Showing posts with label Marehemu PD:Massawe. Show all posts
Showing posts with label Marehemu PD:Massawe. Show all posts

Monday, October 21, 2013

Mwaka Mmoja Baada ya kifo cha Padre Massawe: aliyependa Vijana na Mwanahabari



NILIPOKEA taarifa za masikitiko na zenye mshtuko mkubwa kwa njia ya simu  kupitia kwa Paroko wa wanga PD. Dismas Mfungomali wa simu ya mkononi usiku wa manane kuamkia Oktoba 26, 2012 kuwa  aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Kimisionari la Kanisa Katoliki  la Consolata, Padri Salutarius Lelo Massawe (50) amezama baharini wakati akiogelea Bagamoyo na mwili wake haujaonekana.
Ilikuwa kama ni  ndoto, wakati Jumapili iliyopita tulikuwa naye tukijiandaa na mkesha wa kimisionari kwa vijana wote wa jimbi la Dar es salaam,   ambapo nililazimika kumpigia Mwenyekiti wa Mabalozi wa Vijana wa Consolata (CMC) Ndugu Machota , na kumuuliza, na yeye amepata habari jana.
  Padri Massawe alifariki mjini Bagamoyo wakati akiogelea katika  Bahari ya Hindi na wakuu wenzake wa Shirika la Consolata kutoka nchi  mbalimbali waliokuwa na mkutano  katika Kituo cha Kiroho cha Consolata kilichoko Bunju jijini Dar es Salaam. Baada ya mkutano aliwaeleza wenzake kuwa angependa wakapumzike Bagamoyo kwa kutembelea maeneo ya kimisionari sehemu ambapo Injili iliingia miaka ya 1800.
Walipofika Bagamoyo, walimaliza kutembelea makaburi, kanisa, na sehemu nyingine muhimu za kihistoria na kuamua kuanza kuogelea. Kwa mujibu wa padri aliyekuwa naye ni kwamba majira ya saa 10 jioni,  waliamua kuondoka kwenye maji lakini Padri Massawe alitokomea kimya kimya ndani ya maji na hakuonekana hadi  kesho yake asubuhi alipokutwa pembezoni mwa  bahari kwenye mikoko.
Kutokana na kutokuwa mbinafsi,  alionesha dhahiri moyo wa uzalendo kwa taifa lake.  Kila mara alikuwa akiniambia ninatamani sana Watanzania wawe matajiri wote, nisione masikini wakitaabika hasa kulala njaa. Ni vigumu  kutamka au kuandika sifa  zake  zote, Padri Massawe licha  ya kuwa alikuwa Mkuu wa Shirika la Kimisionari la Consolata hapa Tanzania wadhifa aliokabidhiwa mwaka jana, pia alikuwa mwanahabari makini, aliyefanya kazi  kwa kuzingatia misingi na weledi, huku akiamini kuwa habari njema siku zote humjenga binadamu kiafya na kiroho.
Alijitahidi kutumia jarida la  kimisonari  Enendeni linalotolewa mara nne  kwa mwaka  na shirika lake, yeye kama mhariri mkuu kuinjilisha, alitumia vyombo vya habari vya Tumaini Media, radio, TV na gazeti la Tumaini Letu kufundisha na kuwatia Wakristo moyo.
Padri Salus Lelo (kama tulivyozoea kumwita) ameishi Iringa ambako ndiko yaliko Makao Makuu ya wamisionari wa Consolata kwa kipindi cha takriban mwaka mmoja, hadi anafariki dunia lakini wananchi wa Iringa walionekana wenye majonzi mazito kuliko ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa naye siku zote sehemu nyingine. Hii inaonesha upendo wa dhati ambao aliwaonesha kwa muda mfupi.
Tunajiuliza ni nani kati yetu anayeweza kurithi tunu na  vipaji alivyokuwa navyo Padri Salus Massawe? Je, mioyo yetu inatamani kupata neema kama ya kwake? Tulipofika Iringa eneo la Kanisa Kuu la Jimbo (cathedral)  parokia ya Bikira Maria Consolata alfajiri  31, Oktoba 2012,  ilikuwa ni simanzi, vilio vilivyorindima na kuwafanya umati wa ndugu tuliosindikiza msiba kutoka Dar es Salaam na Moshi kuanza kulia tena.
Waumini walikuwa wamekesha kanisani hapo kwa siku mbili, walipouona mwili wa kipenzi chao waliangua kilio kikubwa. Vilio hivi, vilifuatiwa na mazishi yaliyofanyika katika Parokia ya Tosamaganga,  umati mkubwa ulishiriki, wananchi wa Iringa walitamka wenyewe kuwa tumempoteza kiongozi wa kabila letu, ‘Mtwa’ kwa Kihehe wakimaanisha chifu.
waamini , waliamua kumuwekea historia ya pekee kwa kumzika  kwa heshima za kichifu wa kabila la Wahehe kwa kupigiwa  mizinga  20 angani. Tulijiuliza hivi na mapadri wanapigiwa mizinga kama wanajeshi? Lakini hayo hata yeye hakujua kama yatatokea akifariki. Kifo cha Padri Massawe  kinaweza kujengwa taswira nyingi miongoni mwa jamii.  Ni kwanini yeye? Na ni kwanini pale Bagamoyo? Lakini  yote tumuachie Mwenyezi Mungu.
Waliosoma naye SAUT  wanasikitika hasa wanapokumbuka, uhamasishaji usio na kikomo wa Padri Massawe kwenye michezo, shughuli za kijamii, burudani, vikao, kuanzishwa kwa asasi ya kutetea uhai wa binadamu (Pro-Life) ambayo alikuwa mwasisi na mwenyekiti wa kwanza. Mashindano ya mpira wa miguu maarufu SAUT kama FAWASCO, alihakikisha darasa lake la ‘Mass Comm (2005-08)’ linachukua kombe na likafanya hivyo.
Jumapili jioni alikutana na kikundi cha  wazaliwa wa Kibosho ‘Konkya’ waliokuwa wakiishi Mwanza na mikutano ilikuwa ikifanyika pale Kilimanjaro Hotel Mabatini, tukiwa naye. Wakati wa Misa Baba Askofu  wa Jimbo la Iringa, Taracius Ngalalekumtwa,  alieleza jinsi ambavyo Padri Massawe amefanikiwa kujenga mahusiano mazuri na jamii nje na ndani kila mara akionesha uso wa matumaini na mapendo.
Pamoja na upadri wake,  kupangiwa kazi za ofisini,  hata wakati wa masomo alikuwa padri anayejitahidi kukutana na makundi ya watu wote, wenye mali, wasio na mali, wenye elimu na wasio na elimu, alikuwa padri anayetambua utu wa kila mtu, kuhakikisha kila mwanadamu anayekutana naye anakuwa na amani na furaha moyoni.  Mara kadhaa nilimpelekea watu walio kata tamaa na  wenye changamoto mbalimbali za kimaisha, lakini walirudi na hali mpya, wamebadilika.
Huyo hakuwa padri anayegawa fedha, mali ila alikuwa akigawa upendo wa dhati, furaha, amani na matumaini. Ndiyo maana askofu anasema: ‘ Padri Massawe alikuwa zaidi ya padre kwani alitumikia nafasi yake kama mkuu wa shirika, mwalimu, padri, daktari na kiongozi wa kijamii  huku akijitahidi kujenga mahusiano na kila anayepishana naye.
‘Usihesabu umri wako kwa miaka uliyonayo, hesabu umri wako kwa kuangalia watu ambao umehusiana nao vizuri. Padri Massawe alijitahidi kuhusiana  vizuri na kila aliyepishana naye bila kujali dini, imani au kabila lake,’ anasema  Baba Askofu.
Katika mkutano uliofanyika Bunju, ambao marehemu alikuwa mwenyeji,  ulihudhuriwa pia na padri Mtanzania ambaye ni Makamu Mkuu wa Shirika la wamisionari Wakonsolata duniani,  kutoka Roma,  Padri Detrick Mpandawazima,  ambaye walikuwa wote baharini na alishuhudia akifariki, alimtaja marehemu Padri Massawe kama kiongozi mwenye kipaji kikubwa ambaye bado alihitajika kulitumikia shirika hilo na taifa la Tanzania.
Tutamkumbuka kwa kujitahidi kuomba neema ya Mungu ili tuishi maisha mazuri ya kumtumikia Mungu. Kuishi maisha ya kujitoa kwa ajili ya wengine na kusambaza upendo wa Mungu. 
sasa ni mwaka mmoja toka ututoke tunazidi kukumbuka kwa mengi ulifanya kwetu, Tunamuombea Mwenyezi Mungu aipokee Roho yake na ampumzishe kwa amani. Amina!

Wednesday, October 31, 2012

MAZISHI YA PD:MASSAWE HUKO TOSAMAGANGA IRINGA

Mkuu wa Shirika la Consolata Tanzania  amezikwa jana huko Tosamaganga Iringa

Picha inayoonekana ni marehemu Padre Salutaris Lello Masawe aliyekuwa Mkuu wa Shirila la Wamisionari wa Consolata Tanzania ambaye amezikwa leo katika makaburi ya Jimbo la Iringa yaliyopo Tosamaganga.




Add caption

Wakristo Wakatoliki wameshauriwa kujiuliza kuwa wanahusiana na wengine vipi kama ishara ya kujiandaa kuufikia uzima wa milele mbinguni.
Hayo yamezungumzwa leo na Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa alipokuwa akihubiri wakati wa Misa ya Mazishi ya Padre Salutaris Lello Massawe ilifofanyika katika Kanisa la Moyo Mt. wa Yesu Parokia ya Tosamaganga jimboni humu.
Amesema binadamu hataulizwa endapo alitenda matendo ya upendo bali ataulizwa kama alikuwa na roho ya ubinadamu na haki katika kuwajali wengine.
“Swali la kujiuliza kila wakati katika maisha ni kwamba, umehusiana na watu wangapi wakakubariki? Na tena hatutaulizwa endapo tulitenda upendo bali tutaulizwa kama tulikuwa na roho ya ubinadamu na haki katika kuwajali wengine” amesema
Amesema Mungu ana mzaha katika kuvichukua viumbe wake kwani huchukua muda anaoutaka ambao binadamu haujui lakini jambo la msingi ni kujiandaa kiroho ili kuwa tayari wakati wowote.
“Munu ana mzaha pia. Mzaha wenyewe ni kiama huu ambao kila mtu anajiuliza kwa nini Massawe ameondoka wakati ambao hakutarajiwa? Kila mtu anajiuliza, kwa nini mapema? Kwa nini ghafla? Huo ndiyo mzaha wenyewe ila yeye anajua kila mtu atamchukuaje na kwa wakati gani” amesema.
Akimzungumzia Massawe Mhashamu askofu Ngalalekumtwa amesema alikuwa ni mtu mwenye bidii, uaminifu katika kuwajibika na alikuwa na maneno ya kutia moyo.
“Kazi za kitume alizitenda kwa bidii na kwa uaminifu. Pia alikuwa na maneno ya kutia moyo. Aliadhimisha matendo ya wokovu kwa nidhamu. Tunaimani kabisa kuwa huko alikokwenda ni kuzuri” amesema.
Amewataka Wakristo kuwa ni watu wa kutenda haki na kujituma katika kuwasaidia wanaohitaji msaada kwa kutenda matendo ya upendo wakijua kuwa maisha ya mwanadamu ni safari ya kumtafuta Mungu.
“Tendeni matendo ya haki, matendo ya upendo kwa kuwasaidia wahitaji kwa kujua kuwa safari ya mwanadamu ni kumtafuta Mungu; binadamu kajaliwa moyo mkubwa wa kuweza kumwelekea Mungu” amesema.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na madhehebu ya kidini kutoka ndani na nje ya nchi ambapo jumla maaskofu wanne walihudhuria mazishi hayo.
Maaskofu hao ni pamoja na Mhashamu Desderius Rwoma wa Jimbo Katoliki la Singida, Mhashamu Alfred Maluma wa Njombe, Mhashamu Evaristo Chengula wa Mbeya pamoja na Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Iringa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania..

Tuesday, October 30, 2012

BURIANI PADRE LELO MASSAWE

Mwili wa Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Consolata, nchini Tanzania, Padre Salutaris Lucas Massawe unazikwa leo katika Parokia ya Mshindo mkoani Iringa.
Padre Massawe, alikufa kwa kuzama baharini Oktoba 25 katika ufukwe wa Bagamoyo mkoani Pwani.
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEg2XGJBri0B-ul7xK-dRrqUC7wXsI_b3ERAxdWi-BA1sS3cTlV8DwAIGm-I675DPPeUm3zJQtCElyiOZoh9G3oOmAjN1fnwP_5G5YAVj8zU2pSRz4ZAXdkO-AHH19jUAcP26H20fKTeBFk/s1600/P.+Lelo.jpg
Padre massawe na mapadre wenzake washirika la consolata kutoka mataifa mbali mbali barani afrika walikwenda Bagamoyo kupumzika baada ya mkutano wa wakuu wa Shirika la Waconsolata Barani Afrika, uliokuwa unafanyika consolata mission centre bunju,  Jiji la Dar es Salaam.
   
Septemba 7, 2011 alichaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Waconsolata nchini Tanzania hadi alipokufa Oktoba 25, 2012.
Kabla ya kuwa mkuu wa shirika hilo, Padre Massawe alifanya kazi za umissionari katika nchi za Ethiopia na Italy.
HISTORIA YA MAREHEMU 
Marehemu Padre Salutaris Massawe alizaliwa tarehe 8 Julai 1962, katika kijiji cha kibosho wilaya ya moshi vijijini. 
Alisoma shule ya Msingi Singachini kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1978 
mwaka 1979-1985 alikuwa akisoma katika  Sekondari Maua Seminari iliyoko mkoani kilimanjaro. 
 
Aliendelea na masomo ya Falsafa na Taalimungu kwenye Chuo cha Waconsolata kilichoko mjini Nairobi kuanzia mwaka 1985 hadi mwaka 1988.

Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre, kunako tarehe 27 Juni 1993 alipewa daraja takatifu la Upadre katika kanisa la Kristo Mfalme na Askofu Amedeus Msarikie wa Jimbo la Moshi wakati huo. 

Mungu alimpa maisha ya duniani na sasa amemwita, ili ampe maisha ya mbiguni yasiyo na mwisho....
Raha ya milele umpe, ee bwana...
na mwanga wa milele umwangazie
apumzike kwa amani
amina,


 


NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR