Friday, March 15, 2013
Wasifu wa Baba Mtakatifu Francis!
Baba Mtakatifu Francis ni Myesuiti wa kwanza kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni Papa wa kwanza katika historia ya Kanisa kutoka nje ya Bara la Ulaya na Papa wa kwanza katika historia ya Kanisa kutoka katika nchi za Amerika ya Kusini, nchi ambazo kwa sasa zina idadi kubwa ya waamini wa Kanisa Katoliki. Kwa mara ya kwanza Jina la Mtakatifu Francis linatumiwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Lakini ikumbukwe kwamba, kuna watakatifu wanne wenye majina ya Francis. Hawa ni akina Mtakatifu Francis wa Assisi, Msimamizi wa Italia; Mtakatifu Francis wa Sale, Mwalimu wa Kanisa na Msimamizi wa Waandishi wa Habari; Mtakatifu Francis Xsaveri, Myesuit na Msimamizi wa Wamissionari pamoja na Mtakatifu Francis wa Paulo, Mkaa pweke na mwanzilishi wa Shirika la Ndugu wadogo wa Calabria.
Kardinali Jorge Mario Bergoglio, SJ, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires, Argentina, alizaliwa tarehe 17 Desemba 1936 mjini Buenos Aires. Yeye ni mtoto wa Mzee Mario na Mama Regina Sivori, waliobahatika kupata watoto watano. Katika ujana wake, alisoma na kufuzu kama mtaalam wa kemia, baadaye akaacha kazi hii na kujiunga Seminarini huko Villa Devoto.
Tarehe 11 Machi 1958 alijiunga na malezi ya Kinovisi katika Shirika la Wayesuit akaendelea pia na masomo dunia nchini Cile na kunako mwaka 1963 alirejea tena Buenos Aires na kujipatia shahada ya uzamili kutoka katika Kitivo cha Falsafa, Chuo Kikuu cha San Josè huko San Miguel.
Kati ya mwaka 1964 na mwaka 1965 alikuwa ni Jaalim wa Fasihi Andishi na Saikolojia katika Chuo cha Bikira Maria wa Santa Fe. Kunako mwaka 1966 akafundisha masomo haya kwenye Chuo Kikuu cha Salvatore cha Buenos Aires. Kuanzia mwaka 1967 hadi mwaka 1970, alijiendeleza kwa masomo ya Taalimungu katika Chuo Kikuu cha San Josè kilichoko San Miguel na kujipatia shahada ya uzamili.
Tarehe 13 Desemba 1969 akapewa daraja takatifu la Upadre. Kati ya mwaka 1970 hadi mwaka 1971 alikamilisha hatua ya tatu ya majiundo yake kama Myesuit huko Hispania na tarehe 22 Aprili 1973 akaweka nadhiri za daima. Kati ya mwaka 1972 hadi mwaka 1973 alikuwa ni mlezi wa Wanovisi, Jaalim, Mshauri na Gombera wa Chuo cha Massimo. Tarehe 31 Julai 1973 akateuliwa kuwa Mkuu wa Jimbo la Argentina kwa upande wa Shirika, utume ambao aliutekeleza kwa muda wa miaka 6. Kati ya Mwaka 1980 hadi mwaka 1986, alikuwa ni Gombera wa Chuo cha Massimo na Paroko wa Parokia ya Patriaki San Josè, Jimboni San Miguel.
Kunako mwaka 1986 alikwenda nchini Ujerumani kumalizia masomo yake katika Shahada ya Uzamivu na wakuu wake wa Shirika wakampatia jukumu la kuwa mkuu wa malezi ya kiroho na muungamishi katika Chuo cha Salvatore.
Tarehe 20 Mei 1992 Papa Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Buenos Aires, akawekwa wakfu kama Askofu tarehe 27 Juni 1992. Tarehe 3 Juni 1997 akateuliwa kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo kuu la Buenos Aires na tarehe 28 Februari 1998 akasimikwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires baada ya kifo cha Kardinali Antonio Quarracino na hivyo kuwa pia ni Mkuu wa Kanisa Katoliki Argentina.
Mwenyeheri Yohane Paulo II akamteuwa na kumsimika kuwa Kardinali kunako tarehe 21 februari 2001. Ameshiriki katika Sinodi ya Maaskofu iliyofanyika kunako mwaka 2001. Akashiriki pia kwenye mkutano wa Makardinali wakati wa uchaguzi wa Papa kati ya tarehe 18 na 19 Aprili 2005. Alikuwa ni mjumbe wa Halmashauri ya Sinodi ya kumi na moja ya Maaskofu kuanzia tarehe 2 hadi 23 Oktoba 2005.
Mjini Vatican alikuwa ni mjumbe wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri, Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri na Mjumbe wa Sekretarieti ya Sinodi.
Nchini Argentina alikuwa ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Argentina.
Rais wa Tume ya Baraza la Maaskofu kwa ajili ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Argentina. Alikuwa ni mratibu mkuu wa Mahakama ya Kanisa; Mratibu wa Mahakama ya Jimbo kuu la Buonos Aires. Tangu mwaka 2005 hadi 2011 alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina.
Ni mwandishi wa Vitabu vifuatavyo:
- 1982: Meditaciones para religiosos
1986: Reflexiones sobre la vida apostólica
1992: Reflexiones de esperanza
1998: Diálogos entre Juan Pablo II y Fidel Castro
2003: Educar: exigencia y pasión
2004: Ponerse la patria al hombro
2005: La nación por construir
2006: Corrupción y pecado
2006: Sobre la acusación de sí mismo
2007: El verdadero poder es el servicio
Subscribe to:
Posts (Atom)
-
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya...
-
Isidore Bakanja, ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya imani ya Kikristo, Akiongozwa na maisha rahisi kama layman Katoliki wakati wa mauaj...
-
Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza anatualika kutambua kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya ...