Kifo
ni kitendawili ambacho binadamu ameshindwa kabisa kukitegua. Anabaki
kuhoji na kujihoji bila kupata jibu la kwa nini anakufa. Mbele ya kifo
binadamu anabaki kutoa visingizio vya kujitetea na kulaumu, hatimaye
anakiona kifo kuwa mwiko
Zamani
mwiko ulikuwa masuala ya „mapenzi”, kumbe kifo na misiba hakikuwa kitu
cha kuogopa sana. Lakini sasa ni kinyume, mambo ya mapenzi yamegeuka
kuwa kitu cha kawaida kabisa isipokuwa kifo kimekuwa kiboko chetu.
Watu
tunakiogopa na pengine hatutaki hata kukisikia. Tunapolazimika kwenda
msiba basi tunawaachia wengine walipambe jeneza maua, nasi tukisubiri
kwenda kutia sahihi kwenye kitabu cha maombolezo na kutoa rambirambi
kwenye bahasha kisha kukaa mbani na jeneza huku tukizungumza chinichini.
Sanasana tunajisahaulisha kwa kuimba nyimbo za maombolezo au kusikiliza
nyimbo za Injili. Tunaogopa kabisa kukizungumzia kifo au walau
kukijadili. Mbele ya kifo binadamu tunabaki kulaumiana, kushikana uchawi
na hasa tunamlaumu Mwenyezi Mungu.
Mathalani, kuna baadhi ya
wakristu wa kale hata wa sasa walisali na kuomba msaada kwa Mungu au kwa
kupitia watakatifu fulani kusudi waepushwe na kifo. Sala hizo
zinapoacha kupokelewa, binadamu anachukia, na kumlaumu Mungu. Kristu
aliwahi pia kulaumiwa pale alipokataa mwito wa Marta na Maria
walipomwomba aenda kwao kumponyesha kaka yao Lazaro aliyekuwa mgonjwa.
Yesu akaenda huko kwa kuchelewa kusudi siku nne baada ya kifo. Siku ile
alipojionesha msibani, Maria na Marta wakamjia juu na kumlaumu sana.
“Bwana ungalikuwapo ndugu yetu asingalikufa”. Hata katika nafasi hiyo,
bado hatutaki kulijibu swali ni sababu gani Yesu alifika duniani. Je
Yesu alifika duniani ili kuendeleza uhai huu wa kibaolojia au kushinda
mauti?
Tukitaka kujua ukweli wa mwenendo mzima wa maisha yetu,
hatuna budi kuangalia pia hatima yake, yaani kuelewa kwamba maisha yetu
yana mwanzo (yaani kuzaliwa) na yana ukamilifu wake. Ama sivyo
tutaendelea kukiogopa kifo, nacho kitaendelea kupeta na kutuogofya
zaidi.
Ndugu zangu, tulishukuru Kanisa limetutengea mwezi mzima
wa Novemba tulioishauanza ili tukitafakari kitendawili hiki cha kifo.
Asiyetaka kukitafakari kifo anaonywa na methali ya kiswahili isemayo:
“Asiyejua kufa na atazame kaburi.” Kwa hiyo tunaalikwa pia kwenda
makaburi mara nyingi kuwaona wenzetu walioishapambana na kifo, nao
watatusaidia kutafakari vizuri zaidi fumbo hilo la kifo.
Hebu
tujaribu kutafakari kidogo na kupata jibu stahiki juu ya kifo na hatima
ya maisha yetu. Tuanze utafiti wetu na Wayahudi, hasahasa manabii na
wanazaburi. Wenzetu walianza utafiti mpya juu ya kifo wakitegemeza hoja
zao juu ya kitu hiki “upendo”. Yaani kama Mungu aliingia katika
mahusiano na binadamu na kufanya naye maagano iwe kwa njia ya manabii wa
aina yoyote ile ni kwa sababu Mungu alimpenda binadamu na hivi akataka
kuwa na mawasiliano naye. Ukimpenda mtu kwa dhati, huwezi ukamwacha tu
kienyeji.
Hiyo ndiyo sheria ya upendo. Kwa hiyo ukisema: “Mungu
ninakupenda”, naye akikuambia “Ninakupenda”, basi upendo huo hauwezi
kwisha. Namna hii ya kufikiri, ina nguvu sana katika maisha. Katika
Agano la kale, Mungu anawaambia wayahudi: “Wewe una thamani machoni
pangu, nami ninakupenda” (Isaya). Hapo yaonesha wazi kuwa Mungu anao
mradi wa kumpenda kiumbe chake kwa sababu amemwumba. Kwa hiyo katika
Injili, tunaona kuwa katika mradi huo, Mungu amewekeza katika upendo kwa
njia ya udalali ambao ni yeye mwenyewe katika nafsi ya pili ya Mungu,
Yesu Kristu.
Injili ya leo imechukuliwa toka mazungumzo juu ya
chakula cha uzima Ekaristi. Mradi huo wa Mungu umeanishwa kwa neno moja
tu “Mapenzi”. Neno hilo limetamkwa na Yesu karibu mara nne: “sikushuka
kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu”; halafu, “bali niyafanye
mapenzi yake aliyenipeleka”; halafu tena “Mapenzi yake aliyenipeleka ni
haya”; na mwisho “Kwa kuwa mapenzi yake baba yangu ni haya”.
Hebu
tumwangalie kwa undani Dalali aliyekabidhiwa kutekeleza mradi wa Mungu
kwa wanadamu anasema: “Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala yeyote
ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe”. Hivi ndiyo Mungu anavyomwaminisha
Yesu mradi huo wa mapendo kwa binadamu. Mungu anauaminisha ubinadamu
wote kwa Yesu bila masherti. Kwa hiyo ili kuelewa maana ya kifo na
ukombozi toka kifo, yabidi tuingie katika mradi huo wa mahusiano ya
upendo (mapenzi) na Yesu.
Hoja ya msingi ya kuingia katika
mahusiano hayo ni ile anayoisema Yesu mwenyewe, “Kwa kuwa mimi sikushuka
kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake
aliyenipeleka.” Hivi ni dhahiri kwamba Yesu amefika duniani kama dalali
ili kutekeleza mradi wa Mungu, yaani kunadisha na kuendeleza mahusiano
hayo ya upendo. Mungu amemdhamini Kristu mwanae mradi mzima wa upendo.
Kama anavyothibitisha Yesu mwenyewe: “Mapenzi yake aliyenipeleka ni
haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali
nimfufue siku ya mwisho.” Hapo ndipo palipojaa uhondo! Maana yake bila
Kristu, hatuwezi kupata jibu sahihi juu ya kifo, jibu linalookoa na
kuelewa mwisho au hatima yetu. Na Yesu aliye mdhamini wa mradi huo
hataki kujiangusha mwenyewe anaposema, “Katika wote alionipa nisimpoteze
hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho” anamaanisha kwamba
atatuwapelekesha hao aliokabidhiwa hadi kieleweke.
Kufufuliwa
siku ya mwisho, kadiri ya mwinjili Yohane haimaanishi mwisho wa dunia,
bali ni Kalvario, juu ya msalaba siku ile anaposulibiwa na kufa. Tendo
la mwisho la Yesu la upendo ni pale alipoitoa roho na maisha yake ya
kimungu, nguvu ya upendo aliyoitolea yote kabisa wakati wa uhai wake na
kuihitimisha pale msalabani. Siku hiyo ya mwisho anaitoa roho yake na
maisha yale ya milele yanaingia kwenye mahusiano ya daima na Mungu, na
maisha hayo hayana mwisho. Hayo ndiyo mapenzi ya Mungu.
Mradi huo
unatekelezeka tu endapo tutamtambua Mungu katika Kristu: “Kwa kuwa
mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na
kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”
Maana yake, upendo huo wa Baba utatekelezeka kwa namna tatu: kwanza
kwa yule “amtazamaye Mwana,” kumbe yatubidi kuona au kutazama.
Kuutazama au kuuona huu mradi wa Mungu na kumtambua Kristu ambaye ndiye
mdhamini mkuu wa Mungu. Halafu yabidi “kumwamini Yesu”, yaani kutoa
ushuhudi wa binafsi kwa huyo mdhamini pekee. Kisha matokeo ya kumtambua
na kuishi kama alivyoishi huyo mdhamini yatakuwa ni “kufufuliwa naye”.
Kwa
hiyo katika maisha yetu yatubidi tuyadhihirishe hayo mahusiano ya
mapendo na Mungu kwa njia ya Kristu mdhamini wa mapendo. Kwa wale
wenzetu walioishazaliwa kwa Baba, yaani waliofariki, wameutambua tayari
uso wa Yesu na kumwaminia hivi sasa wamepokea maisha ya kimungu. Kwao
hao sisi leo tunawapa ushirikiano kwa kuwa karibu sana nao, na siyo leo
tu bali daima. Kama maisha yao hayakuwa makamilifu, sisi tuwaombee yaani
kuwaonesha upendo, kwani Mungu amewekeza upendo katika Yesu Kristu.
Showing posts with label Fumbo la Kifo. Show all posts
Showing posts with label Fumbo la Kifo. Show all posts
Subscribe to:
Posts (Atom)
-
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya...
-
Isidore Bakanja, ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya imani ya Kikristo, Akiongozwa na maisha rahisi kama layman Katoliki wakati wa mauaj...
-
Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza anatualika kutambua kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya ...