzania.

Monday, October 28, 2013

MJUE Kardinal Polycarp Pengo

Polycarp Pengo ni kardinali wa pili kutoka Tanzania, akiwa aliteuliwa mara baada ya kifo cha Laurean Rugambwa, kardinali wa kwanza kutoka kusini kwa Sahara.

Maisha yake.

Alizaliwa Mwazye (mkoa wa Rukwa) tarehe 5 Agosti 1944.
Baada ya masomo ya ngazi mbalimbali, alipewa upadrisho mwaka 1971 na Askofu Charles Msakila wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga, akasoma teolojia ya maadili huko Roma, Italia, akijitwalia digrii ya udaktari mwaka 1977.
Kisha kufundisha somo hilo kwa muda mfupi kwenye seminari kuu ya Kipalapala (mkoa wa Tabora), alichaguliwa kuwa gombera wa seminari kuu ya Segerea hadi mwaka 1983.
Aliteuliwa askofu wa Nachingwea tarehe 11 Novemba 1983, akapewa daraja takatifu hiyo na Papa Yohane Paulo II tarehe 6 Januari 1984.
Tarehe 17 Oktoba 1986 alihamishiwa jimbo jipya la Tunduru-Masasi.
Tarehe 22 Januari 1990 alifanywa askofu mwandamizi wa Dar-es-Salaam na mwaka 1992, kardinali Laurean Rugambwa alipojiuzulu, akawa askofu mkuu.
Aliteuliwa na Yohane Paulo II kuwa kardinali tarehe 21 Februari 1998, akikabidhiwa parokia ya Nostra Signora de La Salette mjini Roma.
Pamoja na majukumu mbalimbali katika idara za Papa, tangu mwaka 2007 hadi 2013 alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Afrika na Madagaska

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR