Showing posts with label UCHAGUZI 2015 CCM. Show all posts
Showing posts with label UCHAGUZI 2015 CCM. Show all posts

Monday, July 6, 2015

HATIMA YA TAIFA LETU: Siku saba za urais ndani ya CCM

Dodoma. Ni wiki ngumu kwa Chama cha Mapinduzi (CCM). Ndivyo unavyoweza kusema kwani chama hicho kinachotawala kitafanya vikao vyake vya juu vitakavyohitimishwa kwa kumpata mgombea wake wa urais.
Mchakamchaka utaanza na kikao cha Kamati ya Maadili keshokutwa kukutana. Tayari CCM imetangaza kuwa itatumia vigezo 13 ilivyojiwekea kuwachambua wagombea 38 waliochukua na kurejesha fomu ili kupata majina ya wachache watakaopigiwa kura na mkutano wake mkuu.
Awali, kulikuwa na watangazania 42 waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa na CCM, lakini wanne kati yao hawakurejesha fomu. Kamati Kuu itakayokutana Alhamisi itakuwa na kazi ya kuwachuja hadi kubakia wasiozidi matano yatakayopigiwa kura Ijumaa ijayo katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na kubaki matatu.
Katibu wa Baraza la Ushauri wa Wazee wa CCM, Pius Msekwa juzi alilieleza gazeti hili kuwa mbali na sifa hizo, suala jingine litakalotizamwa ni iwapo wagombea hao walikiuka kanuni na taratibu za uchaguzi wakati wote wa mchakato.
Majina matatu yatakayopitishwa katika kikao cha NEC ndiyo yatapigiwa kura na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM utakaokaa Julai 11 na 12 na kupata mwakilishi mmoja wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Uzoefu unaonyesha kuwa chama hicho huzingatia mambo mengi katika kufanya uteuzi, ikiwa ni pamoja na kutafuta mtu atakayeondoa makundi yaliyoundwa wakati wa uteuzi wa mgombea urais.
Baadhi ya mambo yanayotajwa kuwa yatakuwa karata muhimu katika mchujo huo ni suala la Muungano, jinsia, eneo la kijiografia, rekodi ya mtia nia na kukubalika kwa kada hasa katika kipindi hiki ambacho upinzani umeimarika. Hofu inayoonekana kukikumba chama hicho ni ya kumpata mgombea mwenye sifa na anayekubalika na atakayeweza kukabiliana vyema na yule atakayesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
Kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kwamba hana mgombea anayemuunga mkono kinaonyesha jinsi mchujo huo utakavyokuwa mgumu.
Kauli ya Takukuru
Kutokana na unyeti wa wiki hii, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah amesema vijana wake wako Dodoma na kuwatahadharisha wagombea wote kuzingatia sheria.
“Nawashauri wagombea wote wazingatie Sheria ya Gharama za Uchaguzi na Sheria ya Kupambana na Rushwa, wafanye mambo kistaarabu na ambaye atakwenda kinyume, sheria itachukua mkondo wake,” alisema.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema jeshi hilo limejiandaa vizuri kwa ugeni huo mkubwa.

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR