NILIPOKEA taarifa za masikitiko na zenye mshtuko mkubwa kwa njia ya simu kupitia kwa Paroko wa wanga PD. Dismas Mfungomali wa simu ya mkononi usiku wa manane kuamkia Oktoba 26, 2012 kuwa aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Kimisionari la Kanisa Katoliki la Consolata, Padri Salutarius Lelo Massawe (50) amezama baharini wakati akiogelea Bagamoyo na mwili wake haujaonekana.
Ilikuwa kama ni ndoto, wakati Jumapili iliyopita tulikuwa naye tukijiandaa na mkesha wa kimisionari kwa vijana wote wa jimbi la Dar es salaam, ambapo nililazimika kumpigia Mwenyekiti wa Mabalozi wa Vijana wa Consolata (CMC) Ndugu Machota , na kumuuliza, na yeye amepata habari jana.
Padri Massawe alifariki mjini Bagamoyo wakati akiogelea katika Bahari ya Hindi na wakuu wenzake wa Shirika la Consolata kutoka nchi mbalimbali waliokuwa na mkutano katika Kituo cha Kiroho cha Consolata kilichoko Bunju jijini Dar es Salaam. Baada ya mkutano aliwaeleza wenzake kuwa angependa wakapumzike Bagamoyo kwa kutembelea maeneo ya kimisionari sehemu ambapo Injili iliingia miaka ya 1800.
Walipofika Bagamoyo, walimaliza kutembelea makaburi, kanisa, na sehemu nyingine muhimu za kihistoria na kuamua kuanza kuogelea. Kwa mujibu wa padri aliyekuwa naye ni kwamba majira ya saa 10 jioni, waliamua kuondoka kwenye maji lakini Padri Massawe alitokomea kimya kimya ndani ya maji na hakuonekana hadi kesho yake asubuhi alipokutwa pembezoni mwa bahari kwenye mikoko.
Kutokana na kutokuwa mbinafsi, alionesha dhahiri moyo wa uzalendo kwa taifa lake. Kila mara alikuwa akiniambia ninatamani sana Watanzania wawe matajiri wote, nisione masikini wakitaabika hasa kulala njaa. Ni vigumu kutamka au kuandika sifa zake zote, Padri Massawe licha ya kuwa alikuwa Mkuu wa Shirika la Kimisionari la Consolata hapa Tanzania wadhifa aliokabidhiwa mwaka jana, pia alikuwa mwanahabari makini, aliyefanya kazi kwa kuzingatia misingi na weledi, huku akiamini kuwa habari njema siku zote humjenga binadamu kiafya na kiroho.
Alijitahidi kutumia jarida la kimisonari Enendeni linalotolewa mara nne kwa mwaka na shirika lake, yeye kama mhariri mkuu kuinjilisha, alitumia vyombo vya habari vya Tumaini Media, radio, TV na gazeti la Tumaini Letu kufundisha na kuwatia Wakristo moyo.
Padri Salus Lelo (kama tulivyozoea kumwita) ameishi Iringa ambako ndiko yaliko Makao Makuu ya wamisionari wa Consolata kwa kipindi cha takriban mwaka mmoja, hadi anafariki dunia lakini wananchi wa Iringa walionekana wenye majonzi mazito kuliko ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa naye siku zote sehemu nyingine. Hii inaonesha upendo wa dhati ambao aliwaonesha kwa muda mfupi.
Tunajiuliza ni nani kati yetu anayeweza kurithi tunu na vipaji alivyokuwa navyo Padri Salus Massawe? Je, mioyo yetu inatamani kupata neema kama ya kwake? Tulipofika Iringa eneo la Kanisa Kuu la Jimbo (cathedral) parokia ya Bikira Maria Consolata alfajiri 31, Oktoba 2012, ilikuwa ni simanzi, vilio vilivyorindima na kuwafanya umati wa ndugu tuliosindikiza msiba kutoka Dar es Salaam na Moshi kuanza kulia tena.
Waumini walikuwa wamekesha kanisani hapo kwa siku mbili, walipouona mwili wa kipenzi chao waliangua kilio kikubwa. Vilio hivi, vilifuatiwa na mazishi yaliyofanyika katika Parokia ya Tosamaganga, umati mkubwa ulishiriki, wananchi wa Iringa walitamka wenyewe kuwa tumempoteza kiongozi wa kabila letu, ‘Mtwa’ kwa Kihehe wakimaanisha chifu.
waamini , waliamua kumuwekea historia ya pekee kwa kumzika kwa heshima za kichifu wa kabila la Wahehe kwa kupigiwa mizinga 20 angani. Tulijiuliza hivi na mapadri wanapigiwa mizinga kama wanajeshi? Lakini hayo hata yeye hakujua kama yatatokea akifariki. Kifo cha Padri Massawe kinaweza kujengwa taswira nyingi miongoni mwa jamii. Ni kwanini yeye? Na ni kwanini pale Bagamoyo? Lakini yote tumuachie Mwenyezi Mungu.
Waliosoma naye SAUT wanasikitika hasa wanapokumbuka, uhamasishaji usio na kikomo wa Padri Massawe kwenye michezo, shughuli za kijamii, burudani, vikao, kuanzishwa kwa asasi ya kutetea uhai wa binadamu (Pro-Life) ambayo alikuwa mwasisi na mwenyekiti wa kwanza. Mashindano ya mpira wa miguu maarufu SAUT kama FAWASCO, alihakikisha darasa lake la ‘Mass Comm (2005-08)’ linachukua kombe na likafanya hivyo.
Jumapili jioni alikutana na kikundi cha wazaliwa wa Kibosho ‘Konkya’ waliokuwa wakiishi Mwanza na mikutano ilikuwa ikifanyika pale Kilimanjaro Hotel Mabatini, tukiwa naye. Wakati wa Misa Baba Askofu wa Jimbo la Iringa, Taracius Ngalalekumtwa, alieleza jinsi ambavyo Padri Massawe amefanikiwa kujenga mahusiano mazuri na jamii nje na ndani kila mara akionesha uso wa matumaini na mapendo.
Pamoja na upadri wake, kupangiwa kazi za ofisini, hata wakati wa masomo alikuwa padri anayejitahidi kukutana na makundi ya watu wote, wenye mali, wasio na mali, wenye elimu na wasio na elimu, alikuwa padri anayetambua utu wa kila mtu, kuhakikisha kila mwanadamu anayekutana naye anakuwa na amani na furaha moyoni. Mara kadhaa nilimpelekea watu walio kata tamaa na wenye changamoto mbalimbali za kimaisha, lakini walirudi na hali mpya, wamebadilika.
Huyo hakuwa padri anayegawa fedha, mali ila alikuwa akigawa upendo wa dhati, furaha, amani na matumaini. Ndiyo maana askofu anasema: ‘ Padri Massawe alikuwa zaidi ya padre kwani alitumikia nafasi yake kama mkuu wa shirika, mwalimu, padri, daktari na kiongozi wa kijamii huku akijitahidi kujenga mahusiano na kila anayepishana naye.
‘Usihesabu umri wako kwa miaka uliyonayo, hesabu umri wako kwa kuangalia watu ambao umehusiana nao vizuri. Padri Massawe alijitahidi kuhusiana vizuri na kila aliyepishana naye bila kujali dini, imani au kabila lake,’ anasema Baba Askofu.
Katika mkutano uliofanyika Bunju, ambao marehemu alikuwa mwenyeji, ulihudhuriwa pia na padri Mtanzania ambaye ni Makamu Mkuu wa Shirika la wamisionari Wakonsolata duniani, kutoka Roma, Padri Detrick Mpandawazima, ambaye walikuwa wote baharini na alishuhudia akifariki, alimtaja marehemu Padri Massawe kama kiongozi mwenye kipaji kikubwa ambaye bado alihitajika kulitumikia shirika hilo na taifa la Tanzania.
Tutamkumbuka kwa kujitahidi kuomba neema ya Mungu ili tuishi maisha mazuri ya kumtumikia Mungu. Kuishi maisha ya kujitoa kwa ajili ya wengine na kusambaza upendo wa Mungu.
sasa ni mwaka mmoja toka ututoke tunazidi kukumbuka kwa mengi ulifanya kwetu, Tunamuombea Mwenyezi Mungu aipokee Roho yake na ampumzishe kwa amani. Amina!