Showing posts with label watakatifu wote. Show all posts
Showing posts with label watakatifu wote. Show all posts

Friday, November 1, 2013

Sikuku ya Watakatifu woteleo tarehe 01/11/2013

Somo La Kwanza: Ufunuo.7:2-4, 9-14
Wimbo Wa Katikati: Zaburi: 24:1-6 (K) 6
Somo La Pili: 1 Yoh. 3:1-3
Injili: Mathayo 5:1-12
Sikukuu ya Watakatifu wote
Kalenda ya Kanisa Katoliki inajumuisha sikukuu za watakatifu wengi na hata wafia dini. Lakini Novemba mosi, ni sikukuu ya watakatifu wote. Kweli tunasherehekea sikukuu za watakatifu fulani fulani katika siku tofauti lakini Novemba Mosi, tunasherehekea sikukuu ya watakatifu wote, wale tunaowajua na wale tusiowajua. Watakatifu ni wengi na wamefanya kazi nyingi tofauti tofauti lakini zote zikiwa na umuhimu wake katika kuiendeleza na kuikuza imani yetu. Watakatifu ni wengi na hatuwezi kuwajua wote. Hivyo sikukuu hii inawajumuisha pamoja kama kundi moja la watu walioyaishi maisha yao vyema hapa duniani. Sikukuu hii ni kichocheo katika maisha yetu ya imani kwani inatubidi tufuate nyayo zao, tuishe tukimtegemea Mungu zaidi ya chochote. Watakatifu walio pamoja na Mungu mbinguni wanatuombea na kutupa moyo sisi watakatifu tulio safarini kwenda mbinguni. Watakatifu tunao sherekea siku yao leo ni  mashujaa wa imani na kielelezo kwetu, wanatupa moyo kuwa, “Ndiyo kumfuata Kristo kunawezekana.” Kesho Novemba mbili tutawakumbuka marehemu wote. Hawa ni ndugu zetu, wasafiri wenzetu ambao tayari wameiacha dunia hii lakini bado hawajafika mbinguni, wanavikwa mavazi meupe (Ufu.7:9) wanatakaswa kabla ya kuingia mbinguni
Sherehe ya watakatifu wote inatukumbusha kuufuata wito wetu wa kuwa wana wa Mungu. Baada ya mwanadamu kuupoteza utu wake kwa kutenda dhambi, Mungu alimtuma mwanae ulimwenguni ili wale wote wamuaminio wapate ufalme wa milele (Yn. 3:16). Watakatifu wameshaupata ufalme huu wa milele ni wajibu wetu sisi wakristo kufuata mfano wao. Wao walishinda adui wa roho kwa kutumaini neema za Mungu.
Injili ya leo inatuonesha furaha ya watakatifu ilivyo, na njia inayotuwezesha kufika kufika mbinguni. Tunasikia kwamba, “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Kumbe basi, tukitaka vita vya miaka michache hapa duniani vitatuletea furaha na heri ya milele. Inatubidi basi tuvumilie kabisa katika imani yetu, tujaribu kila tuwezavyo tuvishinda vishawishi kwani Mungu hatajaribu zaidi ya neema aliyotupa kuvishinda vishawishi hivyo.  Watakatifu tunaowakumbuka leo, wanatupenda wanatuombea kwa Mungu  ili tuwe pale walipo, karibu na Mungu na kwenye heri ya milele.  Sikukuu hii haina budi kuamsha matumaini makubwa mioyoni mwetu.
Sala:
Ee Mungu niongezee kiu na njaa ya kuyafanya mapenzi yako na siku moja niwe pamoja na watakatifu mbinguni tukikusifu na kuiombea dunia.
Amin

NCHI YANGU FAHARI YANGU TOUR