Katika Maandiko Matakatifu tunasoma yafuatayo: "Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani, akakaa huko siku arobaini akijaribiwa na shetani" (Marko 1:12-13).Yesu anaenda Jangwani
na kukaa huko kwa muda wa siku arobaini. Lengo la kwenda jangwani si
kujaribiwa ila kujiandaa kwa kazi iliyokuwapo mbele yake, kazi ya kumkomboa mwanadamu. Yesu alikwenda kutafakari kazi yake yote na yale yatakayompata katika kazi hiyo. Yesu alikwenda kutengeneza dira ya utekelezaji wa kazi ya ukombozi.
Read More
Nasi tunapoanza Mwaka Mpya 2015 tunahitaji kuingia katika 'jangwani' la kiroho na kimaisha ili kujitengenezea dira ya utekelezaji kwa mwaka mzima. Tujiwekee malengo binafsi, malengo ya familia, Jumuiya, kanda, kigango, parokia, jimbo na mahali pa kazi. Ni kipindi cha kujiwekea malengo ya kiroho, kiuchumi na kijamii. Mathalani. Mfano :
KIROHO: Jipangie mwaka huu unataka kufika wapi? Panga
mambo yako ya kukua kiroho;tafakari ya Neno la Mungu; sala binafsi,
sala za familia, ushiriki wako katika Jumuiya, kanda, kigango, parokia
na kijimbo. Panga kushiriki mafungo ya kiroho, semina za kiroho, hija na
matendo ya huruma. Ushiriki wako katika vipindi vya Kwaresma, Pasaka,
Majilio na Krismas n.k.
KIUCHUMI: Tengeneza dira ya kiuchumi mwanzoni mwa mwaka kwa kupanga unataka kufika wapi kiuchumi mwaka huu. Usiache suala la uchumi likuendeshe bali
wewe ulitawale kwa kufuata utakachojipangia mwanzoni mwa mwaka.
Utajikuta unafanya mambo mengi kwa mpangilio hadi unafurahia maisha. Panga bajeti ya mwaka mzima; mapato na matumizi yako yaandike ili yakuongoze.
Bajeti yako
iwe shirikishi ili itekelezeke, isiwe siri yako. Shiriki au ongoza
kupanga bajeti ya mwaka ya familia, jumuiya, parokia, jimbo na mahali pa
kazi. Iheshimu bajeti hiyo. Bajeti yako ianze na matumizi ili ikuongoze
kupanga mapato. Kama mapato ni madogo kulingana na matumizi; fanya
ubunifu, fikiria fursa mpya na zifanyie kazi, pia punguza matumizi
yasiyo ya lazima, kadi za michango isiyo ya lazima, vikao visivyo na tija vitakavyokugharimu n.k. Wakati mwingine ni heri ya lawama kuliko fedheha!
Panga
zaka yako, sadaka, majitoleo, michango ya Jumuiya, mavuno ya parokia,
mavuno ya jimbo n.k usikurupuke kila siku na kwenda kutoa 'makombo'
hayana nafasi mbele ya Mungu ni sawa na kujiletea 'laana' maishani
mwako.
Mambo mengine muhimu ya kupanga katika dira ya mwaka huu ni
pamoja na kushiriki matukio muhimu ya kijamii. Ni mwaka wa kura za maoni
ya kupata katiba ya nchi yetu, usithubutu kupanga kutokushiriki, huo ni
wajibu wa kila raia wa Tanzania.
Kushiriki uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.
Ili tupate viongozi wazuri, wachamungu, waadilifu na wakweli, jitokeze
ili uchaguliwe na/au uchague kiongozi atakayetufaa kuiongoza jamii na
nchi yetu.
Mwaka wa Familia utafungwa rasmi mwaka huu, Je, umeambulia nini kiimani? Umejiwekea mikakati
gani ya kutengeneza mapungufu yaliyo ndani ya familia yako? Shiriki
vyema semina za mwaka wa familia. Huu pia ni Mwaka wa Watawa Duniani,
Je, unashiriki namna gani katika kuhamasisha, kukuza na kulea miito
mitakatifu ndani ya Kanisa?
Huu
ni mwaka wa uchaguzi wa viongozi wa Kanisa - walei kuanzia ngazi ya
Jumuiya ndogondogo hadi Taifa. Jitokeze uchaguliwe na uchague viongozi
hao. Shiriki kikamilifu kwani kanisa linakuhitaji.
Yote
hayo yanatuhitaji kwenda 'jangwani' ili kujipanga. Tumshirikishe Mungu
kupitia sala na mafungo. Tumkabidhi Mungu malengo yetu ya mwaka 2015. Tujitathmini mara
kwa mara juu ya utekelezaji wa malengo hayo. Tuache kuishi kwa mazoea,
mwaka 2015 tuwe wahalisia, tusibahatishe! Tuepuke mikwaruzano, tuongeze
furaha na ufanisi. Tuwe 'Kristu' katika maisha yetu ya kila siku ili
kuisaidia jamii. Tuache kulalamika lalamika, tuchukue hatua.
Showing posts with label Heri ya mwaka mpya 2015. Show all posts
Showing posts with label Heri ya mwaka mpya 2015. Show all posts
Wednesday, January 7, 2015
Subscribe to:
Posts (Atom)
-
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya...
-
Isidore Bakanja, ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya imani ya Kikristo, Akiongozwa na maisha rahisi kama layman Katoliki wakati wa mauaj...
-
Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza anatualika kutambua kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya ...