Showing posts with label 28SEPTEMBA. Show all posts
Showing posts with label 28SEPTEMBA. Show all posts

Monday, September 29, 2014

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA 24 YA MWAKA A, 28SEPTEMBA

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA 24 YA MWAKA A, 28SEPTEMBA



Tunakualika katika tafakari yetu, Dominika ya 24 ya mwaka A wa Kanisa tukilenga kukua katika toba na msamaha wa Mungu ulio wa kudumu. Katika historia, kadiri ya mangamuzi ya watu njia rahisi ya kujibu dhuluma ilikuwa ni kwa njia ya hasira na zaidi jino kwa jino (Kut 21:24) wakijaribu kutafuta mlinganyo sahihi (proportionality to the offence) lakini leo hii kadiri ya somo la kwanza toka kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira tunaalikwa kutawala hasira zetu, kuacha chuki na kuacha kulipiza kisasi maana haya ni machukizo mbele ya Mungu. Ni hali ambayo huongeza taabu katika jumuiya badala ya kupunguza taabu. Basi kama mmoja wetu atashupaa katika haya, naye vivyohivyo atatendewa vivyohivyo yaani atajiondoa katika ufalme wa Mungu. Kumbe ndugu yangu mpendwa, leo tunaalikwa kupiga hatua katika safari ya kiroho tukiunganika na mausia ya Bwana kadiri ya Injili.

Mtume Paulo akiendeleza fundisho tunalolipata katika somo la kwanza anasema sisi hatuishi kwa ajili yetu wenyewe kama watu wenye chuki na visasi waishivyo bali twaishi kwa ajili ya Bwana. Anafundisha hili kwa sababu katika jumuiya ya kirumi mjini Roma kuna utengano kati ya wanaoshika sheria ya kufunga kadiri ya utamaduni wa mwanzo walipopokea imani na wale wanaojiona wa kisasa wanoshika sheria ya mapendo kwa ndugu. Kumbe ili kusahihisha dosari hii Mt. Paulo anasema sisi sote ni mali ya Bwana katika yote na hata tukifa tunakufa katika yeye. Ndiyo kusema matendo, maneno yetu, nyajibu zetu, sheria tunazoshika, familia zetu, parokia zetu, majimbo yetu tunayoyasimamia ni mali ya Kristu. Kwa hivi tuwajibike tukitambua hilo na mwishoni mapenzi ya Mungu yafanyike. Mafundisho ya Mt Paulo ni msaada kwa jumuiya zetu zinapojikuta ziko katika mgongano kwa sababu ya mwono tofauti. Zinaalikwa pande mbili pinzani kuketi na kutatua shida kwa pamoja kwa kuheshimiana.

Tunaendelea bado kutafakari Injili ya Mathayo, na leo Mwinjili atuambia kuwa msamaha ni wa kudumu. Msamaha hauna mipaka bali kama ulivyo upendo unaovumilia basi na msamaha wapaswa kuwa namna hii. Mt Petro akiwa bado katika mawazo ya kiyahudi ya kusamehe kimahesabu, yaani mara saba, anamwuliza Kristu nisamehe mara ngapi ndugu akinikosea? Kristu anakuja na fundisho jipya ya kwamba hakuna tena suala la mahesabu katika kusamehe bali mapenzi ya Mungu yatimizwe daima. Kristu anataka tuondoke katika mazoea ya kila siku na hivi tuingie katika mpango wa milele ambao ni msamaha wa kudumu. Mfano wa mtumwa katika Injili, mtumwa aliyesamehewa deni, deni ambalo asingeweza kulilipa mpaka anakufa kwa hakika ni kielelezo cha huruma ya Mungu iliyo milele!

Pamoja na huruma ya Mungu iliyo milele bado mwanadamu ni dhaifu, haoni vema. Huyu mtumwa aliyesamehewa deni lote yeye mwenyewe hakuweza kuwasamehe wajoli wake. Hiki ni kielelezo cha udhaifu wa mwanadamu ambaye daima hushindwa kusamehe na hasa kosa au dhambi inapojirudia. Ni picha ya kuwa tunahitaji daima huruma ya Mungu. Basi ndugu yangu mpendwa, tukumbuke kuwa kusamehe ni zawadi, ni fadhila tunayopaswa kuiomba daima ili tuweze kuunganika na Kristu mfufuka anayetutaka kusamehe daima na anayesamehe daima. Kinyume cha fadhila hii basi tutakuwa tumejiweka pembeni katika ufalme wa Mbinguni.

Tumalizie tukisema, Suala la kusamehe ni wajibu wa kila mtu awaye yote si wenye mamlaka ya juu tu katika jumuiya bali na wale wanaoongozwa na tukumbuke kuanguka katika dhambi ya kutosamehe na kukuza chuki zisizoisha ni hatari kubwa iliyo mbele yetu. Yaweza kuzuia na hivi tukakosa kuingia mbinguni. Fikiri kidogo mtu asemaye “Mimi nitakapokufa mtu fulani asikaribie na hata kuweka udongo kwenye kaburi langu!! Chuki ya ujazo huu haina maelezo lakini yatishishia usalama wa roho ya mtu huyo aliyefariki!! Tafakari kidogo!Tumwombe Mungu daima atutangulie na kutulinda katika kutekeleza wajibu wa kusamehe. Tumsifu Yesu Kristu.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya Cpps
TAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA 24 YA MWAKA A, 28SEPTEMBA

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR