Miaka 10 tangu Mwenyeheri Maria de Mattias alipotangazwa kuwa Mtakatifu: Wanovisi wanne waweka nadhiri za kwanza Jimboni Dodoma
Kumbu kumbu ya miaka kumi tangu Mtakatifu Maria de Mattias kutangazwa kuwa Mtakatifu imesherehekewa na Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu kwa: Makongamano, Ibada ya Misa Takatifu na Mafungo ya kiroho.
Shirika la Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu nchini Tanzania limeadhimisha Kumbu kumbu hii kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma katika Kikanisa cha Makao Makuu ya Shirika hili, nchini Tanzania sanjari na Wanovisi wanne kuweka nadhiri zao za kwanza. Hawa ni Sr. Immaculata Sayumwe, Sr. Leticia Kisena, Sr. Maria Mrema pamoja na Sr. Theresia Mwendwa.
Katika Ibada ya Misa Takatifu, Askofu Nyaisonga amewataka watawa kulinda na kutunza thamani ya maisha na wito sanjari na kuienzi Damu Azizi ya Kristo mto wa rehema na chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake. Amewataka watawa kujiamini kwa kuwa Mwenyezi Mungu anaendelea kutembea pamoja nao katika hija ya maisha na imani. Watawa wanatakiwa kukumbuka kwamba, nadhiri zao ni bendera ya ushindi na mwenge unaowaangazia wengine nuru katika maisha.
Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na viongozi wa Kanisa, Watawa na Waamini walei kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Dodoma.