Friday, February 27, 2015

Masomo ya Jumapili ya Pili ya Kwaresima Mwaka B (Tarehe 01/03/2015)

01

 Marchi
 Jumapili ya 2 ya Kwaresima Masomo ya Mwaka "B".
SOMO  1: Mwa. 22:21- 2, 9a, 10-13, 15-18

Somo katika kitabu cha Mwanzo.
Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Uchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya Kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, Kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketeza badala ya mwanae. Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni, akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga uliopo pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote duniani watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.

WIMBO WA KATIKATI. Zab. 116:10, 15-19. 
K. Nitaenenda mbele za Bwana
         Katika nchi za walio hai..

Tafakari ya Masomo ya Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima mwaka B wa kanisa( tarehe 1/3/2013)

Ninjesusakuleteeni tafakari ya Neno la Mungu, tukitafakari masomo Dominika ya II ya Kwaresima. Mama Kanisa ametuwekea Neno la Mungu linalotutaka kuimarisha imani yetu kwa Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Mpendwa mwana wa Mungu katika tafakari yetu Dominika ya kwanza ya kwaresima tuliona majaribu dhidi ya Bwana wetu Yesu Kristu na sasa Dominika hii tumewekewa majaribu dhidi ya Ibrahimu. Ibrahimu ni Baba mnyenyekevu ambaye kwanza aliambiwa na Mungu aende nchi asiyoijua na alitii wito huo wa Mungu bila kuangalia usalama wake bali tegemeo katika Mungu anayemwita. Baadaye katika uzee wake akiwa amempata mtoto, mwanae wa pekee Isaka, ghafla anaombwa na Mungu akamtoe sadaka ya kuteketezwa na anaitika bila kusita.
Ibrahimu anakubali ombi la Mungu na anaanza safari kuelekea mlima wa kafara! Mara anapofikia wakati wa shughuli yenyewe malaika wa Bwana anamwambia usitende jambo hilo, tayari ninajua unamcha mwenyezi Mungu. Mara kondoo anaonekana kwa ajili ya kafara badala ya mtoto Isaka! Kwa tendo la imani hii kuu, Mungu anamwahidia Ibrahimu uzao kama nyota za angani, mchanga wa pwani na baraka tele zisizo na mwisho. Kwa sababu ya imani kuu ya Ibrahimu Kanisa humwita Baba wa Imani.
Mpendwa mwanatafakari, kwangu mimi yatosha tu kufurahia matunda ya imani ya Ibrahimu! Kumbe imani inazaa na kujenga upya utajiri usioisha, kizazi kisichoisha na baraka zisizo na mwisho. Basi tufanye nini? Ni kusadiki na kujiimarisha katika kutekeleza mpango wa Mungu daima tulioupokea kwa njia ya ubatizo na hasa wakati huu wa kwaresima. Wote twafahamu kuwa katika kipindi hipi wapo wakatekumeni wanaojiandaa kwa ubatizo, hawa wanaitwa na Mungu kuacha yote ya kipagani, chuki, rushwa, ulevi na mambo kama hayo na wanatakiwa kujikabidhi mikononi mwa yule anayewaita pasipo kuwa mashaka. Wanaalikwa kuiga mfano wa Ibrahimu Baba wa imani anayejitoa bila kuangalia usalama wake, aliye tayari kutoa sadaka ya mwanae bila woga bali akiwa na tumaini yakwamba Mungu atatenda yote.
Katika somo la pili Mtume Paulo anawaandikia Warumi sura ya 8 akiwaimarisha katika imani yao. Anajua wakati fulani wanapata mateso kwa sababu ya imani hiyo, lakini anawaambia cha msingi ni kujenga imani kama ya Ibrahimu ili Mungu akae pamoja nao. Na hivi Mungu akiwa upande wao hakuna nguvu nyingine ya kuweza kuwashinda. Kristu mzaliwa wa kwanza amekuja kwa ajili ya wokovu, amekufa na kufufuka taji ya ushindi dhidi ya dhambi. Kristu ametuletea upendo usiokwisha hata kama tunamkosea, yeye hubaki akitupenda bila kurudi nyuma.
Mpendwa msikilizaji, somo la Injili toka Mwinjili Marko sura 9 linaweka mbele yetu Yesu akiwa mlimani katika faragha pamoja na Yakobo, Petro na Yohane. Jambo la Bwana kuwa mlimani ni alama ya uwepo na utukufu wa Mungu. Daima Mungu anaongea na watu wake akiwa mlimani. Katika mantiki ya kuwa mlimani katika Innjili tunakumbuka mara moja, jinsi Mungu alivyomkabidhi Musa amri akiwa mlimani Sinai (Kut. 24:15). Ni pale mlimani Mungu anajionesha kwa Eliya (1Wafalme 19:8). Jambo la pili ni lile la kugeuka sura na mavazi meupe kumetameta. Weupe ni alama ya Mungu, alama ya furaha na dhihirisho la Kristu aliye Mtakatifu na Mungu.
Alama ya tatu ni ile ya Musa na Eliya wanapozungumza na Yesu. Hawa ni viwakilishi vya Agano la kale yaani sheria na Manabii na hivi kazi yao ni kumweka mbele yetu Bwana na kisha watatoweka. Kutoweka kwao kuna maana yakuwa sasa Agano la Kale limekwisha na linaanza agano Jipya. Mpendwa msikilizaji, kazi yetu waamini ni kutangaza ukuu wa Mungu na baada ya hapo kupisha njia ili Mungu daima akue wakati huo tukipungua.
Mtakatifu Petro anamwomba Bwana wakajenge vibanda vitatu kimoja cha Bwana, vingine vya Musa na Eliya. Hii ni alama ya sikukuu, kama tujuavyo sikukuu ya vibanda kwa Waisraeli ilikuwa ya maana sana na hasa ilipowakumbusha vibanda vyao huko jangwani. Mtume Petro hajaelewa nini hasa mpango wa Bwana, yeye anaona ni sherehe tu, haoni mateso yaliyo mbele ya Bwana.
Wakiwa bado mlimani linatoka wingu na kuwafunika na sauti inatoka juu ikisema “Huyu ni mwanangu mpendwa msikieni yeye! Wingu katika agano la kale liliwaongoza wana wa Israeli kupita jangwani, baharini kumbe uwepo wa wingu ni uwepo wa Mungu na hivi sauti inapotoka juu katika wingu si kitu kingine bali Kristu anadhihirishwa kuwa mmoja na Baba, yeye ni wa juu na wala si wa dunia hii.
Mara hawa Mitume walipotazama hawakuona mtu bali Yesu peke yake ndiyo kusema wale akina Musa na Eliya hawapo, kama nilivyokwishasema kazi yao imekwisha na anabaki Bwana mkuu wa Agano Jipya na la milele. Baada ya matukio hayo yote Bwana pamoja na Mitume wanaanza kushuka chini mlimani na wananaposhuka anawakataza wasimweleze mtu mpaka Mwana wa mtu atakapofufuka toka wafu.
Hii ni siri ya kimasiha, hataki wasimulie mambo yake mpaka wawe wameelewa vizuri mpango wake wa wokovu kwa njia ya msalaba. Daima Mwinjili Marko atajitahidi kumficha Masiha mpaka atakapowekwa wazi katika sura ya 15 ya Injili yake. Tunatafakari maneno ya akida mpagani anayesema baada ya Yesu kukata roho “hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu” Mk. 15:39. Wito kwako wewe unayenisikiliza ni kujifunza vizuri na kumtambua Bwana ni nani, ili utume wako ulale katika uhakika wa Bwana anayekualika daima kumtumikia kwa uchaji. Kumbuka bila toba ya ndani si rahisi kupokea mafundisho ya imani, Neno la Mungu na yote mema yatokayo kwa Mungu.
Mpendwa ninakuageni kwa furaha nikitumaini utaendelea kuongozwa na Neno la Mungu daima. Utaendelea kuongozwa na Mwana wa Mungu kwa maana ndivyo ulivyoamriwa katika injili “ Huyu ndiye Mwanangu mpendwa msikieni yeye”. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR