Sunday, November 2, 2014

Tabia ya Waamini kuvaa nusu Uchi kanisani

waamnini wanaopenda kuvaa mavazi mafupi kanisani
 
Waumini wa kanisa katoliki la St. Francis mjini Diani kusini mwa pwani ya Kenya walipigwa na butwaa baada ya baadhi yao kuzuiwa kuingia katika kanisa hilo kutokana na mavazi yao yaliokuwa nusu uchi.
Julia baraza ambaye alikuwa amevalia kisibao ,ukanda wa manjano na viatu vyenye kisigino kirefu alishangazwa na sheria hizo mpya ambazo zilimsababisha kukosa misa ya asaubuhi.
Kulingana na gazeti la the standard nchini kenya,Julia alisema kuwa watu wawili walimsimamisha nje ya mlango wa kanisa hilo na kumwambia kwamba mtindo wake wa mavazi ulipigwa marufuku katika kanisa hilo na kwamba ametakiwa kuvaa mavazi ya heshima.
Aidha wasichana waliokuwa wamevalia suruali walilazimishwa kujifunga leso juu yake.
Julia alisema kwamba iwapo makanisa yataanza kufuata sheria kama hizo basi wengi hawatahudhuria maombi.
Baadhi ya waumini wamesema kuwa mhubiri wa kanisa hilo aliyejulikana kama Joseph pekee alikuwa ametangaza katika ibada ya awali kwamba mavazi yasio ya heshima hayatakubalika katika kanisa hilo.

Van Gaal aapa kuishinda Mancity (Man City vs Man u)


Meneja wa kilabu ya Manchester United Louis Van Gaal anaamini kwamba timu yake itatumia fursa ya kushuka kwa soka ya kilabu ya Manchester City katika uwanja wa Etihad kuishinda kilabu hiyo.
Kilabu ya Manchester City imepoteza mechi zake mbili za mwisho baada ya kushindwa na West Ham na Newcastle.
''Kile tulichokiona katika mechi mbili za mwisho si matokeo ya kuridhisha,alisema Van Gaal.
''Tuna hisia njema kuhusu mechi hii''.''Tunahitaji matokeo mazuri na huenda yakawa dhidi ya Manchester City''.Aliongezea Van Gaal.
Timu za mancity na man United katika derby 
City iko katika nafasi ya tatu wakiwa nyuma kwa alama sita dhidi ya Chelsea.
Tangu ipoteze kwa mabao 5-3 dhidi ya Leicester mnamo Septemba 21,Manchester United haijapoteza na huenda ikaikaribia Mancity katika nafasi ya nne iwapo itashinda mchuano huu wa 'Derby'.
Hatahivyo ushindi dhidi ya Manchester United utakuwa wa nne kati ya timu hizo mbili hatua ambayo haijaafikiwa kwa takriban miaka 44 na timu hiyo.

Siku ya Marehemu tarehe 02/11(Mungu amewekeza siri ya upendo katika Fumbo la KIFO!)

Kifo ni kitendawili ambacho binadamu ameshindwa kabisa kukitegua. Anabaki kuhoji na kujihoji bila kupata jibu la kwa nini anakufa. Mbele ya kifo binadamu anabaki kutoa visingizio vya kujitetea na kulaumu, hatimaye anakiona kifo kuwa mwiko

Zamani mwiko ulikuwa masuala ya „mapenzi”, kumbe kifo na misiba hakikuwa kitu cha kuogopa sana. Lakini sasa ni kinyume, mambo ya mapenzi yamegeuka kuwa kitu cha kawaida kabisa isipokuwa kifo kimekuwa kiboko chetu.

Watu tunakiogopa na pengine hatutaki hata kukisikia. Tunapolazimika kwenda msiba basi tunawaachia wengine walipambe jeneza maua, nasi tukisubiri kwenda kutia sahihi kwenye kitabu cha maombolezo na kutoa rambirambi kwenye bahasha kisha kukaa mbani na jeneza huku tukizungumza chinichini. Sanasana tunajisahaulisha kwa kuimba nyimbo za maombolezo au kusikiliza nyimbo za Injili. Tunaogopa kabisa kukizungumzia kifo au walau kukijadili. Mbele ya kifo binadamu tunabaki kulaumiana, kushikana uchawi na hasa tunamlaumu Mwenyezi Mungu.

Mathalani, kuna baadhi ya wakristu wa kale hata wa sasa walisali na kuomba msaada kwa Mungu au kwa kupitia watakatifu fulani kusudi waepushwe na kifo. Sala hizo zinapoacha kupokelewa, binadamu anachukia, na kumlaumu Mungu. Kristu aliwahi pia kulaumiwa pale alipokataa mwito wa Marta na Maria walipomwomba aenda kwao kumponyesha kaka yao Lazaro aliyekuwa mgonjwa. Yesu akaenda huko kwa kuchelewa kusudi siku nne baada ya kifo. Siku ile alipojionesha msibani, Maria na Marta wakamjia juu na kumlaumu sana. “Bwana ungalikuwapo ndugu yetu asingalikufa”. Hata katika nafasi hiyo, bado hatutaki kulijibu swali ni sababu gani Yesu alifika duniani. Je Yesu alifika duniani ili kuendeleza uhai huu wa kibaolojia au kushinda mauti?

Tukitaka kujua ukweli wa mwenendo mzima wa maisha yetu, hatuna budi kuangalia pia hatima yake, yaani kuelewa kwamba maisha yetu yana mwanzo (yaani kuzaliwa) na yana ukamilifu wake. Ama sivyo tutaendelea kukiogopa kifo, nacho kitaendelea kupeta na kutuogofya zaidi.

Ndugu zangu, tulishukuru Kanisa limetutengea mwezi mzima wa Novemba tulioishauanza ili tukitafakari kitendawili hiki cha kifo. Asiyetaka kukitafakari kifo anaonywa na methali ya kiswahili isemayo: “Asiyejua kufa na atazame kaburi.” Kwa hiyo tunaalikwa pia kwenda makaburi mara nyingi kuwaona wenzetu walioishapambana na kifo, nao watatusaidia kutafakari vizuri zaidi fumbo hilo la kifo.

Hebu tujaribu kutafakari kidogo na kupata jibu stahiki juu ya kifo na hatima ya maisha yetu. Tuanze utafiti wetu na Wayahudi, hasahasa manabii na wanazaburi. Wenzetu walianza utafiti mpya juu ya kifo wakitegemeza hoja zao juu ya kitu hiki “upendo”. Yaani kama Mungu aliingia katika mahusiano na binadamu na kufanya naye maagano iwe kwa njia ya manabii wa aina yoyote ile ni kwa sababu Mungu alimpenda binadamu na hivi akataka kuwa na mawasiliano naye. Ukimpenda mtu kwa dhati, huwezi ukamwacha tu kienyeji.

Hiyo ndiyo sheria ya upendo. Kwa hiyo ukisema: “Mungu ninakupenda”, naye akikuambia “Ninakupenda”, basi upendo huo hauwezi kwisha. Namna hii ya kufikiri, ina nguvu sana katika maisha. Katika Agano la kale, Mungu anawaambia wayahudi: “Wewe una thamani machoni pangu, nami ninakupenda” (Isaya). Hapo yaonesha wazi kuwa Mungu anao mradi wa kumpenda kiumbe chake kwa sababu amemwumba. Kwa hiyo katika Injili, tunaona kuwa katika mradi huo, Mungu amewekeza katika upendo kwa njia ya udalali ambao ni yeye mwenyewe katika nafsi ya pili ya Mungu, Yesu Kristu.

Injili ya leo imechukuliwa toka mazungumzo juu ya chakula cha uzima Ekaristi. Mradi huo wa Mungu umeanishwa kwa neno moja tu “Mapenzi”. Neno hilo limetamkwa na Yesu karibu mara nne: “sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu”; halafu, “bali niyafanye mapenzi yake aliyenipeleka”; halafu tena “Mapenzi yake aliyenipeleka ni haya”; na mwisho “Kwa kuwa mapenzi yake baba yangu ni haya”.

Hebu tumwangalie kwa undani Dalali aliyekabidhiwa kutekeleza mradi wa Mungu kwa wanadamu anasema: “Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe”. Hivi ndiyo Mungu anavyomwaminisha Yesu mradi huo wa mapendo kwa binadamu. Mungu anauaminisha ubinadamu wote kwa Yesu bila masherti. Kwa hiyo ili kuelewa maana ya kifo na ukombozi toka kifo, yabidi tuingie katika mradi huo wa mahusiano ya upendo (mapenzi) na Yesu.

Hoja ya msingi ya kuingia katika mahusiano hayo ni ile anayoisema Yesu mwenyewe, “Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.” Hivi ni dhahiri kwamba Yesu amefika duniani kama dalali ili kutekeleza mradi wa Mungu, yaani kunadisha na kuendeleza mahusiano hayo ya upendo. Mungu amemdhamini Kristu mwanae mradi mzima wa upendo. Kama anavyothibitisha Yesu mwenyewe: “Mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho.” Hapo ndipo palipojaa uhondo! Maana yake bila Kristu, hatuwezi kupata jibu sahihi juu ya kifo, jibu linalookoa na kuelewa mwisho au hatima yetu. Na Yesu aliye mdhamini wa mradi huo hataki kujiangusha mwenyewe anaposema, “Katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho” anamaanisha kwamba atatuwapelekesha hao aliokabidhiwa hadi kieleweke.

Kufufuliwa siku ya mwisho, kadiri ya mwinjili Yohane haimaanishi mwisho wa dunia, bali ni Kalvario, juu ya msalaba siku ile anaposulibiwa na kufa. Tendo la mwisho la Yesu la upendo ni pale alipoitoa roho na maisha yake ya kimungu, nguvu ya upendo aliyoitolea yote kabisa wakati wa uhai wake na kuihitimisha pale msalabani. Siku hiyo ya mwisho anaitoa roho yake na maisha yale ya milele yanaingia kwenye mahusiano ya daima na Mungu, na maisha hayo hayana mwisho. Hayo ndiyo mapenzi ya Mungu.

Mradi huo unatekelezeka tu endapo tutamtambua Mungu katika Kristu: “Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”
Maana yake, upendo huo wa Baba utatekelezeka kwa namna tatu: kwanza kwa yule “amtazamaye Mwana,” kumbe yatubidi kuona au kutazama. Kuutazama au kuuona huu mradi wa Mungu na kumtambua Kristu ambaye ndiye mdhamini mkuu wa Mungu. Halafu yabidi “kumwamini Yesu”, yaani kutoa ushuhudi wa binafsi kwa huyo mdhamini pekee. Kisha matokeo ya kumtambua na kuishi kama alivyoishi huyo mdhamini yatakuwa ni “kufufuliwa naye”.

Kwa hiyo katika maisha yetu yatubidi tuyadhihirishe hayo mahusiano ya mapendo na Mungu kwa njia ya Kristu mdhamini wa mapendo. Kwa wale wenzetu walioishazaliwa kwa Baba, yaani waliofariki, wameutambua tayari uso wa Yesu na kumwaminia hivi sasa wamepokea maisha ya kimungu. Kwao hao sisi leo tunawapa ushirikiano kwa kuwa karibu sana nao, na siyo leo tu bali daima. Kama maisha yao hayakuwa makamilifu, sisi tuwaombee yaani kuwaonesha upendo, kwani Mungu amewekeza upendo katika Yesu Kristu.

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR