Showing posts with label Uchaguzi 2015: FAHMI DOVUTWA: MGOMBEA URAIS WA TANZANIA KUPITIA CHAMA CHA UPDP.. Show all posts
Showing posts with label Uchaguzi 2015: FAHMI DOVUTWA: MGOMBEA URAIS WA TANZANIA KUPITIA CHAMA CHA UPDP.. Show all posts

Tuesday, October 20, 2015

FAHMI DOVUTWA: MGOMBEA URAIS WA TANZANIA KUPITIA CHAMA CHA UPDP.


Fahmi Nasoro Dovutwa ni Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP). Alizaliwa tarehe 27 Februari 1957 huko Kisarawe mkoani Pwani(Amefikisha miaka 58 mwezi Februari mwaka huu).
Dovutwa alianza elimu yake ya Msingi mwaka 1967 katika shule ya msingi Zanaki hadi alipohitimu mwaka 1974 alipoendelea na masomo ya Sekondari katika shule ya sekondari Azania ambako alihitimu mwaka 1977.
Rekodi za elimu za Dovutwa zimekuwa “kizungumkuti” kupatikana. Hata taarifa zake binafsi alizotoa kwa ajili ya rekodi za Bunge Maalum la Katiba zinasisitiza kuwa ameishia kidato cha nne.
Juhudi za kumpata yeye mwenyewe ili akamilishe rekodi zake hazikufua dafu na ni yeye peke yake tangu nianze kufanya uchambuzi wa watu wanaotajwa kuwania urais, ambaye hakutoa ushirikiano kabisa ili kunifanya nipate rekodi zake sahihi.
Watu wa karibu yake wamenijulisha kuwa kwa muda mrefu amekuwa akijishughulisha na kazi za ujasiriamali katika soko la Magereza jijini Dar Es Salaam hadi baadaye alipochaguliwa kuongoza chama cha UPDP ambacho yeye ni mwenyekiti hadi sasa.
Mwaka 2014 yeye alikuwa ni miongoni mwa watanzania waliopata fursa ya kuteuliwa na Rais wa Tanzania kupitia kundi la vyama vya siasa, na kuwa mjumbe wa bunge maalum la katiba lililofanya kazi yake mjini Dodoma na kukamilisha katiba inayopendekezwa ambayo hata hivyo imeligawa taifa katika vipande viwili.
Dovutwa ameoa na ana watoto.
MBIO ZA UBUNGE
Katika historia ya kisiasa ya Dovutwa, hakutoa pia rekodi zinazoonesha kama aliwahi kugombea ubunge katika jimbo lolote na hata nilipozitafuta sikufanikiwa kuzipata.
MBIO ZA URAIS
Kiongozi huyu alijitosa katika mbio za urais mwaka 2010 akitumia tiketi ya chama chake cha UPDP. Katika uchaguzi ule ambao Jakaya Mrisho Kikwete aliongoza kwa ushindi wa asilimia 62.83, akifuatiwa na Willibroad Slaa aliyekuwa na ushindi wa asilimia 27.5, na Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF akiwa na asilimia 8.28, Dovutwa aliibuka katika nafasi ya mwisho akiwa na asilimia 0.16 ya kura zote kwa kupitwa na Peter Mziray wa APPT (asilimia 1.15), Hashim Rungwe wa NCCR (asilimia 0.31), na Mutamwega Bhatt wa TLP aliyekuwa na asilimia 0.21 ya kura zote.
Katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, Dovutwa hajatangaza popote kuwa atagombea tena nafasi ya Urais lakini duru za kisiasa ndani ya chama hicho ikiwemo kutoka kwa baadhi ya viongozi waandamizi, zimenieleza kuwa anapewa nafasi kubwa ya kugombea tena.
NGUVU YAKE
Jambo la kwanza nalolitizama kama nguvu ya Dovutwa ni “Umaarufu”. Nathubutu kusema kuwa huyu ni mmoja wa viongozi maarufu wa wa vyama visivyo na wabunge. Mikogo yake ya kuvutia katika kampeni za mwaka 2010.
Uvaaji wake kuanzia chini hadi “kofia nyekundu”, vilimtofautisha na mgombea yeyote yule kwenye uchaguzi ule. Mimi binafsi nilijikuta navutiwa sana na staili za kiongozi huyu hata kama sikuwa najua sera za chama chake kwa mwaka 2010. Nguvu hii ya kuvutia macho nayo ni muhimu sana kwa mwanasiasa yeyote, hata kama ukiwa na elimu kubwa, mipango mingi n.k. suala la unavaaje, unavutiaje na ukoje (mtazamo wa nje), halikwepeki katika siasa.
Lakini pia, Dovutwa ni Mjasiriamali mzoefu na sifa hii pia inamuongezea nguvu mtu yeyote yule ambaye anataka uongozi wa juu wan chi. Tena nimeambiwa kuwa amekuwa mjasiriamali mdogo kwa kipindi kirefu na hasa akifanya kazi na vijana wa chini. Natambua kuwa fursa hiyo ilimpa nafasi kubwa ya kuendela kuyaishi maisha ya vijana wa chini na hata kujua masuluhisho ya haraka, ya muda mfupi na muda mrefu, kwa sababu pia ukishaingia ikulu kazi yako kubwa ni kutafuta majawabu ya masuala ya watu. Majawabu ya muda mrefu na muda mfupi.
UDHAIFU WAKE
Udhaifu wa kwanza wa Dovutwa uko katika elimu (hadi hapo atakapowajulisha watanzania elimu yake rasmi tofauti na iliyoko kwenye vyanzo sahihi vya taarifa kama tovuti ya Bunge Maalum la Katiba), udhaifu huu unasimama kama ulivyo kwa sababu taifa letu linakwenda mbele hivi sasa na elimu ni jambo la msingi katika uongozi, hata kama siyo kila kitu.
Kukosekana kwa taarifa za elimu yake tofauti na ilivyo kwa viongozi wengi wa vyama vya siasa ni jambo linaloleta mashaka juu ya weledi wa kiongozi huyu. Kwa karne ya sasa na hapa Tanzania kulikojaa wasomi, ni nadra sana ikatokea kwamba mtanzania mwenye elimu ya Kidato cha nne tu “akawa na ndoto za kuingia ikulu na jambo hilo likatekelezeka”.
Lakini jambo la pili, Dovutwa mara nyingi amekuwa ni mtu wa Kukosa Ajenda na matokeo yake hupenda kurukia ajenda za masuala ambayo hayana tija. Mara kadhaa ameonekana katika vyombo kadhaa vya habari akivishambulia sana vyama vya upinzani lakini akiwa hafanyi hivyo kwa CCM. Hali hii inamuweka katika sahani ya wanasiasa ambao wanashangaza kidogo na nadhani huu ni udhaifu mkubwa sana kama kweli bado ana ndoto za kugombea urais, achilia mbali kuingia ikulu.
Uhusiano wenye mashaka baina yake na CCM ni suala lingine linalosisitiza juu ya udhaifu wake. Dovutwa, akiwa mgombea urais kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka 2010, aliwashangaza watanzania katikati ya kampeni huku Chama Cha Mapinduzi kikionekana kuzidiwa sana na upinzani, hususani CHADEMA na CUF, Dovutwa alijitokeza hadharani (akiwa mgombea) na kutangaza kuwa chama chake na vyama vingine kadhaa visivyo na wabunge na mitandao mikubwa “ati” vinamuunga mkono mgombea wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete.
Hata hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi haikukubaliana na kujitoa huko kwa baadhi ya vyama na kusisitiza kuwa kisheria muda wa kujitoa umekwisha. Tamko na msimamo ule ambao sina uhakika kama kweli ulitokana na vikao vya chama chake, vina maana kuwa huwenda anafanya “kazi maalum” katika siasa za ndani ya nchi. Kwa sababu, katika mantiki ya kawaida, si jambo rahisi chama cha upinzani kufanya maamuzi ya kuunga mkono chama kinachoongoza, katika nchi inayosaka demokrasia kama yetu.
Katika Bunge Maalum la Katiba, Dovutwa ni mmoja wa viongozi ambao pia walishangaza sana watanzania. Yeye ni mmoja wa wabunge wa bunge lile ambao walisimama hadharani mara kadhaa na “kuponda” msimamo wa vyama vya UKAWA lakini bila kueleza kuwa anaunga mkono upande upi.
Ni jambo la hatari sana chama cha siasa au viongozi wa vyama vya siasa wanapokwenda katika kazi kubwa ya kitaifa bila kuwa na ajenda ya msingi ya kuisimamia. Ndiyo maana kulikuwa na sintofahamu hiyo ambayo iliegemea upande mmoja bila kutafakari kuwa vyama vilivyoondoka katika mchakato ule navyo vilikuwa na hoja zao. Viongozi kama Dovutwa walipaswa kufanya kazi ya kujenga hoja kuliko kuendelea “kuponda” UKAWA, jambo lililowapotezea muda na kushindwa hata kujenga taswira za vyama vyao.
Lakini udhaifu mwingine wa Dovutwa ni Kushindwa kukihuisha chama chake. Chama cha UPDP hakijapata ushindi wa kujivunia katika Uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwezi Disemba 2014. Chama hiki kilizidiwa na vyama vipya kama ACT na ADC ambavyo viliambulia viti kadhaa katika maeneo mbalimbali ya nchi. Kama Dovutwa ameshindwa kukihuisha chama chake kisimamie ajenda muhimu za kitaifa hapa nchini lakini pia kufanya vibaya sana hata katika uwakilishi chini wa wananchi, hizo siyo dalili nzuri kwa kiongozi ambaye anatarajia kuwa kiongozi wa nchi.
Baadhi ya viongozi waandamizi wa UPDP walioongea name, wameniambia kuwa chama chao kimekuwa na matatizo makubwa sana katika kufanya uchaguzi wa kikatiba wa kila baada ya awamu. Baadhi yao wameeleza kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho mara kadhaa wamekuwa na uoga kuwa chaguzi zikifanyika kwa uwazi na haki, huwenda wakaangushwa.
Tuhuma hizi pia zinamgusa Dovutwa mwenyewe ambaye amewahi pia kuonekana kwenye kipindi kimoja che televisheni akijitetea kuwa chama chake kitajitahidi kukamilisha chaguzi zake za ndani. Kama Dovutwa anashindwa kusimamia chaguzi za chama chake kwa uhakika na kwa wakati hadi anasuasua sana, ni dalili tosha kuwa kazi ya urais wa nchi inaweza kumuwia ngumu kupita kiasi.
NINI KINAWEZA KUMFANYA APITISHWE
Jambo moja ambalo naona linaweza kumvusha Dovutwa katika harakati za ndani ya chama chake za kupewa ridhaa ya kugombea urais ni Uongozi wake ndani Chama. Dovutwa ndiye kiongozi mkuu wa UPDP na jambo hilo kwa siasa za Afrika lina maana kuwa mara nyingi yeye ndiye mwenye nafasi kubwa ya kupewa ridhaa muhimu kama hizi, mara zinapotokea. Sitashangaa kuona chama chake kikimpitisha kwa sababu yeye ni mwenyekiti wa chama.
Lakini jambo la pili linaloweza kumfanya apitishwe ni kwa sababu aligombea urais mwaka 2010. Mipango na mbinu alizotumia mwaka 2010 pamoja na kwamba zilimpa nafasi ya mwisho lakini tunakubali kuwa kuna baadhi ya watanzania walimpigia kura. Ndiyo kusema kuwa UPDP kama inahitaji kura zaidi katika uchaguzi wa mwaka huu huwenda yeye Dovutwa akapaswa kutumia uzoefu wake wa mwaka 2010 ili kufanikisha jambo hilo.
NINI KINAWEZA KUMWANGUSHA KWENYE MCHUJO?
Jambo la kwanza linaloweza kukifanya chama chake (UPDP) kisimpitishe kugombea urais, nadhani ni itakapotokea kuwa chama hicho kina mgombea urais mwingine mwenye sifa na uwezo mkubwa kumshinda. Kama nilivyoeleza awali, elimu tu ya Dovutwa haieleweki na inawezekana kabisa kuwa hata yeye mwenyewe hapendi kuiweka wazi. Ikiwa chama chake mathalani kikapata mtu mwingine mwenye elimu kubwa sana na uwezo kumshinda, nadhani Dovutwa anaweza kupumzishwa katika nafasi hiyo.
Lakini jambo la pili linaloweza kumfanya asipitishwe ni ikiwa Hoja ya mwaka 2010 ya kumuunga mkono Kikwete itatiliwa mashaka katika vikao vya maamuzi vya chama chake. Baddhi ya viongozi waandamizi wa UPDP waliokubali kuongea nami wamesisitiza kuwa hatua ile ya Dovutwa ya mwaka 2010 haikupita katika vikao vya maamuzi. Ikiwa atatiliwa mashaka kuwa anaweza tena kufanya yale ya mwaka 2010, huwenda sababu hii pia ikamuweka nje ya mbio hizi.
MIPANGO MINGINE IWAPO HATACHAGULIWA NA CHAMA CHAKE (PLAN B)
Ikiwa Dovutwa hatapitishwa kugombea urais wa Tanzania, huwenda akawa na mipango kama mitatu mezani:
Mpango wa kwanza unaweza kuwa kutafuta jimbo na kugombea nafasi hiyo.Lakini nadhani kwa nguvu dhaifu ya chama chake ni vigumu pia kushinda jimbo lolote, maana kama chama hakina wenyeviti wa serikali za mitaa wa kutosha, madiwani n.k ni vigumu kudhani kuwa kitapata “mbunge” kutoka mbinguni.
Mpango wa pili unaweza kuwa ni kuendelea na uongozi wa ndani ya chama chake. Mpango huu ndio anaendelea nao hadi sasa na nimeambiwa kuwa kunaweza kufanyika uchaguzi mwingine katika chama hicho na kwamba bado atatetea nafasi yake ya uenyekiti, jambo ambalo halina shida kidemokrasia.
Na mpango wa tatu unaweza kuwa kuunganisha nguvu za vyama vya upinzani visivyo na wabunge ili kuunda umoja wao. Tayari nina taarifa za kina kuwa baadhi ya vyama visivyo na wabunge vinaendelea na vikao vya chini kwa chini ili vione kama na vyenyewe vinaweza kuunda “UKAWA” yao. Mpango huu utakuwa unamhusu sana Dovutwa kwa sababu natambua ushawishi alionao juu ya vyama visivyo na wabunge.
HITIMISHO
Dovutwa ana changamoto kubwa sana katika siasa za Tanzania. Ukiachilia mbali kwamba yuko katika chama kisicho hata na diwani lakini nisisitize kuwa taswira kadhaa za chama hicho zinamsababishia yeye na wenzake hukumu ambazo wakati mwingine zingeepukika kama zingefanyiwa kazi.
Kama nilivyoeleza pale juu, huyu ni mmoja wa viongozi wa vyama visivyo na wabunge ambaye ana mvuto wa pekee unaotokana na staili zake za kufanya mambo na ubunifu wa mavazi n.k. Hayo peke yake hayatoshi. Ana jukumu kubwa sana la kusimamia uhuishaji wa chama chake na kufuta makosa ya nyuma kuliko kusonga mbele.
Nafasi ya Dovutwa kisiasa ndani ya nchi natumaini kuwa itaendelea kuwa palepale (bila kukua) kwa sababu watanzania wa sasa wanazidi kupata weledi mkubwa unaowasaidia katika ufanyaji wa maamuzi mbalimbali.
Siasa za sasa zinataka viongozi wepesi sana ambao sioni kama Dovutwa ni mmoja wao. Ikiwa mwenyekiti wa chama cha siasa kilichosajiliwa unaombwa wasifu wako na hauutoi kwa wiki kadhaa ina maana kuwa hata wanaokupigia chapuo kuwa una uwezo wa kugombea nafasi fulani ya juu wanakuwa wanakosea sana.
Pamoja na mapungufu lukuki ambayo nimeyabainisha kutokana na hali halisi inayomkabili kiongozi huyu, namtakia kila lililo jema katika mipango yake ya mbele kisiasa huku nikimpa nafasi finyu ya kuwa mgombea mwenye mafanikio ikiwa atafanya hivyo Oktoba mwaka huu

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR