Bi. Anna Mghwira ni mwenyekiti wa kitaifa wa chama kipya cha siasa, ACT – Wazalendo. Alizaliwa tarehe 23 Januari 1959 katika hospitali ya mkoa wa Singida, Kata ya Mungumaji, Kitongoji cha Irao manispaa ya Singida Mjini. (Mwezi Januari mwaka huu ametimiza miaka 56).
Baba mzazi wa Anna alikuwa diwani na kiongozi wa TANU kabla ya CCM hadi mwaka 1985, mama yake alijishughulisha na kilimo na ufugaji na wazazi hawa kwa ujumla walijipatia watoto tisa, akiwemo Bi. Anna.
Bi. Anna Mgwira alianza safari ya kielimu katika shule ya msingi “Nyerere Road” mwaka 1968 – 1974 akaendelea na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Ufundi Ihanja kati ya mwaka 1975 – 1978 kabla ya kuhitimisha masomo ya juu ya Sekondari (Kidato cha V na VI) Lutheran Junior Seminary kati ya mwaka 1979 – 1981.
Anna aliendelea na masomo ya Chuo Kikuu mwaka 1982 baada ya kujiunga Chuo Kikuu cha Thiolojia (Chuo Kikuu cha Tumaini) na kuhitimu shahada ya Thiolojia mwaka 1986.
Mwaka huohuo 1986 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam akitafuta shahada ya Sheria na akaimaliza na kutunukiwa mwaka 1986.
Kati ya mwaka 1987 – 1998, Bi Anna aliendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa, akifanya kazi ndani na nje ya nchi na kupata uzoefu mkubwa sana.
Safari ya Elimu ya Bi. Anna ilikamilikia Chuo Kikuu cha Essex nchini Uingereza ambako alianza shahada ya uzamili ya sheria (LLM) mwaka 1999 na kutunukiwa mwaka 2000.
Licha ya kuwa mwanasheria na mtheologia aliyebobea, pia amefanya kazi za maendeleo kwa muda mrefu na ana uzoefu katika uendeshaji wa serikali za mitaa, uzoefu wa utumishi katika mashirka ya kimataifa, kitaifa na mashirika ya dini ambamo amejihusisha na masuala ya wanawake, watoto, wakimbizi, utawala na haki za binadamu.
Anna ana historia ya kupenda siasa, masuala ya jamii na michakato ya maendeleo kama inavyojidhihirisha katika maandiko yake mbalimbali katika majarida na magazeti ya hapa ndani ya nchi.
Alianza siasa tangu wakati wa TANU akiwa ni mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu Youth League) na aliwahi kushinda tuzo mbalimbali kutokana na ushiriki wa juu katika TANU lakini baadaye ilipoanzishwa CCM alipunguza ushiriki wake ili ajipe muda katika masomo na baadaye ndoa na malezi ya watoto.
Kwa kipindi kirefu hakuwa anajihusisha na siasa hadi alivyoamua kujiunga na CHADEMA mwaka 2009 ambako alishika nafasi mbili tu za Uenyekiti wa baraza la wanawake ngazi ya wilaya na Katibu wa Baraza la wanawake Mkoa.
Mwezi Machi 2015 alijiunga rasmi na chama cha ACT – Wazalendo na katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa chama hicho, yeye ndiye akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza wa ACT.
Bi. Anna aliolewa na Shedrack Maghwiya tangu mwaka 1982 na walibahatika kupata watoto 3 wa kiume: Fadhili, Peter na Elisha. Hata hivyo kwa bahati mbaya, mume wake hivi sasa ni marehemu.
MBIO ZA UBUNGE
Bi. Anna Mghwira alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza mwezi Januari 2012 baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza uchaguzi mdogo katika jimbo la Arumeru Mashariki baada ya kifo cha Solomon Sumari.
Anna alishiriki kura ya maoni ndani ya CHADEMA akihitaji kupewa ridhaa, hata hivyo chama hicho kilimpitisha Joshua Nassari (Josh) na Bi. Anna alikuwa na kazi ya kuendelea kumuunga mkono hadi ushindi ulipotangazwa kwa chama hicho.
Pia, amewahi kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, kupitia CHADEMA japokuwa hakuchaguliwa kushikilia wadhifa huo.
MBIO ZA URAIS
Bi. Anna Mghwira hajatangaza kuwa atagombea urais. Ila, tafiti kadhaa na maoni ya watanzania zinaonesha kuwa yeye ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa ambao wamejipambanua hivi karibuni na kuonesha uwezo mkubwa katika uwanja wa kisiasa na hivyo anapewa nafasi kubwa kuwa anaweza kupewa majukumu makubwa na anaweza kuyahimili.
NGUVU YAKE
Jambo la kwanza linalompa nguvu mwanamama huyu ni Umahiri katika elimu. Yeye nimsomi nguli wa masuala ya sheria lakini ana shahada tatu za vyuo vikuu. Nchi yoyote ingependa pamoja na sifa zingine, iongozwe na Rais ambaye elimu si kikwazo kwake. Kwa nchi kama Tanzania ambayo “mfumo dume” umewakandamiza wanawake kwa kipindi kirefu, Anna anakuwa mmoja wa wanawake wachache wenye uwezo mkubwa sana.
Kwa sababu Bi, Anna ni Mwanamke imara na anayepambana kwa muda mrefu sasa. Kitendo tu cha yeye kuwa mwanamke ni baraka tosha kwa siasa za kisasa ambazo zinaanza kuchangamkia, kukubali na kutafuta mchango wa wanawake katika Nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Jinsia yake inampa fursa ya kuendelea kuaminiwa zaidi katika jamii ambayo inazidi kupoteza imani na uaminifu wa wanaume kama Tanzania.
Lakini nguvu ya tatu ya Bi. Anna ni uthubutu. Ameniambia kuwa hata alipoingia katika ndoa bado alithubutu kujiendeleza kielimu bila kuchoka. Alipambana na changamoto za ndoa na shule. Wanawake wengi huchagua kufanya jambo moja na kuacha mengine, yeye alikwenda nayo yote na kuyakamilisha salama. Uwezo na uthubutu huu vinamfanya kuwa mwanamama imara anayeweza kukabidhiwa uongozi wa taasisi kubwa.
Anna ni mtu wa kuhoji kila jambo, si mwanamama “Ndiyo Mzee”. Wakati natafuta maoni ya watu waliowahi kufanya naye kazi katika Kituo cha Haki za Binadamu, mtendaji mmoja aliniambia kuwa ukimpa Anna kazi ya harakati iliyo kwenye maandishi, hataondoka kwako hadi umpe taarifa za kina za kila jambo na atakuhoji hadi utachoka.
Hata mtaalam mshauri wa chama hicho Prof. Kitila Mkumbo, ameniambia kuwa wakati wanafanya marekebisho ya katiba ya chama cha ACT walikabidhi kazi hiyo kwa jopo maalum la wataalam akiwemo Bi. Anna. Kitila ananiambia kuwa, kwa kiasi kikubwa katika timu yeye ndiye aliyehoji na kutoa mapendekezo ya masuala mengi kuliko hata wataalamu wengine wa sheria ambao walikuwa wanaume.
Mimi binafsi nilipojaribu kumfikia Bi. Anna kwa ajili ya kupata taarifa zake za kina na maisha binafsi, nilijikuta nashushiwa maswali matano mfululizo kiasi kwamba nilirudi kujipanga na kumtafuta tena. Huyu ni mwanasiasa wa kisasa ambaye anahoji kila jambo lililoko mbele yake, sifa hii wanaikosa wakuu wengi sana wa nchi.
Pamoja na kuwa na elimu kubwa, uzoefu wa kutosha wa kukaa nje ya nchi na kufanya kazi na taasisi za kitaifa na kimataifa, Bi. Mghwira ni Mwanamama wa kawaida sana. Watu wa karibu naye wanamtaja hivyo. Si mtu wa kupoteza muda na mambo yasiyo na tija, anapenda kuandika makala zakuelimisha jamii, kufanya kazi na jamii na kujitolea na kujichanganya na wananchi wasio na uwezo na wenye kuhitaji msaada. Sifa zote hizi ni nguvu muhimu kwa binadamu yeyote ambaye anahitaji uongozi mkubwa wa nchi.
UDHAIFU WAKE
Udhaifu mkubwa nilioubaini na hata kujulishwa na watu wa karibu na Bi.Anna Mghwira, yeye ni mwanasiasa mpole sana. Nimeambiwa kuwa ni mpole kupita kiasi na mara nyingi huwa anakuwa msikilizaji mzuri kabla hajaanza kuhoji mambo mfululizo. Moja ya sifa muhimu za Rais ajaye ni uwezo wa kuwa mpole na mkali kutegemeana na mazingira.
Kiwango cha upole cha mwanamama huyu kinazidi kiwango cha ukali alionao na naliona kama ni jambo linalopaswa kufanyiwa kazi kwa sababu taifa letu lilipofikishwa, mara kadhaa nimesisitiza kuwa tunahitaji kiongozi anayeweza kumudu hali zote mbili.
Lakini udhaifu wa pili mkubwa wa Bi. Anna Mghwira ni kutojijenga kisiasa ndani ya nchi. Katika siasa bado namuona kama mchanga, hajakomaa na kuwa na uwezo mkubwa kisiasa kiasi cha kujipa jina kubwa kwa jamii.
Mchango wake katika jamii ni mkubwa kwa sababu amewahi kusimamia masuala mengi ya kijamii na kisheria yanayoonekana, lakini nachokisema hapa ni kuwa, chama chochote kila kina jukumu la kusimamisha kiongozi ambaye anajulikana sana katika tasnia za siasa. Kutojijenga na kuwa juu tokea alipokuwa CHADEMA n.k. nakuchukulia kama udhaifu ambao anahitaji kuufanyia kazi.
NINI KINAWEZA KUMFANYA APITISHWE
Kama ACT Wazalendo itampitisha mwanamama huyu kuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Sababu ya kwanza ya kufanya hivyo inaweza kuwa ni ile dhana ya kumpa mwanamke nafasi.
Chama anachotoka ndicho peke yake kimeweza kumpa mwanamke nafasi ya juu ya uongozi wa chama, nadhani pia bado chama hicho kinaweza kumpa jukumu kubwa zaidi ya hilo kwa sababu tayari kimeshajijengea misingi ya kuwajenga kina mama.
Lakini ikiwa Anna Mghwira atapitishwa, Uzoefu wake kimataifa na katika masuala ya haki za binadamu na kushughulika na masuala ya kijamii kunaweza kuwa moja ya sababu.
Mwanamama huyu amefanya kazi mbalimbali za kitaaluma na kijamii hapa Tanzania, nchini Sweden, Marekani, uingereza na nchi nyingine za Afrika. Amekuwa mwalimu wa Vyuo Vikuu hapa Tanzania na msimamizi wa miradi mbalimbali ya kitaifa ya mashirika ya ndani na nje ya nchi. Uwezo na uelewa wake vinampa fursa ya juu ya kuteuliwa kugombea urais na kuonesha kuwa kina mama wanaweza ikiwa wanapewa fursa sawa na wanaume.
NINI KINAWEZA KUMWANGUSHA KWENYE MCHUJO?
Dhana ileile ya kijinsia inayombeba, pia ndiyo inaweza kumuangusha. Ikiwa ACT itadhani kuwa vyama vingine washindani vitasimamisha wagombea wanaume imara ambao wanaungwa mkono na mfumo dume uliotawala nchi hii, chama hicho kinaweza kumuweka nje Bi. Mgwira na kutafuta mwanachama mwingine “mwanaume” ambaye atakuwa na fursa ya kupambana na wanaume wengine kutoka vyama vingine na kuangaliwa na jamii “ambayo kwa kiasi kikubwa bado inatawaliwa na wanaume”.
Lakini jambo la pili linaloweza kumwangusha ni ugeni wake katika masuala ya kisiasa. Kama nilivyoeleza, Anna Mghwira hana uzoefu wa uongozi wa juu wa kisiasa katika vyama, nadhani nafasi aliyonayo ndani ya chama cha ACT Wazalendo ndiyo inayompa uzoefu wa kwanza wa siasa za kitaifa.
Lakini uzoefu wa jumla unaonesha kuwa vyama mbalimbali hapa Tanzania huteua wagombea urais wake miongoni mwa wanachama wazoefu au wale waliowahi kushika madaraka muhimu katika chama kwa muda mrefu. ACT ikipiga hesabu hizi inaweza kabisa kumuweka nje mwanamama huyu.
MIPANGO MINGINE IWAPO HATACHAGULIWA NA CHAMA CHAKE (PLAN B)
Ikiwa Bi. Anna Mgwira hatapewa fursa ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chake, anaweza kuwa na mipango mitatu mezani:
Mpango wa kwanza ni Kugombea ubunge katika jimbo mojawapo Tanzania. Bahati nzuri nimejulishwa kuwa moja ya majimbo anayojipanga kugombea ni pale Singida. Ikiwa ndivyo basi, mpango huu unaweza kumfaa kwa maana ya kuzidi kujifunza na kupata uzoefu wa siasa za Tanzania kwa upana.
Lakini mpango wa pili ni kuendelea kufundisha vijana katika Vyuo Vikuu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi na ushauri wa kisheria katika jamii. Masuala haya Bi. Anna ana uzoefu nayo, itakuwa tu ni kiasi cha kuendelea pale alipoishia, huwenda mara hii kwa kasi kubwa zaidi.
Nadhani mpango wa tatu ni kuendelea kuongoza chama cha ACT Wazalendo. Nimeambiwa kuwa uongozi (Uenyekiti wake) unapaswa kuisha mwaka 2020 mwezi Februari. Ikiwa ndivyo nadhani ana fursa njema ya kuendelea kufanya uongozi.
HITIMISHO
Bi. Anna Mgwira ni mwanasiasa na kiongozi wa chama kipya ambacho kimeanzishwa na wanachama wengi waliotoka CHADEMA. Safari yake kisiasa na hata ugombeaji wa nafasi zingine kubwa za nchi kwa namna moja ama nyingine lazima utaathiriwa na ustawi au uzorotaji wa CHADEMA.
Ikiwa CHADEMA itazidi kukubalika kwa watanzania na kuwa chama kinachoimarika zaidi kuishinda ACT, ndiyo kusema kuwa yeye na wenzake watakuwa kwenye wakati mgumu sana kujipambanua kisiasa, na hivi ndivyo siasa za Afrika hutizamwa.
Pamoja na “sintofahamu” hizo, namuona Bi. Anna Mgwira kama mmoja wanasiasa watulivu sana na wenye maono mapana katika taifa hili. Kwa maneno yake yeye mwenyewe amenieleza kuwa “…Natamani siku moja nchi hii iongozwe kwa misingi ya udugu na kusaidiana, kwa misingi ya malezi ya maadili bora kama alivyofanya Mwalimu Nyerere – Mimi nimekulia kwenye familia kubwa sana lakini wazazi wetu walitulea sote kama ndugu, na tuliishi kwa furaha kubwa, nina ndoto kuwa Tanzania ijayo ipite katika njia hiyo…”
Nachoweza kusema kwa sasa ni kumwombea mama huyu na mwanamama nguli wa upinzani, na kumtakia safari njema katika nia zake za kisiasa ikiwa hii ambayo ametajwa sana, kwamba ana sifa za kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mchambuzi wa Safu hii ni Julius Mtatiro, Adv Cert in Ling, B.A, M.A, L LB (Continuing): juliusmtatiro@yahoo.com, +255787536759.