Friday, November 1, 2013

Maadhimisho ya Siku ya Watakatifu wote na siku ya Marehemu wote

Papa afafanua kiini cha Maadhimisho ya Siku ya Watakatifu wote na siku ya Marehemu wote.



BabaMatakatifu Francisko akiendelea kutoa tafakari juu ya sala ya Nasadiki, kwa Jumatano hii, alilenga zaidi katika usharika na Watakatifu, kama Kateksimu ya Kanisa Katoliki inavyotukumbusha sisi kwamba, usharika huu ni kwa Mambo Matakatifu na kati ya watu Watakatifu (No. 948 ).

Papa alizama zaidi katika sehemu ya Pili ya kuw ana usharika na Marehemu Watakatifu , ukweli unaohitaji ufafanuzi zaidi katika imani yetu, akieleza pia kwamba, hutukumbusha pia kwamba, hatuko pweke, lakini kuna uwepo wa usharika wa maisha kwa wale wanaokuwa wa Kristu. Usharika mmoja unaoundwa na imani , katika ukweli wake, neno hili Watakatifu hurejea wale wanao mwamini Yesu Kristu kuwa ndiye Bwana wa Maisha na hivyo humwilishwa kwake Yeye ndani ya kanisa kupitia ubatizo. Na kwa namna hiyo , Wakristu wa kwanza waliitwa pia Watakatifu.

Papa aliendelea kufundisha , Usharika wa Watakatifu ni kina halisi cha maana ya Kanisa kwa sababu kama wakristu kupitia Ubatizo , tunafanywa kuwa washiriki wa maisha ya usharika mmoja na upendo wa Utatu Mtakatifu. Na hivyo sote tunaunganishwa mmoja kwa mwingine na kiungo cha ubatizo katika Mwili wa Kanisa. Na kupitia usharika huu wa kidugu, tunawekwa karibu zaidi na Mungu, na tukitakiwa kusaiidiana mmoja kwa mwingine kiroho.

Papa alieleza na kuirejea Injili Yohana ambayo inasema kwamba , kabla ya mateso yake, Yesu aliomba kwa Baba kwa ajili ya umoja kwa wanafunzi wake kwa maneno haya : “Naomba ili wote wawe kitu kimoja kama wewe, Baba , ulivyo ndani yangu , nami ndani yako. Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ndiye uliyenituma "( 17:21). Kanisa , katika kweli yake kamili , ni usharika na Mungu , usharika wa upendo na Kristo na Baba katika Roho Mtakatifu shina la usharika huo. . Uhusiano huu baina ya Yesu na Baba ni dhamana kati ya Wakristo, iwapo pia sisi tumo ndani yake katika umoja huu, na tanuru la moto huu wa upendo katika Utatu Mtakatifu, basi tunaweza kweli kuwa na moyo na roho moja kati yetu kwa sababu upendo wa Mungu unauguza ubinafsi wetu , chuki zetu, utengano na miganyiko yetu ya ndani na nje.

Papa Francisko amesema, iwapo ushariki huu chanzo chake ni mzizi wa upendo ambao ni Mungu, basi pia kuna sababu za kufanya hima kutoa jibu landiyo katika muungano huu na Mungu, maisha ya ushirika wa udugu unaoongoza katika kuwa msharika na Mungu.

Hii ni sehemu ya pili ya usharika, ambayo Papa alitoa msisitizo zaidi, kuwataka watu wa Mungu,kupta uelewa mpana kwamba, imani yetu inahitaji msaada wa wengine , hasa katika nyakati ngumu. Alisema, tazama pia jinsi ilinavyokuwa vizuri kutoa msaada kwa mwingine katika maajabu haya ya imani! Papa alieleza kukemea mwelekea kukubatia tabia ya kutaka kujifungia binafsi, hata katika mazingira ya kidini, kiasi kwamba, inakuwa hata vigumu kwa wengine, hata kuomba msaada wa kiroho, kwa wale wenye uzoefu katika maisha haya ya Kikristu.

Papa alihimiza katika nyakati hizi ngumu ni muhimu kuwa imani kwa Mungu kupitia sala, na wakati huo huo, ni muhimu kupata ujasiri na unyenyekevu kuwa wazi kwa wengine. Papa amekumbusha ushirika wa watakatifu ni familia kubwa, ambapo vipengele vyote ni kusaidia na kusaidiwa yaani kusaidiana mmoja kwa mwingine. Kushirkiana na wengine katika parokia zetu, katika vyama , jumuiya, harakati na vikundi, kama sehemu ya maisha katika safari yetu ya imani, ni kutochoka kuomba msaada wa maombezi na faraja ya kiroho. Ni wakati wetu wa kusikiliza na kuwasaidia wale ambao hawaja jiunga nasi katika safari hii.

Papa alikamilisha Katekesi yake kwa kuchambua kipengele kingine cha usharika wa watakatifu, akisema kwamba, ushariki wa wakatifu huenda zaidi ya maisha ya dunia, inakwenda zaidi ya kifo kwa kuwa huduma milele. Usharika wa kiroho tunaopokea wakati wa Ubatizo hauvunjwi na kifo , lakini umeinuliwa na ufufuko wake Kristu, unao ipeleka roho katika mapito ya utimilifu wa maisha ya milele.

Papa aliendelea kubaini kwmba, kuna dhamana ya kina na isiyokuwa na mwisho kati ya wale ambao bado mahujaji katika dunia hii na wale ambao wamevuka kizingiti cha kifo na kuingia katika umilele. Wote hao huuundwa wakati wa ubatizo hapa duniani,na nafsi hutakatifushwa toharani na kufanywa wenye heri, kuingia katika makazi ya mbinguni ambako ni makazi ya familia moja kubwa. Ushirika huu kati ya nchi na mbinguni ni barabara ya maombezi , ambayo ni aina ya juu ya mshikamano, na pia ni msingi wa maadhimisho ya kiliturujia ya Watakatifu wote na Maadhimisho ya Marehemu wote kama itakavyokuwa siku chache zijazo.

Papa alimalizia kwa kumtaka kila mmoja alifurahie fumbo hili , na kumwomba Bwana neema zake , ili tuweze kuwa karibu zaidi naye na katika usharika na waamini wote, wake kwa waume ndani ya kanisa.
Wito wa Kuombea Iraki
Baada ya Katekesi, Papa akisalimia makundi mbalimbali, pia alilitaja kundi la mahujaji kutoa Iraki ambao walikuwa wakiwakilisha makundi mbalimbali ya kidini, toka yanayojionyesha kama ni utajiri wa Ukristu katika taifa la Iraki . Kundi hili liliongozwa na Kardinali Tauran Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya majadiliano na dini zingine. Papa alitoa wito kwa watu wote kukumbuka kuliombea taifa la Iraki ambalo kila kukicha hukumbana na majanga ya fujo na ghasi za kusitisha zinazofaywa na makundi mabalimbali. Tusali ili Iraki ipate kurejea katika njia ya majadiliano, maridhianao , amani, umoja na utulivu wa kudumu kitaifa.

Sikuku ya Watakatifu woteleo tarehe 01/11/2013

Somo La Kwanza: Ufunuo.7:2-4, 9-14
Wimbo Wa Katikati: Zaburi: 24:1-6 (K) 6
Somo La Pili: 1 Yoh. 3:1-3
Injili: Mathayo 5:1-12
Sikukuu ya Watakatifu wote
Kalenda ya Kanisa Katoliki inajumuisha sikukuu za watakatifu wengi na hata wafia dini. Lakini Novemba mosi, ni sikukuu ya watakatifu wote. Kweli tunasherehekea sikukuu za watakatifu fulani fulani katika siku tofauti lakini Novemba Mosi, tunasherehekea sikukuu ya watakatifu wote, wale tunaowajua na wale tusiowajua. Watakatifu ni wengi na wamefanya kazi nyingi tofauti tofauti lakini zote zikiwa na umuhimu wake katika kuiendeleza na kuikuza imani yetu. Watakatifu ni wengi na hatuwezi kuwajua wote. Hivyo sikukuu hii inawajumuisha pamoja kama kundi moja la watu walioyaishi maisha yao vyema hapa duniani. Sikukuu hii ni kichocheo katika maisha yetu ya imani kwani inatubidi tufuate nyayo zao, tuishe tukimtegemea Mungu zaidi ya chochote. Watakatifu walio pamoja na Mungu mbinguni wanatuombea na kutupa moyo sisi watakatifu tulio safarini kwenda mbinguni. Watakatifu tunao sherekea siku yao leo ni  mashujaa wa imani na kielelezo kwetu, wanatupa moyo kuwa, “Ndiyo kumfuata Kristo kunawezekana.” Kesho Novemba mbili tutawakumbuka marehemu wote. Hawa ni ndugu zetu, wasafiri wenzetu ambao tayari wameiacha dunia hii lakini bado hawajafika mbinguni, wanavikwa mavazi meupe (Ufu.7:9) wanatakaswa kabla ya kuingia mbinguni
Sherehe ya watakatifu wote inatukumbusha kuufuata wito wetu wa kuwa wana wa Mungu. Baada ya mwanadamu kuupoteza utu wake kwa kutenda dhambi, Mungu alimtuma mwanae ulimwenguni ili wale wote wamuaminio wapate ufalme wa milele (Yn. 3:16). Watakatifu wameshaupata ufalme huu wa milele ni wajibu wetu sisi wakristo kufuata mfano wao. Wao walishinda adui wa roho kwa kutumaini neema za Mungu.
Injili ya leo inatuonesha furaha ya watakatifu ilivyo, na njia inayotuwezesha kufika kufika mbinguni. Tunasikia kwamba, “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Kumbe basi, tukitaka vita vya miaka michache hapa duniani vitatuletea furaha na heri ya milele. Inatubidi basi tuvumilie kabisa katika imani yetu, tujaribu kila tuwezavyo tuvishinda vishawishi kwani Mungu hatajaribu zaidi ya neema aliyotupa kuvishinda vishawishi hivyo.  Watakatifu tunaowakumbuka leo, wanatupenda wanatuombea kwa Mungu  ili tuwe pale walipo, karibu na Mungu na kwenye heri ya milele.  Sikukuu hii haina budi kuamsha matumaini makubwa mioyoni mwetu.
Sala:
Ee Mungu niongezee kiu na njaa ya kuyafanya mapenzi yako na siku moja niwe pamoja na watakatifu mbinguni tukikusifu na kuiombea dunia.
Amin

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR