Saturday, October 18, 2014
Kesho Dominika ya tarehe 19/10/2014, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI anatarajiwa kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu mjini Vatican
Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI ni kati ya viongozi wakuu wa Kanisa
wanaotarajiwa kuhudhuria katika ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya
kumtangaza Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI, Jumapili, tarehe 19 Oktoba
2014 majira ya asubuhi kwa saa za Ulaya. Itakumbukwa kwamba, Baba
Mtakatifu Benedikto XVI aliteuliwa na Papa Paulo VI kuwa Kardinali.
Maadhimisho ya Siku ya 88 ya Kimissionari Duniani kwa Mwaka 2014
Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa Siku ya 88 ya Kimissionari Duniani kwa Mwaka 2014.
Mama
Kanisa tarehe 19 Oktoba 2014 anaadhimisha Siku ya 88 ya Kimissionari
Duniani, iliyoanzishwa kunako mwaka 1926 na Papa Pio wa Kumi na moja na
kuanza kuadhimishwa rasmi hapo mwaka 1927 kama siku ya kukoleza ari moyo
wa kimissionari katika kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya
Wokovu. Hii ni siku ambayo inaadhimishwa mwezi Oktoba, ambao kimsingi ni
mwezi wa kimissionari.
Baba
Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 88 ya
Kimissionari Duniani kwa mwaka 2014 anasema kuna umati mkubwa wa watu
ambao haujabahatika kusikia Habari Njema ya Wokovu, Familia yote ya
Mungu inawajibika kushiriki katika Uinjilishaji kwa kutambua kwamba,
Kanisa limeanzishwa na linatumwa kuwatangazia watu juu ya Ufalme wa
Mungu.
Hii ni siku ambayo waamini wanaalikwa kushiriki
kikamilifu kwa njia ya sala na sadaka yao ili kuonesha mshikamano na
Makanisa machanga duniani kama njia ya kumshukuru Mungu kwa neema
sanjari na kuonesha ile furaha ya ndani. Yesu anawatuma wafuasi wake na
kuwategemeza katika shughuli za kimissionari kama inavyojionesha katika
Maandiko Matakatifu pale alipowatuma wafuasi wake Sabini na wawili,
wakarudi huku wakiwa wamesheheni furaha baada ya kutangaza kuhusu Ufalme
wa Mungu na kuwaandaa watu kukutana na Yesu.
Mitume
wanapoonesha furaha yao, Yesu anawataka wafurahi kwa sababu majina yao
yameandikwa mbinguni na kwamba, wamebahatika kuyaona matendo makuu ya
Mungu yakitendwa mbele ya macho yao! Hii si nguvu ya kutoa pepo wachafu,
bali ile nguvu ya upendo ambao wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu. Uzoefu
na mang'amuzi haya yanakuwa ni sababu ya furaha hata kwa Yesu Mwenyewe
kiasi cha kumshukuru Roho Mtakatifu, huku akimtolea sifa Baba yake wa
mbinguni, kwani ile siri kubwa kuhusu Ufalme wa Mungu iliyokuwa
imefichika inajionesha kwa njia ya Yesu Kristo na ushindi wake dhidi ya
shetani.
Hii ni siri ambaye imefunuliwa kwa maskini na
wanyenyekevu wa moyo ambao wamebarikiwa mbele ya Mungu. Hawa ni kama
Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, Wavuvi kutoka Galilaya na Mitume wote
ambao wamebahatika kushikamana na Yesu wakati alipokuwa anawahubiria
watu Habari Njema ya Wokovu.
Baba Mtakatifu anasema, Yesu
anaonesha ile furaha inayobubujika kutoka katika undani wake kutokana na
ufunuo wa mpango wa Mungu katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu,
kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa mwanadamu kwa
njia ya Yesu Kristo. Hii ndiyo furaha iliyokuwa inabubujika kutoka
moyoni mwa Bikira Maria pale alipomtembelea binamu yake Elizabeti
kumshirikisha kuhusu matendo makuu ya Mungu katika maisha yake.
Hii
ndiyo furaha inayoendelea kububujika katika maisha ya waamini hadi
nyakati hizi, anasema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa
maadhimisho ya Siku ya themanini na nane ya Kimissionari Duniani na
kuwawezesha waamini kuingia katika maisha ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.
Mungu Baba ni chemchemi ya furaha, Yesu Kristo ni kielelezo cha furaha
hii na Roho Mtakatifu ndiye mwezeshaji mkuu, changamoto kwa waamini
kumjifunza na kumwendea Yesu ili aweze kuwafariji na kuwakirimia maisha
ya uzima wa milele, wale wote wanaobahatika kukutana na Yesu.
Wale
wanaokombolewa na Yesu, wanaondolewa dhambi, hofu na "jangwa la maisha
ya kiroho" kwani kwa njia ya Yesu, daima waamini wanaweza kupata na
kuendelea kububujika furaha. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Bikira Maria
pamoja na Mitume wake walioamua kubaki pamoja na Yesu ili kushiriki azma
ya Uinjilishaji, Yesu akawa ni sababu ya furaha yao ya ndani!
Baba
Mtakatifu Francisko anasema ulimwengu mamboleo unakabiliwa na hatari
kubwa ya kumezwa na ulaji wa kupindukia unaojikita katika ubinafsi,
mambo yanayousononesha moyo wa binadamu kwa kutaka furaha za mpito
pamoja na dhamiri mfu. Binadamu anachangamotishwa kujichotea wokovu
ulioletwa na Yesu, wafuasi wake wakiwa wa kwanza kuguswa na upendo wake
ili kuwa kweli ni vyombo vya Injili ya Furaha, ili kushiriki ile furaha
ya uinjilishaji.
Maaskofu wana dhamana ya kwanza kabisa katika
utekelezaji wa mchakato wa Uinjilishaji, kwa kujenga na kuimarisha umoja
wa Kanisa mahalia na kuendeleza utume wa Kimissionari hadi miisho ya
dunia, hasa katika maeneo yaliyoko pembezoni mwa dunia, huko ambako kuna
maskini wanaosubiri kwa hamu kubwa kusikia Habari Njema ya Wokovu.
Upungufu
wa miito ya Kipadre na Kitawa ni kielelezo cha Jumuiya kukosa ile
furaha yenye mvuto na mguso, inayobubujika kwa mwamini kukutana na Yesu
kwa kuwashirikisha pia maskini. Hii ni changamoto kwa Parokia na Vyama
vya Kitume kuonesha ushuhuda wa udugu unaojikita katika upendo wa Yesu
pamoja na kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Pale ambapo kuna furaha ya kweli,
hapo pia kuna ari na moyo wa kutaka kuwashirikisha wengine, hapo ni
mwanzo wa miito mitakatifu. Waamini walei wanahamasishwa pia kushiriki
maisha ya kimissionari, ili kutangaza Injili, lakini wanahitaji majiundo
makini.
Baba Mtakatifu anasema kwamba, Siku ya Kimissionari
Duniani ikuze ndani ya waamini wajibu wa kimaadili wa kushiriki kwa
furaha utume wa kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu, kwa
kuchangia kwa hali na mali, kwa kutambua kwamba, sadaka hii ni sehemu
ya mchakato wa Uinjilishaji wa watu unaobubujika kutoka katika upendo.
Baba
Mtakatifu anawataka waamini katika Makanisa mahalia kutokubali kupokwa
ile furaha ya Uinjilishaji. Anawaalika kujizamisha katika furaha ya
Injili kwa kuirutubisha kwa upendo. Furaha ya mfuasi wa Kristo
inajionesha kwa kukaa na Yesu, mwamini anapotekeleza mapenzi ya Mungu na
anaposhirikisha imani, matumaini na mapendo ya Kiinjili.
Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
It was on August 15, 1815 that Saint Gaspar began the Missionaries of
the Precious Blood at the abbey of San Felice in Giano, Italy. Since
that beginning, thousands of Missionaries have been inspired by the zeal
of St Gaspar and have continued the apostolic work that he began. It
is in recognition of our foundation and in anticipation of the
celebration of our bicentennial anniversary in 2015, that the
Congregation has begun a three year observance of our founding.
Subscribe to:
Posts (Atom)
-
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya...
-
Isidore Bakanja, ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya imani ya Kikristo, Akiongozwa na maisha rahisi kama layman Katoliki wakati wa mauaj...
-
Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza anatualika kutambua kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya ...