Showing posts with label uchaguzi zanzibar 2015. Show all posts
Showing posts with label uchaguzi zanzibar 2015. Show all posts

Saturday, October 31, 2015

HATUTARUDIA UCHAGUZI WA ZANZIBAR WASEMA CUF


Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama Cha Wananchi (CUF) Twaha Taslima akizungumza wakati wa Mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana kuhusiana na kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar. Kulia ni Makamu Mwenyeki wa Kamati hiyo, Severine Mwijage. Picha na Omar Fungo

Wakati CUF ikisema hayo, Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kimetaka kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza jinsi mwenyekiti wa ZEC alivyofikia uamuzi wa kufuta matokeo na akithibitika kuwa alishinikizwa, afukuzwe kazi.

Hatuwezi kurudia uchaguzi,” alisema Taslima. “Tunachofahamu ni kuwa uchaguzi umefutwa kinyume na sheria, hivyo ZEC ibatilishe uamuzi wake na kuendelea kutangaza matokeo ya majimbo yaliyobaki ili mshindi ajulikane.” Alisisitiza msimamo wa chama hicho kuwa Jecha alifuta matokeo hayo bila kuwashirikisha makamishna wake kama sheria ya tume hiyo inavyotaka. “Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ibara ya 119 kifungu kidogo cha 10, inataka vikao vya ZEC kuhudhuriwa na mwenyekiti au makamu mwenyekiti na wajumbe wanne na uamuzi kuungwa mkono na walio wengi,” alisema. Alisema makamishna wa tume hiyo katika taarifa yao kwa vyombo vya habari wamepinga kuhusika katika uamuzi huo wa kufuta matokeo ya uchaguzi. Taslima alisema uamuzi huo umetolewa na Jecha mwenyewe kwa kushinikizwa na mamlaka za juu za Serikali. Aliziomba jumuiya za kimataifa kuzishinikiza serikali za Jamhuri ya Muungano na Zanzibar ili zimalize mgogoro huo na kuiepusha Zanzibar kuingia katika machafuko. Wakati CUF ikisema hayo, Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kimetaka kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza jinsi mwenyekiti wa ZEC alivyofikia uamuzi wa kufuta matokeo na akithibitika kuwa alishinikizwa, afukuzwe kazi.
Katibu wa ZLS, Omar Said Shaaban, ambaye alikuwa ameambaatana na rais wake, Wakili Awadh Ali Said, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tamko la Jecha la kufuta matokeo ya uchaguzi halina nguvu na linaweza kuhatarisha amani. “Rais aone haja ya kuunda Tume ya kumchunguza mwenyekiti dhidi ya madai ya kushindwa kufanya kazi zake na ikiwa madai hayo yakithibitika, basi
amuondoe mara moja,” alisema Shaaban kwenye mkutano huo uliofanyika
ukumbi wa Ulemavu, Kikwajuni. Wanasheria hao wametaka uchaguzi huo uendelee kuanzia pale ulipoishia, yaani hatua ya kufanya majumuisho ya kura za urais ili mshindi halali wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, 2015 apatikane na kutangazwa kuwa Rais. Chama hicho kimevitaka vyombo vya dola kuchunguza na kuwakamata na hatimaye kuwafikisha mahakamani watu wote waliohusika kumshinikiza mwenyekiti kutoa tamko la kufuta uchaguzi na matokeo yake.
Mbali ya hayo, chama hicho kimetoa wito kwa viongozi wote wa vyama vya siasa kutathmini wajibu wao katika kuheshimu maamuzi ya wananchi yanayofanywa kwa njia ya demokrasia ili kujenga misingi mizuri ya utawala bora.
 “Tunaamini kwamba Rais wetu wa Zanzibar atang’amua mtego huu unaokusudia kumuweka katika historia ya rais wa Zanzibar aliyewahi kuvunja katiba ya nchi na kumuondolea rekodi nzuri aliyonayo ya kuheshimu sheria na utawala bora,” alisema Shaaban. Kwa upande wake Rais wa chama hicho Awadh Ali Said alisema ZLS imepitia kwa makini katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi Nambari 11 ya 1984 ili kujiridhisha kama mwenyekiti ana uwezo wa kufuta matokeo ya Uchaguzi
na kama sababu zilizoelezwa zinakidhi kufanya uamuzi huo. Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 119 (1) ya katiba ya Zanzibar ya 1984, tume ni mwenyekiti pamoja na wajumbe sita kama walivyoanishwa na ibara hiyo na kwamba maamuzi yoyote ya Tume, lazima yaungwe mkono na wajumbe walio wengi.
Alisema licha ya utashi huo wa kisheria, wajumbe wawili walieleza hadharani kuwa hawajashirikishwa. “Taarifa iliyotolewa kwa waandishi na wajumbe wa Tume, Nassor Khamis na
Ayoub Bakari, kuwa hakukuwa na kikao chochote kilichofikia uamuzi wa kufuta Uchaguzi wa Zanzibar, haijapingwa mpaka sasa na wajumbe wengine wa Tume. Hii inaleta taswira ya wazi kuwa uamuzi huo haukuwa wa Tume, bali ni wa mtu mmoja ambaye ni mwenyekiti, hivyo kuyafanya kuwa ni batili mbele ya macho ya Sheria,” alisema Said. Pia walisema kanuni ya 41(1) imeweka wazi utaratibu kufutwa kwa siku ya uchaguzi na kutangazwa siku nyingine na namna uamuzi huo utakavyofikiwa na sio kufuta matokeo ya uchaguzi au uchaguzi wenyewe.
“Ni kwa bahati mbaya sana mwenyekiti katika tamko lake hakueleza kama utaratibu umefuatwa. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa Sheria,” aliongeza kiongozi huyo wa ZLS. Alisema tamko hilo linaweza kuiingiza nchi katika mgogoro mkubwa wa kikatiba kama vile kumalizika kwa muda wa mwishowa utawala wa serikali ya sasa kwa mujibu wa ibara ya 28 (2) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984.

Ibara hiyo inaeleza kuwa rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe alipokula kiapo. Katika hatua nyingine, mgombea urais wa ADC, Hamad Rashid amewaambia
waandishi wa habari jana kuwa kwenye ukumbi wa Hoteli ya Grand Malt, Malindi kuwa chama chake kimekosa imani na ZEC kutokana na uendeshaji wake kukosa sifa ya kufuata sheria na kanuni.
Alisema kuwa ili uwazi na uwajibikaji viweze kufikiwa, hakuna budi kwa watendaji wa tume huyo kujiuzulu na badala yake iundwe Tume yenye uwakilishi mpana na usio na mrengo wa kisiasa.
Alisema kuwa hatua hiyo kwa kiasi kikubwa inaweza kufanikisha kufanyika kwa uchaguzi wa amani na utulivu huku demokrasia ikichukua mkondo wake. Nayo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imemshauri mwenyekiti wa ZEC kutafakari upya uamuzi wake wa kufuta matokeo ya uchaguzi. Taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa THBUB,  Bahame Nyanduga inasema wamepitia sababu za  kufuta matokeo zilizotolewa na Jecha na kubaini kuwa zinaweza kutatuliwa iwapo makamishna wa ZEC wataweka tofauti zao pembeni. Nyanduga alisema katika taarifa hiyo kuwa kifungu cha 42(6) cha sheria ya uchaguzi Zanzibar kinaipa ZEC mamlaka ya kushughulikia
matatizo ya uchaguzi na kuyapatia ufumbuzi kwa utaratibu ulioanishwa katika kifungu hicho.
Taarifa hiyo ilisema kifungu hicho kinabainisha kwamba ZEC ina mamlaka ya kutangaza matokeo ndani ya siku tatu na endapo kuna matatizo inatakiwa kuyapatia ufumbuzi na kutangaza matokeo ndani ya muda huo. Wakati huohuo, Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-Moon amesema
ameguswa na tatizo la kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar na kutaka limalizwe kwa kufuata sheria zilizopo kwa amani. Katika taarifa iliyotolewa juzi kutoka New York, Marekani, Moon
amewataka wananchi wa Zanzibar kuwa watulivu na kujiepusha na vitendo vya vurugu na kuwashauri viongozi kutotoa matamko yanayoweza kusababisha vurugu.

Fatuma Karume apinga
Naye Fatma Karume, mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, amesema mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha hana mamlaka ya kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar. Jecha alitangaza kufuta matokeo yote  ya uchaguzi kwa upande wa visiwani Jumatano kwa madai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu na sheria
katika upigaji kura.

Uamuzi huo umepingwa vikali na watu mbalimbali, huku waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Madola, Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika(AU) na ubalozi wa Marekani ukitaka ZEC ieleze ni vituo gani vilikuwa na ukiukwaji wa taratibu. Akizungumza na Sauti ya Ujerumani (DW) kuhusu suala hilo, Fatma alidai kuwa Jecha alishinikizwa kuchukua uamuzi huo. “Watu waliwekwa chini ya ulinzi... na wakati huo Jecha hakuwepo,” alisema Fatma.  “Tusema ukweli, Jecha hana jeshi wala polisi. Jecha katumiwa tu kusemamaneno yale. Wazanzibari tumenyimwa haki yetu,” alisema binti huyo wa Rais wa Sita wa Zanzibar. Fatma alisisitiza kuwa uchaguzi haujafutwa kwa kuwa Jecha hana mamlaka ya kufuta uchaguzi na kwamba Serikali imehakikisha matokeo ya uchaguzi
hayatoki.  “Uchaguzi wa Zanzibar ni haki ya Wazanzibari na hakuna mtu anaweza kufuta hiyo haki. Uchaguzi bado upo na wote tumepiga kura, kura zetu zipo na hakuna mtu anaweza kufuta hiyo,” alisisitiza Fatma. Alisema kwa mujibu kwa Katiba ya Zanzibar Baraza la Wawakilishi lilivunjwa Agosti 13, na Katiba hiyo inataka baada ya siku tusini kuwe na Baraza jipya la Wawakilishi. Alisema kama ikifika Novemba 11 au 12 hakuna baraza jipya la wawakilishi, Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein atakuwa anavunja taratibu za kikatiba iwapo ataendelea kuwa Rais.


NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR