Showing posts with label WENYEVITI WAKAMATI ZA BUNGE 2016. Show all posts
Showing posts with label WENYEVITI WAKAMATI ZA BUNGE 2016. Show all posts

Wednesday, March 23, 2016

SPIKA WA BUNGE AFANYA MAAMUZI MAPYA YA KUWANGOA


Dar es Salaam. Spika John Ndugai amefanya mabadiliko ya wajumbe 27 wa
Kamati za Kudumu za Bunge yaliyowangoa wenyeviti watano, huku mmoja
akipoteza nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bunge.

Hatua hiyo imekuja wakati kukiwa na tuhuma za rushwa dhidi ya wabunge wa
baadhi ya kamati na kusababisha baadhi kujiuzulu ujumbe wakishinikiza
uchunguzi ufanyike ili waliohusika wawekwe hadharani na kuchukuliwa hatua.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliacho cha
Bunge inasema Spika Ndugai amefanya mabadiliko hayo kwa kuzingatia
mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya kuunda kamati hizo
siku 59 zilizopita.

Waliongolewa uenyekiti ni Richard Ndassa, ambaye alikuwa Kamati ya
Uwekezaji na Mitaji (PIC), Dk Mary Mwanjelwa (Kamati ya Ardhi, Maliasili
na Mazingira), Martha Mlata (Kamati ya Nishati na Madini).

Waliovuliwa umakamu mwenyekiti ni Dk Raphael Chegeni (Kamati ya Huduma
za Maendeleo ya Jamii) na Kangi Lugola (Kamati za Hesabu za Serikali).

Mabadiliko haya yamefanywa chini ya Kanuni ya 116(3) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge ambayo inatoa mamlaka ya kuteua wabunge kuunda kamati
mbalimbali za Bunge,” inasema taarifa hiyo.

Kwa kuhamishwa kutoka kamati wanazoziongoza, wabunge hao wamepoteza
nafasi zao za uenyekiti, wakati Mwanjelwa, ambaye alipata nafasi ya
Mwenyekiti wa Bunge kutokana na kuwa mmoja wa wenyeviti wa kamati hizo,
amepoteza wadhifa huo wa kuwa mmoja wa wenyeviti watatu ambao humsaidia
Spika kuongoza shughuli za Bunge.

Sifahamu chochote, alisema Dk Mwanjelwa, mmoja wa wenyeviti watatu wa
Bunge, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu mabadiliko hayo.

Ninachoweza kusema uamuzi wa Spika ndiyo wa mwisho, ila sina
ninachofahamu kuhusiana na mabadiliko haya. Yaani ndiyo nimesoma kwenye
mtandao muda si mrefu kabla hamjanitafuta.

Taasisi za Serikali zinazotuhumiwa kutoa fedha kwa wajumbe wa Kamati za
Bunge, ambazo zina jukumu la kuzisimamia, ni Shirika la Nyumba (NHC),
Bima ya Afya (NHIF), Shirika la Umeme (Tanesco) na Mamlaka ya Udhibiti
wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo alisema suala la
taasisi yake kutoa rushwa kwa wabunge limewashangaza, na wanasubiri
vyombo vya uchunguzi kutoa matokeo kuhusu tuhuma hizo.

Matokeo ya uchunguzi kuhusu tuhuma hii ndiyo ambayo yanaweza kuanika
bayana kama kweli tunahusika au lah. Ni jambo ambalo hata sisi
limetushangaza, alisema.

Kutokana na mabadiliko hayo, kamati ambazo viongozi wake wameondolewa
zitalazimika kufanya uchaguzi wa viongozi.

Kamati zinazotakiwa kupata wenyeviti wapya ni ya Nishati na Madini,
Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii
ambayo itatakiwa kufanya uchaguzi wa mwenyekiti na makamu wake, wakati
zitakazochagua makamu ni ya Hesabu za Serikali ya Mitaa (LAAC) na ya
Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Waliohamishwa wazungumza

Akizungumzia suala hilo, Dk Chegeni alisema wajumbe wawili wa kamati
yake, Zitto Kabwe (Kigoma Mjini) na Hussein Bashe (Nzega Mjini),
wamemuandikia Spika barua za kujiondoa kwenye nafasi zao ili kupisha
uchunguzi wa rushwa.

Wajumbe wa kamati wamesikitishwa na taarifa hizi na kwa pamoja tumeamua
kuchukua hatua. Tumemuandikia Spika barua ya kupisha uchunguzi ili
kujiridhisha na madai yaliyobainishwa. Wajumbe wote waliohudhuria kikao
cha leo wamesaini,” alisema Dk Chegeni.

Zitto aliiambia Mwananchi kuwa amemuandikia Spika barua ya kujiondoa,
akitaka uchunguzi ufanyike na atakayehusika achukuliwe hatua kali.

Bashe alithibitisha kujiondoa akitaka uchunguzi ufanyike na watuhumiwa
wote watajwe kwa majina ili hatua zichukuliwe.

Utumishi wangu kwa kamati uko palepale nisingependa kuhamishwa lakini
watuhumiwa wajulikane,” alisema Bashe.

Akizungumzia taarifa zilizochapishwa na gazeti moja jana, Dk Chegeni
alisema: Si kweli. Hata huyo katibu anayeelezwa kutumwa hakuwa nasi
mpaka mwisho wa ziara pale Bima ya Afya. Alitoa udhuru kuwa mwanaye
anaugua na akaruhusiwa kuondoka mapema tu. Leo (Jana) kamati imewauliza
wajumbe na makatibu wote na wamekana kuhusika.

Baada ya kujiridhisha na kutohusika kwa wajumbe wake, Dk Chegeni alisema
kamati imepitisha maazimio matatu, ambayo ni kutaka uchunguzi ufanyike
ili ofisi ya Spika ijiridhishe, watakaobainika wachukuliwe hatua za
kikanuni na kisheria, na gazeti lililoandika habari hiyo lithibitishe
tuhuma hizo na likishindwa liiombe msamaha kamati.

Jana (juzi) nilitumwa na mwenyekiti wangu nihudhurie kikao Spika
kilichokuwa kifanyike saa 5:00 asubuhi, lakini kiliahirishwa. Leo (jana)
hajahudhuria kikao chetu na kanijulisha kuwa anahudhuria kikao hicho
kikichoahirishwa jana (juzi). Sina taarifa za mahojiano na Takukuru,
alisema Lolencia Bukwimba akimzungumzia Ndassa.

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi alisema hajajiuzului ujumbe wa
kamati kama habari zilivyoenea, lakini yeye pamoja na wajumbe wenzake wa
Kamati ya Huduma za Jamii wamemtaka Spika awaeleze kilichotokea kwa kuwa
ndiye kiongozi wao.

Kwa mfano mimi nijiuzulu nini wakati si mtuhumiwa? alihoji.

Nikijiuzulu, maana yake naacha kazi za kibunge.

Alisema anashangaa habari kama hizo zinatokea wapi wakati hajasikia kama
kuna mbunge yeyote aliyehojiwa dhidi ya tuhuma hizo.

Kuhusu tuhuma za rushwa, Mbilinyi alisema si rahisi kwa kitu hicho
kutokea kwa kuwa wabunge hawawezi kuwatuma makatibu wa kamati kufuata
fedha za rushwa.
Kwa sababu huwa tunawaona kama wapelelezi, hivyo si rahisi mtu
akamuamini kiasi cha kumtuma akamchukulie mzigo, alisema.

Pia alisema kwa wakati huu ambao Bunge ni changa, haiwezi kuwa rahisi
wakakubaliana kuchukua rushwa kwa kuwa bado wabunge hawajafahamiana vizuri.

Mbunge wa Jimbo la Bukene, Selemani Zedi alisema hajapata taarifa rasmi
za kuhamishwa kutoka kamati ya PIC kwenda ya Katiba.

Nitawajibika kwenye kamati nitakayopangwa kwa sababu spika anayo
mamlaka ya kunipanga popote,alisema.

Kuhusu vitendo vya rushwa, alivitaka vyombo husika kufanya uchunguzi ili
atakayebainika kuhusika achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Mwaka 2012, wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini walituhumiwa kupokea
hongo kutoka kwenye makampuni ya mafuta ili waunge mkono azimio la
kushinikiza aliyekuwa katibu mkuu wa wizara husika, Eliackim Maswi
angolewe.

Wakati huo, Spika Anne Makinda aliahidi kuwapeleka watuhumiwa kwenye
Kamati ya Maadili na Haki za Bunge ili wachunguzwe na kuahidi kuwa
matokeo ya ripoti hiyo angeiwasilisha bungeni.

Siku hiyo, Spika Makinda pia alitangaza kuivunja kamati ya nishati.

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR