Mpendwa, tunatafakari masomo ya Jumapili ya 25 ya mwaka wa A wa Kanisa,
tukialikwa kuwa na matumaini daima katika kumtafuta Bwana na kutambua
kuwa wema wa Mungu ni wa milele kwa watu wote na fikra zake ni tofauti
na fikra za kibinadamu. Katika somo la kwanza Waisraeli wako utumwani
Babeli kwa sababu hawakutii mausia ya Bwana na zaidi wanaona hawawezi
kusamehewa dhambi zao, wamepoteza tumaini na wanaona kana kwamba Mungu
amewatupa na kuwaacha kabisa. Zaidi ya hilo wanaongeza kosa jingine tena
la kumwona Mungu anayefikiri kama wao, wanafikiri hawezi kuwasamehe
tena.
Mpendwa, katika shida yao hiyo Mungu anamtuma Nabii
Isaya awaambie kuwa fikra na njia za Mungu ni za juu mno ni tofauti na
fikira za kibinadamu kiasi kwamba si rahisi kuzielewa. Zaidi ya hilo
Isaya anawakumbusha kuacha njia zao mbaya na kumrudia Bwana. Kumrudia
Bwana si tu kuacha dhambi, bali
pia kubadili namna ya kumtazama Mungu, Mungu aliye haki na mkamilifu.
Mawazo haya yatajitokeza waziwazi katika Injili ambapo tunaona Mungu
anayewapenda wote wadhambi kwa wema.
Mtume Paulo
akikoleza ujumbe wa nabii Isaya anawaambia Wafilipi, hata kama kuna
shida katika maisha yao watambue kuwa kuishi kwao ni Kristu, ndiyo
kusema la maana katika maisha yao ni Kristu mfufuka. Mara
kadhaa watu wapatapo shida huanza manunguniko dhidi ya Mungu na kusahau
kwamba yote waliyonayo yametoka kwake. Wanasahau kuwa, kwa njia ya
msalaba yaani njia ya mateso, Kristu ametustahilisha kwenda mbinguni.
Ndiyo kusema, hata sisi tuliodhaifu tunapaswa kupitia njia ya mateso ili
kuweza kufika Mbinguni. Kwa hakika mtume Paulo anapoandika barua hii
kwa Wafilipi yuko katika wakati mgumu yaani kuchagua kufa ili akae na
Kristu au kuendelea kuhubiri Injili kwa mataifa, na mwisho anaona
ahitimishe fikra zake akisema kuishi kwangu ni Kristu na kufa ni faida.
Hapa tunaonja imani ya Paulo ilivyozama katika Mwana wa Mungu.
Tujiulize je kwetu sisi kuishi na kufa, twaweza kuvipokea kama alama
ya ushindi katika imani kama Mtume Paulo? Mpendwa msikilizaji jitafiti
na hivi unapokuwa umechoka, unapokuwa umefikia mwisho wa maisha yako
uweze kusema nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza na imani
nimeilinda sasa kufa kwangu ni faida na kuishi kwangu ni Kristu!
Mpendwa mwana wa Mungu tukiongozwa na mwinjili Mathayo, tunapata kuonja kuwa mawazo ya Mungu ni ya juu sana kuliko yetu. Jambo
hili linajionesha wazi katika Injili ya leo pale ambapo Bwana wa shamba
anawaajiri watu mbalimbali katika masaa tofauti na mwishoni anawalipa
ujira sawa. Mpendwa katika hali ya kawaida, Bwana huyu angepaswa
kuwalipa tofauti kwa maana muda wa kazi ulikuwa tofauti. Kuwalipa ujira
sawa pia ni namna ya kusema kuwa uvivu uendelee katika ulimwengu, tuseme
hakuna ile haki ya kawaida yaani common justice!
Hii ni namna yetu ya kufikiri na hata namna ya watu wa wakati huo,
lakini je Mwinjili anataka kutuambia nini? Je Bwana afikiri kama sisi?
Kwa
hakika kuwalipa ujira sawa maana yake, wema wa Mungu ni kwa ajili ya
wema na wabaya. Wale walioajiriwa kwanza ndio walisadikiwa kuwa wema na
wale wa baadaye ndio kundi wakilishi la walio wabaya. Pamoja na hilo
kuna jambo jingine jema, kwamba mwenye shamba anapenda kila mmoja afanye
kazi, asiishi bila wajibu, ajisikie katikati ya jumuiya ya watu kwa
maana kazi huleta heshima. Kwa jinsi hiyo kazi ya wokovu inaendelea na
inawaletea heshima watu wote.
Mfano huu wa mwenye shamba
unatufundisha kuwa Mungu si mhasibu wala meneja anayewalipa watu
kulingana na jasho lao tu, bali kulingana na upendo wake aliokusudia
tangu alipoumba ulimwengu. Hatuna uwezo wa kupata stahili yoyote toka
kwa Mungu kwa nguvu zetu bali kwa uweza wake, huruma yake na mapendo
yake ya milele. Kwa wazo hili tunarudi kwa nabii Isaya anayetuambia kuwa
njia zake ni za juu mno na mawazo yake hatuwezi kuyafikia. Tunaalikwa
kutambua kuwa wokovu si kwa maveterani peke yao bali hata vijana
wanaokuja saa kumi na moja jioni! Hakutakuwa na upendeleo wowote katika
wokovu cha msingi ni kumtafuta Bwana madamu anapatikana. Tumsifu Yesu
Kristu.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya Cpps
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
-
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya...
-
Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza anatualika kutambua kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya ...
-
Isidore Bakanja, ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya imani ya Kikristo, Akiongozwa na maisha rahisi kama layman Katoliki wakati wa mauaj...
No comments:
Post a Comment