Showing posts with label
masomo ya dominika 21 mwaka A.
Show all posts
Showing posts with label
masomo ya dominika 21 mwaka A.
Show all posts
Mwamini
mwana wa Mungu unayetegea sikio Radio Vatican, Tumsifu Yesu Kristo.
Tunakuleteni tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 21 mwaka A
tukiongozwa na Nabii Isaya, Mtume Paulo na Mwinjili Matayo, ambao
wanatuambia kuwa imani thabiti katika Yesu Kristo Mwana wa Mungu ni
msingi wa wokovu wetu. 
Nabii
Isaya katika somo la kwanza anatoa mafundisho yake wakati wa utawala wa
Hezekia, yaani wakati wa utawala huu aliyekuwa mtunza mfuko anatumia
vibaya mali aliyokabidhiwa yaani hajali shida za watu. Anajitazama yeye
binafsi, anajiimarisha katika utajiri binafsi na anakuza jina lake.
Ni
kwa shida hii Nabii Isaya anafundisha kinyume na madhulumu yanayofanywa
na wenye madaraka. Anawaambia kuwa watanyanganywa funguo na
watakabidhiwa wengine wenye kushika sheria ya Bwana. Funguo ni alama ya
madaraka, ni alama ya utawala na hivi nabii anawaambia kuwa madaraka
yenu yatapokonywa na Mungu. Mpendwa msikilizaji, ndiyo kusema hivi leo
kuna wenye mamlaka wengi ambao wamejiimarisha katika mali, katika ubaya,
kiasi kwamba wanapopita mitaani petu wanajionesha katika sura hiyo!
Wanatoa harufu ya dhuluma.
Nabii anawaonya kuacha mali hizo na
kumrudia Bwana. Hata hivyo tukumbuke kuwa Mungu hachukizwi na mali bali
na tunaweza kuwa na mali na madaraka halali kama vitu hivi vinatupatia
nafasi ya kuwaongoza wengine vema tukiwajalia haki na ustawi wa maisha
yao.
Mtume Paulo anatualika kutambua mara na kuacha ubaya
tukiongozwa na hekima ya Mungu ambayo inapita ufahamu wa kibinadamu. Kwa
jinsi hiyo hatuna budi kuitafuta na kuipokea hekima ya Mungu ili
itusaidie katika kutawala taifa la Mungu na mali tulizokabidhiwa na
Mungu mwenyewe. Mtakatifu Paulo anazidi kutuambia jinsi hekima ya Mungu
ilivyo ya ajabu ya kwamba katika ubaya wa Wayahudi yaani wanapomkataa
Masiha, mara moja milango inafunguka kwa ajili ya mataifa ndiyo sisi!
Hakika hekima yake haichunguziki, hatuna uwezo wa kuielewa vema kumbe
yafaa kusadiki na kujiweka katika maongozi ya Mungu. Ndiyo kusema katika
udhaifu wetu Mungu aweza kuibua jambo la ajabu kwa ajili ya wokovu
wetu.
Mwinjili Mathayo anatuletea Kristu aliye katika harakati za
uchungaji, yuko Kaisaria Filipi, yuko katika kutekeleza utume wake
uliomleta duniani. Huko anataka kuhakiki kama watu na mitume wanamfahamu
kina au bado. Anaweka swali mbele ya mitume, Je watu wasema mimi ni
nani? Na ninyi mwasema mimi ni nani? Jibu toka jumuiya ya watu ni kwamba
Yesu ni mmojawapo wa manabii, ni Ni nabii Eliya, ni Yohane Mbatizaji na
mwishoni jibu la Mitume linatolewa na Mtakatifu Petro akisema “wewe
ndiye Kristo, mwana wa Mungu aliye hai” Jibu hili la Mtakatifu Petro
ndilo linabeba kiini cha injili, ni ufunuo wa Masiya mpakwa mafuta wa
Bwana.
Kwa njia ya jibu hili mwinjili Mathayo anataka watu wote
wamjue Kristo kama masiya na hakuna tena mfalme mwingine zaidi yake.
Watu walitoa jibu kuwa ni nabii lakini sasa mwinjili anatuambia wakati
wa manabii umekwisha na hivi ni Kristo pekee mwana wa Mungu aliye hai.
Mpendwa hivi leo ukiulizwa Yesu ni nani utasema nini? Kwangu mimi Kristu
ni mkombozi wa maisha yangu anayenipenda katika udhaifu wangu,
anayeniita kila siku kutubu na kumrudia yeye kwa njia ya kitubio. Ni
yule anayewapenda wote bila ubaguzi maskini kwa matajiri.
Tupige
hatua kidogo mbele katika tafakari yetu tuone je jibu la Mt Petro
linaishia pale tu au lina matunda? Jibu la Mtakatifu Petro lina matokeo
makubwa mno, Mtakatifu Petro atakuwa mwamba ambapo Kanisa la Kristu
litajengwa. Na si mwamba tu bali ni mwamba wa kujengea, ni mwamba wa
imani. Makatifut Petro amekiri imani ambayo lazima ikue na izae matunda.
Mwamba huu ni imara na hivi hata nguvu za kuzimu haziwezi kuubomoa.
Anakabidhiwa funguo ambazo tulisikia Nabii Isaya akizungumzia kwamba
mtunza hazina atanyanganywa na Bwana. Tunarudia tena kusema kuwa funguo
ni alama ya madaraka, uwezo juu ya taifa la Mungu.
Oneni
mpendwa, ni mamlaka gani Mtakatifu Petro amepewa ili ailinde imani!
Asimamie Kanisa, afundishe, aonye na zaidi aimarishe imani ya waamini
wote wa taifa la Mungu. Leo hii wajibu huu anao Baba Mtakatifu, Khalifa
wa Mtakatifu Petro, Askofu wa Roma na mchungaji mkuu wa Kanisa lote la
ulimwengu. Tunao wajibu wa kumwombea ili imani yake ibaki imara na abaki
katika kuhudumu na kusimamia taifa takatifu la Mungu akijiimarisha
katika imani na umisionari. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa
kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.