Showing posts with label MJUE HAMAD RASHID MGOMBEA URAIS ZANZIBAR KUPITIA ADC.. Show all posts
Showing posts with label MJUE HAMAD RASHID MGOMBEA URAIS ZANZIBAR KUPITIA ADC.. Show all posts

Tuesday, October 20, 2015

MJUE HAMAD RASHID MGOMBEA URAIS ZANZIBAR KUPITIA ADC.

HAMAD RASHID: NANI NI NANI URAIS UPINZANI?
HISTORIA YAKE
Hamad Rashid Mohamed ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwakilisha wananchi wa jimbo la Wawi, Pemba. Alizaliwa tarehe 01 Machi 1950 huko Zanzibar na kusoma katika shule ya msingi ya Wavulana ya Chake kati ya mwaka 1958 hadi 1967. Amesoma Sekondari (kidato cha kwanza hadi cha nne) kati ya mwaka 1968 – 1970 katika Shule ya Sekondari Chanjamjawiri huko huko Zanzibar (Mzunguko wa Kwanza).
Hamad Rashid alisoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Fidel Castro kati ya mwaka 1970 – 1971. Na wakati huohuo kati ya mwaka 1974 – 1976, alipata mafunzo ya muda mrefu ya masuala ya Kibenki katika Chuo cha Mafunzo cha Benki ya NBC.
Baadaye mwaka 1980 Hamad Rashid alijiunga katika chuo cha Itikadi cha Zanzibar na kupata stashahada kati ya mwaka 1981 na mwaka 1981 alienda kusoma katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Francis Xavier kilichoko huko Antigonish katika mji wa Nova Scotia nchini Canada, na kuhitimu stashahada ya Maendeleo ya Jamii mwaka 1982.
Kwa upande wa ajira, Kwa miaka mitano (1972 – 1977), Hamad Rashid aliajiriwa na Benki ya watu (People’s Bank) kama karani na mwaka 1979 hadi 1982 akateuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Ushirika Tanzania.
Kisiasa Hamad Rashid amekuwa mwanachama wa ASP na baadaye CCM, kabla hajahamia Chama Cha Wananchi CUF baada ya kufukuzwa CCM mwaka 1988. Amekuwa Katibu wa Vijana wa ASP kati ya mwaka 1970 – 1972, amefanya kazi na benki ya ASP kati ya mwaka 1972 hadi 1977, amekuwa mwakilishi wa CCM katika Chama Cha Ushirika kati ya mwaka 1978 – 1988 na amewahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kuanzia mwaka 1982 – 1988.
Uanachama wa Hamad Rashid na wenzake kadhaa ndani ya CCM ulikoma mwaka 1988 baada ya chama hicho kuwavua nyadhifa zao zote za uongozi wa kichama na kiserikali kwa sababu ya tuhuma kadha wa kadha ambazo ni vigumu kuzithibitisha hadi leo. Yeye mwenyewe na wenzake mara kadhaa wamesisitiza kuwa walifukuzwa kwa kuonewa na kw sababu tu walionekana wanatetea misimamo thabiti ambayo CCM haikuipenda kwa woga usio na maana.
Mwaka 1992 Hamad Rashid alikuwa mmoja wa waasisi na waanzilishi wa Chama Cha Wananchi CUF ambako ametumikia nyadhifa kadhaa za ndani ya chama ikiwemo ukurugenzi wa chama katika vipindi kadhaa, ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa, Ujumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la taifa n.k.
Hamad Rashid akiwa CUF alikuwa mmoja wa viongozi waliofanya kazi kubwa katika kusimamia mazungumzo ya kutafuta muafaka kati ya CUF na CCM (akiiwakilisha CUF).
Hamad Rashi ameoa na ana watoto.
MBIO ZA UBUNGE
Akiwa ndani ya CCM, Hamad Rashid ni mmoja wa wanasiasa walioanza kuwa wabunge takribani miongo zaidi ya mitatu iliyopita. Amekuwa mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 1978 - 1988 na wakati huo pia akiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania kati ya mwaka 1980 – 1982 na Naibu Waziri wa Madini, Fedha na Uchumi wa Tanzania kati ya mwaka 1982 – 1988.
Lakini hata katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995, Hamad Rashid alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na kutumikia nafasi hiyo hadi mwaka 2000.
Kuanzia mwaka 2000 - 2005 Hamad Rashid aliteuliwa na Rais wa Tanzania wakati huo, Benjamin Mkapa, kuwa Mbunge katika Bunge la Tanzania. Mwaka 2005 alijitosa katika jimbo la Wawi akiomba kuchaguliwa kuwa mbunge na aliungwa mkono na asilimia 75 ya wapiga kura kwenye masanduku. Kuchaguliwa kwake kulimfanya achaguliwe pia na wabunge wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, kuwa kiongozi mkuu wa kambi hiyo, wadhifa ambao aliutumikia hadi mwaka 2010.
Kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alitupa karata zake kwa mara nyingine pale Wawi na kufanikiwa kuchaguliwa tena lakini mara hii hakuweza tena kuendelea na wadhifa wa kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa sababu CUF haikuwa na wabunge wengi ili kufikia vigezo vya kuongoza kambi hiyo.
Hadi niandikapo kumhusu, yeye ni mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania japokuwa Chama Chake (CUF) kilikwishamvua uanachama mwaka 2012 kutokana na tofauti kati yake na viongozi wenzake. Alipovuliwa uanachama moja kwa moja ilikuwa na maana ya kupoteza nafasi ya ubunge kwa mujibu wa katiba, lakini alikwenda kutafuta haki katika Mahakama Kuu ya Tanzania ambako liliwekwa zuio la muda la kutekeleza wa uamuzi wa vikao vya CUF hadi mahakama itakapoamua juu ya shauri alilolipeleka. Hadi mwaka huu wa uchaguzi bado mahakama haijaamua shauri ambalo Hamad Rashid alilifungua dhidi ya chama chake na ndiyo kusema kuwa atamaliza kipindi chake cha ubunge mwezi Julai na hivyo mvutano ulioko mahakamani kuisha kwa mtindo huo.
MBIO ZA URAIS
Hamad Rashid hajatangaza kugombea Urais wa Jamhri ya Muungano wa Tanzania lakini nilipofanya utafiti na kuwauliza baadhi ya viongozi na wanachama wa ADC walimtaja kama mmoja wa watu muhimu ndani ya chama hicho wenye sifa, uwezo vigezo na ari ya kuweza kugombea urais, kuleta ushindani na hata kushinda wakitokea vyama vya upinzani. Hiyo ndiyo sababu iliyomfanya aingie kwenye orodha hii.
NGUVU YAKE
Mambo makubwa matatu nayatizama kama karata zinazompa Hamad Rashid nguvu na ubavu wa kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania:
Kwanza, kiongozi huyu ni mzoefu sana katika masuala ya ndani na nje ya serikali. Hamad Rashid amekuwa serikalini kwa miaka zaidi ya 30, amesimamia masuala mengi ndani ya serikali na ni watanzania wachache sana wenye rekodi kama yake. Kwa sababu Rais bora pia huhitaji kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu masuala ya kiserikali, Hamad Rashid ameshavuka kigezo hiki na kinampa nguvu thabiti.
Lakini jambo la pili ni uelewa mkubwa. Kati ya viongozi ambao ukipishana nao unaona kabisa ngazi kubwa ya uelewa wao ni pamoja na Hamad Rashid, yeye si msomi sana, si Daktari wala Profesa na si mtu mwenye shahada nyingi lakini akianza kujenga hoja au kushauri njia za utatuzi wa masuala ya wananchi unaweza kuona uwezo wa baadhi ya maprofesa na madaktari wakiwa chini yake, yeye ni mmoja wa wanasiasa ambao hunifanya niamini kuwa elimu si kila kitu katika uongozi, inahitaji kuambatana na masuala mengine mengi ndiyo inakuwa na manufaa kwa jamii. Uelewa wa Hamad Rashid kwa maana ya mambo ya Tanzania na ya kimataifa unamvusha katika chujio la watu ambao wanaweza kutiliwa mashaka kiuwezo katika uongozi wa juu wa nchi.
Lakini jambo la mwisho linalozidisha nguvu yake ni ile rekodi ya kuweza kufanya kazi na baadhi ya viongozi wakuu waliowahi kuongoza taifa hili pamoja na wale wa upinzani. Tangu enzi za Nyerere, Hamad Rashid hakukosa japo kuteuliwa kuongoza wizara nyeti, na hata wakati wa Mwinyi vivyo hivyo. Ulipokuja mfumo wa vyama vingi na baada ya yeye na wenzake kufukuzwa CCM alianza kufanya kazi na viongozi wenye majina makubwa katika vyama vya upinzani. Rekodi hii nayo inamuweka juu sana, kwamba katika kipindi chote hicho ameweza kuchota uzoefu wa kutosha wa masula ya uongozi wa nchi na hapo huwezi kumtilia shaka.
UDHAIFU WAKE
Jambo moja ambalo nalichukulia kama udhaifu mkubwa sana wa Hamad Rashid ni ile hali ya kutovumilia kukaa bila kuwa kiongozi hata kama mazingira ya wakati husika hayaruhusu nia yake kutekelezeka. Watu waliofanya kazi na kiongozi huyu kwa muda mrefu kutoka ndani ya CUF wamenifahamisha kuwa yeye huhitaji kuwa kiongozi mahali popote pale alipo, na jambo hilo lisipotokea huweza kuchukua hatua zozote ambazo atadhani zinafaa kwa wakati husika.
Watu wenye tabia kama yake hupata matatizo makubwa sana katika siasa za Afrika ambako masuala ya uongozi si ya kupokezana vijiti na hata katika siasa za Tanzania ambako viongozi katika vyama wanakaa muda mrefu ili kutekeleza dhana nyingine ya kuvihuisha vyama walivyomo. Kwa mtu ambaye si mvumilivu, siasa za Afrika ni ngumu sana kwenye eneo hili na inaonekana Hamad Rashid hajakubaliana na jambo hilo, matokeo yake atapata matatizo ya kisiasa katika majukwaa mengi atakayopitia na jambo hili limewaponza wanasiasa wengi wa Afrika.
Lakini jambo la pili, Hamad Rashid ni mtu mwenye mipango mingi isiyotekelezeka. Baadhi ya wanachama waliojiunga katika chama cha ADC na baadaye kujiondoa wamenieleza kuwa walishawishika sana baada ya kusikia viongozi wakiwaeleza masuala mengi ambayo yeye alikuwa pia akiyataja kama mipango ya muda mfupi na muda mrefu ya chama hicho. Lakini hadi leo wananieleza kuwa masuala muhimu ambayo walitarajia angeyafanyia kazi hakuyakamilisha. Lakini pia baadhi ya viongozi waliofanya naye kazi ndani ya CUF wanamtaja sana kwa sifa hii ambayo kiuongozi naichukulia kama udhaifu uliopitiliza.
Na mwisho, Hamad Rashid wakati mwingine haelewi mahali gani aongee jambo gani, hasa anapokuwa na machungu yanayosumbua akili yake. Akiwa katika Bunge Maalum la katiba aliwashangaza watu wengi pale alipotumia sehemu kubwa ya hotuba yake kumshambulia hasimu wake kisiasa, Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Kwa mtizamo wangu, Hamad Rashid alihamishia ugomvi wake na wa viongozi wake au na chama chake cha zamani kwenda katika bunge la kitaifa linalotunga katiba. Alipoteza muda mwingi sana kufanya mashambulizi kwa mtu ambaye hayumo bungeni na hawezi kumjibu. Watu wengi ambao tumekuwa tukimfahamu kiongozi huyu kwa busara na utulivu mkubwa, tuligutushwa sana na hali ile na inaweza kupelekea ikahitimishwa kuwa si mfano bora wa uongozi au wa mtu anayetajwa kuwa na sifa na vigezo vya kuweza kuwa Rais wa nchi.
NINI KINAWEZA KUMFANYA APITISHWE
Kama ADC itafikiria na hata kumpitisha Hamad Rashid kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sababu moja kubwa itakuwa ni kuhuisha ujenzi wa chama hicho kichanga. Ikumbukwe kuwa ADC ni chama kipya, hakina hata miaka minne katika ulingo wa kisiasa, kwa vyovyote vile kinahitaji mtu mwenye uelewa, uzoefu na uwezo kama wake.
Lakini jambo la pili linaweza kufanya apitishwe ni kwa sababu ya umaarufu. Pamoja na kwamba ni Mzanzibari, lakini Hamad Rashid ni kiongozi anayefahamika sana ndani ya Tanzania Bara na visiwani. Viongozi wengi wa Zanzibar hufanikiwa kuwa maarufu katika visiwa hivyo tu. Yeye ni mmoja wa wale waliovuka mipaka na nadhani chama hicho kipya kinahitaji kuwa na mgombea wa aina hii ili kiwavute wapiga kura.
Lakini jambo la tatu linaloweza kumvusha pia ni kwa sababu yeye ni mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika uanzishaji wa chama hicho. Na katika siasa za Afrika, watu wa aina hii hupewa uzito mkubwa pale ambapo hutokea wanataka nafasi ya uongozi.
Na mwisho, uzoefu wa kufanya kazi Tanzania Bara na Zanzibar kwa pamoja vinampa Hamad Rashid nafasi ya kipekee ya kuwa mgombea wa Urais wa chama hicho. Kwamba yeye ni Mzanzibari ambaye amefanya kazi Zanzibar muda mrefu lakini pia akifanya upande wa Bara. Ni mmoja wa viongozi wanaotoka Zanzibar huku wakifahamu vizuri sana masula ya Bara na hii ni faida muhimu kwa ADC.
NINI KINAWEZA KUMWANGUSHA KWENYE MCHUJO?
Moja ya masuala yatakayoweza kumkwamisha kwenye mchujo wa nafasi hii ni ikiwa chama chake (ADC) kitaamua kuweka mgombea kutoka Tanzania Bara ili aweze kupambana vilivyo na hata kuwa na uwezo wa kulinda kura nyingi zitakazopigwa kwa mkumbo wa U-bara na U-Zanzibari.
Tukumbuke kuwa wapiga kura walioko Tanzania Bara ni kwa mamilioni na chama chochote kile cha siasa kingependa kuvutia waliko wapiga kura wengi kwa sababu siasa zile za umoja wa kitaifa zimeanza kupotea na wazanzibari wameanza kupoteza uwezo na nguvu za kupata nafasi ya Urais wa Jamnhuri ya Muungano wa Tanzania, labda hadi siku “Nyerere mwingine” atakapozaliwa.
MIPANGO MINGINE IWAPO HATACHAGULIWA NA CHAMA CHAKE (PLAN B)
Kama Hamad Rashid hatapaendekezwa na chama chake kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naamini moja kwa moja atakuwa mmoja wa wgombea Urais wa Zanzibar. Tayari natambua kuwa mwaka huu akiwa bungeni Dodoma (Bunge la Bajeti), aliutangazia umma kuwa ana mpango wa kugombea Urais wa Zanzibar na nadhani huu ni mpango wa kwanza kwake, wakati anastaafu siasa za Ubunge.
Lakini mpango wa pili unaoweza kuwa mezani kwa kiongozi huyu ni kuendelea na biashara. Hamad Rashid ni mfanyabiasha wa kadri na amekuwa hivyo katika kipindi kirefu sana. Kama hatogombea Urais wa Tanzania naona akijikita katika biashara na kufanikiwa sana.
HITIMISHO
Kwa sababu Hamad Rashid ni Mtanzania mwenye asili ya Zanzibar na anayetokea upande wa Zanzibar, tena kisiwani Pemba. Sioni akiwa na nafasi kubwa sana katika siasa za kitaifa ndani ya miaka mitano ijayo.
Shida ya siasa za Zanzibar ni kwamba kama wewe hauko CUF au CCM ni kama vile huna mahali pa kufanyia siasa, na nadhani hili ndilo linalomkuta. Wanasiasa wengi wakubwa wanaotoka Pemba au Unguja na waliohama CCM walifanikiwa ikiwa walikwenda CUF, na waliohama CUF walifanikiwa ikiwa walikwenda CCM, ni vigumu kabisa kufanya siasa Zanzibar nje ya CUF na CCM na jambo hili linamgusa moja kwa moja Hamad Rashid.
Anaweza kuamua kuja kufanya shughuli za siasa Tanzania Bara ambako nako navyoona hali ya mambo, ndani ya miaka michache ijayo Wazanzibari watakuwa na nafasi ndogo sana ya upenyo wa kisiasa maana hali ya “usisi” na “umimi” imeshakuwa kubwa mno na kila upande (Bara na Zanzibar) umeanza kumuona mwenzie kwa jicho kali.
Lakini, kwa sababu Hamad Rashid ni mwanasiasa wa siku nyingi na anajua njia nyingi za kupita, nawajibika kuweka akiba ya maneno na kumtakia kila la heri katika safari yake ngumu kisiasa, kiongozi huyu ambaye amewavutia vijana wengi sana wa Zanzibar na Tanzania bara, kujiunga katika siasa za kitaifa.

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR