Wednesday, October 10, 2012

.Bikira Maria anapewa heshima zaidi

Bikira Maria kati ya Waorthodoksi

Kwa kiasi kikubwa imani ya Waorthodoksi kuhusu Maria inalingana na ile ya Wakatoliki, ingawa hawakubali jinsi baadhi ya dogma hizo zilivyotangazwa na jinsi zinavyofafanuliwa.

Bikira Maria katika Uprotestanti

Martin Luther alipoanza Matengenezo ya Kiprotestanti aliandika kwa heshima juu ya Bikira Maria, lakini kadiri mabishano yalivyozidi kati ya madhehebu ya Kikristo, Waprotestanti walizidi kupinga mafundisho ya Kanisa Katoliki juu ya Mama wa Yesu. Siku hizi baadhi yake, hasa Waanglikana na Wamethodisti wanamrudishia Maria nafasi yake kama kielelezo cha imani na cha kupokea neema ya Mungu.

Bikira Mariamu katika Uislamu

Kurani inamtaja mwanamke mmoja tu, tena mara 34: ni Mariamu, mama wa nabii Isa. Akichanganywa na dada wa Haruni na Musa, aliyekuwa na jina hilohilo, anatajwa kama binti Imrani. Pia habari nyingine kadhaa zinapishana na zile za Injili.

Hata hivyo anapewa heshima ya pekee, kama inavyoonekana katika sura ya 3:43: “Na kumbukeni malaika waliposema, ‘Ewe Mariamu, kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuchagua na kukutakasa na kukutukuza kuliko wanawake wa walimwengu”. Tena katika aya 3:46: “Na kumbukeni waliposema malaika: ‘Ewe Mariamu, bila shaka Mwenyezi Mungu anakupa habari njema za Neno litokalo kwake, jina lake Masihi Isa mwana wa Mariamu, mwenye heshima katika dunia na ahera, na yu miongoni mwa waliokaribishwa’”.

Aliambiwa amefanywa “ishara” pamoja na mwanae, ingawa haisemwi ni ishara ya nini. Sura ya 19, yenye jina lake, inaeleza kwamba Malaika Jibrili (Gabrieli) akimpasha habari ya mimba alisema, ‘Hakika mimi ni mjumbe wa Mola wako ili nikupe mwana mtakatifu’. 

Akasema, ‘Ninawezaje kupata mtoto hali hajanigusa mwanamume yeyote, wala mimi si mwasherati?’ Akasema, ‘Ni kama hivyo; Mola wako amesema: Haya ni rahisi kwangu, na ili tukufanya ishara kwa mwanadamu na rehema itokayo kwetu, na ni jambo lililokwisha hukumiwa’ ” (19:19-21). “Na mwanamke yule aliyejilinda tupu yake na tukampulizia roho yetu na tukamfanya yeye na mwanawe ishara kwa walimwengu” (21:91).

Pamoja na kusifiwa kwa usafi wake, anaongezewa sifa za imani na unyenyekevu: “Na Mariamu binti Imrani aliyejilinda uchi wake, na tukampulizia humo Roho yetu na kayasadikisha maneno ya Mola wake, na vitabu vyake; na alikuwa miongoni mwa wanyenyekevu” (66:12).

Altare ya Bikira Maria


Dogma za Kanisa Katoliki kuhusu Bikira Maria



Kuna mafundisho makuu manne kumhusu Bikira Maria ambayo ni lazima kila Mkatoliki ayasadiki kutokana na ufunuo wa Mungu:
1. B. Maria mkingiwa dhambi ya asili
2. B. Maria Mama wa Mungu
3. B. Maria Bikira daima
4. B. Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho
Mkingiwa Dhambi ya Asili

Malaika alimsalimia Maria “umejaa neema” (Lk 1:28) maana ndiye tunda bora la ukombozi ulioletwa na Yesu. Ni imani ya Wakatoliki kwamba kwa stahili za Mwanae alikingiwa asirithi kwa wazazi dhambi ya asili na madonda yanayotokana nayo, wala asitende dhambi maisha yake yote. Kwa maneno mengine, Bikira Maria tangu atungwe mimba Mungu alimkinga na kila doa la dhambi kwa kutazamia stahili za Yesu Kristo aliye Mkombozi wa binadamu wote. Ndiye aliyekombolewa kwa namna bora kushinda viungo vyote vya Kanisa. Maisha yake yote hakutenda dhambi hata moja. Mapokeo ya mashariki yanamuita “A Panagia” = “Mtakatifu tu”. Dogma hiyo ilitangazwa na papa Pius IX mwaka 1854, halafu mwaka 1858 Bikira Maria alijitambulisha kama Mkingiwa kwa Bernadeta Soubirous huko Lurdi (Ufaransa). Tena mwaka 1917 huko Fatima (Ureno) aliwafunulia Lusia, Fransisko na Yasinta Marto moyo wake safi usio na doa.
 

Mama wa Mungu

Injili ya Yohane inaanza kwa kishindo, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” (Yoh 1:1). Huyo Mungu Mwana alitwaa ubinadamu katika Bikira Maria akazaliwa mtoto, jina lake Yesu, maana yake Mungu Mwokozi. Huyo ni binadamu kama sisi katika yote isipokuwa dhambi. Ubinadamu wa Yesu unategemea Nafsi yake ya Kimungu: akisema, ‘Mimi’, ni kwa Nafsi yake hiyo. Ndiyo maana aliwaambia Wayahudi, “Kweli nawaambia, kabla Abrahamu hajazaliwa, nalikuwepo” (Yoh 8:50). “Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai” (Yoh 5:26).

Mtume Paulo akaeleza, “Wakati maalumu ulipotimia Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke” (Gal 4:4). Bikira Maria ni Mama wa Mungu kwanzia wakati huo: tangu Bikira Maria alipojaliwa kumchukua mimba, kumzaa, kumnyonyesha na kumlea mtu ambaye kwa asili ni Mungu. Cheo hicho kimemuinua juu kuliko hata malaika. “Malaika alimwambia, ‘Hicho kitakachozaliwa kitaitwa Kitakatifu, Mwana wa Mungu’” (Lk 1:35).

Dogma ilitangazwa mwaka 431 kwenye Mtaguso wa Efeso uliomuita “Mzazi wa Mungu”, ukisema Maria anastahili kuitwa hivyo kwa sababu Mwana wa milele wa Mungu, ambaye ni Mungu sawa na Baba, alifanyika mtu toka kwake. Akiwa mja mzito alishangiliwa: “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?” (Lk 1:42-43). Ungamo hilo la Elizabeti likakamilishwa na Mtume Thoma aliyemuambia Yesu mfufuka: “Bwana wangu na Mungu wangu!” (Yoh 20:28).
Bikira na Mama

Wakristo na Waislamu wote wanakiri kuwa Yesu alitungwa bila ya mchango wa mwanamume. La ajabu zaidi katika imani hiyo ni kwamba hata uzazi wenyewe haukuondoa ubikira wake, bali uliutakasa: ni Bikira daima. Ingawa akili inasita, ni lazima kukiri na malaika, “Hakuna lisilowezekana kwa Mungu” (Lk 1:38). Yosefu, ingawa kisheria alikuwa mume wake, hakutenda naye tendo la ndoa.

Ni imani ya Wakatoliki na Waorthodoksi kuwa Mama wa Yesu anastahili kuitwa “Bikira daima” kwa sababu alimchukua mimba akiwa bikira, akamzaa bila ya kupotewa na ubikira, akabaki bikira hadi mwisho wa maisha yake. Hamu yake ya kuwa bikira hata kisha kuchumbiwa inajitokeza katika jibu alilompa malaika aliyemtabiria mimba: “Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?” (Lk 1:35). Ni kielelezo cha Wakristo ambao Mtume Paulo aliwaandikia: “Nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi” (2Kor 11:2), “mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine” (1Kor 7:35).

Wanaosemwa katika Injili “ndugu zake Yesu” si watoto wa Bikira Maria, bali ndugu wa ukoo waliokuwa jirani sana na familia hiyo takatifu. Kama Bikira Maria angekuwa na watoto wengine, Yesu angekuwa amefanya kosa la kuwanyang’anya Mama yao na kumfanya awe Mama wa mtume Yohane alipomkabidhi msalabani, “‘Mwana, tazama Mama yako’. Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake” (Yoh 19:27).

Katika Agano Jipya yupo Yakobo anayeitwa na mtume Paulo “ndugu yake Bwana” (Gal 1:19): Yakobo huyo alikuwa maarufu katika Kanisa la Yerusalemu (Mdo 12:7; 15:13-21; 21:18-20; Gal 2:9). Yakobo huyo si mtume Yakobo kaka yake Yohane (Lk 6:12-16), bali ni Yakobo ndugu yake Yose na mama yao kwenye Injili anaitwa “Maria mwingine”, si Maria Mama wa Yesu. “Walikuwepo pia wanawake waliotazama kwa mbali. Miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome na Maria mama wa akina Yakobo mdogo na Yose” (Mk 15:40). Maria lilikuwa jina la kawaida kwa Wayahudi: akina Maria wakiwa wengi hivyo, tujue kuwatofautisha kwenye Injili, ambazo zinamtaja Bikira Maria kama “Mama wa Yesu”.
Kupalizwa Mbinguni mwili na roho

Baada ya maisha haya ya duniani Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho, ishara ya mwanamke mshindi. “Ishara kubwa ikaonekana mbinguni, ambapo mwanamke aliyevikwa jua, pia na mwezi chini ya miguu yake, na taji la nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake” (Ufu 12:1). Maneno ya shangilio lake yametimia: Mungu “amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza” (Lk 1:52).

Imani hiyo ya mapokeo ya kale, yanavyoshuhudiwa na Mababu wa Kanisa, ilitangazwa rasmi na Papa Pius XII kwa niaba ya maaskofu wote mwaka 1950.
Heshima za Liturujia ya Kiroma kwa Maria

Kuna ibada za Mama Bikira Maria zinazoadhimishwa katika liturujia ya Kiroma. Hapa zimepangwa kulingana na heshima zinavyozidiana:
Sherehe

8 Desemba – Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili 1 Januari – Bikira Maria Mama wa Mungu 25 Machi – Bikira Maria Kupashwa Habari 15 Agosti – Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni
Sikukuu

31 Mei – Maamkio ya Bikira Maria 8 Septemba – Kuzaliwa kwa Bikira Maria
Kumbukumbu

Juni – Moyo Safi wa Maria 15 Septemba – Mama Yetu wa Huzuni 22 Agosti – Bikira Maria Malkia 7 Oktoba – Bikira Maria wa Rozari 21 Novemba – Bikira Maria Kutolewa Hekaluni
Kumbukumbu za Hiari

11 Februari Bikira Maria wa Lurdi 13 Mei – Bikira Maria wa Fatima 16 Julai – Bikira Maria wa Mlima Karmeli 5 Agosti – Kutabaruku Kanisa la Bikira Maria 12 Septemba – Jina takatifu la Maria 12 Desemba – Bikira Maria wa Guadalupe

Tena kila Jumamosi isiyo na adhimisho maalumu, Kanisa huadhimisha kumbukumbu ya Mama wa Mungu.

Pia zipo heshima za binafsi kwa Bikira Maria: mashariki zinatumika tenzi na nyimbo mbalimbali, k.mf. Akatistos inayomuita “daraja linalounganisha dunia na mbingu”, “ngazi aliyoiona Yakobo” “kina kisichochunguzika kwa macho ya malaika” (Mwa 28:12); magharibi]] anaheshimiwa kwa rozari.

Wakristo wanaomheshimu Bikira Maria hawamuabudu hata kidogo, lakini wanamtolea heshima ya juu kuliko watakatifu wengine. Tofauti ni kwamba Mungu tu anastahili kuabudiwa (kwa Kigiriki, ‘latria’) watakatifu wanapewa heshima (‘dulia’) na Bikira Maria heshima zaidi (‘yuper-dulia’). Kanisa Katoliki linakiri neema zote za Mungu zinampitia Maria.

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR