Saturday, March 30, 2013

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Pasaka kwa Mwaka 2013

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Pasaka kwa Mwaka 2013 nchini Tanzania ni: Amani na Maendeleo!



Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salama akitoa ujumbe wake wa Siku kuu ya Pasaka kwa Mwaka 2013 inayokwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, anawaalika Wakristo kwa namna ya pekee kabisa kuombea amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, hasa kutokana na kushamiri kwa vitendo vya choko choko za kidini nchini Tanzania zilizopelekea: madhulumu na mauaji ya viongozi wa kidini pamoja na uchomaji moto wa nyumba za Ibada.

Kinzani za kidini zinazoendelea nchini Tanzania ni changamoto kwa Wakristo na Waislam kukutana na kujadiliana mustakabali wa Tazania. Kwa vile Serikali inayowajibu wa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu inapaswa kuwapo ili kufuatilia majadiliano haya.

Kwa miaka mingi Wakristo na Waislam nchini Tanzania wameishi na kupendana kama ndugu na wala tofauti zao za kidini halikuwa ni jambo la kuwagawa! Lakini mambo yamebadilika katika miaka ya hivi karibuni kiasi cha kuwafanya watu kuanza kujiuliza, hivi kweli ni nani anayehusika na uchochezi wa vurugu za kidini na kwa manufaa ya nani?

Majadiliano ya kidini ni njia muafaka inayoweza kumaliza choko choko za kidini, kila upande ukilijadili suala hili katika ukweli, upendo na haki. Kardinali Pengo anaendelea kuwasihi Wakristo na watanzania wenye nia njema kuepukana na kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi kutokana na madhulumu wanayokabiliana nayo. Anasema, ulinzi na usalama wakati wa Maadhimisho ya Juma kuu ni kazi na jukumu la Serikali, kumbe anatumaini kwamba, Wakristo wataweza kuadhimisha Mafumbo ya Imani yao kwa amani na utulivu.

Kardinali Pengo anasema, atakwenda Kanisa kuadhimisha Mafumbo ya Ukombozi, kama ni kufa ni afadhali afie Kanisani na wala hataacha kwenda kusali kwa sababu ya vitisho vya ulipuaji wa Makanisa vilivyozagaa nchini Tanzania wakati huu.

Kardinali Pengo amevishauri vyombo vya dola kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya ukweli, uwazi na maadili ya kazi. Anasema, Serikali haiwezi kuacha Tanzania kutawaliwa na "wahuni wachache" wanaoleta vurugu kwa kisingizio cha dini na kukazia kwamba, hatua madhubuti hazina budi kuchukuliwa ili haki, amani na utulivu viweze kudumishwa.

Itakumbukwa kwamba, Waziri mkuu Mizengo Pinda wa Tanzania na ujumbe wake walipotembelea Radio Vatican hivi karibuni alibainisha kwamba, Serikali ya Tanzania inatarajia tarehe 4 Aprili 2013 kukutana na viongozi wa kidini na wadau mbali mbali ili kwa pamoja kuweza kujadili mustakabali wa Tanzania kwa kuangalia amani na utulivu kama nyenzo muhimu katika ustawi na maendeleo ya Tanzania.

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR