Jumapili tarehe 29 Juni 2014 Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Sherehe za Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, kwenye Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hawa ni “vigogo” wa imani
waliojitosa kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa mataifa kwa
njia ya mahubiri, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao,
wakawa tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.
Hii
ni Jumapili ambayo Baba Mtakatifu anatarajiwa kutoa Pallio Takatifu kwa
Maaskofu wakuu wa Majimbo makuu walioteuliwa hivi karibuni, kama
kielelezo cha umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu na Khalifa wa
Mtakatifu Petro. Hii pia ni siku ya mshikamano kwa kuonesha upendo kwa
Baba Mtakatifu kwa njia ya sala,
lakini kwa kuchangia katika Mfuko maalum wa huduma ya mshikamano na
upendo unaotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, sehemu mbali mbali
za dunia.
Mchango huu unaotolewa na waamini pamoja na watu wenye
mapenzi mema unamwezesha Baba Mtakatifu kuwasaidia watu waliokumbwa na
majanga asilia kama vile matetemeko ya ardhi, mafuriko, njaa, ukame. Ni
msaada unalenga kumsaidia mtu mzima katika mahataji yake: kiroho na
kimwili, kwa kuchangia maboresho katika sekta ya elimu, afya na
maendeleo endelevu. Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele kwa ajili ya
kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwa
kuwajengea uwezo ili kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri
mkuu.
“Usiwasahau maskini” ni maneno ambayo Kardinali Claudio Hummes alimwambia Baba Mtakatifu Francisko mara
tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Maneno haya
yakaingia na kunata katika akili na moyo wa Baba Mtakatifu Francisko,
ambaye leo hii maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni anawapatia
kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake, si kwa maneno tu bali
kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Papa akamchagua Mtakatifu Francisko wa
Assis mpenda amani, mazingira na mhudumu wa maskini kuwa msimamizi wake,
leo hii mjini Vatican wimbo umebadilika, mwenye macho aambiwi tazama!
Siku ya Upendo wa Papa ilianzishwa kunako tarehe 8 Agosti 1871 na Papa Pio IX katika Waraka wake wa kichungaji “Saepe Venerabilis”
na tangu wakati huo, kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, Kanisa
linashikamana na Papa kuonesha upendo na ukarimu kwa kuchangia mfuko
unaogharimia shughuli mbali mbali za upendo zinazotekelezwa na Baba
Mtakatifu sehemu mbali mbali za dunia.
Nawe unaweza kushikamana
na Papa kwa kuchangia katika mfuko huu! Kwa njia hii, unashiriki
kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya kwani maisha na utume wa
Kanisa unaendelea kupanuka siku hadi siku!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
-
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya...
-
Isidore Bakanja, ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya imani ya Kikristo, Akiongozwa na maisha rahisi kama layman Katoliki wakati wa mauaj...
-
Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza anatualika kutambua kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya ...
No comments:
Post a Comment