Showing posts with label Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa Siku ya 88 ya Kimissionari Duniani kwa Mwaka 2014.. Show all posts
Showing posts with label Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa Siku ya 88 ya Kimissionari Duniani kwa Mwaka 2014.. Show all posts

Saturday, October 18, 2014

Maadhimisho ya Siku ya 88 ya Kimissionari Duniani kwa Mwaka 2014

Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa Siku ya 88 ya Kimissionari  Duniani kwa Mwaka 2014.

Mama Kanisa tarehe 19 Oktoba 2014 anaadhimisha Siku ya 88 ya Kimissionari Duniani, iliyoanzishwa kunako mwaka 1926 na Papa Pio wa Kumi na moja na kuanza kuadhimishwa rasmi hapo mwaka 1927 kama siku ya kukoleza ari moyo wa kimissionari katika kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Hii ni siku ambayo inaadhimishwa mwezi Oktoba, ambao kimsingi ni mwezi wa kimissionari.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 88 ya Kimissionari Duniani kwa mwaka 2014 anasema kuna umati mkubwa wa watu ambao haujabahatika kusikia Habari Njema ya Wokovu, Familia yote ya Mungu inawajibika kushiriki katika Uinjilishaji kwa kutambua kwamba, Kanisa limeanzishwa na linatumwa kuwatangazia watu juu ya Ufalme wa Mungu.

Hii ni siku ambayo waamini wanaalikwa kushiriki kikamilifu kwa njia ya sala na sadaka yao ili kuonesha mshikamano na Makanisa machanga duniani kama njia ya kumshukuru Mungu kwa neema sanjari na kuonesha ile furaha ya ndani. Yesu anawatuma wafuasi wake na kuwategemeza katika shughuli za kimissionari kama inavyojionesha katika Maandiko Matakatifu pale alipowatuma wafuasi wake Sabini na wawili, wakarudi huku wakiwa wamesheheni furaha baada ya kutangaza kuhusu Ufalme wa Mungu na kuwaandaa watu kukutana na Yesu.

Mitume wanapoonesha furaha yao, Yesu anawataka wafurahi kwa sababu majina yao yameandikwa mbinguni na kwamba, wamebahatika kuyaona matendo makuu ya Mungu yakitendwa mbele ya macho yao! Hii si nguvu ya kutoa pepo wachafu, bali ile nguvu ya upendo ambao wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu. Uzoefu na mang'amuzi haya yanakuwa ni sababu ya furaha hata kwa Yesu Mwenyewe kiasi cha kumshukuru Roho Mtakatifu, huku akimtolea sifa Baba yake wa mbinguni, kwani ile siri kubwa kuhusu Ufalme wa Mungu iliyokuwa imefichika inajionesha kwa njia ya Yesu Kristo na ushindi wake dhidi ya shetani.

Hii ni siri ambaye imefunuliwa kwa maskini na wanyenyekevu wa moyo ambao wamebarikiwa mbele ya Mungu. Hawa ni kama Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, Wavuvi kutoka Galilaya na Mitume wote ambao wamebahatika kushikamana na Yesu wakati alipokuwa anawahubiria watu Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu anaonesha ile furaha inayobubujika kutoka katika undani wake kutokana na ufunuo wa mpango wa Mungu katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa mwanadamu kwa njia ya Yesu Kristo. Hii ndiyo furaha iliyokuwa inabubujika kutoka moyoni mwa Bikira Maria pale alipomtembelea binamu yake Elizabeti kumshirikisha kuhusu matendo makuu ya Mungu katika maisha yake.

Hii ndiyo furaha inayoendelea kububujika katika maisha ya waamini hadi nyakati hizi, anasema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya themanini na nane ya Kimissionari Duniani na kuwawezesha waamini kuingia katika maisha ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mungu Baba ni chemchemi ya furaha, Yesu Kristo ni kielelezo cha furaha hii na Roho Mtakatifu ndiye mwezeshaji mkuu, changamoto kwa waamini kumjifunza na kumwendea Yesu ili aweze kuwafariji na kuwakirimia maisha ya uzima wa milele, wale wote wanaobahatika kukutana na Yesu.

Wale wanaokombolewa na Yesu, wanaondolewa dhambi, hofu na "jangwa la maisha ya kiroho" kwani kwa njia ya Yesu, daima waamini wanaweza kupata na kuendelea kububujika furaha. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Bikira Maria pamoja na Mitume wake walioamua kubaki pamoja na Yesu ili kushiriki azma ya Uinjilishaji, Yesu akawa ni sababu ya furaha yao ya ndani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema ulimwengu mamboleo unakabiliwa na hatari kubwa ya kumezwa na ulaji wa kupindukia unaojikita katika ubinafsi, mambo yanayousononesha moyo wa binadamu kwa kutaka furaha za mpito pamoja na dhamiri mfu. Binadamu anachangamotishwa kujichotea wokovu ulioletwa na Yesu, wafuasi wake wakiwa wa kwanza kuguswa na upendo wake ili kuwa kweli ni vyombo vya Injili ya Furaha, ili kushiriki ile furaha ya uinjilishaji.

Maaskofu wana dhamana ya kwanza kabisa katika utekelezaji wa mchakato wa Uinjilishaji, kwa kujenga na kuimarisha umoja wa Kanisa mahalia na kuendeleza utume wa Kimissionari hadi miisho ya dunia, hasa katika maeneo yaliyoko pembezoni mwa dunia, huko ambako kuna maskini wanaosubiri kwa hamu kubwa kusikia Habari Njema ya Wokovu.

Upungufu wa miito ya Kipadre na Kitawa ni kielelezo cha Jumuiya kukosa ile furaha yenye mvuto na mguso, inayobubujika kwa mwamini kukutana na Yesu kwa kuwashirikisha pia maskini. Hii ni changamoto kwa Parokia na Vyama vya Kitume kuonesha ushuhuda wa udugu unaojikita katika upendo wa Yesu pamoja na kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Pale ambapo kuna furaha ya kweli, hapo pia kuna ari na moyo wa kutaka kuwashirikisha wengine, hapo ni mwanzo wa miito mitakatifu. Waamini walei wanahamasishwa pia kushiriki maisha ya kimissionari, ili kutangaza Injili, lakini wanahitaji majiundo makini.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Siku ya Kimissionari Duniani ikuze ndani ya waamini wajibu wa kimaadili wa kushiriki kwa furaha utume wa kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu, kwa kuchangia kwa hali na mali, kwa kutambua kwamba, sadaka hii ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa watu unaobubujika kutoka katika upendo.

Baba Mtakatifu anawataka waamini katika Makanisa mahalia kutokubali kupokwa ile furaha ya Uinjilishaji. Anawaalika kujizamisha katika furaha ya Injili kwa kuirutubisha kwa upendo. Furaha ya mfuasi wa Kristo inajionesha kwa kukaa na Yesu, mwamini anapotekeleza mapenzi ya Mungu na anaposhirikisha imani, matumaini na mapendo ya Kiinjili.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR