Maonesho ya shughuli za miito mitakatifu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa, kwa mwaka 2013, huko Rio de Janeiro, Brazil
Maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa huko Rio de Janeiro, Brazil kwa Mwaka 2013 yanaendelea kwa mwendo kasi wa kuhamasisha mashirika ya kitawa na kazi za kitume, yanayotaka kushiriki katika maonesho ya shughuli na utume wao miongoni mwa vijana, kujiandikisha kuanzia sasa, ili kuwawezesha kushiriki katika Maonesho ya Miito wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa kwa Mwaka 2013.
Lengo ni kuendelea kuhamasisha miito mbali mbali ndani ya Kanisa kwa kutambua kwamba, mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache.
Maonesho haya yanatarajiwa kuwekwa katika eneo la kitalii mjini Rio de Janeiro, kwa lengo la kutaka kuwahamasisha vijana kuchangamkia wito na maisha ya kipadre na kitawa; kwa kujitoa kimasomaso kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Maonesho haya yatakuwa na matangazo ya maneno kutoka kwa watakatifu mbali mbali ambao wamekuwa na mvuto wa pekee katika maisha na utume miongoni mwa Vijana.
Kamati ya Maandalizi inabainisha kwamba, kutakuwepo na shuhuda, mahubiri, michezo na matamasha ya muziki rasmi kwa ajili ya vijana. Lakini, nafasi kubwa zaidi itatolewa kwa vijana kupata nafasi ya kusali, kutafakari na kushiriki katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kutambua kwamba, Ekaristi ni chimbuko la miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Vijana watapata nafasi ya ukimya na kuabudu Ekaristi Takatifu kwani Mwenyezi Mungu anapenda kuzungumza na mtu kutoka katika undani wake.
Baada ya vurugu na makelele ya maisha, kijana anahitaji muda wa ukimya na tafakari ya kina, kuhusu hatima ya maisha yake bila kusahau uhusiano wake na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani wanaomzunguka. Ili kweli maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa yaweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani toba na wongofu wa ndani kama sehemu ya mchakato wa kukumbatia hija ya utakatifu wa maisha, vijana watapata fursa ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, katika mahema maalum yaliyotengwa kwa ajili ya Ibada hii.
Wakati wote huu, Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Rio de Janeiro, itaendelea kushiriki bega kwa bega na mahujaji hawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kama njia ya kuonesha upendo, ukarimu na mshikamano wao na vijana; wanaopaswa kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa katika maisha, matumaini, shida na mahangaiko yao ya kila siku. Mashirika ya Kitawa na Kitume, Jimboni humo, yanayo fursa na mwanya wa pekee wa kushirikisha karama na utume wake miongoni mwa vijana.
Ushiriki wa Mashirika haya kwanza kabisa, utategemea uwepo wake nchini Brazil, umuhimu wa Mashirika haya sehemu mbali mbali za dunia na Sheria za Kanisa zitakuwa ni mwongozo muhimu wa kuchagua Mashirika yote yatakayopania kujiunga na Maonesho ya shughuli za miito wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa, huko Rio de Janeiro, Brazil.