Mama Kanisa anakianza
kipindi cha Kwaresima, yaani siku arobaini za toba na wongofu wa ndani;
kusali na kufunga; kusoma na kulitafakari Neno la Mungu pamoja na
kumwilisha imani katika matendo, kwa Jumatano ya Majivu. Waamini
wanakumbushwa kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini watarudi tena.
Hizi ni nyakati za toba na zimewekwa na Mama Kanisa kwa ajili ya mazoezi
ya maisha ya kiroho; zinajikita katika liturujia ya toba, kuhiji kama
ishara ya toba, kujinyima kwa hiyari kama sehemu ya kufunga na kutoa
sadaka kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; ni
mwaliko wa kushiriki kidugu kazi za mapendo na kimissionari
zinazotekelezwa na Mama Kanisa.
Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baba
Mtakatifu Francisko kwa Mwaka 2014 unaongozwa na kauli mbiu “Maana
mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, Jinsi alivyokuwa maskini kwa
ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba, ninyi mpate kuwa matajiri
kwa umaskini wake”. Huu ni mwaliko kwa waamini kuonesha moyo wa ukarimu
kwa jirani zao kama ilivyokuwa nyakati za Mtakatifu Paulo aliyewahimiza
Wakorintho kuwasaidia ndugu zao waliokuwa wanateseka mjini Yerusalemu.
Baba Mtakatifu katika tafakari hii anaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu ambaye ni tajiri na mwingi wa rehema kwa njia ya
Yesu Kristo, Mwanaye wa pekee amejinyenyekesha na kuwa maskini, ili
aweze kuwa karibu na binadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Hiki ni
kielelezo cha upendo wa Mungu ambao ni neema na baraka inayotolewa kwa
binadamu anayependwa na Mwenyezi Mungu, kiasi cha hata Kristo kujisadaka
maisha yake.
Huu ndio upendo unaoshirikisha, unajenga na kuimarisha umoja na udugu
kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho,
Mwenyezi Mungu amefikiri na kutenda kama binadamu katika mambo yote
isipokuwa hakutenda dhambi.
Kwa njia ya umaskini wa Yesu, Mwenyezi Mungu amependa mwanadamu aweze
kutajirika, hii ndiyo mantiki ya Fumbo la Umwilisho na Fumbo la Msalaba.
Alibatizwa mtoni Yordani si kwa vile alikuwa anahitaji toba, wongofu wa
ndani na msamaha, bali
alipenda kuonesha mshikamano wa dhati na binadamu mdhambi kwa kujitwika
dhambi zake mabegani mwake, ili aweze kuwafariji, kuwaokoa na kuwakomboa
kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka huu
anasema, Yesu alijifanya kuwa jirani na Msamaria mwema, kwa kuguswa na
mahangaiko ya binadamu, ili hatimaye, aweze kumwonjesha huruma na
mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Utajiri wa Yesu
unajionesha kwa namna ya pekee kwa kumtegemea Baba yake wa mbinguni,
katika kutekeleza mapenzi yake na hatimaye kuvikwa taji la utukufu. Yesu
anatambua kwamba, ni Mwana pekee wa Mungu, Masiha anayewaalika wafuasi
wake kujitajirisha kutoka kwake na kushiriki udugu na kujitahidi
kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwa kuishi kama watoto wa Mungu na
ndugu zake Kristo.
Kila wakati Mwenyezi Mungu anaendelea kumkomboa mwanadamu kutoka katika
umaskini wake kwa njia ya umaskini wa Yesu, kwa kuonja na kuguswa na
umaskini wa jirani zao tayari kujifunga kibwebwe kusaidia kupambana na
umaskini: wa hali, kipato na maadili. Umaskini ni kielelezo cha kukosa
imani, mshikamano na matumaini. Umaskini wa kipato unawakumba wote
wanaoishi katika mazingira ambayo ni kinyume kabisa cha utu na heshima
ya binadamu.
Hawa ni watu wanaopokonywa haki na mahitaji msingi kama vile: chakula,
maji, malazi, huduma bora za afya, fursa za kazi na ajira, maendeleo na
ukuaji wa kitamaduni. Kanisa linaendelea kujisadaka kwa ajili ya
kupambana na umaskini wa kipato katika mikakati yake ya kichungaji
inayopania kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linaiona na
kuitambua sura ya Kristo miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Kanisa linapania kuhakikisha kwamba, utu na heshima
ya binadamu vinaendelea kupewa kipaumbele cha pekee kwa kukomesha
ubaguzi ambao wakati mwingine ni chanzo kikuu cha umaskini. Kanisa
linahimiza matumizi bora ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi na
maendeleo ya wengi. Jamii iongozwe katika misingi ya haki, usawa, kiasi
na ushirikiano.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna umaskini wa kimaadili, unaomfanya
mwanadamu kuwa ni mtumwa wa dhambi, ulevi wa kupindukia, mcheza kamari
na mtazamaji wa picha za ngono. Hili ni kundi la watu lililopoteza dira
na mwelekeo wa maisha kwa kukata tamaa! Ni watu wanaoogelea katika utupu
kwa kukosa fursa za ajira pamoja na kuendelea kudhalilishwa utu na
hehima yao kama binadamu: wanakosa chakula na malazi; hawana haki ya
kupata huduma bora katika sekta ya elimu, afya na maendeleo. Matokeo
yake ni watu kuelemewa mno na umaskini wa kimaadili kiasi hata cha
kutema zawadi ya maisha!
Umaskini huu ni chanzo kikuu cha myumbo wa uchumi kimataifa na matokeo
yake ni umaskini na utupu wa maisha ya kiroho. Hali hii inajionesha pale
mwanadamu anapomn’goa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vyake,
kiasi hata cha kutema upendo na huruma yake. Hapa mwanadamu anadhani
kwamba, anaweza kujitegemea mwenyewe na wala haitaji msaada kutoka kwa
Mwenyezi Mungu. Lakini ikumbukwe kwamba, ni Mungu peke yake anayeweza
kukomboa na kumwokoa mwanadamu.
Baba Mtakatifu anasema, Injili ni dawa inayoponya umaskini wa maisha ya
kiroho, changamoto na mwaliko kwa kila Mkristo kuhakikisha kwamba,
anashiriki kutangaza Injili ya Kristo katika medani mbali mbali za
maisha, ili watu waonjeshe upendo na huruma ya Mungu; ili hatimaye,
waweze kushirikishwa maisha ya uzima wa milele. Waamini wawe ni
watangazaji amini wa Injili ya Furaha inayojikita katika huruma na
matumaini; mwanga na faraja kwa wote wanaotembea katika giza na uvuli wa
mauti. Ni mwaliko wa kumfuasa Kristo aliyethubutu kuwaendea maskini;
akaonesha sifa ya kuwa mchunga mwema kwa kumwendea Kondoo aliyekuwa
amepotea, ili kumwonjesha upendo wake. Kwa kushikamana na Yesu, waamini
wanaweza kuwa na ujasiri wa kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji
Mpya na maendeleo endelevu.
Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi hiki cha Kwaresima anawataka
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha ushuhuda wa pekee kwa
maskini wa hali, maadili na maisha ya kiroho wanaokutana nao kila siku
ya maisha yao, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya
Yesu Kristo. Kwaresima ni muda muafaka wa kujisadaka kwa ajili ya
kuwasaidia wengine, kwa kutambua kwamba, kwa njia hii pia tunafanya
toba.
Waamini wanaweza kuwatajirisha jirani zao na hivyo kushiriki katika
mchakato wa kuganga na kuponya umaskini unaomwandama binadamu. Ni
matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini wataweza kukitumia
kipindi hiki cha Kwaresima ili kupata neema na baraka zinazobubujika
kutoka kwa Kristo mwenyewe!
Ujumbe huu umehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican