Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata
somo la kwanza
anatualika kutambua kuwa Mungu haachi
kutimiza ahadi yake ya kale kwamba atamtuma Nabii atakayetangaza hukumu zake
kwa haki, atakayesema yale ya Bwana na kama atasema kinyume atakufa. Manabii
wengi walitangaza ujumbe wa Mungu lakini hasa katika zama zetu Mungu anasema
nasi kwa njia ya Masiha kama ambavyo Wayahudi walielewa ujumbe huo wa Neno la
Mungu.
Masiha yaani mkombozi ametufundisha
yote na kutujalia Ubatizo na sakramenti nyingine. Kwa njia hiyo kama wana wa
Pentekoste tunaalikwa kutangaza yaliyo ya Mungu na kama ni kinyume basi
tutapotea katika njia zetu.
Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto
katika barua yake ya I sura ya saba, anaweka wazi miito mbalimbali katika
Kanisa na anataka kila mmoja afahamu kwa uhuru kamili, wajibu wake mbele ya
wito huo katika kutekeleza mapenzi ya Mungu. Wito wa ndoa ni wito mtakatifu
ambao wamweka mtu katika wajibu wa familia yaani kuhudumu familia na yote
yahusuyo maisha ya ndoa.
Kwa jinsi hiyo, Mtume Paulo anaona
wajibu huo usipotendwa kwa unyenyekevu na hekima waweza kumfanya mwanafamilia
azame huko na kusahau wito wake wa kushughulikia masuala ya uinjilishaji. Suala
muhimu ni kuwa makini kutambua kuwa ndoa ni kwa ajili ya huduma ya familia,
Kanisa na Mungu mpaji.
Anatafakari juu ya wito wa upadre na
maisha ya kitawa akisema kwa wito huu mmoja aweza katika umakini wake
kushughulikia zaidi maisha ya missioni yaani kupeleka habari njema kwa mataifa.
Awaalika wenye wito huu kuona kuwa wanawajibika zaidi kufungua mioyo yao kwa
Mungu kwa ajili ya wokovu wa watu na wao wenyewe. Wakumbuke useja unatoa zaidi
nafasi ya uwajibikaji katika shamba la mizabibu na hivi madai kwao ni makubwa
zaidi kuliko wengine.
Mpendwa unayenisikiliza yafaa
kukumbuka jambo moja, ikiwa mmoja atakuwa na mashaka upi ni wito mzuri au wa
juu! Toka ndoa twampata Padre na mtawa na hivi Kristu ameweka Sakramenti zote
katika uwiano mkamilifu akitakatifuza maisha ya watu kadri ya wito wa kila
mmoja, yaani kadri ya karama na vipaji alivyomjalia.
Mwinjili Marko anaweka mbele yetu
yule Nabii tuliyehaidiwa katika somo la kwanza atakayetangaza kazi ya Bwana.
Bwana yuko katika utume na anawaponya wagonjwa, si kwa nguvu ya mazingaombwe
bali kwa nguvu ya mkono wa Mungu. Anatangaza vita kinyume na pepo ambapo kwa
kawaida ni ile hali ya kutokuwa na roho wa kweli na hivi wenye pepo wanakuwa
bado hawajakutana na Bwana.
Anataka wana wa Mungu wasibaki chini
ya utawala wa shetani bali wawe huru katika yeye. Kwa jinsi hiyo mara
wakutanapo na Bwana lazima pepo wakimbie kwa sababu yupo aliye Mungu mwenye
nguvu, mwenye ufalme mabegani mwake. Bwana anatoa sauti kali “fumba kinywa
chako umtoke” hii yamaanisha ugomvi uliopo katika ya pepo wachafu na maisha
safi ya Kikristo.
Basi mpendwa mwana wa Mungu
tekelezeni mausia ya Bwana wakati wote ili kukaa katika wito wako kwa furaha na
matumaini ukikumbuka kuwajibika kadiri ya wito huo katika kutenda yaliyo ya
Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.
No comments:
Post a Comment